HOJA: HEKIMA YA MASKINI HUDHARAULIWA (4)

Katika toleo lililopita (soma hapa) tulichambua habari za “Umaskini wa kipato na utajiri ni matokeo” na tukaishia kwenye kipengele cha “utata wa mikopo na madeni”. Leo hii tunahitimisha mada hii kwa kuzingatia kwamba hata kama hekima ya maskini hudharauliwa bado ni bora kuliko utajiri; na jinsi inavyohitajika wakati huu kuiokoka Tanzania:

Hata kama hekima ya maskini
hudharauliwa bado ni bora kuliko utajiri
Askofu Sylvester Gamanywa


Baada ya kupitia uchambuzi kuhusu nafasi ya maskini mwenye hekima katika jamii; na nafasi ya tajiri katika jamii; tunaweza kuhitimisha kwamba; hata kama “hekima ya maskini hudharauliwa” bado hekima yake ni “bora kuliko utajiri”!

Haya si maneno yangu binafsi bali yamesemwa na mwandishi wa vitabu vya hekima katika Biblia ambaye alitokea kuwa tajiri mkubwa kuliko matajiri wote katika ulimwengu wa enzi zake. Naye si mwngine bali ni mfalme Sulemani aliyefanya utafiti na kugundua uzito wa hekima ukilinganisha na utajiri:

“Maana hekima ni bora kuliko marijani, wala vyote vinavyotamanika havilingani nayo.” (Mith.8:11)
Neno marijani limetafsiriwa kwa Biblia ya Kingereza cha Amplified kama vito vya thamani yaani (rubies or pearls)

Itakumbukwa kwamba, Sulemani wakati wa ujana wake kabla hajawa mfalme aliulizwa na Mungu aombe chochote anachotaka, yeye akaomba hekima na maarifa ili vimsaidie kuhukumu maelfu ya wana wa Israeli. Bila shaka aliona jinsi baba yake Daudi allivyotawala kwa mabavu na vita ya kumwaga damu nyingi, akaona yeye aombe hekima ya Mungu ili imsaidie aweze kuhukumu kwa hekima badala ya mabavu.

Mungu alimjalia Sulemani hekima kuliko wafalme wote na akajipatia umaarufu wa kimataifa kwa jinsi alivyokuwa na hekima ya kuamua mambo. Ndiyo maana alikuwa na uzoefu wa kuandika kuhusu uzito na ubora wa hekima ukilinganisha na mali ya madini ya dhahabu na fedha: “Si afadhali kiupata hekima kuliko dhahabu? Naam yafaa kuchagua ufahamu kuliko fedha.” (Mith.16:16)

Kufuatia ubora wa hekima kuwa uko juu kuliko utajiri; ndiyo maana nahamasisha kwa kusema kwamba, hekima ya maskini hata kama itadharauliwa kwa sababu ya umaskini wake; bado ndiyo itakayoweza kuokoa nchi kutoka kwenye majanga yanayotishia kuiangamiza. Tukikumbuka maandiko ya msingi wa mada hii kwamba, “Hekima ya maskini” iliwahi kuokoa mji uliokuwa umezungukwa ili uharibiwe na majeshi ya maadui.

Sio siri kwamba, nchi yetu, mahali ilipofikia nayo imezungukwa na maadui wa amani na utulivu na wamejizatiti kuiangamiza bila huruma. Kwa bahati mbaya wale waitwao matajiri wa duniani hii, hawana hekima ya kuinusuru nchi hii, na badala yake wao ndio wanaongoza katika kuvutia maadui waliopania kuiharibu nchi.

Napenda kutumia fursa hii, kuitimisha “hekima za maskini” mahali popote walipo tukusanyike kwa pamoja na “kuunganisha hekima” kwa ajili ya kuinusuru nchi. Najua hata baada ya kuinusuru nchi huko mbele ya safari huenda historia ikajirudia ambapo “maskini walionusuru nchi hawatakumbukwa tena!” Lakini ni heri 100% kusahauliwa baada ya kuokoa nchi! Mungu hatawasahau maskini waliokubali kupokea hekima ya Mungu na kuokoa nchi.

Hekima ni tunda la uchaji Mungu, na
uchaji Mungu” una “kinga” kuliko mali

Ni ajabu lakini kweli kwamba, hekima yenye thamani kuliko utajiri “haipatikani kwa mali” bali ni “karama kutoka kwa Mungu” mwenyewe. Na kigezo cha kuipata hekima hii ni “kumcha Mungu” ambako nako hakuhusiani na utajiri:

“Kumcha BWANA ndio mwanzo wa hekima, wote wafanyao hayo wana akili njema, sifa zake zakaa milele.” (ZAB.111:10)

Kuna msemo ya wajasiriamali usemayo ati “pesa huzaa pesa”! Maana yake kama ukitaka kupata fedha lazima uwe na fedha ya kuwekeza katika vitegauchumi upate kuzalisha na kuongeza mapato mengi zaidi. Hii ni kanuni ya kibiashara. Lakini “ukitaka kupata hekima au kuongeza kiwango cha hekima zaidi, kanuni yake ni kuongeza viwango vya uchaji Mungu kwa sababu yeye ndiye mwenye mamlaka ya kuachilia hekima hiyo kwa ajili ya wale wamchao kwa mioyo ya dhati.

