Latest Posts

CHAGUO LA GK: HESHIMA (KWA MAMA) YAKE JANET OTIENO

Twatumai u mzima mdau wa GK na kwamba Jumapili yako inaenda vema. Hata kama sivyo, bado ni jambo la kumshukuru Mungu kwa maana pumzi unayo, na unaweza kuendelea kusemezana naye.

Kwa wiki hii tukiwa bado kwenye msimu wa Upendo kwa Mama inayoratibiwa na Mkundi Promotions, basi hebu tuelekee nchini Kenya na kukutana na mwanamama Janet Otieno ambaye anatukumbusha kwamba hapa duniani hakuna kama mama, na muhimu sana kumpenda, kwenye video yake mpya ambayo ameitoa wiki hii, Heshima.

Tazama video ifuatayo kisha kama uko kanda ya kaskazini, tukutane kwenye uwanaja wa Chuo Kikuu cha Ushirika, (Moshi Cooperative University) tarehe 30 Novemba kwenye tamasha la Upendo kwa Mama, kisha tusubirie ratiba ya mji unaofuatia.

Onyesha upendo kwa mama.

SOMO: HAWAJAKUKATAA WEWE, WAMENIKATAA MIMI NISIWE MFALME WAO


Kutokana 3:4,11 Mungu alimteua Musa aende kuwatoa Israel mikononi mwa farao,Mungu akampa mamlaka Musa juu ya Israel Kwa hiyo walikuwa ni wao wamsikilize anachosema wafanye maana Mungu alikuwa anawasiliana Na Musa Na kumpa agizo,
Ndivyo ilivyokuwa kwa Samueli walikuwa wamsikilize Na kufanya hivyo hivyo,
Lakini walifika mahali wakakataa kumsikiliza,

1samuel 8:7
Mungu akasem hawajakukataa wewe kuwa mfalme wao Bali wamenikataa mimi....
Ndugu yangu katika kristo huyo Mchungaji anayekufundisha Neno la Mungu,Mungu amemuweka mbele yako umsikilize kupitia lile neno la Mungu analolipokea Kwa ajili ya maonyo kwako au Kwa ajili ya Baraka kwako,lakini unapokataa Na kudharau ujuwe ujamkataa yeye Bali umemkataa Mungu,ndiyo maana kunawatu wanamateso mengi wamekimbia huku Na huko kutafuta Maombi lakini hakuna mabadiliko unajuwa ni Kwa nini Kwa sababu wamemkataa Mungu,
Badilika uwe Na utii Kwa Mtu wa Mungu aliyewekwa mbele yako akuongoze...

RATIBA YA MAAZISHI YA MAREHEMU GEORGE NJABILI
Marehemu George 'Bonge' Njabili
Kwa sasa msiba upo nyumbani kwa marehemu Tabata Bima karibu na Shule ya St Mary's ambapo watu mbali mbali wanaweza kufika kutoa pole kwa familia ya Marehemu.

Ratiba ya kuuaga mwili itaanza kesho saa 4 kamili aubuhi nyumbani kwa marehemu hadi hapo itakapo ishia kisha msafara utaanza kuondoka kuelekea katika kanisa la Kiinjili la Kilutheri Mtoni ambapo watu watapata nafasi ya kuaga tena kabla ya safari ya kuupeleka mwili Tukuyu, mkoani Mbeya.

Kwa mujibu wa mtoa ratiba, Benjamin Kihogo ambaye pia ni mwalimu wa kwaya ya Mtoni, ameeleza kwamba pia watu wanaweza kuchangia kwa kupitia namba ya kaka wa marehemu Tigopesa 0654 02 14 23 Mpesa 0754 46 41 02.

KWAHERI RAFIKI GEORGE, NASI TUNAFUATIA - MSAMI
Na Joseph Msami,
GK Author.
Marehemu George bonge, Joseph Msami na Ritha Chuwalo.
Nimesikitishwa sana na msiba wa huyu mutumishi na rafiki yangu! Nilipomwona zaidi ya miaka kumi iliyopita nilimpenda na kumwomba awe rafiki yangu. Wakati huo hata simu za mikononi zilikuwa siyo nyingi akanipa no ya mezani ofisini kwake.
Niliwasiliana naye sana na hata mara nyingine nahisi nilikuwa namsumbua. Lakini nimejifunza sana unyenyekevu wake mkuu ambao siwezi kuusahau na namna alivyokuwa akimpokea mtu yeyote utadhani wanafahamiana naye kwa muda mrefu!

Imeniuma sana kumpoteza mtu huyu muhimu. Pia nimetiwa changamoto ya kujiandaa muda wowote (Zaburi119:1-5) ili andiko likitimia niwe tayari.

Natamani ningekuwa Dar nishuhudie safari ya mwisho ya rafiki yangu. Nawaombea sana hususani shemeji (mke wa George). Mungu hatawapungukia.

