HOJA: UHALIFU UTAPUNGUA KATIKA JAMII KWA KUPUNGUZA IDADI YA WAHALIFU

©Dreamstime
Jamii yetu inalalamika kwa sababu ya kuongezeka kwa uhalifu katika jamii. Juhudi nyingi zinafanyika katika kupambana na uhalifu ili kuudhibiti usiongezeke. Lakini uovu ni matokeo ya vitendo vya wahalifu katika jamii. Uhalifu unapoongezeka maana yake idadi ya wahalifu nayo imeongezeka. Ndiyo maana napendekeza kwamba, njia ya kupunguza uhalifu ipo ila haitumiki. Ninakupa kisa kimoja ambacho kitakufungua macho:

Askofu Sylvester Gamanywa
“Walimu wa sheria na Mafarisayo wakamleta mwanamke mmoja aliyefumaniwa akizini. Wakamsimamisha katikati ya umati wa watu wote. Wakamwambia Yesu, “Mwalimu, huyu mwanamke amekutwa akizini. Katika sheria, Mose alituamuru kuwapiga kwa mawe wanawake wa namna hii, mpaka wafe. Sasa Wewe wasemaje?’’ Walimwuliza swali hili kama mtego ili wapate sababu ya kumshtaki. Lakini Yesu akainama akaanza kuandika ardhini kwa kidole Chake. Walipoendelea kumwulizauliza akainuka, akawaambia, “Kama kuna mtu ye yote miongoni mwenu ambaye hana dhambi na awe wa kwanza kumtupia jiwe.’’ Akainama tena na kuandika ardhini. Waliposikia haya, wakaanza kuondoka mmoja mmoja, wakianzia wazee, hadi Yesu akabaki peke Yake na yule mwanamke akiwa amesimama mbele Yake. Yesu akainuka na kumwambia, “Wako wapi wale waliokuwa wanakuhukumu kuwa mwenye hatia?’’Yule mwanamke akajibu, “Hakuna hata mmoja Bwana.’’Yesu akamwambia,“Hata Mimi sikuhukumu. Nenda zako, kuanzia sasa usitende dhambi tena.’’ (YH.8:3-11)

“Wahalifu wa siri” wanapo watuhumu “wahalifu waliofichuliwa”

 

Unaweza kusema kuna tofauti gani kati ya “wahalifu wa siri” na “wahalifu waliofichuliwa” Tofauti `iko katika misemo ya misamiati. Maana ya wahalifu wa siri ni matendo yao maovu yanaendelea sirini, faraghani, au kwa mbinu za hali ya juu zilizofichika.

Na “Wahalifu waliofichuliwa” ni watu wale ambao matendo yao maovu yamejulikana hadharani kwa ushahidi usio na shaka upo. Lakini ukweli wa mambo, ni kwamba, bado hawa wote ni “wahalifu tu” kwa sababu ya ubaya wa maovu yao ule ule wenye madhara yale yale, isipokuwa tu “madhara ya maovu yaliyotendwa kwa siri” athari zake zaweza kujuliakana hadharani peke yake pasipo kujulikana chanzo chake.

Lakini kwa kesi yetu hapa ni mazingira ambayo, uhalifu wa aina moja unapotendeka, wanaokamatwa na kuhukumiwa kwa hatia ni baadhi tu, lakini wengine wanaendelea na uhalifu kama kawaida. Mfano halisi hapa ni wa Mwanamke alikamatwa akizini. Hapakuwepo na shida kumleta kwenye mahakama ya sheria ya torati kwa sababu “ushahidi wa zinaa” ni pale analipokutwa akizini. Kumbuka kwamba, amri ya Torati inakataza mwanamke aliyekwisha kuolewa kujamiiana na mtu mwingine ambaye si mume wake. Na adhabu ya kosa hilo ni “kupigwa mawe hadi kufa”!

Mahali ambapo sheria hii haikuzingatiwa katika kesi hii ni pale ambapo, aliletwa mhalifu mmoja tu, na mhalifu wa pili hakuletwa mahakamani. Aliletwa mwanamke tu. Kumbuka zinaa lazima itendwe na watu wawili. Mwanamke na mwanamume. Hapa aliletwa mwanamke tu, lakini mwanamume hakujumuishwa. Na hapa ndipo kuna “double standards”! Unamshitaki mmoja na kumwacha mwingine aliyestahili hukumu ile ile.

