HOJA: HEKIMA YA MASKINI HUDHARAULIWA (3)

Katika toleo lililopita (soma hapa) tulichambua habari za “hekima ya masikini yenyewe sio maskini”, na kisha tukagusia kuhusu “maskini walivyo soko la matajiri” na tuliishia kwenye kipengele cha “ushiriki wa baadhi ya matajiri wanavyodidimiza uchumi wa maskini.”

Umaskini wa kipato na utajiri ni matokeo

Askofu Sylvester Gamanywa
Najua kwamba iko nadharia nadharia kongwe inayoamini kwamba, utajiri ni “uteule” kutoka kwa Mungu; na “umaskini wa kipato” “ ati ni “chaguo” na mapenzi ya Mungu! Tafadhali zingatia kwa makini maneno niliyoyawekea alama za masikio. Madai kwamba utajiri ni “uteule” wa Mungu. Kwa tafsiri kwamba kila tajiri ameumbiwa uwezo wa kutajirika. Na umaskini wa kipato ni “chaguo” la Mungu kwa tafisiri kwamba, kuna watu ambao wamenyimwa kwa makusudi uwezo wa kutajirika.

Ni kweli kwamba, Mungu ndiye anayetoa “uwezo wa kupata utajiri” kama alivyosema mwenyewe: “Bali utamkumbuka BWANA, Mungu wako, maana ndiye akupaye nguvu za kupata utajiri; ili alifanye imara agano lake alilowapa baba zako, kama hivi leo. (KUM. 8:18) Kwa hapa Muktadha wa maandiko haya, hauwalengi baadhi ya watu bali ni kwa kila mtu aliyeko katika Agano la Mungu!

Pia ni kweli kwamba Mungu anatambua “uwepo wa umasikini wa kipato” kama ilivyoandikwa: “Kwa maana siku zote mnao maskini pamoja nanyi; lakini mimi hamnami siku zote.” (MT. 26:11) Kwa hapa Muktadha wa maandiko haya, hauwalengi aina ya watu maskini wa kipato, bali “walemavu wa viungo” au “wasiojiweza”!

Kwa mantiki hii, na muktadha wa maandiko tuliyonukuu, tumejifunza kwamba sio Mungu mwenye kuamua kuwashushia huyu “uwezo wa utajiri” na huyu “uwezo wa ufukara”! Nilitaka tuwe makini sana katika eneo hili kwa sababu hizi ngome za nadharia zenye kupotosha fikira za wengi!

Haya tukirejea kwa hoja ya msingi hapa ni kutaka kujua Mungu anahusika vipi katika hizi pande mbili? Kwa matajiri na maskini wa kipato? Mungu mwenyewe ana sehemu gani na kwa kiwango gani kwa kila upande?

Tuamini au tusiamini, tukubali au tusikubali, ukweli unabaki pale pale kwamba, Mungu hana upendeleo wa kimaumbile kwa binadamu. Umaskini wa kipato au utajiri ni matokeo ya maamuzi binafsi ya pande husika. Ukija upande wa Mungu utakuwa ameweka vigezo sawa ambavyo vikizingatiwa na kila mtu atafanikiwa kiuchumi. Na visipozingatiwa matokeo yake ni umaskini wa kipato.

Kwa maelezo mengine ni uamuzi na uchaguzi binafsi wa kila mtu, na Mungu hahusiki na maamuzi hayo, hata kama anakubaliana na matokeo ya pande zote! Hebu nikukumbushe baadhi ya vigezo sawa alivyoweka Mungu kwa kila mtu kufanikiwa au kutokufanikiwa kiuchumi:

“Nikarudi, na kuona chini ya jua, ya kwamba si wenye mbio washindao katika michezo, wala si walio hodari washindao vitani, wala si wenye hekima wapatao chakula, wala si watu wa ufahamu wapatao mali, wala wenye ustadi wapatao upendeleo; lakini wakati na bahati huwapata wote.” (MHU. 9:11)

Kutokana na maandiko haya hapa juu, tunasoma kipengele kimoja muhimu kinachosema: “…lakini wakati na bahati huwapata wote..”! Neno bahati hapa lina maana ya “fursa”! wakati lina maana ya majira au msimu. Muktadha wa maneno haya ni sawa na kusema kwamba: Mungu ametoa fursa na msimu wa mafanikio kwa wote!! Binadamu wote tumepewa saa 24. Msimu wa kupanda na kuvuna kwa ajili ya wote waliowekeza!

