HOJA YA ASKOFU GAMANYWA--UKRISTO (5)

Askofu Sylvester Gamanywa, Rais wa Wapo Mission International.
Kwanini nguvu za kanisa la kwanza
 hazionekani katika kanisa la leo? -4

Katika toleo lililopita tuligusia habari kuhusu nadharia ya theolojia mbadala kama chimbuko la kanisa kujitenga na Israeli kiimani na hivyo kupoteza nguvu za Roho Mtakatifu. Leo nimeanza uchambuzi wa chanzo kingine kilichosababisha nadharia ya theolojia mbadala kupata nguvu za ukengeufu wa kiimani. Tutapia kwa ufupi historia ya ubinadamu wa Yesu Kristo duniani japokuwa anatambulika kuwa ni Mwokozi wa Ulimwengu :

Hatuwezi kutenganishani
ubinadamu wa Yesu na Uyahudi wake

Wakristo wengi tunamtambua na kumkiri kuwa ni Mwana wa Mungu, Ni Mungu! Aidha wakristo wengi wanamtambua na kumkiri Yesu kuwa japokuwa ni Mwana wa Mungu aliamua kuja duniani, akafanyika binadamu kamili sawasawa na sisi. Bado huu pia ni ukweli wa kitheolojia na kihistoria. Ndivyo alivyokuwa. Yesu hakuwa mzuka au mzimu, alikuwa binadamu kamili. Hata hivyo, kwa bahati mbaya, tunao baadhi ya watu waitwao wakristo ambao ni wengi, wasiomtambua na kumkiri Yesu Yesu kama Myahudi na Mfalme wa Israeli!!

Kusema kweli, itikadi, au nadharia au mtazamo wa kutomkumtambua Yesu kama Myahudi halisi, hakuna tofauti yoyote na kutokumtambua Yesu kama kweli alikuwa binadamu kamili! Nasema hivi kwa sababu, hakuna  binadamu ambaye ni binadamu kamili asiye na asili ya ukoo, kabila na utaifa kamili duniani. Mizimu na mizuka wanaojitokeza kama binadamu ndio sio binadamu kamili.

Kama kweli tunaamini kwamba Yesu alikuwa binadamu kamili, lazima pia tukubaliane na ukweli wa kihistoria kwamba alizaliwa duniani akitokea katika ukoo, kabila, na utaifa wa mahali fulani. Huu ni ukweli wa kihistoria na kibailojia ambao usipoaminiwa na kukubaliwa kunazalisha “imani potofu” katika jamii ya waitwao Wakristo.

Ni kwa kusudi la kutoa elimu kwa ajili ya baadhi ya wasioamini, ukoo na utaifa wa Yesu Kristo duniani, napenda kuwapitisha kwenye maandiko matakatifu ili kuwathibitishia madhumuni ya makala hii kwamba, shida ya kanisa la leo kutokuwa na nguvu za Roho Mtakatifu kama kanisa la kwanza kulisababishwa na ukengeufu wa itikadi ya kujitenga na shina la imani ya Ukristo ambalo ni Israeli.

Yesu alizaliwa kama mfalme wa Myahudi,
 na alizikwa kama mfalme wa Myahudi

1.   Utabiri wa kuzaliwa kwa Yesu

Biblia nzima, kuanzia Agano la Kale mpaka Agano Jipya, imenukuu taarifa za utabiri na ujio wa Mkombozi wa Ulimwengu, ambaye angekuja duniani, na angezaliwa kama binadamu na kutumika kama binadamu. Tunaposoma katika Maandiko ya Agano Jipya tunakutana na utabiri wa malaika Gabrieli ukitolewa kwa Mariamu mama yake Yesu kwamba atachukua Mimba maalum kwa muujiza na atazaa mtoto maalum, na ambaye atarithi kiti cha utawala wa mfalme Daudi:

“Tazama, utachukua mimba na kuzaa mtoto mwanamume; na jina lake utamwita Yesu.  Huyo atakuwa mkuu, ataitwa Mwana wa Aliye juu, na Bwana Mungu atampa kiti cha enzi cha Daudi, baba yake.  Ataimiliki nyumba ya Yakobo hata milele, na ufalme wake utakuwa hauna mwisho. (LK. 1:31-33)

Maandiko yanasema waziwazi hapa juu kwamba, Yesu ametabiriwa atakuwa “Mwana wa Aliye Juu”; kwa maana ubini wake hautatokana na baba mzazi wa kiume ambaye ni binadamu. Lakini immewekwa bayana kwamba bado ujio wake duniani ni “kuwa mfalme wa Israeli kwa kurithi kiti cha Daudi, baba yake”.

