KWA TAARIFA YAKO: KUTOKA UVUTA BANGI HADI INJILI KWA UIMBAJI (2)

Haya msomaji wetu wa Gospel Kitaa karibu kwenye kipengele chetu maalum cha "KWA TAARIFA YAKO", ambacho kinakujia kila siku za alhamisi ndani ya GK kikiwa na lengo la kukupatia habari ambayo iliwahi kutokea lakini yawezekana huijui, ama yawezekana pia unaijua lakini GK ikawa imesahau au kuna sehemu haina usahihi - utapata fursa ya kusahihisha kwa kuandika maoni yako chini kabisa kwenye habari husika. Karibu. 
Sechaba ©Sechaba Pali/fb
Wiki iliyopita tuliona namna gani Sechaba alivyofika na kuanza kuimba na hatimaye kujipatia fursa ya kwenda kuimba nchini Uingereza pamoja na Joyous (bofya hapa kusoma). Hayo KWA TAARIFA YAKO yalitokea ndani ya siku tatu tu, yaani tokea kuimba kwake kwa majaribio hadi kufika Uingereza. Kwake yeye, ilikuwa ni jambo rahisi sana, kiasi kwamba yale ambayo alihisi ni kumridhisha baba yake kipindi akimlazimisha kupiga kinanda na kuiimbia kwaya kanisani kwao, ndicho kilichomtoa.

Hali ya ukumbi wa mazoezi wakati ameanza kuimba ilibadilika ghafla, na kila mtu kujikuta akienda kushuhudia ni muimbaji gani wa kipekee namna hii - na alikuwa wapi. Ajabu ni kwamba wakakuta ni mtu yule yule waliyemdharau na kuambiwa kuwa ni mpishi tu na wala hawezi lolote kuhusu uimbaji. KWA TAARIFA YAKO, unaweza ukakatishwa tamaa na wengi sana, hata wale ambao unaona wanaheshimika kwenye jamii, lakini muhimu kwako ni kutoacha kujaribu tena na tena.

Sechaba alishangazwa na namna watu wanavyomshangaa na kububujikwa na machozi kwa uimbaji wake, ambao yeye mwenyewe aliuona ni wa kawaida tu. Na hapo KWA TAARIFA YAKO unaweza ukawa unadharau kile ulicho nacho ndani yako, lakini ni muhimu ukamuomba Mungu akufunulie ili kikue na hatimaye Mungu ajitwalie utukufu kwa kukiweka ndani yako.

Siku tatu za mabadiliko ya ghafla, zilimtoa Sechaba kwenye upishi na kuhudumia waimbaji waliokuwa wanafanya mazoezi kwenye ukumbi wa Downtown Music Warehouse, sehemu ambayo pia alikuwa akilala - hadi kuwa muimbaji anayehudumu na kundi maarudu nchini Afrika Kusini, Joyous Celebration. Passport ilipatikana ndani ya muda mfupi, na kwa mara ya kwanza akakwea ndege tena kwa ajili ya safari ya kimataifa kuelekea London, Uingereza.

Akiwa huko aliendelea kukonga mioyo ya watu kwa sauti na mfumo wa uimbaji wake, watu wakiendelea kubarikiwa kwa kazi yake mpya. Lakini pamoja na hayo, KWA TAARIFA YAKO Sechaba na bangi na sigara ilikuwa ni kama kawaida. Yeye kwake kinachoendelea, anaona ni kama anaimbaimba tu bila hata hisia zozote - na akishangaa watu wanavyoguswa kila mara anapokuwa na kipaza sauti.

Si ajabu pia hata siku hizi kusikia tetesi ama matukio kwamba fulani lazima 'apulize' ndio aweze kuweka vina na kunata na biti, na kusahau kwamba uimbaji ni injili tosha ambayo mtu anahitaji muongozo wa Roho Mtakatifu ili apate kusema na wale anaowahitaji.