Hakuna maskini wa kipato atakayemwendea Mungu na kumlalamikia kwamba yeye alipewa siku zenye saa pungufu. Muda ule ule unatumika kwa wote tajiri na maskini wa kipato. Fursa hali kadhalika. Fursa, hapa ina maana milango ya kufanikiwa njia za kufanikiwa huwa Mungu anaziachilia kwa kila mtu katika maisha yake hapa duniani. Changamoto ni kwa binadamu anavyoitikia katika maamuzi na matumizi ya fursa na muda ulioko mbele zake!

Kana kwamba hii haitoshi, bado Mungu anamtakia kila mtu duniani, apate kufurahia matunda ya kazi yake kwa kadiri ya kutenda kwake: Tena ni karama ya Mungu kila mtu apate kula na kunywa, na kujiburudisha kwa mema katika kazi yake yote. (MHU. 3:13)

Utata wa mikopo na madeni

Kumekuwepo mijadala yenye utata kuhusu suala zima la mikopo na madeni ya kifedha, na misimamo tofauti kuhusu habari za “mikopo ya kibenki” na “mikopo ya misaada”!

Ninafahamu kuwepo kwa nadharia tofauti kuhusu suala zima la waamini kuchukua au kutokuchukua mikopo ya kibiashara kwenye benki. Wako wasioamini katika kukopa benki na kulipa riba yake. Wako wenye kuamini na kukopa. Kila upande una mistari yake ya kibiblia ambayo unasimamia. Si nia yangu kuingia huko na kuichambua mitazamo ya jinsi ili nisitoke nje ya mada. Baadhi ya maandiko yanayotumiwa kujenga misimamo ni pamoja na haya:

“Na mkiwakopesha watu huku mkitumaini kupata kitu kwao, maonyesha fadhili gani? Hata wenye dhambi huwakopesha wenyedhambi, ili warudishiwe vile vile. Bali wapendeni adui zenu, tendeni mema, na kukopesha msitumaini kupata malipo, na thawabu yenu itakuwa nyingi; nanyi mtakuwa wana wa Aliye juu…..” (Luk.6:34-35)

Nia yangu hapa kwanza nataka kubainisha kuwepo kwa tofauti kati ya ya “kukopa kwa ajili ya mradi wa biashara” ili upanue mtaji wako na una uhakika kwamba utarejesha mkopo huo pamoja na riba; na “kukopa kutokana na kubanwa na shida binafsi” ambayo huna fedha ya kugharimia ufumbuzi wake kisha unaamua kwenda kwa jamaa, marafiki ili kukopa kama msaada wa kutatua shida hiyo binafsi.

Kwa habari ya mikopo ya kibiashara” yenyewe ina kanuni na masharti yake ambayo pande zote mbili zinakubaliana kufanya biashara pamoja ili kila upande ufaidike kiuchumi. Lakini tunapokuja kwenye suala la “kibano cha shida binafsi” ambayo mkopo unaoomba sio kwa ajili ya kuzalisha bali ni kutumia kutatua shida. Hapa ndipo umakini unahitajika sana, na pande mbili zinapojadili ajenda hii, ili mitazamo na matarajio vianishwe mapema. Yasifanyike makubaliano ya haraka na dharura wakati hakuna mikakati thabiti na makini ya kurudisha mkopo ambao fedha zake hazielekezwi katika kuzalisha chochote.

Kibiblia, mikopo ya jinsi hii ndiyo iliyowekewa masharti magumu na Mungu ili kuhakikisha utu wa mtu unapewa kipaumbele hasa unapofika wakati wa “kukaza hukumu” yaani kumchukulia hatua mdeni aliyeshindwa kulipa mkopo aliahidi ataulipa kwa muda muafaka. Kwa jamii ya waaminio tumekatazwa kukopesha ndugu ambaye ni muhitaji na hana uwezo wa kutatua shida iliyomkabili.

Katika mazingira kama haya, ninashauri kwamba, mwenye kukopesha lazima atoe fedha yake huku akiwa na matarajio ya aina tofauti tofauti; kulipwa au kuchelewa kulipwa au kutokulipwa kabisa! Na hasa anapojua kwamba mwenye kukopa, anatumia lugha ya mkopo ili asaidiwe lakini, kiukweli mkopaji ni maskini hana kipato cha uhakika cha kurudisha mkopo aliochukua. Mwenye kukopesha anapokuwa amejiandaa kisaikolojia, kuwa tayari kukubaliana na matokeo, basi kunakuwepo amani pande zote wakati wote.

Share on Google Plus

About Gospel Kitaa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.