HOJA: HALI HALISI YA MKENGEUKO WA MAADILI KATIKA JAMII

Tunapoitazama jamii yetu hivi sasa kwa jicho la maadili, tutakubaliana kwamba, tuko katika hali ya kuchanganyikiwa kimaadili, na hata pengine twaweza kusema kwamba hata maana ya msamiati wa maadili nayo imebadilika kabisa. Katika makala zangu za miaka ya nyuma niliwahi kuandika makala kuhusu mkengeuko wa maadili na kuandika kitabu cha “Maadili kwa kizazi kipya”. Wakati ule hali iliyovyukuwa kimaadili palikuwepo na uhai kidogo wa utambuzi wa maadili. Hivi leo hata utambuzi wa uwepo wa maadili umezimika katika jamii! Kupitia makala hii nakuletea maana ya misamiati ya maneno mawili ambao ni “maadili” na pili “Mkengeuko”:


Tafsiri ya msamiati wa neno “Maadili” na aina zake

  1. Tafsiri ya Kiswahili Sanifu
Askofu Sylvester Gamanywa
Tafsiri ya Kamusi ya Kiswahili Sanifu imelitafsiri neno maadili kuwa ni: 1 mwenendo mwema 2. Onyo au mafundisho yatolewayo kwa njia ya hadhiti au shairi na yenye nia ya kufundisha; mafundisho mazuri. Hata hivyo, tafsiri hii haitoi picha kamili ya neno maadili kwa asili yake, na hivyo wengi ndio maana kwa kutokujua maana halisi hata matumizi yake yamekuwa hafifu.

  1. Tafsiri ya kifalsafa kuhusu maadili
Katika kutoa picha ambayo ni pana zaidi, napenda kuyajengea hoja maadili kuwa yamegawanyika katika sehemu kuu mbili. Aina ya kwanza ni maadili ya kiimani (morals of faith) Kimsingi, haya ni maadili ya utambuzi wa kupambanua mema na mabaya na kutenda mema na kuacha mabaya. Maadili ya imani hujengwa kwenye misingi ya sheria na amri za Mwenyezi Mungu. Lengo kuu la ‘Maadili ya kiimani’ ni kumjengea mhusika ‘hofu ya moyoni’ ambayo humwezesha kujizuia kufanya mambo yaliyo kinyume na mapenzi ya Mwenyezi Mungu.
 
Aina ya pili ya maadili ni ya maadili ya kitaaluma (professional ethics). Haya ni maadili yaliyojengwa juu ya misingi ya miiko ya kitaaluma katika kila taaluma husika. Kila taaluma inayo maadili yake yenye kulinda viwango vya ubora. Taaluma kama udaktari, uhandisi, ualimu, sheria, uhasibu, uongozi na utawala zote zinayo maadili yake ambayo wanataaluma hujifunza ili yawaongoze katika kulinda miiko na viwango vya nidhamu na ubora wa kitaaluma.

Tafsiri ya msamiati wa “mkengeuko”

Asili ya matumizi ya neno ‘mkengeuko’. Kwa lugha ya Kingreza ni Depravity likiwa na maana ya hali ya kutoka katika uadilifu asilia (a departure from a state of original integrity). Maneno mengine yanayotafsiri mkengeuko ni : upotovu, uharibifu wa tabia.

Mkengeuko wa maadili (Moral depravity) ni uharibifu wa tabia ndani ya moyo wa mtu ambapo hutumia hiari au utashi wake kukiuka sheria ya maadili (violation of moral law) ambayo hudai uwajibikaji wa kimaadili.

Kidini, mkengeuko wa maadili unajulikana kama uasi dhidi ya sheria za Mungu. Katika eneo la utashi ndani ya moyo, mtu huamua kuasi kwa kufanya mapenzi yake binafsi yatakayokidhi tamaa zake binafsi. Twaweza kusema kwamba uasi wa jinsi hii ni ‘ubinafsi ulikokithiri’!

Tunaposema juu ya kuwepo kwa mkengeuko wa maadili, maana yake ni ‘kutoweka kwa hofu ya Mungu katika mioyo ya watu’. Matokeo ya kutoweka kwa hofu ya Mungu mioyoni mwa watu ni ‘kuondokewa na woga wa kufanya maovu’. Hii ni tabia inayodhihirisha hali ya uasi na kupuuza hukumu ya adhabu ya Mwenyezi Mungu dhidi ya watenda maovu.

Baada ya kutoweka kwa hofu ya Mungu ndani ya moyo wa mhusika, kinachofuatia ni ‘kushuka kwa viwango vya heshima na mwenendo mwema’. Mtu huacha kujiheshimu na kuanza kusema au kutenda mambo ya aibu, yasiyo ya staha.

Kwa kuwa maadili ya kiimani hujengwa ndani ya moyo wa mtu binafsi; mkengeuko wake nao pia huanza ndani ya moyo wa mtu binafsi. Kwa kadri mtu aliyekengeuka kimaadili anapoendelea kuishi katika jamii, huanza ushawishi wa kuwafanya walio karibu naye nao kuiga mfano wake. Hali hii hutokea katika familia, ambapo mzazi asiye na maadili ya kiimani humwambukiza mtoto wake.

Mkengeuko wa ‘maadili ya kiimani’ ndilo chimbuko la mkengeuko wa ‘maadili ya kitaaluma’. Maadili ya kitaaluma hujengwa juu ya uaminifu na uadilifu. Uaminifu na uadilifu hujengwa katika misingi ya kuzingatia miiko ya kitaaluma. Mkengeuko wa maadili ya kitaaluma ni ‘hali ya kutoweka kwa uaminifu na uadilifu’ unaofuatiwa na ‘kuvunja miiko’ ya kitaaluma.