2.    Kuzaliwa kwa Yesu

Usiku wa kuzaliwa kwa Yesu, Mungu alituma jopo la malaika ambao waliwaendea wachungaji wa kondoo waliokuwa Bethlehemu ili kuwajulisha habari za kuzaliwa kwa Mwokozi wao ambaye atawarejesha katika mahusiano na Mungu wa Israeli:

“Malaika akawaambia, Msiogope; kwa kuwa mimi ninawaletea habari njema ya furaha kuu itakayokuwa kwa watu wote;  maana leo katika mji wa Daudi amezaliwa, kwa ajili yenu, Mwokozi, ndiye Kristo Bwana.”(LK. 2:10, 11)

Kupitia maandiko hapa juu, tunasoma juu ya maneno haya, “…katika mji wa Daudi…” amezaliwa kwa ajili yenu, Mwokozi, ndiye Kristo Bwana…” Huyu anayezungumuziwa ni Yesu ambaye japokuwa ni Mwokozi wa ulimwengu, lakini ni Mwokozi wa Wayahudi kwanza!! Nitaliongelea baadaye maana ya hili neno “.Kwa Myahudi kwanza…..”

3.    Mamajusi walifunuliwa kuzaliwa kwa mfalme wa Wayahudi

Kundi jingine muhimu linalotajwa kuhusika na ugunduzi wa ujio wa Yesu Kristo duniani walikuwa ni mamajusi. Hawa walifahamu kwa kutazama nyota ambayo iliashiria waziwazi kwamba, mfalme amezaliwa katika Bethlehemu. Wafanya kosa la kwenda kuulizia habari hizi kwa mfalme Herode ambaye ndiye aliyekuwa “mfalme wa wayahudi” lakini chini ya Utawala wa Kirumi. Walipofika kwake waliuliza sio “kazaliwa nani?” bali “yuko wapi”!

“Yesu alipozaliwa katika Bethlehemu ya Uyahudi zamani za mfalme Herode, tazama, mamajusi wa mashariki walifika Yerusalemu, wakisema,  Yuko wapi yeye aliyezaliwa mfalme wa Wayahudi? Kwa maana tuliiona nyota yake mashariki, nasi tumekuja kumsujudia.” (MT. 2:1, 2)

Hapa tunashuhudia mamajusi wakimtafuta mfalme aliyezaliwa. Hawakuwa na mashaka kwamba kazaliwa mtoto wa aina gani. Walikuwa wakitafuta yuko wapi, ili wamsujudie kama mfalme.!

4.    Yesu alizaliwa kama myahudi na kufanyiwa sheria zote za kiyahudi

Wayahudi walikuwa na sheria kamili za kijamii zinazohusu taratibu mtoto wa kiyahudi anapozaliwa anatakiwa kufanyiwa nini, na kwa mchakato upi. Baada ya kuzaliwa kwa Yesu, siku ya nane ilibidi afanyiwe tohara kama ilivyo desturi ya wayahudi wote:

“Hata zilipotumia siku nane za kumtahiri, aliitwa jina lake Yesu; kama alivyoitwa na malaika kabla hajachukuliwa mimba.” (LK. 2:21)

Katika ulimwengu wa enzi hizo, tohari lilikuwa tendo kubwa linalowatofautisha wayahudi na mataifa mengine ambayo si wayahudi. Kutahiriwa kulimaanisha kuingia katika Agano la Mungu na Ibrahimu, na asiyefanyiwa tohari hiyo hakustahiri kushiriki Baraka za ukoo wa wana wa Ibrahimu.

Yesu Kristo, hakuishia kutahiriwa peke yake, bali mambo mengine yanayopasa torati ya Musa ilibidi yatekelezwe juu yake kama mtoto wa kiyahudi:

“Kisha, zilipotimia siku za kutakasika kwao, kama ilivyo torati ya Musa walikwenda naye hata Yerusalemu, wamweke kwa Bwana,” (LK. 2:22)

Mambo yote ya utakaso kwa mujibu wa torati yalifanyikia Hekaluni kwa makuhani, na ndivyo Yesu Kristo alivyofanyiwa na wazazi wake wa kimwili ambayo walikuwa ni wayahudi. Walihakikisha kila taratibu na kanuni zinazingatiwa  kwa ajili ya Yesu ndipo waliporudi Nazareti:

“Basi, walipokwisha kuyatimiza yote kama yalivyoagizwa katika sheria ya Bwana, walirejea Galilaya mpaka mjini kwao, Nazareti.” (LK. 2:39)

