SOMO: MIAKA 1,000 YA UTAWALA WA YESU KRISTO DUNIANI NA VITA VYA GOGU NA MAGOGU

Askofu Zachary Kakobe.
Tulijifunza katika somo la “kuja kwa Yesu Kristo mara ya pili duniani na vita vya Har-magedoni”, jinsi ambavyo Yesu Kristo atakavyo kuwa mtu wa Vita au Bwana wa Vita halisi. Yesu Kristo atawaua wenye dhambi wote waliojipanga kupigana naye mahali paitwapo kwa kiebrania Har-magedoni. Wale wote watakaouawa hapa, ndege watashiba nyama zao; kisha yule Mnyama ( Mpinga Kristo ) na yule nabii wa uongo watakamatwa na kutupwa wangali hai katika ziwa la moto ( UFUNUO 19:20-21 ). Baada ya tukio hili, Shetani naye atakamatwa na kutupwa kwenye shimo refu sana na kufungiwa humo kwa miaka elfu moja. Biblia zetu za Kiswahili zinaliita shimo hili “:kuzimu”, hata hivyo ni muhimu kufahamu kwamba hapa siyo Jehanum. Kingereza linatumika neno “bottom less pit” ( UFUNUO 20:1-3 ). Baada ya kufungwa Shetani miaka elfu moja, ndipo utawala wa Yesu Kristo duniani pamoja na watakatifu wake, utakapoanza ( UFUNUO 20:4-6 ). Ni makusudi ya somo letu la leo kujifunza kwa undani juu ya Utawala huu wa Yesu Kristo miaka 1,000 duniani. Tutaligawa somo letu katika vipengele vitatu:-

( 1 ). MAKUSUDI YA UTAWALA WA YESU KRISTO MIAKA 1,000 DUNIANI.

( 2 ). HALI YA MAISHA ITAKAVYOKUWA DUNIANI WAKATI WA UTAWALA WA YESU KRISTO DUNIANI.

( 3 ). VITA VYA GOGU NA MAGOGU.

( 1 ). MAKUSUDI YA UTAWALA WA YESU KRISTO MIAKA 1,000 DUNIANI.

Mwanzoni kabisa katika mpango wa Mungu, mwanadamu alikusudiwa kuishi maisha ya amani, furaha na mafanikio, chini ya utawala wa Mungu

mwenyewe. Adamu alipotenda dhambi aliukatisha mpango huu kwa mwanadamu na akatolewa katika bustani ya Edeni. Hapo ndipo maisha magumu kwa mwanadamu yalipoanza. Ardhi ililaaniwa na tukaanza kula chakula kwa jasho, na kuishi maisha ya taabu tofauti kabisa na mpango wa Mungu kwa mwanadamuj ( MWANZO 3:16-19 ). Ndipo Mungu alipoanza mpango wa kumrudisha mwanadamu katika amani na furaha aliyomkusudia, na hatimaye akaja Yesu Kristo duniani mara ya kwanza na kufa kwa ajili ya dhambi zetu. Hata hivyo katika kukamilisha kile alichokikatisha Adamu, Mungu katika mpango wake amekusudia kuonyesha ulimwengu maisha yale aliyoyakusudia kwa wanadamu, kama wasingekubali kuuacha Utawala wake na kuugeukia utawala wa Shetani. Kwa kuwa Shetani atakuwa amefungwa miaka 1,ooo, wanadamu wataweza kutawaliwa bila kushawishiwa na Ibilisi kutenda dhambi na kuwa katika serikali moja duniani kote iliyo chini ya mtawala Yesu Kristo. Utawala huu utawaongezea majuto wanadamu wenye dhambi waliomkataa Mungu awatawale, kwa kuona wema wake.( 2 ). HALI YA MAISHA ITAKAVYOKUWA DUNIANI WAKATI WA UTAWALA WA YESU

KRISTO DUNIANI.1.KUTAKUWA NA AMANI YA AJABU DUNIANI

Hakutakuwa na vita kabisa kati ya mwanadamu na mwanadamu. Siraha zitabadilika kuwa vyombo vya amani ( ISAYA 2:4 ; MIKA 4:3; ZEKARIA 9:10 ). Juhudi za kuleta amani zimeshindikana kuletwa na umoja wa Mataifa hivi sasa. Haya yote yatatimia wakati wa Utawala wa Yesu. Katika utawala huu hakutakuwa na Mbu, Funza, Kunguni, Nzi au wadudu wowote wabaya kama bacteria n.k; Vile vile hakutakuwa na ndege wa kula nafaka wala wanyama waharibifu ( HOSEA 2:18 ). Kutakuwa na amani ya ajabu pia kati ya mnyama na mnyama. Simba atakula majani, Chui atalala pamoja na mwana Mbuzi, Simba na Ng’ombe watakuwa pamoja. Nyoka hatakuwa na madhara tena ( ISAYA 11:6-9 ). Hakutakuwa na wizi au unyang’anyi. Wakati huo hakutakuwa na haja ya kufunga milango kwa makufuli ( EZEKIELI 34:25, 28 ).

2.FURAHA ITAJAA KABISA ULIMWENGUNI

Hakuna huzuni wala masikitiko ulimwenguni ( ISAYA 9:3-4 ; YEREMIA 31:13 ).

3.UTAKATIFU KUTAWALA DUNIANI.

Kama ilivyokuwa kipindi cha waamuzi katika Agano la kale, watakatifu wanaotawala na Kristo watakuwa ni waamuzi. Watashauri watu na kuwahukumu kwa hekima kuu itakayoleta maisha ya uaminifu na yote yanayompendeza Mungu ( ISAYA 1:26 ).