Vigezo vya utambuzi wa chimbuko la maadili

  1. Vituo vya mawasiliano ya binadamu 

    Binadamu tofauti na viumbe wengine aliumbwa ili awe mtawala wa mazingira na viumbe vingine. Katika kutimiza wajibu wake binadamu amepewa aina kuu mbili za uwezo. Uweza wa mawasiliano na uweza wa mahusiano. Mawasiliano na mahusiano ni vitu vinavyomtambulisha binadamu kuwa ni kiumbe tofauti na viumbe wengine wote.

Katika eneo la mawasiliano, binadamu ameumbiwa vituo maalum vya kufanya mawasiliano ambavyo ni: kituo cha akili na kituo cha moyo. Kituo cha akili humwezesha binadamu kufanya mawasiliano na ulimwengu wa asili, wakati ambapo kituo cha moyo humwezesha kufanya mawasiliano na ulimwengu usioonekana, maarufu kwa jina la ulimwengu wa roho.

Vituo hivi viwili, kila kimoja kinayo mambo manne yanayokiwezesha kufanya kazi zake kwa ufanisi. Kituo cha akili kimeumbiwa mambo manne yafuatayo: i) Fikira (thought) ii) ubunifu (imagination) iii) kumbukumbu (memory) na iv) kujitambua (consciousness).

Mambo manne yaliyomo katika kituo cha moyo ni: i) utashi(free-will) hisia (emotions) iii) Dhamiri (conscience) na iv) utambuzi wa rohoni(intuition)


  1. Uchambuzi kuhusu yaliyomo katika kituo cha akili
Tafsiri ya fikira maana yake ni mchakato ambamo akili inapokea mawazo, kuyachambua, kuyapanga hadi kutengeza kitu cha kufanyia maamuzi. Fikira ni wazo lililotengenezwa katika ‘kituo cha akili’ tayari kwa matumizi.

Tafsiri ya neno Ubunifu (imagination) maana yake ni uwezo wa kutengeneza wazo jipya kwa ajili ya kufanya maamuzi mapya ili kupata ufumbuzi mpya. Maana ya kumbukumbu (Memory) ni eneo la akili lenye kutunza, kuhifadhi taarifa na kuzikumbuka kila zinapohitajika. Kujitambua (Consciousness) maana yake ni pale akili zinapojitambua na kujijua kuwa ni nafsi.


  1. Uchambuzi kuhusu yaliyomo katika kituo cha moyo
Utashi (free-will) maana yake ni uwezo wa kufanya uamuzi wa hiari katika kuchagua kufanya au kutokufanya jambo. Wakati Mwenyezi Mungu alipotangaza kumfanya binadamu alimkusudia awe na mamlaka ya utawala. Mamlaka ya utawala inahitaji uhuru na uwezo wa kufanya maamuzi. Ili kufanya maamuzi lazima yawepo mazingira ya uhuru wa kuwaza, kupambanua, na utashi wa kumua; kuridhia maamuzi yatakayofanywa; lakini pia kuwa tayari kuwajibika kwa ajili ya matokeo ya maamuzi yaliyofanywa.

Hisia (emotions) ni mihemuko, hisia kubwa, jazba, mishtuko, michomo ya moyo. Kazi ya hisia ni kuitikia mambo mbali mbali ambayo binadamu anakutana nayo katika maisha. Hisia ni mwitikio wa mambo yanayodhihirika katika maisha ya binadamu yawe mema au mabaya. Kimsingi, kuna aina kuu mbili za hisia. Kuna hisia chanya na hisia hasi. Hisia chanya ni upendo, amani, furaha, huruma, tumaini, Hisia hasi ni pamoja na chuki, hasira, ghadhabu, uchungu, wivu, kukata tamaa, wasiwasi, hofu, mashaka, kuvunjika moyo nk.

Dhamiri (conscience), imefananishwa na vitu kama chombo cha kugundua vitu vilivyo ndani/chini ya maji kwa mawimbi ya sauti (sonar); au gurudumu tuzi (gyroscope); au chombo kinachotumia na marubani kuangalia vitu kwenye skrini vile vilivyo karibu (radar). Vyote hivi ni vifaa vya kutoa taarifa za mara kwa mara (continuous feedback).

Hali kadhalika na dhamiri pia ni chombo cha kiroho ambacho kazi yake ni kutoa taarifa za mara kwa mara kuhusiana na tabia na mienendo yetu. Huu ni uwezo ndani ya nafsi unaomwezesha binadamu kupambanua kati ya mema na mabaya (good and evil), na kati ya yaliyo sahihi na yasiyo sahihi (wrong and wright).

Dhamiri ni kitivo cha ufahamu na hisia asilia ya kupambanua mema na mabaya, ambayo hutumika kutoa hukumu ya kimaadili na mwenendo wa mtu.

Sehemu ya Utambuzi wa rohoni (intuition) kazi yake ni kutoa maongozi ya kiroho ambayo chanzo chake hakitokani na kumbukumbu ya akili. Mahali pengine imeitwa ‘sauti ndogo ya utulivu’ ambayo husema na mtu ndani ya moyo mhusika. Kamusi ya Kingereza ya Webster’s Unabridged Dictionary imelitafsiri neno intuition kuwa ni: “the immediate knowing or learning of something without the conscious use of reasoning; instantaneous apperception.

Itaendelea wiki ijayo

Share on Google Plus

About Gospel Kitaa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.