HOJA: HALI HALISI YA MKENGEUKO WA MAADILI KATIKA JAMII (2)

Makala iliyopita ilichambua habari kuhusu tafsiri ya misamiati ya maadili na aina zake pamoja na tafsiri za msamiati wa “mkengeuko” na aina zake. Leo tunaendelea na nada hii tukilenga kuchambua vichocheo vikuu vya mkengeuko wa maadili katika jamii yetu:

Ujue utandawazi unavyochochea
mkengeuko wa maadili katika jamii

Askofu Sylvester Gamanywa
Mojawapo ya vichocheo vikuu vinavyoongoza kuendelelza mkengeuko wa maadili katika jamii ni utandawazi. Hata hivyo, kabla ya kuingia moja kwa moja kwenye uchangiaji huo, ni bora kwanza tujielimishe kuhusu utandawazi wenyewe ni kitu gani, faida na changamoto zake za kiulimwengu. Baada ya kuyachambua hayo, ndipo tunakapokuja kuanisha maeneo ambayo utandawazi unachochea mkengeuko wa kimaadili katika jamii.

Kwa kifupi, tafsiri nyepesi ya msamiati wa utandawazi maana yake ni Mfumo wa mahusiano ya kimataifa katika nyanja mbali mbali k.v. biashara, uchumi, au siasa uliowezeshwa na maendeleo ya teknolojia ya habari yanayofanya mataifa kuwasiliana kwa urahisi. (Kamusi ya Kiswahili Sanifu) Kama ilivyo kawaida katika kutathmini ufanisi wa kila jambo lazima uchunguze faida na athari zake kama zipo, na kisha kuweka mikakati ya kukabiliana na changamoto ikiwa ni lazima. Hapa chini nakudokezea kwa ufupi baadhi ya faida za utandawazi, athari zake kwa ujumla ni mwisho nitakuingiza kwenye changamoto zenyewe za utandawazi kwa upana:
 • Baadhi ya faida za utandawazi
Kuziwezesha nchi kufanya mambo zinazoweza kufanya kwa viwango vya ubora zaidi. M.f nchi ikiweza kununua chuma kwa bei rahisi kutoka nchi nyingine, haina haja ya kujitengenezea chuma kwa gharama kubwa, badala yake inaendelea kutengeneza vitu vingine vyenye tija na gharama nafuu

Kuna soko pana zaidi. Unaweza kuuza bidhaa nyingi zaidi na kupata faida, na hata kutengeneza ajira.

Walaji nao hunufaika. Ushindani hufanya bidhaa kuwa na bei za chini, na upatikanaji haraka wa bidhaa mpya
 • Baadhi ya athari za ujumla
Ukosefu wa ajira katika nchi za maendeleo ya viwanda, kwa sababu kuhamishia viwanda kwenye maeneo ambayo kuna malipo ya chini ya vibarua

Nchi maskini sana za ulimwengu wa tatu, hususani katika Afrika, kutumbukia katika umasikini zaidi kwa sababu jamii kubwa ya raia wake haina elimu ya kutosha ikilinganishwa na nchi zilizoendelea; na hazina teknolojia mpya kama nchi tajiri

Maambukizi ya mkengeuko wa maadili ya kimaani na kiutamaduni kwa sababu ya mwingiliano wa walioharibika kitabia, waliojaa tamaa ya kupata faida kubwa bila kujali maadili mema katika nchi husika

FAIDA NA CHANGAMOTO ZA UTANDAWAZI
FAIDA
CHANGAMOTO
 1. Ongezeko la uhuru wa biashara kati ya mataifa

