MBWA MZEE HAFUNDISHWI MBINU MPYA, UKIMLAZIMISHA SANA ATAKUNG'ATA

Faraja Naftal Mndeme,
GK Contributor.

Mbwa mzee ©One Tribe Wellness

Kuishi kwingi ni kuona mengi. Mwanadamu ni muunganiko wa vitu vingi sana ambavyo ukiviangalia juu juu unaweza usivielewe. Mkusanyiko wa mambo mengi unayoyaona leo ni mkusanyiko wa tabia nyingi zilizojengeka jana. Hakuna jambo ambalo linaibukaibuka kwa sababu limeibuka tu, kila jambo lina mwanzo wake ingawa inaweza kuwa ngumu kukubali au kulitafuta lilipoanzia. Ujenzi wa jamii bora yenye maendeleo ya kifikra na uhuru wa kuweza kutoa maoni na kusimama katika ukweli wa vitu kwenye dunia ya tatu imekuwa ngumu kutokana na ujenzi wa jamii yetu tangu mwanzo tunapozaliwa. Unaweza kuona jamii ambao haipendi mabadiliko ukailaumu lakini kumbe ndivyo tangu mwanzo ilivyojengwa. Maisha yamewekwa kufurahiwa na sio kuhuzunika kwayo.

Unapomuona mtu alivyo leo na vitu vyake vingi anavyofanya ujue kuna maamuzi fulani aliyafanya jana inaweza isiwe moja kwa moja au inaweza kuwa moja kwa moja. Tabia fulani unayoiona kwa mtu ni matokeo ya kile ambacho amekuwa nacho tangu mwanzo. Jaribu kuangalia jamii ambayo imejengwa kwenye uhuru wa kujielezea na kuthubutu, utaona mtoto na baba wanaweza kuwa marafiki na wakacheka na wakaambiana vitu mbali mbali. Lakini huku kwetu Afrika baba akiingia ndani ya nyumba unaweza fikiri ni Jenerali ameingia nyumbani. Pia mama akiingia nyumbani unaweza kufikiri ni Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mwakaleli Mbeya. Je unafikiri mtoto anayelelewa kwenye mazingira haya siku akikua akawa na familia unafikiri yeye naye atakuwaje?

Msingi wa kila jambo kwenye maisha ni kitu muhimu. Iwapo unafuatilia vitu utakuja kugundua watu wengi ambao ni watu wazima leo wanapenda kusoma vitabu mbalimbali vya kujieleimisha utagundua walivyokuwa watoto walipenda sana kusoma vitabu vidogo vidogo vya hadithi, Mfano Manenge na Mandawa, Juma na Rosa n.k. Usomaji wa hadithi hizo kipindi hicho ndio ulijenga msingi mpaka leo watu hawa wamekuwa watu wazima wenye kupenda kusoma. Ni ngumu kuanza kitu ukubwani na ukakiendeleza Maana hautaweza kufikia ukamilifu wake na unaweza kukumbwa na vikwazo mbalimbali.

Ukiona Mtu anaamua kufanya maamuzi magumu kwenye maisha yake ujue kuna mahali ametokea na amaechoshwa na jambo fulani. Ni ngumu kufanya maamuzi magumu kwenye maisha bila kujua umetokea wapi na kipi unachokihitaji maishani mwako.

Jamii yenye kudhubutu na kuamua, ni jamii ambayo tangu mwanzo kuna msingi uljengwa. Ni rahisi kwenda kwenye ATM machine na unakuta mlinzi kawekwa na huku kwenye eneo hilo kuna kamera za ulinzi ndani. Cha kujiuliza, je teknolojia tunaitumiaje? Ni rahisi kupanda kwenye daladala huku konda anatukana na nauli utampa tu. Pamoja na maneno mabovu anayoongea, je unafikiri ni sawa? Maamuzi ya mtu unayoyaona leo yameathiriwa na hali fulani ya jana kwenye maisha yake.

Mbwa akishizeeka sana meno hung'oka. Usitarajie utampa mfupa mgumu atafune kwani kwake itakuwa mateso. Uzee wa umri pia ni uzee wa tabia fulani kwenye maisha yako. Unafikiri unapomuona leo jambazi alianza na ujambazi? Hapa alianza kuwa kibaka. Na tabia ikishajengeka kwenye maisha ya mwanadamu kuiondoa ni shughuli kubwa; ni kama kujaribu kuondoa ngozi ya mwili. Inahitaji muda na uvumilivu.

Ni vizuri kujenga tabia njema ya ujenzi wa jamii huru kwenye kila jambo tangu mwanzo wa utoto wetu.

Mbwa Mzee Hafundishwi Mbinu Mpya,Ukimlazimisha Sana Atakung'ata.

+255719742559
God Bless Y’All

Share on Google Plus

About Gospel Kitaa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.