KWA TAARIFA YAKO: KUTOKA UVUTA BANGI HADI INJILI KWA UIMBAJI

Haya msomaji wetu wa Gospel Kitaa katibu katika kipengele chetu maalumu cha "KWA TAARIFA YAKO" ambacho kinakujia kila siku za alhamisi ndani ya GK kikiwa na lengo la kukupatia habari ambayo iliwahi kutukia lakini yawezekana huijui, ama yawezekana pia unaijua lakini GK ikawa imesahau au kuna sehemu haina usahihi utapata fursa ya kusahihisha kwa kuandika maoni yako chini kabisa kwenye habari husika. Karibu

Kila mmoja wetu ana namna alivyokutana na Yesu, na historia hiyo ina msisimuko wa aina tofauti maishani. Tukitazama kwa upande wa muimbaji Sechaba Pali kutoka Afrika Kusini, naye ana historia ya kipekee kutoka kuwa mbakaji na mvuta bangi hadichombo cha kueneza injili kwa njia ya uimbaji.Sechaba Pali ©Music Industry Online
Sechaba, mzawa wa bondeni amekuwa na mguso wa kipekee pale anapoimba. Zamani anaeleza kwamba alikuwa muimbaji wa nyimbo za injili, lakini sasa ni muabudu. Kutofautisha hilo KWA TAARIFA YAKO ni kwamba pamoja na kuwa muimbaji wa nyimbo za injili, alikuwa akivuta bangi kwa kwenda mbele.

Licha ya kukulia kwenye nyumba yenye kuamini katika injili, na kulazimishwa na baba yake kupiga kinanda na kuimba kanisani, alikuwa akiendelea na bangi yake kama kawaida kila mara anapopata fursa.

Kwa utukutu wake akiwa mdogo, alifeli mara mbili darasa la sita na hivyo kufukuzwa shule, hatua ambayo KWA TAARIFA YAKO ilifanya asiendelee zaidi kutokana na wazazi wake kukosa fedha ya kumuenndeleza kwenye shule nyingine.

Sechaba ambaye hadi sasa amejinywakulia tuzo kadhaa ikiwemo ya South African Music Awards, kwa kipindi hicho alikuwa anafahamika maeneo ya nyumbani kwa sauti yake murua na kwa kuimba kwake kwenye kwaya kanisani. Baada ya kushindwa shule aliamua kwenda jijini Johannesburg kwa ajili ya kutafuta maisha (kama ambavyo aliaga), lakini KWA TAARIFA YAKO kilichompeleka huko ni kutafuta pesa za malezi kwa ajili ya binti ambaye alimpa ujauzito.

Akiwa Jo'burg, hakuwa na malazi, hivyo ikamlazimu kujiunga na kundi la watoto wa mtaani, mfumo ambao aliishi kwa muda wa miaka 2 na nusu. Na kutokana na maisha yalivyokuwa magumu na kupigwa na baridi usiku, hakuwa anapata usingizi jua linapozama - tofauti na wenzake ambao walikuwa wakilala 'unono'. Katika kuwauliza kulikoni, basi hapo ndipo KWA TAARIFA YAKO ikawa mwanzo wa kutambulishwa bangi.

Kwa kuanza kutumia bangi, ndipo hapo anakiri kuwa usingizi ulianza kupatikana, lakini kama msemo wa mtaani usemavyo, "bangi nibangue..." alikuwa akianza kuimba kila mara akivuta bangi, na wenzake kuungana naye katika 'mapambio ya bangi'.

Juhudi za kusaka pesa zikiendelea, alianza kupata umaarufu kwenye parking mojawapo ya taxi, ambapo kila alipokuwa anaosha magari alikuwa akiimba na kusikilizwa na wateja wake. Haikuishia hapo tu, kwani kwenye kibanda kimojawapo cha 'mama n'tilie' alipewa fursa ya kula bure iwapo tu atakuwa anaimba, na KWA TAARIFA YAKO hilo kwake likawa jepesi mno, na akafurahia kuimba.

Mtazame Sechaba kwa pamoja na Joyous akiimba wimbo wa Eloyi.


Harakati za kusaka maisha bora ziliendelea hadi hapo alipokuwa anafanya kazi ya usafi sehemu iliyoitwa Downtown Music Warehouse, ambapo pia alikuwa akijihifadhi hapo hadi alipopandishwa cheo na kuwa mpishi kwa ajili ya waimbaji wanaofanya mazoezi hapo.

Siku ya siku wakati anapeleka chakula kwa wanaofanya mazoezi, (siku hiyo wakiwa Joyous Celebration), alisikia mtu mmoja akiimba wimbo ambao binafsi anaupenda sana, lakini kilichomchukiza ni kwamba aliyekuwa anaimba hakuutendea haki, KWA TAARIFA YAKO Sechaba aliomba nafasi ajaribu kuimba, akanyimwa akiambiwa kwamba kazi yake ni kugawa chakula na si vinginevyo.

Jamaa aliondoka kwa unyonge huku akiwa anajisikia vibaya mno. Lakini wakati anarudi kutoa vyombo, ndipo hapo akaitwa na kiongozi mmojawapo wa JC na kumuambia amuimbie. Ikawa kama ndoto ya mchana, aliposogelea kipaza sauti akaomba pia apige kinanda, hapo ndipo wakadhani kwamba anawatania na hamaanishi anachokiongea.

Sechaba aliamua kwamba kama wamemruhusu kuimba basdi wamruhusu pia apige kinanda. Na alipofanya hivyo, KWA TAARIFA YAKO kilichotokea hapo ni kujipatia hati ya kusafiria na tiketi ya ndege kwenda jijini London, Uingereza ka ajili ya uimbaji. Lakini haya yote alikuwa akiyafanya huku bangi na uvutaji wa sigara ikiwa ni kawaida kwake. Kitu gani kilifuata baada ya hapo? Ungana nasi wiki ijayo kwa sehemu ya pili.

 Hiyo ndio KWA TAARIFA YAKO, vinginevyo tukutane wiki ijayo.

Share on Google Plus

About Gospel Kitaa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.