HOJA: HALI HALISI YA MKENGEUKO WA MAADILI KATIKA JAMII (4)

Makala iliyopita tulikuwa tukijifunza Maeneo ya utandawazi yanayoongoza kuchochea mkengeuko wa maadili. Humo tulichambua habari za “Mitandao ya kijamii” na “mitandao ya simu za mkononi”. Leo naomba nikushirikishe mtazamo wa Yesu Kristo kuhusu kizazi kilichokuwa kimeathiriwa na mkengeuko wa maadili

Askofu Sylvester Gamanywa

Mkengeuko wa maadili enzi za Bwana Yesu duniani

Athari za mmomonyoko wa maadili katika jamii hazikuanza hivi leo kwenye kizazi chetu. Hata enzi za Yesu Kristo alipokuwepo duniani, kizazi kile kilikuwa kimeathirika kimaadili na mpaka Yesu akawa anakitafsiri kuwa ni kizazi kikaidi, kizazi cha zinaa na kadhalika. 

"Na alipowaona makutano aliwahurumia kwa sababu walikuwa wamechoka na kutawanyika kama kondoo wasio na mchungaji. Ndipo alipowaambia wanafunzi wake, mavuno ni mengi, lakini watendakazi ni wachache" (Mt 9:36-37)

Sasa maandiko tuliyosoma hapa juu yanatupeleka kwenye somo muhimu juu ya mtazamo wa Yesu alivyoutafsiri mkengeuko wa kimaadili enzi hizo. Kwanza tumesoma kwamba “aliwahurumia”. Kisa cha kuwahurumia ni kwa sababu aliwoana “wamechoka” na “kutawanyika” kama “kondoo wasio na mchungaji”! Katika kuchambua maandiko haya, napenda kwanza tupitie tafsiri ya misamiati ya haya maneno ya “uchovu” na “mtawanyiko” aliougundua Yesu kwenye makutano yake:
  1. Tafsiri ya uchovu na mtawanyiko
Maandiko yanatupa picha ya mtazamo wa Yesu kwa jinsi alivyowaona makutano waliokuwa wakimfuata na kumsikiliza. Kwa macho ya Yesu, makutano japokuwa walikuwa wakimfuata kwa wingi na wakiwa mahali pamoja kumsikiliza; bado yeye aliwaona kila mmoja ni amechoka na kutawanyika sawa na kondoo asiye na mchungaji.

Unajua utamaduni wa kuchunga kondoo wa mashariki ya kati ya enzi hizo, mchungaji hutangulia kondoo na kondoo humfuata kwa nyuma. Sisi tumezoea mchungaji kutanguliza kondoo mbele na yeye kufuata kwa nyuma ya kondoo. Lakini Mashariki ya kati mchungaji hutangulia kondoo na huwaita kwa sauti na humfuata nyuma. Kwa utaratibu huu, utaona kwamba, kama kondoo wa jinsi hii hawana mchungaji mbele yao anayewaongoza kwenda mahali, maana watajiendelea wenyewe kwa uzoefu lakini itafikia mahali ambapo watasambaratika kila kondoo na njia yake.

Tukirejea tafsiri ya mtazamo wa Yesu kuhusu uchovu na mtawanyiko wa makutano yake, ni kwamba “uchovu” unaotajwa na Yesu na hali ya kukata tamaa na kupoteza matumaini kutokana na matatizo sugu ya kiroho, kiafya, mpaka kiuchumi.

Kumbuka kwamba, mfumo wa utawala wa enzi hizo haukuwa mfumo unaojali sana maslahi ya raia wake. Ulikuwa ni mfumo wa kifalme ambao raia wote ni mali ya mfalme. Ardhi yote ni mali ya mfalme. Na shughuli za uzalishaji wa uchumi ni mali ya mfalme.

Tukirejea kwenye mfumo wa kidini, walikuwepo viongozi wa dini ya kiyahuni, ambao nao walikwisha “kuchakachua maadili” ya kiimani’ na wanawaongoza watu kwa desturi za kibinadamu badala ya kuzingatia misingi ya kimungu kwa mujibu wa torati ya Musa.

Kwa mazingira haya, jamii ya makutano yaliyomjia Yesu walikwisha kukata tamaa ya kuwa raia huru, na kujikatia tamaa, na hapakuwepo na mwelekeo wenye matumaini.