4.UTUKUFU WA BWANA UTAFUNULIWA.

Kila mtakatifu atakayetawala pamoja na Yesu Kristo atakuwa katika utukufu mkubwa tofauti na wale wanaotawaliwa ( ISAYA 40:5; ISAYA 35:2; ISAYA 11:10 ).

5.UTAKUWA NI WAKATI WA FARAJA BAADA YA HASIRA.

Baada ya mapigo ya Dhiki Kuu na Vita vya Har- magedon, huu utakuwa ni wakati wa faraja baada ya hasira ( ISAYA 12:1; 54:7-10; 40:11 ).

6.UTAKUWA NI UTAWALA WA HAKI TU

( ISAYA 9:7; 11:5; YEREMIA 23:5; 33:15 ).

7.DUNIA ITAJAWA NA KUMJUA BWANA

Kila mtu atamjua Mungu-wema wake, uzuri wake, haki yake n.k. Kila mtu atamjua Yesu kuwa ni Mungu na kujawa na maarifa kamili ya mpango wake kwa wanadamu ( ISAYA 11:9; HABAKUKI 2:14 )

8.LAANA JUU YA ARDHI ITAONDOLEWA

Laana ya MWANZO 3:17-19 itaondolewa. Hakutakuwa na miiba wala magugu. Mvua itakuwa ya manyunyu safi. Ukilima kidogo, unavuna sana. Hakuna kula kwa jasho ( EZEKIELI 34:26-27 ).

9.HAKUNA KUUGUA DUNIANI

Magonjwa niya Shetani kwa kuwa Shetani amefungwa hakuna kuugua kabisa. Hospitali zitakuwa hazina kazi ( ISAYA 33:24 ).
HAKUTAKUWA NA VILEMA, VIPOFU WALA VIZIWI DUNIANI.

Kazi zote hizi zilitokana na Shetani kupewa nafasi kumtawala Adamu. Zitamalizwa katika Utawala huu ( ISAYA 29:18; 35:3-6 ).
11. KUTAKUWA HAKUNA KUFA

Watu watazaliwa tu, lakini hakuna kufa. Watu watakuwa wengi duniani ( AMOSI 9:15; ZEKARIA 14:9-11 ).
12. HAKUNA KUONEWA, NJAA, KIU WALA MATESO.

( ISAYA 49:10; 14:3-7 ). Nyakati hizo zitajaa kuimba tu! hakuna jua kali wala baridi kali.
13. DUNIA ITAPENDEZA MNO NA HAKUTAKUWA NA UMASKINI.

Kila sehemu kutakuwa na maua mazuri mno wala hakutakuwa na majangwa kabisa ( ISAYA 65:21-24; 35:1-2,7 ).

( 3 ). VITA VYA GOGU NA MAGOGU.

Mwishoni mwa miaka hii elfu, Shetani atafunguliwa kutoka kifungoni mwake na ataanza kuwadanganya wanadamu wote na kuwashawishi ili wafanye vita na Yesu na wtakatifu wake. Watu wote kwa kuwa wana asili ya dhambi watashawishika. Na waasi watajikusanya nchi ya Gogu na Magogu, iliyo kaskazini ya Parestina, Mashariki ya kati; na kuja kuishambulia maskani kuu ya Watakatifu Yerusalemu. Hapo ndipo itatokea vita ya Gogu na Magogu. Hasira ya Mungu itawaka na wanadamu wote wataangamizwa kwa kuliwa na moto utakaoshuka kutoka mbinguni. Watasalia watakatifu tu walio pamija na Yesu. Shetani naye atakamatwa na kutupwa katika ziwa la moto ( UFUNUO 20:7-10 ). Wale wote walioliwa kwa moto, watakuwa wote Jehanum ya moto kusubiri ufufuo wa pili, au ufufuo wa hukumu

. .. .. .. .. .. .. .. .. .. .. .. .. .. .. .. .. .. .. .. .. .. .. .. .. .. .. .. .. .. ..

Mpendwa msomaji, baada ya kusikia yote haya kutoka kwa nabii aliyetumwa kukuletea ujumbe huu, usifanye moyo wako kuwa mgumu. Hii ni nafasi ya kipekee ya kuokoka. Je, unajuaje kama utaamka kitandani baada ya kulala usiku wa leo? Wakati uliokubalika wa wokovu ni sasa (2 WAKORINTHO 6:2). Labda utaniuliza, ili uokoke, ufanyeje? Jibu ni rahisi, kwa imani ukitubu dhambi zako kwa kumaanisha kuziacha, na kumwambia Yesu Kristo akusamehe, utasamehewa sasa hivi, na msamaha wa dhambi, huambatana na wokovu (LUKA 1:77). Je, uko tayari kuokoka sasa hivi? Najua uko tayari. Basi fuatisha sala hii kwa dhati toka moyoni, “Mungu baba asante kwa kuniletea ujumbe huu.Natubu dhambi zangu zote, kwa kumaanisha kuziacha. Yesu Kristo nakuomba unisamehe dhambi zangu na kunipa uwezo wa kushinda dhambi na kuniokoa kutoka katika mateso ya moto wa milele. Asante, kwa kuniokoa katika Jina la Yesu. Amen”. Tayari sasa umeokoka, na kwa hakika unakwenda mbinguni sasa, hata ukifa leo. Ili uzidi kuukulia wokovu, hakikisha unahudhuria mafundisho katika Kanisa linalohubiri wokovu. MUNGU AKUBARIKI !!!

Neno la Uzima kutoka kwa  Askofu Zachary Kakobe        
Tovuti       : www.bishopzacharykakobe.org

Share on Google Plus

About Ambwene Mwamwaja

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.