BUNGE MAALUM UKINGONI, OMBEA KILA HATUA

Makamu mwenyekiti wa Bunge Maalum, Mhe. Samia Suluhu Hassan
Hatimaye baada ya kamati za Bunge Maalum kumaliza kuwasilisha mapendekezo na marekebisho ambayo wanaona yanafaa kwa ajili ya rasimu ya katiba iliyopendekezwa - kifuatacho ni kujipanga kwa ajili ya upigaji wa kura, imefahamika.

Mwenyekiti wa kamati ya uandishi, Mhe. Andrew Chenge, ambaye aliwasilisha Rasimu ya Katiba inayopendekezwa wiki hii, ameeleza siku ya Jumamosi kuwa kinachofuata kwa hivi sasa ni kuweka yale ambayo ni ya msingi.

"Kazi ya uandishi si nyepesi, huwezi ukayabeba yote (yanayopendekezwa). Kwa kuwa ni Katiba ya nchi, Katiba itabeba mambo ya msingi na mengine yakafafanuliwe na sheria za nchi.”

Anaeleza Chenge na kuongeza, "Mengi mazuri ya msingi yapo, tutafanya kila lililo ndanu ya uwezo wetu wa kisheria, liingie. Tuwahakikishie watanzania kwamba tunataka kuwa na katiba nzuri."

Wajumbe wa Bunge Maalum wanatarajia kuanza kupiga kura siku ya Jumatatu, baada ya rasimu ya katiba inayopendekezwa kuwasilishwa upya na kamati ya uandishi.

Baada ya taratibu zote kukamilika, na iwapo Bunge Maalum litaipitisha, hatua itakayofata ni kwa wananchi, kuamua kama wanaipitisha kuwa katiba yao ama kuikataa - na iwapo ikikataliwa, basi Katiba ya sasa ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, ndio itakayoendelea kutumika.

Iwapo hujasoma nyaraka hizi, fanya hivyo sasa (GK inakukusanyia nyaraka hizo muhimu) kwani ni jukumu lako kama mwananchi kujua kinachoendelea kwa mustakabali wa taifa hili. Ama kama asemavyo Mhe. Chenge,  "Nyinyi Watanzania ndio mtaamua mtakapozisoma hizi hati mbili, ukweli uko wapi. Msingi wa rasimu ya katiba unaopendekezwa ni Rasimu ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba, hakuna kitu kingine, tumeiboresha - na ndio msingi wa wajumbe hawa.

Pamoja na kuwepo kwa makundi yalioonyesha dhahiri kuchoshwa na namna mchakato unavyoendeshwa na hatimaye kuondoka Bungeni, na hivyo kukosekana kwa maridhiano kama ambavyo ilitarajiwa iwe, iwapo Rasimu ya Katiba unayooendekezwa itapita na kupitishwa pia na wananchi, basi huo ndo utakuwa mwanzo wa kupata Katiba mpya, iliyoshirikisha makundi mbalimbali ya wanajamii kwenye utunzi wake.

Pamoja na hayo, jambo ambalo limeibua tafakuri, ni kuhusu mjumbe mmojawapo, Mhe. John Cheyo, ambaye alisisitiza kutopindisha maneno na majina, akisisitiza Tanzania inaundwa na Tanganyika na Zanzibar, hivyo basi ni vema Katiba ikatamka waziwazi jina Tanganyika na si kutaja Tanzania Bara.

Kilichopo mbele yako ni kuombea kila hatua ya mchakato huu, iende kwa ukamilifu sawasawa na mapenzi ya Mungu. Mungu husikia unachonena, fanya sasa pasi kusubiri.

Tutaendelea kukufahamisha maendeleo ya kuzailwa kwa Tanzania mpya, kutoka kitovu cha nchi, Dodoma.
Share on Google Plus

About Gospel Kitaa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.