Yesu alianza huduma zake
 kwa wayahudi kwanza

Yesu alipoanza huduma zake za kutangaza ufalme wa Mungu, kipaumbele chake kilikuwa wazi kabisa. Alijitambulisha kuwa ametumwa kwa kondoo wa Israeli kwanza:

“Akajibu, akasema, sikutumwa ila kwa kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli.” (Matt.15:24)

Na pia tunashuhudia kwamba Yesu alipotaka kuwatuma wanafunzi wake wapelelke habari za ujio wake kule alikotarajia kufika yeye mwenyewe baadaye; hakuwaruhusu kwenda nje ya mipaka ya taifa la Israeli, bali aliwasisitiza kuwaendea wayahudi kwanza:

“Afadhali shikeni njia kuwaendea kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli.” (MT. 10:6)

Maelekezo haya hayamaanishi kwamba, Yesu hakutaka watu wengine nje ya Israeli wapate wokovu wake, bali ukweli usiopingika ni kuwa kipaumbele kilikuwa ni taifa la Israeli kwa sababu wao ndio waliokuwa na Agano na Mungu na warithi wa ahadi za maagano ya kimungu.

Wakati Yesu alipokutana na yule mwanamke msamaria kisimani walikuwa na mazungumuzo mengi lakini hatimaye walifikia kipengele cha ibada, na mahali sahihi pa kuabudia. Ni katika sehemu hii Yesu alipoweka waziwazi kwamba, wokovu unaojia ulimwengu mzima, hautatoka mahali pengine isipokuwa wayahudi:

Ninyi mnaabudu msichokijua; sisi tunaabudu tukijuacho; kwa kuwa wokovu watoka kwa Wayahudi. (YN. 4:22)


Utabiri wa Dhiki dhidi ya Wayahudi

Baadhi ya wakristo wasiotambua utaifa na ufalme wa Yesu Kristo kwa wayahudi, wamekuwa wakitafsiri habari za ujio wa dhiki kuu itakayokuja kuwa ni kwa ajili ya kanisa. Lakini maandiko yale wanayotafsiri hivyo, Yesu aliyawatabiriwa wayahudi naa sio mataifa wala kanisa:

“Wakati huo watawasaliti ninyi mpate dhiki, nao watawaua; nanyi mtakuwa watu wa kuchukiwa na mataifa yote kwa ajili ya jina langu.” (MT. 24:9)

Utabiri kuhusu mateso yatakayowapata wayahudi umetafsiriwa kuwa ni utabiri wa mateso dhidi ya kanisa. Ni kweli kwamba kanisa nalo limepitia mateso na adha mbali mbali kwa vizazi vilivyotangulia. Lakini kiini cha maneno tuliyosoma hakikulenga kanisa kama tunavyolitafsiri hivi leo. Haya ni mateso dhidi ya wayahudi ambao watamwamini Yesu na kumtambua kuwa ndiye Masihi wa kweli wa Wayahudi.

Hata mateso kwa kanisa la kwanza yalianza kwa wayahudi waliokuwa wamemwamini Yesu Kristo, ukianza na mitume wake pamoja na wafuasi wao. Lakini bado mateso haya hayakuwa na maana ya dhiki kuu aliyowatabiriwa wayahudi. Dhiki hiyo ni maalum itakayotokea kwa kipindi maalum, na walengwa wakuu watakuwa ni wayahudi. Hata yale mateso ambayo wayahudi waliyapata kwenye vita kuu na mauaji ya kimbari ya wayahudi milioni sita, bado hayakuwa ni dhiki kuu iliyotabiriwa.

Dhiki kuu iliyotabiriwa ilikusudiwa kutokea wakati taifa la Israeli limekusanyika na kurejea katika nchi yao na kujitawala kama taifa huru, mpaka na kujenga hekali na kuanza kutoa dhabihu kama zamani zake! Kipindi hiki bado hakijafika lakini sehemu ya maandalizi yake imeshaanza tayari. Ninachootaka kusisitiza hapa ni kwamba Yesu aliwatabiria wayahudi habari za dhiki kuu itakayowajia na wajipange kukabiliana nayo:

“Lakini watakapowafukuza katika mji huu, kimbilieni mwingine; kwa maana ni kweli nawaambia, Hamtaimaliza miji ya Israeli, hata ajapo Mwana wa Adamu.” (MT. 10:23)

Maandiko haya hapa juu yataja waziwazi kwamba dhiki hii itakapofika, Israeli itakuwa ni nchi kamili na miji yake yote. Dhiki hii inaonesha kwamba nchi yao itavamiwa na msako mkali utafanyika dhidi ya wayahudi ambao wanamtabua Yesu Kristo kama Masihi wa kweli. Aidha, inaonesha waziwazi kwamba dhidi hiyo itakuwapo kwa kipindi maalum na atakayekuja kuikomesha ni Yesu Kristo atakaporudi mara ya pili duniani.

