SOMO: SUBIRA NDANI YA KRISTO NI NJIA YA KUFANIKIWA

” Subira hufanya mtu kutunukiwa cheti baada ya kumaliza hatua fulani” Mtumishi Gasper Madumla ( wa kushoto ) akitunukiwa cheti cha kuzuru maeneo ya kihistoria ya kibiblia nchini Uturuki,Misri na Israeli.

~ Subira ndani ya maisha yetu ya wokovu ni jambo la muhimu sana,sababu hatuwezi kuvuka kama hatuna SUBIRA.Musa anawaambia wana wa Israeli wasimame tu,hao wamisri wanaowaona hawatawaona tena(Kutoka 14:13). Musa anawaambia wasimame,

yaani wakaze mwendo,

Wasonge mbele,wawe na Subira kwa Bwana,nao watamuona Mungu akiwatendea mambo ya ajabu.

Watu wengi tunapenda kufanikiwa katika nyanja tofauti tofauti,lakini kama tutakosa kuwa na subira tukizidi sana kutumika vizuri bila lawama mbele za Bwana,basi ni dhahili kabisa hatutafanikiwa. Ipo siri kubwa ndani ya subira.

Wengi wamemuona Bwana akiwatendea pale walipoamua kuvuta subira.

Na pia wengi,wamepoteza miujiza yao kwa kushindwa kusubiri tu.

Imeandikwa ;

” Zamani za Herode, mfalme wa Uyahudi, palikuwa na kuhani mmoja, jina lake Zakaria, wa zamu ya Abiya, na mkewe alikuwa mmojawapo wa uzao wa Haruni, jina lake Elisabeti.

Na wote wawili walikuwa wenye haki mbele za Mungu, wakiendelea katika amri zote za Bwana na maagizo yake bila lawama.

Nao walikuwa hawana mtoto, maana Elisabeti alikuwa tasa, na wote wawili ni wazee sana. ” Luka 1:5-7

Bwana Yesu asifiwe…

Zamani za Herode,mfalme wa Uyahudi,kuhani alikuwa akiingia patakatifu pa patakatifu mara moja kwa mwaka. Kuhani ambaye ameangukiwa na kura,ilimbidi ajitakase yeye kwanza kabla ya kuwatakasa kundi kubwa la watu linalomsubiri nje ya hekalu la Bwana.

Zakaria alifuata taratibu iliyokuwepo ya kuingia mahali patakatifu pa patakatifu tena alikuwa ni mtu mwenye haki mbele za Bwana,hivyo kwa lugha nyingine Zakaria alifiti kuingia patakatifu pa patakatifu huku watu walimsubiri nje ya hekalu kama ilivyo desturi ya kiyahudi.

Zakaria na mkewe Elisabeti walikuwa watumishi wa Mungu wenye SUBIRA.

Hivyo,

Zakaria na Elisabeti walihudumu ndani ya Bwana kwa subira bila lawama yoyote hali hawana mtoto tena ni wazee sana. Utumishi wa namna hii si wa kawaida hata kidogo,sababu leo tumeona wengi wakimnungunikia Bwana Mungu.

Ndiposa nimejifunza baadhi ya mambo ndani ya maisha yetu ya wokovu,kwamba;

◇ Unaweza ukawa mkamilifu mbele za Mungu,lakini ukapewa mwiba

~ Zakaria alimwelekea Bwana Mungu lakini papo hapo mkewe alikuwa tasa. Utasa ulikuwa ni kama mwiba,tena kipindi kile utasa ulikuwa ni jambo la aibu kwa mwanamke, tazama asemavyo Elisabeti

” Hivi ndivyo alivyonitendea Bwana katika siku zile alizoniangalia ili kuniondolea aibu yangu mbele ya watu. ” Luka 1:25

◇ Ukitumika vizuri mbele za Bwana pasipo lawama yoyote ile,basi tegemea kufanikiwa kwako katika kila nyanja.

~ Zakaria na mkewe Elisabeti,hawakuona faida yoyote ya kulalamika kwa kutopata mtoto.

~ Zakaria hakuona kutokuwa na mtoto ni kitu cha kushikamana nacho,bali alijua jambo moja kwamba amtumikie Bwana Mungu tu.