Sechaba Pali ©Citizen SA
Umaarufu wa Sechaba ulizidi kukua kadri siku zinavyoenda, huku pia na matukio akiwa nayo ya kutosha mtaani - hadi siku moja TB Joshua alipomuona kwenye runinga mwaka 2010, na kuvutiwa naye moja kwa moja na kumuambia mmoja ya wasaidizi wake "yafaa sauti hii imuimbie Mungu, namhitaji huyu mtu" Ndipo hapo KWA TAARIFA YAKO ikawa mwanzo wa kufunguliwa kwa Sechaba.

Wakati anafika Nigeria (ambapo na yeye pia alikuwa akimfahamu TB Joshua kupitia mahubiri yake) aliona ni ajabu kutafutwa na mtu mkubwa namna hiyo, na hivyo hakukataa wito. KWA TAARIFA YAKO ujio wake Nigeria ulikuwa ndo mwanzo wa safari ya uponyaji wake. Lakini pamoja na kwamba siku ya ibada alijua fika kwamba maeneo hayo ni ya kanisa, mfukoni alikuwa na sigara zake kama kawaida - na akaomba kutoka nje kidogo apunge upepo, lengo likiwa ni kuweka stimu sawa.

Pamoja na kwamba siku hiyo alikuwa akitegemea uponyaji, lakini hakuwa tayari kuacha kuvuta. Wakati anavuta sigara yake, mhubiri mmoja wa pale alimuona na kuanza kumuhubiria KWA TAARIFA YAKO jambo hili lilimkera sana Sechaba kiasi kwamba alilazimika kuwasha sigara mbili kwa pamoja akizivuta ili kupunguza hasira ambazo aliona kama zinataka kumpeleka pabaya. Ukorofi ulikuwa desturi kwake. Lakini hatimaye kutokana na muhubiri huyo kutokata tamaa, hatimaye Sechaba alimuabia kwamba kama vipi akae na boksi lake la sigara hadi ibada itakapoisha ili arejeshewe, wakaafikiana.

Maafikiano hayo ni kama vile Sechaba alijikoroga, kwani ndani kilichokuwa kinamsubiri ni kufunguliwa. Wakati TB Joshua anapita kuombea watu, Sechaba naye alipitiwa na kuombewa, jambo ambalo KWA TAARIFA YAKO anasema kuwa hajawahi kukutana nalo katu. Sechaba alikuja kukiri ukorofi aliokuwa nawo na kisha kusema kwamba zamani alikuwa mwanamuziki wa nyimbo za injili, lakini sasa ni muabudu. Kwani alikuwa akifungua fungua mdomo na kutoa sauti, lakini sasa anamubudu Mungu.

KWA TAARIFA YAKO Kufunguliwa kwa Sechaba kumeleta hatua mpya kwenye maisha yake, japo hadi sasa kuna changamoto anakabiliana nazo, ikiwemo kesi ya kubaka mwaka 2012 (licha ya kusema kwamba walikubaliana akijua kwamba ana umri wa miaka 17) msichana mwenye umri chini ya miaka 18. Maeneo mengi, roho ya uzinzi imekuwa ikisumbua waimbaji, ikiwemo habari zisizo rasmi kuhusu walimu wa kwaya. Cha muhimu zaidi ni kujiweka karibu na Mungu na kuzidi kumuomba muongozo wake kila mara.

Msichana huyo alipata ujauzito na kujifungua mtoto, ambapo kesi hiyo imetolewa hukumu ya miaka 5 jela kwa Sechaba, huku wakili wake akiweka pingamizi na kuomba mahakama ifikirie upya kwani Sechaba amebadilika tayari na anamlelea mtoto huyo. Pamoja na hilo KWA TAARIFA YAKO Sechaba ana watoto 9 waliopatika kwa nyakati tofauti kwenye mahusiano ambayo amewahi kuwa nayo, ambapo mahakama iliamuru kuwa awalelee watoto wote, na kwamba hatakiwi kufanya kazi maeneo ambayo yana watoto kwani tayari jina lake liko miongoni mwa wabakaji.

Hiyo ndio KWA TAARIFA YAKO wiki. Tuandikie maoni yako kuhusu habari hii, vinginevyo tukutane wiki ijayo.


Share on Google Plus

About Gospel Kitaa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.