HOJA: HEKIMA YA MASKINI HUDHARAULIWA

Nimelazimika kusitisha makala iliyokuwa ikiendelea (viacheni vyote vikue) kwa sababu mazingira nayo yamebadilika. Mazingira yetu yanabadilika kila siku kiasi cha kutokuendeleza makala moja kwa muda zaidi ya majuma tatu kutokana na mambo mapya yanayozidi kuibuka na kufanya makala kupoteza uzito wake. Aidha, nimelazimika kuleta mada mpya kutonakana na umuhimu na uzito wake kwa mazingira ya sasa. Mada yenyewe nimeibatiza kichwa cha habari cha “hekima ya masikini hudharauliwa, wala maneno yake hayasikilizwi.”

Yaliyoandikwa katika Biblia
ni “halisi” na wala sio “hadithi”
Askofu Sylvester Gamanywa

Watu wengi wanaposoma Biblia, ati kwa kuwa ni kitabu cha karne nyingi za miaka, basi hata maandiko yake nayo yamepitwa na wakati; au pengine ni sawa na hadithi za kujitungia. Kwa utafiti na uzoefu wangu, nimesoma vitabu vingi vya zamani sana na vya kisasa; vya kidini na vya kisekula; sijaona kitabu ambacho maandiko yako hayapitwi na wakati kama Biblia. Kuanzia Agano la Kalel mpaka Agano Jipya; kila nisomapo ninazidi kushangazwa na maandiko yake jinsi yalivyo halisi, yasivyopitwa na wakati, na yanadhihirisha uhalisia wa maisha ya kizazi hiki kuliko nadharia na itikadi za vitabu vingine vyote.

Mojawapo ya kifungu cha maandiko ambacho kila ninapokisoma na kulinganisha na maisha yetu ya sasa, nakuta uhalisia wake ni halisi pengine na hakuna ubishi dhidi yake. Maandiko haya ni kama yalivyoandikwa na mwandishi maarufu wa kitabu cha Mhubiri, ambacho kimejaa hekima iliyothibitishwa na mwandishi kwa uzoefu wake binafsi:

"Ndipo niliposema, Bora hekima kuliko nguvu; walakini hekima ya maskini hudharauliwa, wala maneno yake hayasikilizwi". (Mhubiri 9:16)

Japokuwa maandiko haya yameandikwa vizazi vingi vilivyopita; ukweli wake uko halisi kwa kizazi hiki pengine hata kuliko vizazi vilivyopita. Mfalme Sulemani alikuwa akisimulia kisa cha mji mmoja uliokuwa umewekewa mikakati ya kutekwa na kuharibiwa; na mfalme wa mji ule pamona na wenye hekima wa mji hawakuwa na ufumbuzi wa kuunusuru na janga hilo tarajiwa. Ndipo akatokea “mtu maskini” mmoja ambaye alitoa ushauri wake, ukafanyiwa kazi, na kweli na mji ukanusurika kuvamiwa.

Sasa kilichomshangaza Sulemani ni baada ya matokeo makubwa ya ushauri wa maskini; hakuna aliyetaka kumkumbuka masikini aliyeunusuru mji. Ndipo Mwandishi akaweka mithali yake akisema; “bora hekima kuliko nguvu”; hapa akimaanisha kwamba “matumizi ya hekima” ni bora zaidi kuliko “matumizi ya nguvu”! Huu ni ukweli halisi hata kwa mazingira yetu ya sasa pengine kuliko vizazi vilivyopita. Uzoefu wa Sulemani ulibaini kwamba, “matumizi ya nguvu” hayana matokeo mazuri ikilinganisha na “matumzi ya hekima”!

Lakini kitu cha pili kilichomshangaza Sulemani hata akalazimika kukitia kwenye kumbukumbu ya maandiko ni jinsi ambavyo; “hekima ya masikini inavyodharauliwa; na maneno yake hayasikilizwi”! Kwa msomaji makini anaweza kuhoji usahihi wa maandiko ya Sulemani kwamba, “mbona hekima ya masikini ilipokelewa, na ushauri wa maneno yake ulifanyiwa kazi hata ukaunusuru mji?

Jibu makini hapa sio kwamba hekima ya maskini haikupokelewa na ushauri wake hakuzingatiwa; hoja ya msingi hapa, ni “kutokutambulika, wala kupongezwa hadharani kwa hekima ya maskini”! Kila wazo jema linapotolewa likafanya kazi kwa manufaa ya wengi, ni haki na utu na uungwana kwake yule mwenye kutoa wazo hilo; apate heshima yake stahili na shukrani kwa mchango wake husika.

