NAMNA HUKUMU YA KUNYONGWA ILIVYOTOLEWA KWA HILA KWA MKRISTO PAKISTAN

Aasiya Noreen (Asia Bibi) ©CNN
Mwaka 2010, mama wa watoto wanne (CNN ikiripoti 5), Aasiya Noreen almaarufu kama Asia Bibi alikuwa mtu wa kwanza kuhukumiwa kifo kupitia sheria inayokataza kufuru dhidi ya dini (ya kiislamu) nchini Pakistan. Kwa mujibu wa vyanzo vya habari, inaelezwa kuwa chanzo ni kubishana pale ambapo alikatazwa kutumia glasi ya maji kwa kuwa yeye ni mkristo, tofauti na ilivyo kwa wamiliki wa glasi hiyo, waislamu. Kufikia leo, hukumu hiyo imesisitizwa na mahakama kuu ya Lahore baada ya kuitupilia mbali rufaa ya washtakiwa.

Mwanzoni mwa kesi, mwanamama huyo alipata faraja pale ambapo wanasiasa wawili maarufu walijitokeza kumtetea. Lakini faraja hiyo iligeuka shubiri baada ya wanasiasa hao kuuwawa mmoja baada ya mwingine. mmojawao akiuwawa na mlinzi wake mwenyewe. Tumaini likatoweka.

Tukio la kuuwawa wanasiasa hao lilichukua sura mpya pale ambapo mtuhumiwa wa mauaji alifikishwa mahakamani na kupokelewa kwa kumpambia njia kwa maua 'rose' na wanasheria, mithili ya bwana harusi aingiapo ukumbini. Hatua iliyofuata kwenye kesi hiyo ni jaji kuikimbia nchi kuhofia usalama wake.

Tukirejea kwa Bibi, yeye pamoja na wanasheria wake wamekuwa wahikangaika tokea mwaka 2010, kuona ni namna gani atanusurika na adhabu ya kifo - na hatimaye kurejea kwenye majukumu yake ya kila siku. Lakini pamoja na hayo, kuna utata, na huenda asiachiwe hata kama kesi itaendelea kusikilizwa kwa muda mrefu zaidi, maana hofu mojawapo ya vyombo vya dola ni ya wao kuonekana wabaya pale ambapo watamuachia Bibi huru. (licha ya kuripotiwa na mashahidi kwamba ni kesi ya kusingiziwa)

GK imefahamu kuwa pamoja na rufaa ya wanasheria kuanza kusikilizwa, hakuna mashahidi wa upande wa walalamikaji ambao walijitokeza, na hivyo ajabu zaidi, hao ambao hawakujitokeza, wakapewa ushindi. Hukumu imesalia kama ilivyokuwa.

Inaaminika kwamba mama huyo mwenye umri wa miaka kati ya 43 - 49 anaweza asiachiwe kutokana na namna vifungu vya sheria vilivyowekwa.

1. Hakuna tafsiri iliyowekwa kuhusu maana ya kufuru.

2. Ushahidi hautakiwi kusikilizwa upya mahakamani namna ilivyokuwa, kwani inaaminika ni kama kukufuru upya pale ambapo itarejewa ama kunukuliwa namna kosa lilivyotendeka.

3. Hakuna hatua itakayochukuliwa dhidi ya mlalamikaji ambaye atapeleka mashtaka ya kufuru aidha kimakosa ama kwa kisirani

Mojawapo ya maandamano mwaka 2010 kushinikiza Asia Bibi aachiwe huru. ©The Guardian
Pamoja na kupoteza matumaini, bado wanasheria wanaomsimamia Asia Bibi wanapanga kwenda mahakama ya juu zaidi ili kukata rufaa ya tukio hilo ili kuona haki itakavyozingatiwa, huku makundi kama umoja wa wapakistani wa jamii za pembezoni, (All Pakistan Minorities Alliance) ikifanya maandamano mara kadhaa kushinikiza kuachiwa kwa Bibi.

Pakistan ni taifa la kiislamu linaloongozwa na Katiba ya mwaka 1973, iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2012, ambapo wakristo nchini humo hupata misukosuko kutokana na imani yao kuwa tofauti na dola.


Share on Google Plus

About Gospel Kitaa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.