SOMO: MAMBO YATAKAYOLIFANYA JINA LA YESU LIKUPE MATOKEO

Leo nimeamka nikiwa na mzigo na kiu ya kukupa siri hizi zitakazo kusaidia kuwa na ubora na ufanisi katika matumizi ya Jina kuu la Yesu.
Maana kwa Wakristo wengi limekuwa ni jina lisilotoa matokeo na kufanya makubwa kama lilivyofanya nyakati za Mitume wa Yesu na kanisa la kwanza. Naomba ujitahidi kulipitia somo hili kwa umakini na moyo uliofunguka na hakika utapokea kiwango kipya cha ufunuo na upako uliomo ndani ya jina hili kuu la Yesu.
Nakukaribisha, katika jina la Yesu.

Mstari wa kusimamia:
"Kwa maana kila atakayeliitia jina la BWANA ataokolewa" (Warumi 10:13).

Utangulizi:
Matatizo mengi tuliyonayo yametokana na KUFUMBA MDOMO na kuacha KULITUMIA JINA LA YESU KWA IMANI.
Wengi wanalitumia JINA LA YESU kama kibwagizo cha maombi, na kwa namna hiyo haliwezi kutoa matokeo.

Unapotaka jina la Yesu likupe matokeo lazima ujue na kufanyia kazi mambo yafuatayo:

1. Ni jina TULILOPEWA KISHERIA NA MUNGU kutawala na kumilki na kufunga na kufungua chochote duniani kama Ufunguo wa Ufalme wa mbinguni:

"Kwa maana hakuna JINA JINGINE TULILOPEWA litupasalo kuokolewa kwalo" (Mdo 4:12).
Biblia inasema hili JINA LA YESU tumepewa liwe la kwetu kisheria.
Ni JINA TULILOPEWA si "jina tuliloazimwa" kwa muda.
Ukielewa na kuamini kwamba JINA LA YESU NI MALI YAKO pamoja na mamlaka na nguvu iliyomo ndani yake, Hakika Utaanza kulitumia bila hofu na mashaka wala hautalisema kama kibwagizo cha maombi, na litakupa matokeo na miujiza isiyokuwa ya kawaida.

2. Elewa kwamba IMANI YAKO KUHUSU JINA LA YESU inapaswa kuwa sawa na IMANI YAKO KWA YESU MWENYEWE.

Unajua kuna watu WANAMWAMINI MNO YESU, na wanaamini kama angekuwepo "Live" kimwili, angeweza kutatua na kukomesha kila msiba wao.
Lakini watu hawa HAWANA IMANI YA KIWANGO HICHOHICHO kwa JINA LA YESU.
Zingatia hili:
Yesu kama "mwili" ameketi mkono wa kuume mbinguni anatuombea sasa (Waebrania 7:25, 1Yoh 2:1-2, Warumi 8:33-34).
Yesu kama "mwili" yuko mbinguni akituandalia makao (Yohana 14:1-3).

Hivyo Yesu akiwa kama "mwili" hawezi kutokea na kukusaidia.
Yesu yuko pamoja nasi siku zote hata ukamilifu wa dahari kupitia Roho wake mtakatifu ambaye ametupa kama arabuni (guarantee) hata siku ya unyakuo na kupitia JINA LAKE.
Ili Yesu atokee katika ulimwengu wa roho na kukifanya ukitakacho itakubidi uliamini jina lake kwa kiwango kilekile unachomwamini Yeye kama angekuwepo live!

"Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika kuwa watoto wa Mungu, ndio wale WALIAMINIO JINA LAKE" (Yoh 1:2).
Mstari huu wa Biblia unaongelea na kutuonyesha "IMANI KATIKA JINA LA YESU" ambayo ni kuliamini jina lake kwa kiwango kilekile ambacho unakiamini kama Yesu angekuwepo mzimamzima!

Ukisoma Matendo 3:16, utagundua kwamba KILICHOMFANYA KIWETE ATEMBEE NI IMANI KATIKA JINA LA YESU.

Utakapoanza kuambatanisha imani yako yote KATIKA JINA LA YESU kwa kiwango kilekile ambacho ungemwamini Yesu kama ungekutana naye live, hakika miujiza mikubwa itaanza kutokea maishani mwako na kupitia maneno na mikono yako!

"Nimewaandikia ninyi mambo haya ili mjue ya kwamba mnao Uzima wa milele ninyi MNAOLIAMINI JINA LA MWANA WA MUNGU" (1Yoh 5:13).

Kumbuka uzima wa milele ni nuru iliyomo ndani ya mwamini ambayo inapong'aa gizani, giza haliiwezi na halitakuja kuiweza milele (Yoh 1:4-5).
Na huu uzima wa milele unaopindua giza uko mikononi na ndani yao WANAOLIAMINI JINA LA MWANA WA MUNGU, JINA LA YESU!