◇ Haitakiwi kujihesabia haki,

~Ikiwa mtu atajihesabia haki,basi ni dhahili atafanana na tabia ya Farisayo. Mafarisayo hupenda kujikweza,tena hunena pasipo kutenda. Tazama mtu mwenye kujihesabia haki;

” Yule Farisayo akasimama akiomba hivi moyoni mwake; Ee Mungu, nakushukuru kwa kuwa mimi si kama watu wengine, wanyang’anyi, wadhalimu, wazinzi, wala kama huyu mtoza ushuru. Mimi nafunga mara mbili kwa juma; hutoa zaka katika mapato yangu yote. ” Luka 18:11-12

Lakini Zakaria na mkewe hawakujikweza,ingawa wao walikuwa ni wenye haki mbele za Mungu.

Haleluya…

Nasema haleluya…

” Subira ndani ya kristo ” ni hali ya uvumilivu ndani ya maisha ya wokovu. Wokovu ni mchakato wa maisha halisi yenye ushindi dhidi ya nguvu za giza. Ndani ya maisha haya,tunahitaji SUBIRA/UVUMILIVU WA HALI YA JUU.

~ Labda pata picha hii,kama Zakaria angelikuwa ni mmoja wa waamini wa sasa. Hivi unafikiri angeombaje katika hali ile ile aliyonayo Zakaria. Labda angelingangana kila siku kwa kuomba apate mtoto kiasi cha kushindwa kuomba mambo mengine ya kiroho.

~Uvumilivu ni sehemu ya tunda la roho;

” Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu,” Galatia 5:22

~Uvumilivu pia ni moja ya tabia ya Mungu wetu. Mungu anatupenda mno na kutuvumilia sana kupita hata maelezo ya kibinadamu. Biblia inasema Mungu aliupenda ulimwengu hata akamtoa mwanae wapekee,ili kila atakaye mwamini Yesu awe na uzima.,. Hakutaka kuadhibu mara moja bali alituvumilia akamtoa mwanaye wa pekee.( Yoh.3:16)

Mafanikio ya kuzaliwa kwa Yohana (mbatizaji) yalitokana na kiwango cha subira ya utumishi wa Zakaria na Elisabeti,ingawa pia yapo makusudi mengi ya Mungu.

Alikadhalika,mafanikio yako ya kiroho hata ya kimwili yamefichwa ndani ya SUBIRA KATIKA KRISTO YESU.

◇Ibrahimu na Sara,wanatufundisha pia habari ya kuwa na subira kwa BWANA MUNGU.

Watu hawa (Ibrahimu na Sara) hawakuchoka kutumika kwa kazi ya Mungu bila lawama. Wala hatusikii kukata tamaa kwa aina yoyote,bali tunaona jinsi Ibrahimu akisimama imara na Bwana Mungu wake hata akapewa Isaka kwa SUBIRA.

Wapo wengi waliofanikiwa pale walipotia ufahamu wa kusubiri.

Siku ya leo,watu hupenda kupata mambo haraka haraka pasipo kuwa na subira. Tatizo limelikumba kanisa la leo,ndio maana unaona wengi wakihama hama makanisa wakitafuta miujiza ya fasta fasta. Sijui kwako mpendwa kama una SUBIRA NDANI YA KRISTO.

Wengine waombapo wakitaraji kupokea siku hiyo hiyo,na wasipopokea hufa moyo!

Ikumbukwe kuwa;

Bwana Mungu wetu ni mwaminifu, Yeye hujibu,hachelewi wala hawai.

Haleluya…

Hata waswahili husema;

Subira yavuta heri.

Napenda nikusihi; Uwe na subira kwa Bwana,huku ukiwa unatumika mbele yake pasipo lawama yoyote ile kama vile Zakaria na Elisabeti walivyotumika mbele za Bwana MUNGU. Haijalishi unapitia jambo gani,

Iwe ni umaskini,

Iwe ni hitaji la kuoa au kuolewa,

Iwe ni ugonjwa,

Iwe ni mateso yoyote ile,BALI MSUBIRI BWANA ATAKUTENDEA,MSUBIRI TUU.

Napenda pia nikutie moyo katika maombi kwa kunipigia namba yangu ya simu hii;

0655-11 11 49.

Blog = Njia kweli na uzima

UBARIKIWE SANA.

Share on Google Plus

About Ambwene Mwamwaja

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.