KWA TAARIFA YAKO: WIMBO WA KWANZA WA DINI KUONYESHWA KWENYE EATV NA KUMBI ZA STAREHE

Haya msomaji wetu wa Gospel Kitaa karibu kwenye kipengele chetu maalum cha "KWA TAARIFA YAKO", ambacho kinakujia kila siku za alhamisi ndani ya GK kikiwa na lengo la kukupatia habari ambayo iliwahi kutokea lakini yawezekana huijui, ama yawezekana pia unaijua lakini GK ikawa imesahau au kuna sehemu haina usahihi utapata fursa ya kusahihisha kwa kuandika maoni yako chini kabisa kwenye habari husika. Karibu.


KWA TAARIFA YAKO hii leo GK inataka kukwambia kuhusu wimbo ama video ya kwanza ya muziki wa injili kuonyeshwa katika kituo maarufu cha runinga Afrika mashariki cha channel 5 almaarufu kama EATV kilichochini ya kampuni ya IPP nchini Tanzania. Kabla ya kuutaja wimbo huo na mwimbaji kumbuka ya kwamba kituo hiki awali kilikuwa hakipigi nyimbo za injili za Tanzania ama Afrika mashariki na ikitokea wamepiga basi zilikuwa nyimbo za kutoka nchi za magharibi ya mbali.

KWA TAARIFA YAKO wimbo uliopata bahati ya kupigwa ama kuonyeshwa kwa mara ya kwanza katika kituo hicho ulikuwa wimbo uitwao 'Kuna dawa' wimbo ulioimbwa na mwanadada Esther Wahome kutoka nchi jirani ya Kenya, wimbo huo ulipigwa kwa mara ya kwanza kwenye kipindi cha Top 10 ama Top 20 kama bado nakumbuka vyema, ulipigwa siku ya kwanza siku inayofuatia haukuwekwa, ukaja kuwekwa siku zinazofuatia lakini pia ilikuwa kwa mdondo. KWA TAARIFA YAKO pia wimbo huu ndio ulikuwa wa kwanza kwa nyimbo za injili nchini Kenya kupigwa kwenye klabu za usiku na sehemu nyinginezo, lakini pia album yake ikiuza nakala nyingi zaidi ya milioni kwa muziki wa Kenya.KWA TAARIFA YAKO hapana shaka wimbo huo na mapokeo ya watazamaji ndiyo yaliyozalisha kuanzishwa kipindi cha muziki wa injili ama tayari kulikuwa na mpango wa kuanzishwa kwa kipindi hicho ambacho kilipoanza kurushwa kila asubuhi kupitia runinga hiyo kwaya ya Dar es salaam gospel (D.G.C) kutoka kanisa la Pentecostal Kurasini jijini Dar es salaam nyimbo zake zilikuwa zikirushwa sana kila asubuhi kupitia album yao ya 'Hakuna Jina Lingine', pamoja na waimbaji wengine binafsi na vikundi vilikuwa vikionyeshwa kila asubuhi na kufanya watu hususani wakristo kuangalia runinga hiyo kila asubuhi.

KWA TAARIFA YAKO wimbo wa 'Kuna dawa' awali uliimbwa kwa lugha ya kikuyu ya mwanamama huyo wakiuita 'Ni kuri dawa' kisha akaamua kuuimba kwa kiswahili na kujikuta akimtangaza Yesu Kristo kwa upana wake kupitia wimbo huo si nchini kwake tu lakini pia hata nje ya Kenya yakiwemo mataifa ya magharibi ambako Esther alipata mialiko na kufanya matamasha kama huko Newcastle nchini Uingereza. KWA TAARIFA YAKO Esther yupo kwenye ndoa yake kwa miaka 18 sasa, na kuwa mfano wa kuigwa nchini Kenya hasa kwakuweza kuhimili nafasi yake kama mama wa watoto watatu na mke kwa familia yake lakini pia akijishughulisha na biashara.KWA TAARIFA YAKO kutokana na mafanikio hayo ya muziki na kuweza kumudu mambo yote kwa pamoja (familia na huduma), na kujihusisha kwake kwenye mambo ya kujitolea katika mambo ya kijamii,  mwaka 2012 mwimbaji huyu alipendekezwa kuwania taji la urembo liitwalo Mrs Universe beauty pageant. Pia mwimbaji huyu amepata mialiko mingi sana ya kuimba ikulu mbele ya Rais Moi na wageni ama dhifa mbalimbali katika nyumba hiyo ya taifa la Kenya.
  

KWA TAARIFA YAKO kipaji cha mwimbaji huyu kiliibuliwa na mtengenezaji wa vipindi katika runinga ya taifa la Kenya 'Kenya Broadcasting Television' (KBC) wakati mtengenezaji huyo alipomuona Esther akiimba kanisani huko Nyeri na kumuwezesha mwimbaji huyo kuonekana katika kipindi cha muziki wa injili kwenye runinga kiitwacho 'Sing and Shine'. Na mara baada ya kumaliza tu elimu yake ya kidato cha nne Esther alirekodi album yake ya kwanza, akikaririwa kwamba anafuata nyayo za mwimbaji wake anayempenda sana ambaye si mwingine bali ni Rebecca Malope.

KWA TAARIFA YAKO Esther ni mwimbaji wa kwanza nchini Kenya wimbo wake uitwao 'Furahia' kujumuishwa kwenye album ya pamoja na waimbaji wengine nyota wa muziki wa nje ya kanisa kutoka Afrika. Lakini pia ni miongoni mwa waimbaji wa nchini humo ambao wamelinda ushuhuda wao kwakutoandikwa vibaya kwenye vyombo vya habari, huku akiweka wazi kwamba uimbaji wake ni wito alioitiwa na Mungu na endapo kuna masuala ya fedha katika kushirikishwa kwake katika huduma basi na yeye anastahili haki yake ya mgao wa hizo pesa.

Hiyo ni KWA TAARIFA YAKO kwa wiki hii, vinginevyo tukutane wiki ijayo….

Share on Google Plus

About Ambwene Mwamwaja

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.