Lakini, utamaduni na mazoea ya binadamu katika jamii, tafsiri potofu kuwa “hekima ya maskini” ya mara moja haithaminiki. Wengine hutafsiri kwamba ilikuwa ni “bahati yake tu” ambayo mtu yeyote angeipata na hivyo muhusika hana haki wala uhalali wa kutambulika na kupongezwa hadharani.

Ni kutokana na uzito wa maandiko haya, ndio umenifanya nilazimike kuleta mada hii ili kwa pamoja tutafakari na kujiuliza maswali ya msingi ambayo majibu yake yaweza kutusaidia kama watanzania kupata ufumbuzi wa matatizo ya umaskini sugu wa kipato.
 
Kwanini hekima ya tajiri ndiyo huheshimiwa
na maneno yake kusikilizwa kuliko masikini?

Kabla sijaanza uchambuzi wangu katika kujibu swali la msingi, naomba kwanza tukubaliane kimtazamo; hata kama ni kwa muda tu; kwa wakati unaposoma makala hii! Tafadhali, hebu weka kando kwa muda “mawazo na mtazamo hasi” dhidi ya matajiri!

Wakati huo huo tukubaliane kwamba aina ya “tajiri” tunayemzungumuzia hapa sio yule wa “jamii ya mafisadi”, wenye kujipatia mali kwa njia za wizi na udanganyifu, pamoja na biashara zilizo haramu. Kimsingi, wenye kuupata utajiri kwa njia hizi, sio “matajiri halisi”! Hawa ni majambazi walioupata utajiri kwa njia haramu na hivyo hatuna jema la kujifunza kutoka kwao.

Maana yangu hasa hapa nataka tufute kasumba ya kudhani kila mwenye kumiliki utajiri ni fisadi. Tukubali na kutambua kwamba wako “matajiri halisi na halali” walioupata utajiri kwa kazi ya mikono na matunda ya akili zao. Hawa ndio Biblia inawaongelea na ndio mfano ambao nataka tuwe nao wakati tukisoma mada hii.

Baada ya angalizo, sasa naomba uchambuzi wangu uanze na sababu zinazochangia “hekima ya tajiri kuheshimiwa na maneno yake kusikilizwa kuliko masikini”! Yaani nimeona tuanza na kinyume cha swali la msingi la sababu za “kudharauliwa kwa hekima ya maskini.” Maana kama “Hekima ya maskini hudharauliwa” kuna upande wa pili unaodhihirisha kwamba “hekima ya tajiri ndiyo inayoheshimiwa”!

Uchunguzi niliofanya kwa haraka, nimebaini kama sababu kuu tatu ambazo Hekima ya Tajiri huheshimiwa. Ya kwanza ni “chimbuko la utajiri halisi”; pili ni “mipango makini ya uzalishaji” na tatu ni “miiko ya kutunza utajiri unapatikana”

   1. Chimbuko la utajiri halisi ni mawazo

Hakuna utajiri unaopatikana kwa miujiza. Utajiri hupatikana kuanzia kwenye mawazo ya kiuchumi na uzalishaji. Japokuwa kila mtu anaweza kuwa na mawazo ya kiuchumi akilini, lakini si kila mtu mwenye uwezo wa kuyachuja na kuyapanga na kuyaamini kwamba yataleta matokeo kama yakitekelezwa.

Ndiyo maana tunao mabingwa wengi wa kusema habari za uchumi na uzalishaji lakini maisha yao yanategemea misaada yaw engine; wakati baadhi ya watu wasio na ujuzi wa kifalisafa wanaweza kuwaza na kutekeleza mawazo yao na yanawapatia uchumi endelevu.

Utajiri huzaliwa katika mawazo makini yaliyochujwa na kufanyiwa utafiti kabla ya kuyafanyia utekelezaji.

Angalizo: Ingawa kila tajiri humiliki mali; lakini sio kila mwenye kumiliki mali nyingi ni tajiri. Kwanini? Kwa sababu kuna wengi wanaomiliki mali kwa njia za wizi na udanganyifu; na wengine kwa njia haramu kama bandi na dawa za kulevya! Hawa wanaweza kuonekana wanamiliki mali nyingi, lakini ukweli halisi si matajiri halisi! Utajiri wao haukupatikana katika njia za asili na halali za uzalishaji mali ambazo ni fursa kwa binadamu wote. Na ndiyo, maana watu wa namna hii, huwa hawa mawazo ya maana ya kusaidia wengine kiuchumi kwa sababu hakupata mali kwa njia ya mawazo makini.