Kutokana na uchovu wa makutano, kila mtu katika makutano hayo alikuwa na mawazo yake tofauti katika kufanya maamuzi. Kumbuka kwamba, hapaokuwepo na taasisi inayowajumuisha kwa nia ya kuwaongoza kijamii, kwa hiyo, hawakuwa na mtazamo wa kitaasisi, bali kila mtu, sawa na kuku wa kienyeji, alijitafutia chakula chake mwenyewe.
  1. Athari za uchovu na mtawanyiko wa akili
Kutokana na uchovu na mtawanyiko wa kiakili wa makutano; inaonesha tayari walikwisha kuathirika kwa habari ya uwezo wa kukabiliana na matatizo na kuyatafutia ufumbuzi. Uwezo wao wa kufiriki ulikwisha kuathirika na kila alipojitokeza mtu mwenye uwezo wa kutatua matatizo walikuwa tayari kumtawaza awe mfalme wao, ili aendelee kuwasaidia. Ndivyo walivyomchukulia hata Yesu mwenyewe.

Hali hii ndiyo inalikabili taifa letu pamoja na nchi nyingi za kiafrika. Tumekwisha kuathirika kwa sababu ya uchovu na tumetawanyika kimawazo. Ndiyo maana tunapokutana na changamoto hasi, tunajikuta hatuna mtazamo wa aina moja wa kukabiliana na matatizo! Wakati baadhi yetu tukutanapo na matatizo ama tunaamua kwenda “likizo ya kufikiri” kwa muda; wengine huamua “kuyasusia matataizo” na kuyatelekeza ili yajitatue yenyewe; na wengine huamua kushinikiza watu wasiohusika wasadie kufikiri! Na kundi hili hufikia uamuzi huu wa kuwalazimisha wengine wasiohusika ndio wawasaidie kutatua matatizo yao kwa lazima hususan baada ya kujikuta katika mazingira magumu, hawana msaada wa kibinadamu na wakati huo huo binadamu wenzao wapo lakini hawataki kutoa msaada!


Visa vya mifano hai kuhusu uchovu na mtawanyiko wa kimawazo
  1. Abiria walipoamua kufunga barabara magari yasipite
Wiki nilikuwa safari kutoka Dodoma nikirejea Dar es salaam. Tulipofika eneo karibu na Kibaigwa tukakuta magari yamesimama na barabara imefungwa kw akuwekwa mawe katikati ya barabara. Tulipouliza kisa cha kufungwa kwa barabara ndipo tuliposimuliwa kisa kimoja cha aina yake kama ifuatavyo:

Basi moja la abiria lililokuwa likielekea Kagera lilipofika hapo likaharibika, na limekuwepo hapo tangu jana yake. Abiria wamejikuta wamekwama hapo. Hakuna matengenezo yanayofanyika. Abiria wakaamua kurudishiwa nauli zao ili wajitafutie usafiri mwingine wakanyimwa. Abiria hao wakajaribu kuwasiliana na SUMATRA ili angalau wapate ushauri huko nako wakagonga mwamba.


Wakati huo huo kuna abiria wenye watoto wadogo na wamelala hapo usiku kucha hakuna huduma yoyote ya chakula wala maji! Kila gari linasosimamishwa ili kuomba msaada lakini kila gari inawapita bila kutoa msaada wowote. Mwishowe kwa hasira, abiria wakaamua kufanya “maamuzi magumu”! Wakaamua kuingia porini na kusomba mawe na kuamua kufunga barabara ili magari yasipite hapo mpaka “kieleweke”!
  1. Madereva wa bodaboda Kibamba wafunga barabara Kwa saa mbili
Kabla hatujaingia jijini Dar es Salaam, tulipofika kibamba tukakutana mkwamo wa magari ambayo papnde zote hayaendi. Msafara wetu tunaokuja Dar umesimama, na msafara wa kutoka Dar kwenda Kibaha nao umesimama huko huko. Gari letu lilikuwa umbali wa mita kama mia tatu kutoka kwenye tukio lililosababisha mkwamo wa magari.

Tulipofuatilia huko mbele, kumbe kuna maiti imelala katikati ya barabara. Tukaambia hiyo ni maiti ya dreva wa bodaboda ambaye aligongwa na gari na kufariki hapo hapo! Dreva aliyegonga aliamua kutokusimama akaenda zake. Ndipo ghafla madereva wa bodaboda wakakusanyika na kuwa kikubwa na wakafanya maamuzi magumu ya kufunga barabara magari yasipite hapo.

Kwa upande wetu hatukuwa na njia ya kando ya kupenya ili tuendelee na safari kwa sababu kila upande kuna mabonde na makorongo ambayo gari haiwezi kupita. Kituko kingine, madereva wengine wasio na uvumilivu wakaamua michepuko kupita pembeni wakafunga njia ya madereva walioko mbele yao washindwe kuendelea na safari! Tulikwama hapo tangu saa 2.00 usiku na kuondoka eneo hilo ilikuwa ni saa 4.00 usiku.

Msomaji unaweza kuhoji kwamba, katika maelezo yote haya, mkengeuko wa maadili uko wapi? Tukutane toleo lijalo tutaanzia hapa tulipoishia leo!

Itaendelea wiki ijayo
Share on Google Plus

About Gospel Kitaa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.