NILIMUAMINI MUNGU TU, NA AKANITENDEA - MERIAM IBRAHIM

Meriam Ibrahim akiwa studio za Fox News kwenye mahojiano na Kelly (hayupo pichani) ©Fox News
Meriam Ibrahim (mwanamke aliyehukumiwa kifo kwa ajili ya kubadili dini) ameweka kumbukumbu na kubadili vichwa vya habari duniani kwa namna nyingi kutokana na hukumu iliyokuwa inamkabili, akituhumiwa kubadili dini kutoka uislamu kwenda ukristo. 

Mama huyo wa watoto wawili ambaye kwa sasa anaishi nchini Marekani, amehojiwa hivi karibuni na kituo cha runinga cha Fox News, na hapa Gospel Kitaa inakuletea kilichojiri kwa ufupi baada ya kufuatilia mahojiano hayo.

"Kipindi ambacho niko jela, nilipewa siku tatu za kubadili dini na kuwa muislamu, huku pia nikitembelewa na wanazuoni wa Kiislamu wakinukuu Quran ili niwe upande wao na kuwa huru, yaani kwamba niachane na ukristo."

Meriam anasema kwamba imani ndio maisha, na kama mtu hana imani, ina maana basi ni mfu, ndio maana yeye alishikilia imani yake hadi mwisho, akilazimika kujifungua mtoto huku akiwa amefungwa minyororo miguuni (soma hapa). hayo yote hayakumzuia kushikilia msimamo wake wa kumfuata BWANA Yesu.

"Sikuwa na makosa, sikuwa nimemkosea mtu yeyote, kosa pekee nililofanya ni kuishi vile nitakavyo, inanisikitisha kuishi nje ya nchi yangu kwa matatizo, Sudan ni nyumbani kwangu, kuna ndugu na jamaa zangu, marafiki wangu wako huko." Anaeleza Meriam kuhusu kifungo na hukumu iliyokuwa inamkabili.

"Kama wewe ni mkristo, na ukabadili dini kuwa muislamu, huwezi tena kurejea kwenye dini ya ukristo maana utahukumiwa kifo, na haya yanawatokea wanawake wengi huko Sudan, ila wanashindwa kijitangaza kuhofia usalama wao." anaongeza tena Meriam kuhusu wanawake nchini humo.

Pamoja na mateso ambayo wakristo wanakutana nayo nchini humo, pia wanawake wa jamii ya kikristo wanaoishi kwenye maisha magumu, hutakiwa kubadili dini ili serikali iweze kuwapa msaada utakaowainua kiuchumi, vinginevyo hubaki na mateso yao.

Meriam ambaye anaeleza kuwa watoto wake kwa sasa wana furaha kuwa na familia yao, wanazidi kumtegemea Mungu kwenye maisha yao, kwani amewatoa kwenye hali ya hatari, na kwamba zaidi wanahitaji maombi yako mpenzi msomaji.

Lakini katika yote, Meriam anatukumbusha kwamba imani hutuvusha kwenye hali yoyote tuliyo nayo, na nukuu yake inajieleza;

"Hali ilikuwa ngumu, lakini nilikuwa na hakika kwamba Mungu atasimama nami. Na siku nilipoachiwa huru, nilicheka, nililia, nilikuwa mtu mwenye furaha sana pale ambapo niliachiwa huru." (bofya hapa kusoma)

Kama mwanamama huyu alisimama kidete kwa imani yake akiamini itakuwa hivyo licha ya mateso ya kila aina aliyopata jela na hata kwenye jamii inayomzunguka, na akashinda. Je wewe, imani yako imesimamia wapi?

Charisma News imeandika

Share on Google Plus

About Gospel Kitaa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.