Utaniambia kwamba, hata kupata mali kwa njia haramu nayo pia ni mawazo yaliyofanyiwa kazi yakaleta matokeo! Ni kweli kwa upande wa pili, wa mawazo haramu, yaliyotumia njia haramu ili kupata mali haramu! Ndiyo maana hawa kwa msamiati sahihi ni “Matajiri haramu” na hekima yao haitabuliki katika jamii, na wakijulikana hadharani watafilisiwa kwa sababu si “matajiri halali”


   2.  Utajiri hupatikana kwa mipango makini

 Japokuwa asili ya utajiri ni mawazo, lakini mawazo pekee hayawezi kuleta utajiri mpaka yatengenezewe michanganuo makini ya miradi ya uzalishaji ambayo huwa ndio miongozo ya kuzalisha mali na kumiliki utajiri.

Kwa hiyo, mipango makini ni hatua ya kuyatafsiri mawazo kuja kwenye uwezekano wa kutekelezeka kwa vitendo. Na hapa ndipo ufundi wa hekima ya tajiri unapoanzia kumpatia heshima. Ana mipango ambayo ameibuni kutokana na mawazo na kuitekeleza na ikaleta matokeo halisi ya umilikaji mali.

Unaweza kusema kwamba, matajiri wengi wanatekeleza mipango yao kwa sababu ya kupata mikopo kutoka kwenye taasisi za fedha, vinginevyo mipango yao isingelitekelezeka. Huo ni ukweli nusu. Nusu ya ukweli iliyosalia ni kwamba, tasisi za fedha hazitoi fedha kwa kila michanganuo unaowasilishwa kwao mpaka wamethibitisha kwamba mpango husika utazalisha na kurudisha mkopo. Ni muhimu kuzingatia ukweli huu.


    3. Utajiri hudumu kwa nidhamu ya vipambele vya matumizi
Sasa tumefikia kipengele muhimu sana hapa, ambacho humpa tajiri heshima na fursa ya kusikilizwa. Nidhamu ya matumizi ya fedha na mali zake. Kuna watu wengi sana ambao hufanikiwa katika hatua mbili za mwanzoni, lakini hukwama kuingia katika orodha ya matajiri kwa sababu ya kukosa hekima ya matumizi ya fedha na mali walizozalisha kwa juhudi nyingi!
Nimebaini aina mbili za matajiri. Kuna “matajiri wa msimu” na “matajiri wa muda mrefu”. Tofauti kati yao ni nidhamu ya vipaumbele katika matumizi ya fedha na mali zao. “Matajiri wa msimu” hufanikiwa kuzalisha na kupata faida, lakini kwa sababu ya maisha ya anasa na kutoweka akiba na kupanga vipaumbele makini; hujikuta faida waliyozalisha haidumu kwa muda mrefu; na hivyo hujikuta wakianza upya mikaka ya uzalishaji.

“Matajiri wa muda mrefu” wana hekima ya “kutunza faida” au kuweka vipaumbele vya kuifanya “faida izalishe faida”nyingine! Wana nidhamu katika matumizi ya faida kwa mambo ya anasa au kwa mambo yasiyo na tija!

Ni kutokana na ukweli huu, ndiyo maana hekima ya tajiri huheshimiwa na maneno yake kusikilizwa katika jamii.

Majumuisho ya sababu za hekima ya tajiri kuheshimiwa
Tajiri anaheshimiwa na kusikilizwa kwa kuwa hekima yake imethibitika kwa vitendo. Tumeona hatua ambazo tajiri huzipitia na mchakato mzima mpaka kutambulika kuwa ni tajiri wa kuheshimika katika jamii.

Kwa hiyo, hekima ya tajiri inaheshimiwa kwa sababu ya uzoefu wake katika kuwaza, kupanga na kutekeleza mawazo yakaleta matokeo.

Jambo jingine la kuzingatia pia ni ukweli kwamba tajiri akitoa mawazo, hasa kama yanatakiwa kugharimiwa, mawazo yake yatakubaliwa upesi kwa misingi kwamba ataombwa achangie gharama za utekelezaji wa mawazo yake. Kwa hiyo, tajiri anaheshimiwa na kusikilizwa kwa sababu akitoa mawazo anao uwezo wa kugharimia mwenyewe.

Itaendelea wiki ijayo
Share on Google Plus

About Gospel Kitaa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.