Dalili za kupungukiwa na hekima:

“Lakini mtu wa kwenu akipungukiwa na hekima, na aombe dua kwa Mungu, awapaye wote kwa ukarimu, wala hakemei; naye atapewa.” Yak.1:5)

Unaona? Hekima hupatika kwa Mungu kwa dua na sio kwa hongo wala rushwa kama ilivyo katika kutafuta utajiri. Na tumesoma kwamba, Mungu hana uchoyo wa kutoa hekima kwa kila aombaye ana fursa ya kusikilizwa na kupokea hekima.

1. Ukosefu wa Ubunifu katika ufumbuzi wa matatizo sugu

Tanzania imekuwa inakabiliwa na matatizo sugu ya kiuchumi, huduma duni za elimu na afya. Ukifanya tathmini yenye kuzingatia kanuni za hekima, utaona waziwazi kwamba usugu wa matatizo haya hautokani na ukosefu wa fedha au rasirimali za asili. Kilichokosekana ni “hekima ya maamuzi” katika kuweka vipaumbele vya maendeleo. Changamoto kubwa kuhusu ukosefu wa hekima ni kwamba waliotakiwa kuwa nayo hawajui kwamba hawana!

Ingekuwa heri kama wahusika katika kufanya maamuzi ya hekima wangelikuwa wanajua kwamba, wanahitaji hekima ya Mungu katika utendaji wao ili iwaongoze katika kufanya maamuzi. Ndiyo maana hata maamuzi yasiyo na hekima yanapofanyika, wenye kuamua hawajui kwamba wameamua pasipo hekima!

Ndiyo maana utashangaa kuona kwamba yanafanyika maamuzi ambayo matokeo yake yanaonekana kwamba hayana tija, bado wahusika wanang’ang’ania kwa nguvu kuyasimamia. Na hata yasipoleta matokeo kama yalivyoamuliwa bado wahusika hawataona kwamba waliamua pasipo hekima ndiyo maana hawakufanikiwa!

Kwa hiyo,mtu anayetambua kwamba amepungukiwa na hekima, hiyo nayo ni hekima ya aina yake. Na kwa vyovyote lazima atakuwa ni mchaji Mungu na uhusiano wake na Mungu unamsaidia kuona upungufu wa hekima ya Mungu katika maamuzi mbali mbali. Huyu ndiye maandiko yanamhimiza kwamba, akigundua kuwa “…amepungukiwa na hekima na aombe dua kwa Mungu…”

2. Ukosefu wa ushawishi wa kupatanisha mahasimu

Sio siri kwamba nchi yetu sasa imezalisha makundi yenye kugombana na kukataa kusemezana kwa sababu tu ya kutofautiana itikadi na mahasimu hawako radhi kulegeza misimamo yao ili kusikilizana. Na uzoefu unaonesha kwamba, pande husika zinaposhindwa kupatana maana yake, amekosekana “mtu mwenye hekima” kati yao mwenye kauli yenye ushawishi wa kusilikizwa na kupatanisha mahasimu!

Hali hii ikiachwa iendelee pasipo kuchukua hatua za kuzuia madhara yawezayo kutokana na misimamo isiyotafuta suluhu; kuna hatari nchi ikaingia katika machafuko na mauaji ya kimbari, na hasa pale ambapo kichocheo kikubwa kinagusa imani za kidini.

Kwa kuwa Tanzania sasa tumefikia mahali hapa, hii ndiyo dalili nyingine kwamba “tumepungukiwa na hekima ya Mungu” na hivyo ni lazima tutii wito wa maandiko tuombe dua kwa Mungu mwenye kutoa hekima kama zawadi.


3. Mamlaka yenye kufuatwa kwa utashi wa hiari

Mwanafalisafa ya nadharia za uongozi aliwahi kusema: “everything raise and fall under leadership” yaani kila jambo husimama au kuanguka kwa kutegemea uongozi. Uongozi ndio wenye kufanya maamuzi naa kuweka vipaumbele na kushirikisha watekelezaji. Ili kufanikisha mchakato huu, lazima uongozi uwe umejaa hekima ya Mungu ambayo ina ushawishi wa kufuatwa na wafuasi kwa hiari zao wenyewe.

Iwapo uongozi utapungukiwa na hekima ya Mungu wakati wa maamuzi makini, wafuasi waliotarajiwa kupokea na kutekeleza hawataweza kujitoa kwa hiari kwa sababu maamuzi yenyewe hayatekelezeki. Ikiwa uongozi utaamua kushinikiza au kulazimisha maamuzi yake yatekelezwe kwa lazima, hapo ndipo huzaliwa hisia na mitazamo hasi ya kuasi mamlaka. Nchi ikifika mahali hapo, tayari mamlaka iliyopo inakuwa imepoteza ushawishi wa kufuatwa kwa hiari. Matokeo ndiyo tunayashuhudia katika nchi nyingi za kiafrika, uarabuni na Asia kwa jumla.

HITIMISHO

Hekima ya maskini hudharauliwa na maneno yake hayasikilizwi. Lakini hekima yenyewe ina nguvu na uwezo wa kuzuia majanga yanayoikabili nchi kama watakuwepo watu wenye hekima hiyo. Mali na fedha haviwezi kuleta hekima hata kama fedha hizo zitatumika sana katika kusuluhisha mahasimu. Hekima yenye uguvu za kuzuia majanga na mabalaa hupatikana kwa Mungu kwa wahusika wanapoamua kumcha Mungu na kumtafuta kwa dua zilizojaa unyenyekevu. Tanzania sasa imefikia mahali ambapo ni “hekima ya Mungu” peke yake.

Mwisho
Share on Google Plus

About Gospel Kitaa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.