Pengine hii haitoshi kufikisha ujumbe wangu hapa. Kwenye kesi wakuu wa dini ya kiyahudi, ndio waliokuwa wamemleta hukumuni mwanamke aliyekamatwa akizini. Na walikuja kwa kishindo huku wakiweka bayana ukweli wa kisheria kuhusu sheria iliyovunjwa na adhabu iliyowekwa na Musa. Wao wakijifanya wasimamizi wa sheria ya Musa walitaka kuona kama Yesu atakwepa, au kuipinga sheria isichukue mkondo wake kwa ajili ya kuadhibu uhalifu uliofanyika.

Yesu naye hakutaka kuingia katika mtego wao kirahisi. Kwa kuwa aliwajua unafiki wao, na kwa kuwa aliwajua kuwa na wao pia ni “wahalifu wa siri” akaamua kuweka mtego wa kuwanasa pale pale. Badala ya Yesu kupingana na matakwa ya sheria, akatoa idhini kwa mtu anayejitambua kwamba yeye si “mhalifu wa siri” mwenye kutenda uhalifu wa aina ile ile: basi ajitokeze wa kwanza na kumpiga mwanamke mzinzi mawe, ili kutimiza sheria.

Kama tulivyosoma matokeo ya kisa, ni kwamba, hakuna hata mmoja, aliyethubutu kumtupia jiwe Yule mwanamke aliyeletwa hukumuni kwa Yesu! Huu ulikuwa ni ushahidi usio na shaka kwamba, “hawa wakuu wa dini ya kiyahudi, wote walikuwa ni wazinzi”! Wote walikuwa na hatia ya uhalifu ule ule wa mtuhumiwa waliyekuwa wakidai ahukumiwe kwa mujibu wa sheria.

Kama nilivyotangulia kusema awali, ya kwamba, “wahalifu wa siri” wanaposhinikiza hukumu ya adhabu itendeke dhidi ya “wahalifu waliofichuliwa hadharani” lakini watu wenye kuleta mashtaka dhidi ya uhalifu; wao wenyewe wanastahili hukumu ile ile na wao.

Wakuu wa dini ya kiyahudi, pamoja na kwamba walijulikana hadharani kwamba, ni wachaji Mungu na ndio wa kuigwa kwa mfano wa maisha ya uchaji Mungu; kumbe wao ndio walikuwa vinara katika kuendesha maovu lakini mafichoni.

Tafadhali tusitoke nje ya mada. Msingi wa mada sio “kuwatetea na kuwalinda wahalifu” ili waendelee na uhalifu wao katika jamii pasipo kuchukuliwa hatua. Kumbuka sheria inayotajwa hapa ni sheria iliyowekwa na Mungu mwenyewe kwa hiyo haina mjadala hata kidogo.

Msingi wa mada hii, ni kuweka bayana unafiki uliokithiri wa “wahalifu wa siri” wenye kufanya maovu yenye kuleta madhara makubwa kwa jamii, lakini hao hao ati ndio “wanaharakati wa kukemea maovu yanayofichuliwa hadharani”!

Hapa ni muhimu turejee kwa Yesu jinsi alivyoamua utata wa kesi. Alisema “yeye ambaye hana dhambi” na awe wa kwanza kumpiga jiwe mwanamke mzinzi. Washtaki wote waliondoka bila kuaga na kumwacha mwanamke peke yake na Yesu. Msingi wa mada hapa ni kuturejesha kwenye uhalisia wa mambo hasa

Ufumbuzi ni kufuta uhalifu kwa kuwabadili wahalifu

 

Yesu akainuka na kumwambia, “Wako wapi wale waliokuwa wanakuhukumu kuwa mwenye hatia?’’Yule mwanamke akajibu, “Hakuna hata mmoja Bwana.’’Yesu akamwambia,“Hata Mimi sikuhukumu. Nenda zako, kuanzia sasa usitende dhambi tena.’’ (YH.8:10-11)

Kwanza kabisa, tunamwona Yesu kama vile hajali kuhusu dhambi iliyotendwa na mwanamke. Wala hatumwoni Yesu akihangaika kumhoji kwanini alifanya dhambi ile na kuhatarisha maisha yake. Uamuzi wa Yesu kwa mwanamke ulikuwa: “Hata mimi sikuhukumu. Nenda zako, kuanzia sasa usitende dhambi tena.”!