 1. Ongezeko la mtaji wa kifedha kuwawezesha wawekezaji kutoka nchi zilizoendelea kuwekeza katika nchi zinazoendelea

 1. Mashirika kuwa na uhuru mkubwa wa kufanya kazi nje ya mipaka ya nchi zao

 1. Vyombo vya habari vya kimataifa kuuleta ulimwengu mahali pamoja

 1. Ongezeko la wepesi wa mawasiliano na ushirikishanaji taarifa muhimu kati ya mashirika na watu binafsi ulimwengu mzima

 1. Urahisi wa usafirishaji wa haraka wa bidhaa na watu

 1. Ongezeko la hali ya kutegemeana kati ya mataifa


 1. Kuenea kwa tabia ya maisha ya kupenda vitu na uchu wa kujipatia utajiri wa haraka haraka

 1. Kuongezeka kwa ajira za watu kutoka nchi zilizoendelea kwenda nchi zinazoendelea ili kupunguza matumizi ya mishahara kunakotokana na viwango vidogo vya mishahara (cheapest labor)

 1. Tishio la kusafirisha magonjwa bila kukusudia kutoka nchi moja hadi nyingine

 1. Tisho la vyombo vya habari kumilikiwa na mashirika makubwa yasiyojali tamaduni na maadili ya kijamii ya nchi husika

 1. Kuongezeka ugomvi wa kibiashara ndani ya nchi zilizoendelea zitakazochochea vita vya kiraia ndani nchi zinazoendelea kwa sababu ya kushindania utajiri na rasilimali za nchi husikaChangamoto za utandawazi 


Uchu wa kupenda mali na utajiri wa haraka haraka
Katika ushindani wa biashara kuna vivutio vingi sana ambavyo wafanyabiashara hutumia ushawishi mwingi kuuza bidhaa zao, ikiwemo mikopo ya bidhaa ili mtu alipe kidogo kidogo kwa muda mrefu. Wananchi wa kawaida ambao hawakuzoea kuona vitu vizuri na vya thamani madukani hushawishika kupata vitu hivyo pasipo kujua kwamba vinahitaji fedha ili kuvipata. Hapo ndipo vishawishi hujitokeza vya kutafuta fedha za haraka haraka ili kupata vitu kwa haraka haraka.


Wageni wanaochukua ajira za wenyeji nchini
 

Kwanza ni lazima tukubali kwamba uchumi wetu hauwezi kukua kutokana na sisi wenyewe peke yetu bila ushirikiano na raia wa mataifa mengine hapa duniani, hususan mataifa tajiri. Lakini lazima pia tuwe makini kukumbuka kwamba ziko changamoto za kupata wawekezaji kutoka nje! Baadhi yake ni pamoja na kujikuta tunajaza watu kutoka nje wanaoletwa na makampuni ya nje. Kumbuka huko nje kwenye nchi zilizoendelea viwango vya ajira na kodi viko juu sana kuliko vya nchi zinazoendelea. Wawekezaji kutoka nje wanapoleta watu wao ili kufanya kazi kwa viwango vya kodi na ajira za hapa nchini, huweza kupungua matumizi makubwa katika uzalishaji na kupata faida kubwa. Wakati huo huo wenyeji huishia kuwa vibarua wasionufaika na uchumi w anchi ambao wao wamehusika kuuzalisha.

Vyombo vya habari visivyojali maadili


Tukubali au tusikubali, vyombo vikubwa vya habari vya kimataifa vinamilikiwa na mashirika ya nchi zilizoendelea ambazo zinajali biashara kuliko maadili ya kijamii na kitaifa. Dhana ya utandawazi ni kila mtu kuwa huru kufanya atakalo pasipo kuingiliwa na mtu mwingine. Hii ni pamoja na uhuru wa kusoma, kusikiliza au kutazama taarifa mbaya na picha chafu kwa kisingizio cha burdani. Hivi sasa sio siri tunawashuhudia vijana wetu wakienda nusu uchi kwa sababu ya maigizo wanayokutana nayo kwenye media za kisekula.

Vita vya kiraia kwa ajili ya kugombania rasilimali za nchi


Ukifuatilia kwa makini katika nchi ambazo zimekumbwa na vita vya kiraia, kwa haraka unaweza kuona dalili za kugombania mapato na matumizi ya rasilimali za asili katika nchi husika. Na nyuma yake kuna wapambe wanaochoochea na kugharimia vita hivyo vizidi kushamiri wakati wahusika wanakusanya utajiri uliomo katika nchi husika.

Itaendelea wiki ijayo

Share on Google Plus

About Gospel Kitaa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.