3. Elewa kwamba MAMLAKA YOTE ALIYONAYO YESU imefungwa ndani ya JINA LAKE.

Yesu alipofufuka na kuwatokea wanafunzi wake, aliwaambia AMEIPINDUA SERIKALI YA SHETANI.
Aliwaambia ANAYO MAMLAKA YOTE MBINGUNI NA DUNIANI (Mathayo 28:18).
Lakini ukisoma Biblia yako vizuri utagundua hii mamlaka yake IMEWEKEZWA KATIKA JINA LAKE.
Wafilipi 2:5-11 inatuambia kwamba:
Yesu alipokubali kutii na kujinyenyekeza hata mauti ya msalaba na kutimiza kusudi la babaye alilompa, ndipo Mungu alimkirimia JINA LIPITALO MAJINA YOTE ili kila kitu cha MBINGUNI, DUNIANI NA KUZIMU kitii na kujisalimisha kwa Yesu Kristo (kipige goti) na kikiri kuwa YESU KRISTO NI BWANA kwa utukufu wa Mungu Baba.
Hii ni mamlaka na mamlaka hii imewekwa ndani ya JINA LA YESU.

Ukielewa kuwa mamlaka yote aliyonayo Yesu imewekwa katika jina lake kama yasemavyo maandiko, itakusaidia kupandisha Imani yako na thamani yako katika jina la Yesu na litaanza kukupa matokeo kila ukilitumia.
Jina la Yesu linafanya kazi kwa wenye maarifa na siri hii.

4. Elewa kwamba jina la Yesu ni kitu halisi (ni roho) kwenye ulimwengu wa roho.

Usipoelewa kwamba jina hili la Yesu ni KITU HALISI (ROHO) katika ulimwengu wa roho, hautaweza kulitumia kufanya mambo makubwa rohoni.

Daudi alijua siri hii, alijua ya kuwa JINA LA BWANA ni kitu halisi katika ulimwengu wa roho kiasi kwamba wakati Goliati anakuja na Panga, fumo na mkuki, Yeye (Daudi) naye alichukua silaha halisi isiyoonekana kwa macho ila inayotajwa kwa mdomo, JINA LA BWANA na akapata ushindi wa kishindo dhidi ya Goliati na kuua MAKUMI ELFU YA WAFILISTI.
Kasome 1Samweli 17 utaona jambo hili kwa uwazi.

"JINA LA BWANA NI NGOME IMARA wenye haki hulikimbilia wakawa salama" (Mith 18:10).

Kwa leo niishie hapa,
Mwl Dickson Cornel Kabigumila
www.yesunibwana.org
TANZIA: MWIMBAJI NYOTA WA INJILI TANZANIA HATUNAYE TENA

Tasnia ya muziki wa injili leo imempoteza mwimbaji wake nyota na mwalimu wa kwaya ya Uinjilisti Mtoni almaarufu kama Lulu choir kutoka kanisa la Kilutheri, George Bonge Njabili aliyefariki dunia mchana wa leo katika hospitali ya taifa ya Muhimbili jijini Dar es salaam.

Taarifa zilizotolewa na rais wa shirikisho la waimbaji bwana Addo November Mwasongwe kupitia ukurasa wake wa Facebook amesema, marehemu George alianguka akiwa nyumbani kwake maeneo ya Tabata jijini Dar es salaam wakati akijiandaa kuelekea kazini tukio ambalo halikuchukua mda mrefu na mwimbaji huyo kutwaliwa kabla hajafikishwa hospitalini.

Marehemu George atakumbukwa kwa huduma yake njema ya uimbaji kupitia kwaya ya Lulu ambako aliongoza nyimbo mbalimbali ukiwemo Around the corner Jesus coming, Tazameni Upendo huu, Haleluya na nyingine nyingi huku akiipamba vyema DVD ya kwanza ya kwaya hiyo iliyobebwa na wimbo wa Lulu. Ni takribani miaka mitatu sasa toka aliyekuwa mwalimu mkuu wa kwaya ya Lulu kufariki dunia, kifo ambacho wengi walidhani aliyefariki ni George kiasi kwamba taarifa za kifo chake hii leo kimepokelewa kwa tofauti hasa baadhi ya watu wakidhani alishafariki siku nyingi.


GK itakupatia taarifa zaidi juu ya msiba huu mzito mara itakapopata habari zaidi. Bwana alitoa na Bwana ametwaa jina la Bwana libarikiwe.


Tazama wimbo wa Lulu umjue aliyekuwa mwalimu wa kwaya hiyo akipiga gitaa kuanzia dakika 1:40


Marehemu George Njabili almaarufu kama George Bonge akiwa na mkewe enzi za uhai wake.