JISHINDIE NAFASI YA KUREKODI WIMBO NA VIDEO BURE (NINAWEZA KUIMBA)


Kwa kipindi kirefu sasa , Gospel Kitaa chini ya kampuni mama ya Tuck & Roll (T&C) imekuwa ikichakata namna ya kumrudishia Mungu utukufu kupitia uimbaji, na hii ni zaidi ya waimbaji ambao tumekuwa tukiwasikia na kuwaona kwenye vyombo mbalimbali vya habari nchini na nje ya nchi.

Ninaweza Kuimba ni tukio ambalo T&C imeliandaa kupitia Gospel Kitaa ili kuwawezesha wale waimbaji ambao hawajapata fursa ya kuingia studio na kumuimbia Mungu, sanasana zaidi wanaimba pale wanapokuwa bafuni ama jikoni. Yaani kipaji kipo, ila fursa ndio imekosekana.

Kwa kushirikiana na wadau wengine, GK imeamua kukusanya nguvu kazi na rasilimali kwa ajili ya kuwezesha waliolalia vipaji vyao ili basi wapate kugusa mioyo ya watu wengi zaidi kuliko kuimba tu wakiwa mafichoni. 

Imewahi kusemwa kuwa, "Before this day is done, my life shall touch a dozen lives", kwa lugha rahisi kwamba, kabla siku haijaisha - maisha yangu yatagusa maisha ya wengi zaidi, na hili ndilo ambalo GK inatumai kutimiza kwa njia hii, ili basi hata waimbaji watakaopatikana, wakaguse mioyo na maisha ya mamilioni ya watu kupitia uimbaji. Ndio dhana ya msemo huo ambao mtunzi wake hakutaka kufahamika (preferred to be anonymous).

NINAWEZA KUIMBA

GK imeshirikiana na wadau wengine kuhakikisha kwamba washiriki watakaofanya vizuri zaidi watapata fursa ya kuingia studio na kurekodi albamu, na kisha kurekodiwa video. Yote hii ni bila gharama yoyote, kwani zimebebwa na GK pamoja na wadau wengine ikiwemo kwa sasa ambao tunaweza kuwataja; Araka Pro Media, JM Media, InHouse (kitengo dada cha Gospel Kitaa) na nyinginezo ambazo bado ziko kwenye hatua ya mwisho ya kusogeza jahazi la uimbaji kwa ajili ya utukufu wa Mungu.

UTARATIBU NA USHIRIKI:

Kwa kutumia simu yako, unaweza kushiriki shindano hili kwa kutuma barua pepe ama kwa kutumia WhatsApp ili kuwa mmojawapo kati ya waimbaji 5 watakaopata fursa ya kuingia studio kurekodi wimbo ama albamu nzima, na kisha kupata fursa ya kurekodiwa video na wataalamu walio tayari kufanikisha zoezi hili.1. Rekodi ubeti mmoja (wowote) na kiitikio cha wimbo wa "Ni Tabibu wa Karibu", ulioko kwenye kitabu cha Tenzi za Rohoni (namba 7) ama kwenye kitabu cha Nyimbo za Injili (namba 110). Na kisha utume kwa njia ya WhatsApp kwenda namba +255713554153 ama +255769952893 au kwa njia ya baruapepe; uimbaji@inhouse.co.tz

Unapotuma sauti yako kwa njia ya WhatsApp, jitambulishe kwa ukamilifu kwa kuandika majina yako, umri wako, shughuli unayofanya (kazi), na mahala unapoishi, kwa mfano, kama ni Mbagala, Masaki, Njiro, Ngulelo… ili mradi tu uwe ni mkazi wa Arusha ama Dar es Salaam.

Halikadhalika ukituma sauti kwa njia ya barua pepe, ufanye vivyo hivyo kwa utambulisho, lakini pia sehemu ya 'Subject', iwe imeanza na neno "Ninaweza Kuimba", ikifuatiwa na jina lako na mahali unapoishi. Mathalani kama unaitwa Anna Masama, basi utaandika kwenye subject ya barua pepe: Ninaweza Kuimba - Anna Masama - Ngulelo. Hii itasaidia kutenganisha na kuchambua barua pepe zinazohusu shindano kwa urahisi zaidi.

Mara baada ya kutuma sauti ya ushiriki, utapata majibu ndani ya masaa 24 iwapo sauti yako imefika. Hatua hii haimaaanishi kwamba umeshinda, ila ni uthibitisho tu kwamba sauti imefika mahala husika. Na ikiwa ndani ya masaa 24 haukupata jibu kwamba sauti imepokelewa, basi unaweza kutuma upya kwa kuhakiki namba ama barua pepe isije ikawa imekosewa. (Hutakiwi kutuma upya kama umeshajibiwa kwamba sauti yako imepokelewa).

2. Unatakiwa kushiriki mara moja tu, yaani kwamba ukishatuma sauti yako kwenye namba mojawapo zilizoainishwa hapo juu, basi huna haja ya kutuma kwenda namba nyingine tena ama kwenye barua pepe. Mara moja tu inatosha, vinginevyo itakuwa sababu ya kujiengua kwenye shindano hili.

UMRI
Shindano hili halina ukomo wa umri. Mtu yeyote anayejitambua anaweza kushiriki, ili mradi tu ikiwa yuko chini ya umri wa miaka 18 ridhaa ya mzazi itahitajika ili kuhakikisha kwamba kila kitu kinaenda sawa bila kukiuka sheria za nchi.

ENEO
Shindano hili liko wazi kwa wakazi wa Arusha na Dar es Salaam nchini Tanzania pekee kwa sasa. Msimu huu wa kwanza uko kwenye majiji haya, kwa msimu wa pili panapo neema, wigo wa maeneo ya ushiriki utaongezeka zaidi.

UZOEFU
Mshiriki hatakiwi kuwa ambaye ameshawahi kurekodi studio, anatakiwa mtu wa aina yeyote yule ambaye anadhani ana kipaji cha kuimba lakini hajawahi kupata fursa ya kufanya hivyo, zaidi ya kuimba mwenyewe aidha kwa kujiamini ama kutojiamini.

MUDA
Awamu ya kwanza ni ya upokeaji wa sauti, ambayo itadumu kwa muda wa wiki 3 kuanzia Jumatano tarehe 19 Novemba 2014 na kufikia kilele chake tarehe 24 Disemba 2014, ambapo upokeaji wa sauti utafungwa na kisha uchambuzi kufanyika kabla ya washindi kutangazwa.

ZAWADI
Kutakuwa na washindi 5. Mshindi wa kwanza atapata fursa ya kurekodi albamu yenye nyimbo 8 kwenye studio atakayopangiwa na waandaaji, na pia kutengenezewa video kwa utaratibu utakaopangwa - zote kwa gharama ya waandaaji. Na kisha washindi 4 waliosalia nao watapata fursa ya kurekodi albamu ya pamoja yenye nyimbo 8 na kisha kufanyiwa video kulingana na waandaaji wa 'Ninaweza Kuimba' watakavyoona inafaa.

Washindi watatangazwa kupitia kwenye tovuti ya Gospel Kitaa na washirika wake. Pia mawasiliano ya awali yatafanywa ili kuthibitisha kama wamezingatia masharti na vigezo vilivyotakiwa.

Sauti zimeanza kupokelewa rasmi. Kila la heri kwa washiriki wote.

Share on Google Plus

About Gospel Kitaa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.