Kauli ya Yesu imejumuisha mambo mengi mazito ambayo hayakuandikwa yote kwenye kisa hiki. Jambo la kwanza ni kwamba, Yule mwanamke tayari alikwisha kujuta na kufanya uamuzi moyoni mwake kwamba, akiponyoka pale asingependa kuendelea na uzinzi. Hilo Yesu aliliona moyoni mwa mwanamke Yule. Lakini jambo la pili ni “utume” uliomleta Yesu duniani ambao sio “kuhukumu bali kuokoa”!

Wakati ule misheni yake ni “kufuta uhalifu kwa kumbadili mhalifu”, badala ya “kumhukumu mhalifu afe katika uhalifu” wake. Sheria kazi yake ni “kumwadhibu mhalifu” na sio “kumbadilisha mhalifu”! Kwa msingi huu sheria ni dhaifu na “haina msaada kwa wahalifu”, bali ni kuwaadhibu wazidi kutumikia uhalifu wao wakiwa nje ya jamii huru.

Pamoja na ukweli huu, kwa jicho la mtu yule ambaye ni “mwathirika wa vitendo vya uhalifu” uliosababishwa na “mhalifu”, asipoona kwa macho “sheria imemwadhibu mhalifu wake”; yeye bado hataridhika nafsi mwake kwamba haki imetendeka. Lakini ukweli wa mambo ya kiroho ni mpana sana, kwa sababu kila mtu pasipo msaada wa Yesu, ni mhalifu anayestahili kuadhibiwa kila siku kwa sababu ya kukosea sheria kila siku.

Kwa hiyo hisia ya kutaka haki itendeke kwa wengine inaweza kuwa ni ubinafsi tu wa wengine waadhibiwe lakini yeye aachiwe, asamehewe, asihukumiwe kwa makosa yale yale ambayo alikosewa yeye na kutaka wahalifu wengine wahukumiwe kisheria.

Lakini tukirejea kwa uamuzi wa Yesu, yeye mtazamo wake na utume wake ni kutoa ufumbuzi wa kudumu kwa habari ya uhalifu. Ufumbuzi kamili, ni “kumbadilisha kitabia mhalifu” aondokane na kasumba ya uhalifu ambao unamwendesha kama mtumwa wa hulka mbaya.

Tamko la Yesu kwa yule mwanamke lilikuwa: “…kuanzia sasa usitende dhambi tena.”! Kwa tamko hili mwanamke yule hakuwa tena “mzinzi” mbele za Mungu na jamii. Pili, alipokea uwezo wa “kutokuzini tena”! Yesu asingeliweza kumpa agizo ambalo halina uwezo wa kulitekeleza. Na hii ndiyo neema iliyoletwa na Yesu badala ya sheria iliyoletwa na Musa.

Sheria ilifunua na kuadhibu uhalifu, lakini haikuwa na uwezo wa kumbadili mhalifu asitende uhalifu. Neema ya Yesu imekuja na uwezo wa kumbadili mhalifu asifanye uhalifu tena! Laiti ujumbe huu ungeeleweka kama ulivyo kwa wenye mamlaka ya kufanya maamuzi katika jamii. Wangeliufanyia utafiti ujumbe huu na kuona unaweza kuleta mabadiliko makubwa kiasi kwa habari ya kupambana na uhalifu.

Kazi ya sheria ni kudhibiti uhalifu, kwa maana ya kuuadhibu lakini sio kuuzuia kabisa usitendeke. Uhalifu ni uharibifu wa kitabia kwa sababu ya mkengeuko wa kimaadili. Hakuna sheria yoyote iwe ya kijamii au kimataifa inayoweza kumbadilisha mhalifu kitabia. Ila kazi yake ni kuadhibu.

Nini tunachokihitaji katika jamii? Ni kukoma kwa uhalifu usiwepo! Ufumbuzi wake ni nini? Ni “kubawadilisha wahalifu kitabia wasifanye uhalifu” tena. “Wenye dhambi wakitubu kwa Yesu husamehewa na kupokea uwezo wa kutokutenda dhambi tena.”

Kwanini tusiwahamasishe “wahalifu wa siri”, wanaoendelea na uhalifu kwa siri, wajisalimishe kwa Yesu, kwa nia ya kutaka kuacha kabisa uhalifu, watubu kwake kisha awape uwezo wa kutokutenda uhalifu tena!
mwisho

Share on Google Plus

About Gospel Kitaa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.