USHUHUDA WA JEHANAMU NA SEHEMU YA MANGOJEO YA WAFU (SEHEMU YA MWISHO).

Msomaji wetu wa gospel kitaa hii leo tunakuletea sehemu ya mwisho ya ushuhuda wa Jehanam na sehemu ya mangojeo kama ulivyosimuliwa na Nyisaki Chaula aliyepata bahati hiyo ya kupelekwa mbinguni kimaono na kuonyeshwa hayo. kama hukusoma sehemu zilizopita basi tafuta habari zilizopita jumatatu ya tarehe 19 na 26 mwezi uliopita.BARIKIWA


UTANGULIZI: 
Picha hii ni yakufikirika tu na yale yaliyosimuliwa.

Ndugu yangu kuna shuhuda nyingi sana zinazoanguka duniani, lakini wachache wanaozingatia kwa vile watoaji si wa dini zao au si wa madhehebu yao wala hawajulikani makanisani. Sasa ninakuomba ewe msomaji, tafuta mahali pa utulivu, mwombe Mungu na kusoma ushuhuda huu ili upokee kile ambacho Bwana amekuletea leo.

Msichana Nyisaki Chaula alionyeshwa na Bwana ushuhuda huu akiwa na umri wa miaka 16 mara baada ya kuhitimu elimu ya msingi. Ushuhuda huu alionyeshwa akiwa ameokoka na si kwamba alikufa bali aliona maono. Maono haya alionyeshwa kati ya tarehe 30 - 31/12/1991; yaani kwa siku mbili tofauti.

Msichana huyu hivi sasa ameolewa na Mwinjilistii Lemsy Mheni pale Uyole Mbeya kwa lengo la kukuza huduma yao. Kabila lake ni Mkinga wa Makete, Msichana huyu anapatikana Uyole njia panda ya barabara ya Malawi - Zambia na Dar es Salaam pembeni mwa kituo cha mafuta ya magari pale Uyole, Bwana awatangulie katika usomaji.Sehemu inayofuata ni sehemu muhimu sana, umesoma na kusikia zote za kwanza, sasa naomba utulie.SURA YA 4

MANGOJEO NA JEHANAMU YA PILI:

Mmoja wa wale malaika akaniambia sasa tunakwenda kukuonyesha Jehanamu sehemu ya pili nikasema, Ah kuna sehemu nyingine tena? Akasema Ndiyo, hii imezidishwa ukali mara saba zaidi (Mithali 15:10).
Baada ya mazungumzo hayo, ndani yangu furaha ya uzima wa milele ikatoweka nikawaza iwapo sehemu ile nililia vile? Je hii itakuwaje? Nikawafuata katika sehemu hii ya mangojeo peke yake ilinitoa raha, kwa sababu ilikuwa ni kama mara saba zaidi ya ile ya kwanza. Watu wake walitoa sauti za uchungu mkubwa mara saba zaidi, watu niliowaona ni wale wote waliozijua siri za Mungu na kudharau, ni wale wote waliookoka na baadaye kuacha wokovu. (Ebrania 2:3, 6:4-6) Ni mchungaji na mwaalimu (Yakobo 3:1, Ezekieli 34:2-6) wanalia milele na milele bila kutoa chozi moja. Kabla hata ya kuonyeshwa nililia kwa uchungu sana na kuishiwa nguvu.


Akainuka mtu wa kwanza akasema, Bwana naomba umtume mtumishi wako aniletee tone la maji niuburudishe ulimi wangu. Mpendwa hebu jiulize wewe upo duniani, je unaridhika na tone moja la maji? Basi sehemu ile tone la maji lina thamani sana wanalilia tone hilo usiku na mchana.

Malaika akawaambia mlipokuwa duniani mliichezea neema ya Mungu, sasa hivi ni sehemu ndogo sana ya mateso bado sehemu yenyewe. Yule mtu akajitupa na kuendelea kulia kwa uchungu mno nilimwangalia tena haikuinuka kabisa.

Nikaendelea kuwafuata wale watu huku nikilia na kutembea kwa taabu mno tukamkuta mtu wa pili, akasema, Bwana utupe sekunde 10 tukaihubiri injili ulimwenguni ili waokoke. Yule Malaika akasema mlipokuwa duniani, mlikuwa na muda mwingi sana wa kuihubiri injili, lakini mliutumia kwa tamaa zenu sasa hii ni sehemu ndogo tu, ya duniani, nikalia kwa uchungu sana. Hakuinuka tena, mateso waliyonayo yanawafanya waombe sekunde 10 kuhubiri.

Mpendwa muda uliopoteza kwa mambo yasiyo ya maana utadaiwa, maana wewe ungehubiri injili, Jehanamu ingekosa watu wa kwenda kwa sababu umetumia vizuri, muda wako kuhubiri injili.

Mara nikasikia kigelegele cha kutisha mno nikauliza hivi, kuna mtu ametupwa motoni? Wakasema hapana. Tumesema jehanamu hii imezidishiwa ukali mara saba zaidi. Sasa kigelegele hicho ni cha moto kikishangilia kwa sababu muda wake umefika. Nikasikia mara nyingine tena, nikauliza vilevile nikaambiwa mbona wewe husikii, jehanamu hii imezidishwa mara saba zaidi. Wale watu wanasikia vigelegele vya kutisha lakini hawana la kufanya zaidi ya kusubiri mateso, tofauti na duniani ambapo mtu akipata shida kidogo anajiua, lakini sehemu hii haiepukiki. Tofauti nyingine tena ni kwamba duniani mtu anayo nafasi ya kutubu, lakini sehemu hii hakuna.

Ndani ya ule moto niliwaona FUNZA waliokonda sana, basi nikasikia sauti kutoka upande ule ikisema Bwana watu uliosema utawaleta watakuja lini? Nikashituka na kuuliza je huku kuna mtu, funza hao waliongea lugha ya Kiswahili. Akawaambia wale funza subirini kidogo, hapo ndipo walipoonekana kuwa wamechokozwa. Hakukuwa na maelewano kabisa, walipiga kelele wakisema chakula chetu.

Akaniambia hao funza ulivyowaona wamekonda watakapomshika mwanadamu ipo kazi. Nililia sana hadi wale malaika wakaamua kuniondoa sehemu ile; akasema sasa kawaambie watu wote duniani, usiongeze wala usipunguze. Nikasema Bwana mimi duniani siendi wala hapa sikai nipeleke kwa wale wanaoimba. Basi akanigusa bega, nikashangaa natokea shambani saa kumi na mbili jioni na mama ndipo aliposhituka na kuja kuniona.

Sasa ndugu yangu, nimekueleza jinsi ilivyokuwa na sasa ni juu yako wewe kuchagua, sikuongeza wala sikupunguza (Mathayo 7:13-14, Kumbukumbu 3:19-20).

MIMI SITAONGEZA NA SASA NI KAZI KWAKO KUAMUA (Ufunuo 3:20)

MUNGU NA AKUBARIKI.


Share on Google Plus

About Ambwene Mwamwaja

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.