SOMO: MAMBO YATAKAYOLIFANYA JINA LA YESU LIKUPE MATOKEO


Leo nimeamka nikiwa na mzigo na kiu ya kukupa siri hizi zitakazo kusaidia kuwa na ubora na ufanisi katika matumizi ya Jina kuu la Yesu.
Maana kwa Wakristo wengi limekuwa ni jina lisilotoa matokeo na kufanya makubwa kama lilivyofanya nyakati za Mitume wa Yesu na kanisa la kwanza. Naomba ujitahidi kulipitia somo hili kwa umakini na moyo uliofunguka na hakika utapokea kiwango kipya cha ufunuo na upako uliomo ndani ya jina hili kuu la Yesu.
Nakukaribisha, katika jina la Yesu.

Mstari wa kusimamia:
"Kwa maana kila atakayeliitia jina la BWANA ataokolewa" (Warumi 10:13).

Utangulizi:
Matatizo mengi tuliyonayo yametokana na KUFUMBA MDOMO na kuacha KULITUMIA JINA LA YESU KWA IMANI.
Wengi wanalitumia JINA LA YESU kama kibwagizo cha maombi, na kwa namna hiyo haliwezi kutoa matokeo.

Unapotaka jina la Yesu likupe matokeo lazima ujue na kufanyia kazi mambo yafuatayo:

1. Ni jina TULILOPEWA KISHERIA NA MUNGU kutawala na kumilki na kufunga na kufungua chochote duniani kama Ufunguo wa Ufalme wa mbinguni:

"Kwa maana hakuna JINA JINGINE TULILOPEWA litupasalo kuokolewa kwalo" (Mdo 4:12).
Biblia inasema hili JINA LA YESU tumepewa liwe la kwetu kisheria.
Ni JINA TULILOPEWA si "jina tuliloazimwa" kwa muda.
Ukielewa na kuamini kwamba JINA LA YESU NI MALI YAKO pamoja na mamlaka na nguvu iliyomo ndani yake, Hakika Utaanza kulitumia bila hofu na mashaka wala hautalisema kama kibwagizo cha maombi, na litakupa matokeo na miujiza isiyokuwa ya kawaida.

2. Elewa kwamba IMANI YAKO KUHUSU JINA LA YESU inapaswa kuwa sawa na IMANI YAKO KWA YESU MWENYEWE.

Unajua kuna watu WANAMWAMINI MNO YESU, na wanaamini kama angekuwepo "Live" kimwili, angeweza kutatua na kukomesha kila msiba wao.
Lakini watu hawa HAWANA IMANI YA KIWANGO HICHOHICHO kwa JINA LA YESU.
Zingatia hili:
Yesu kama "mwili" ameketi mkono wa kuume mbinguni anatuombea sasa (Waebrania 7:25, 1Yoh 2:1-2, Warumi 8:33-34).
Yesu kama "mwili" yuko mbinguni akituandalia makao (Yohana 14:1-3).

Hivyo Yesu akiwa kama "mwili" hawezi kutokea na kukusaidia.
Yesu yuko pamoja nasi siku zote hata ukamilifu wa dahari kupitia Roho wake mtakatifu ambaye ametupa kama arabuni (guarantee) hata siku ya unyakuo na kupitia JINA LAKE.
Ili Yesu atokee katika ulimwengu wa roho na kukifanya ukitakacho itakubidi uliamini jina lake kwa kiwango kilekile unachomwamini Yeye kama angekuwepo live!

"Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika kuwa watoto wa Mungu, ndio wale WALIAMINIO JINA LAKE" (Yoh 1:2).
Mstari huu wa Biblia unaongelea na kutuonyesha "IMANI KATIKA JINA LA YESU" ambayo ni kuliamini jina lake kwa kiwango kilekile ambacho unakiamini kama Yesu angekuwepo mzimamzima!

Ukisoma Matendo 3:16, utagundua kwamba KILICHOMFANYA KIWETE ATEMBEE NI IMANI KATIKA JINA LA YESU.

Utakapoanza kuambatanisha imani yako yote KATIKA JINA LA YESU kwa kiwango kilekile ambacho ungemwamini Yesu kama ungekutana naye live, hakika miujiza mikubwa itaanza kutokea maishani mwako na kupitia maneno na mikono yako!

"Nimewaandikia ninyi mambo haya ili mjue ya kwamba mnao Uzima wa milele ninyi MNAOLIAMINI JINA LA MWANA WA MUNGU" (1Yoh 5:13).

Kumbuka uzima wa milele ni nuru iliyomo ndani ya mwamini ambayo inapong'aa gizani, giza haliiwezi na halitakuja kuiweza milele (Yoh 1:4-5).
Na huu uzima wa milele unaopindua giza uko mikononi na ndani yao WANAOLIAMINI JINA LA MWANA WA MUNGU, JINA LA YESU!

3. Elewa kwamba MAMLAKA YOTE ALIYONAYO YESU imefungwa ndani ya JINA LAKE.

Yesu alipofufuka na kuwatokea wanafunzi wake, aliwaambia AMEIPINDUA SERIKALI YA SHETANI.
Aliwaambia ANAYO MAMLAKA YOTE MBINGUNI NA DUNIANI (Mathayo 28:18).
Lakini ukisoma Biblia yako vizuri utagundua hii mamlaka yake IMEWEKEZWA KATIKA JINA LAKE.
Wafilipi 2:5-11 inatuambia kwamba:
Yesu alipokubali kutii na kujinyenyekeza hata mauti ya msalaba na kutimiza kusudi la babaye alilompa, ndipo Mungu alimkirimia JINA LIPITALO MAJINA YOTE ili kila kitu cha MBINGUNI, DUNIANI NA KUZIMU kitii na kujisalimisha kwa Yesu Kristo (kipige goti) na kikiri kuwa YESU KRISTO NI BWANA kwa utukufu wa Mungu Baba.
Hii ni mamlaka na mamlaka hii imewekwa ndani ya JINA LA YESU.

Ukielewa kuwa mamlaka yote aliyonayo Yesu imewekwa katika jina lake kama yasemavyo maandiko, itakusaidia kupandisha Imani yako na thamani yako katika jina la Yesu na litaanza kukupa matokeo kila ukilitumia.
Jina la Yesu linafanya kazi kwa wenye maarifa na siri hii.

4. Elewa kwamba jina la Yesu ni kitu halisi (ni roho) kwenye ulimwengu wa roho.

Usipoelewa kwamba jina hili la Yesu ni KITU HALISI (ROHO) katika ulimwengu wa roho, hautaweza kulitumia kufanya mambo makubwa rohoni.

Daudi alijua siri hii, alijua ya kuwa JINA LA BWANA ni kitu halisi katika ulimwengu wa roho kiasi kwamba wakati Goliati anakuja na Panga, fumo na mkuki, Yeye (Daudi) naye alichukua silaha halisi isiyoonekana kwa macho ila inayotajwa kwa mdomo, JINA LA BWANA na akapata ushindi wa kishindo dhidi ya Goliati na kuua MAKUMI ELFU YA WAFILISTI.
Kasome 1Samweli 17 utaona jambo hili kwa uwazi.

"JINA LA BWANA NI NGOME IMARA wenye haki hulikimbilia wakawa salama" (Mith 18:10).

Kwa leo niishie hapa,
Mwl Dickson Cornel Kabigumila
www.yesunibwana.org
Share on Google Plus

About Ambwene Mwamwaja

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.