Ushahidi mwingine wa kuthibitisha kwamba dhiki kuu iliyotabiriwa na Yesu ni kwa ajili ya Wayahudi, na pale ambapo Yesu Kristo anasema habari za chukizo la uharibifu kusimama katika patakatifu. Kama nilivyosema hapo awali, taifa la Israeli litakuwa limerejea nchini Israeli na kuwa nchi huru jambo ambalo tayari limeshafanyika tangu mwaka 1948.

Lakini kinachongojewa  kwa hivi sasa ni  muujiza wa ujenzi wa hekalu la kuabudia ili waanze upya zoezi la kutoa dhabihu kama zamani. Baada ya kufikia hatua hii ndipo atakapokuja yule mwenye kusababisha kuwepo kwa dhidi kuu dhidi ya wayahudi na kulinajisi hekalu lao. Na hapo ndipo mateso dhidi ya wayahudi yataanza kwa nguvu sana:

“Basi hapo mtakapoliona chukizo la uharibifu, lile lililonenwa na nabii Danieli, limesimama katika patakatifu (asomaye na afahamu),  ndipo walio katika Uyahudi na wakimbilie milimani;  Ombeni, ili kukimbia kwenu kusiwe wakati wa baridi, wala siku ya sabato.  Kwa kuwa wakati huo kutakuwapo dhiki kubwa, ambayo haijatokea namna yake tangu mwanzo wa ulimwengu hata sasa, wala haitakuwapo kamwe. “(MT. 24:15, 16, 20, 21 SUV-SW)

Unaona maneno haya? “Chukizo la uharibifu….limesimama katikaa patakatifu..” na “waliopo katika Uyahudi wakimbilie milimani…..” na “…kusiwe wakati wa baridi, wala siku ya sabato..” Haya maneno ya “Patakatifu”, “Uyahudi,” na “sabato” yote yanawalenga wayahudi waliomo katika nchi yao; na wenyekufanya ibada kwenye hekalu lao; na sasa wanasakamwa dhidi ya imani yao juu ya Masihi wa kweli.

Alisulubiwa Msalabani
kama Mfalme wa Wayahudi

Mwisho kabisa, nisingependa kuacha kuelezea juu ya mateso ya Yesu Msalabani na maziko yake. Ni muhimu kutambua kwamba, Yesu alishtakiwa kwa madai ya kiimani na kisiasa. Shtaka la kwanza alijitambulisha kuwa ni Mwana wa Mungu, ambapo wayahaudi wenzake walimwona anakufuru. Na shtaka la pili alijitambulisha kuwa yeye ni mfalme. Jaji mkuu aliyesikiliza kesi ya Yesu na wayahudi waliomshtaki ambao walitaka adhabu ya kifo, katika kuandika mashtaka yaliyotolewa dhidi ya Yesu aliandika juu ya msalaba kama ifuatavyo:

“ Naye Pilato akaandika anwani, akaiweka juu ya msalaba, imeandikwa, YESU MNAZARETI, MFALME WA WAYAHUDI.” (YN. 19:19)

Kwa maandiko haya, Pilato aliandika anwani akaiweka juu ya msalaba wa Yesu. Lakini Mathayo yeye aliandika kwa wazi zaidi kuhusu kile Yohana alichokiita “anwani”. Yeye alisema “mashtaka yake:

“Wakaweka juu ya kichwa chake mashitaka yake, yaliyoandikwa HUYU NI YESU, MFALME WA WAYAHUDI.” (MT. 27:37)

Maziko ya mwili wa Yesu

Mwisho kabisa ni habari ya maziko ya mwili wa Yesu baada ya kufa kwake msalabani. Kwa wengine suala la maziko halina maana kubwa kwao kwa sababu mbali mbali. Lakini hapa mimi nimelipa uzito kwa sababu tumeanza mwanzo wa mada hii kwa toleo hili na historia ya kuzaliwa kwa Yesu kama Myahudi. Na sasa tunashuhudia kwamba maziko yake yalifanyika kwa desturi za kiyahudi:

“Basi wakautwaa mwili wake Yesu, wakaufunga sanda ya kitani pamoja na yale manukato, kama ilivyo desturi ya Wayahudi katika kuzika.” (YN. 19:40 SUV-SW)

Itaendelea Jumanne ijayo..

Share on Google Plus

About Ambwene Mwamwaja

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.