TUNAWEZA KUBORESHA ZAIDI CHAGUZI ZIJAZO, TUWE MAKINI


Jumapili ya tarehe 14, ilishuhudiwa maelfu ya wananchi wakijitokeza kupiga kura kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa/vijiji, ambapo wajumbe wa serikali pamoja na wenyeviti walichaguliwa. Hongera kwa kila aliyechaguliwa, na pole kwa kila aliyeangushwa, ila yote kwa yote tunaamini ushirikiano utakuwepo kwa ajili ya kuwaletea wananchi maendeleo.

Wakati zoezi likiendelea, GK ilizungukia baadhi ya vituo jijini Arusha na kushuhudia namna zoezi linavyoendelea, ambapo jambo la kwanza linalopongezwa ni kujitokeza kwa watu, vijana kwa wazee - kutumia haki yao ya Kikatiba kuchagua viongozi stahiki. Pongezi hizi pia zivifikie vyama vya siasa kwa juhudi za kuelimisha wananchi wapate kujitokeza siku ya upigaji. Yawezekana kabisa mhusika kutoka chama A alihamasisha wananchi, lakini wakaenda kupiga kura kwa ajili ya chama B. Kikubwa hapo tumeangalia hamasa, na hapo ni heko kwa wote waliowakumbusha wananchi kujiandikisha na kisha kwenda kupiga.

Pamoja na hayo, kuna changamoto ambazo ni sharti serikali ikazishughulikia ili kuziepuka kipindi kijacho, ili kuweka mambo sawa kwa wanancho. Baadhi yake ni kama ifuatavyo, kama ambavyo GK imeshuhudia kwenye vituo mbalimbali.

1. Msimamizi mmoja kwa wananchi chini ya 1000

Kuna baadhi ya maeneo yalionekana dhahiri kwamba msimamamizi amezidiwa na idadi ya watu, na kwa mujibu wa maelezo ambayo GK imepata kutoka vituoni, serikali ilipanga msimamizi mmoja kwenye kituo ambacho waliojiandikisha walikuwa chini ya watu 1000. Hiyo ina maana kwamba kama kituo kimeandikisha wapiga kura 800, basi watakuwa na msimamizi mmoja tu. Na kuanzia 1000, basi hapomkutakuwa na wasimamizi wawili. Shida ikatokea baasa ya watu kumalizana na ratiba ya ibada pamoja na sherehe mbalimbali zilizokuwepo na kisha kuelekea vituoni, hapo ndipo msururu wa watu ukawa unaongezeka ilhali muda nao umeyoyoma. Hili lingeweza kuepukika kwa kuwa na wasimamizi wawili.


2. Upigaji wa kura maeneo ya nje
Sehemu nyingine za upigaji wa kura zilikuwa nje, mathalani chini ya miti. Hapo pia kuna hatihati ya kuvurugika kwa shughuli nzima, ikizingatiwa kwamba kama mvua ingenyesha, basi zoezi ingebidi liahirishwe na kurejewa upya ndani ya siku saba. GK imeshuhudia wananchi kwenye kituo kimojawapo wakiangukiwa na manyunnyu, lakini pamoja na hayo, hawakukata tamaa na kueleza kwamba watakuwepo hadi kieleweke. Ieleweke kwamba mwitikio wa watu umekuwa mkubwa kuliko miaka ya nyuma. kama mvus ingenyesha na watu kuondoka kutokana na uchaguzi kuahirishwa, basi hapana shaka siku ya kupiga kura upya kuna wengine ambao walikuwepo siku ya kwanza, hawatorudi tena.
3. Ubandikwaji wa majina

Kuna baadhi ya maeneo wananchi wamepata shida kuona majina yao, na hivyo kuanza kuhaha kutafuta huku ikibidi kumuuliza msimamizi ambaye pia kwa wakati huo anahudumia msururu wa watu, wale wenye kujua kusoma na hata wale wasiojua kusoma, ikiwemo wale wasioweza kufuata utaratibu. kama kungekuwa na utaratibu mzuri wa makaratasi ya majina kubandikwa sehemu moja inayoonekana na wote basi ingesaidia kupunguza msongamano usio na lazima. Pamoja na hayo, kuna maeneo makaratasi yalishaanza kuchanika ama majina kufutika na hivyo kutoonekana. Hili limekuwa kikwazo kwenye maeneo mengi.

4. Uchapishaji wa makaratasi
Kama kuna uzembe wa hali ya juu umefanyika, basi ni kwenye uchapaji wa majina ya wagombea. Kuna sehemu majina yamechanganywa na hivyo kupelekea kushindwa kuelewa maandalizi yote yalikuwa ni ya kazi gani. Mathalan, jina la mgombea wa chama B limeandikwa kwenye nembo ya chama A. Inakanganya. Lakini pia pamoja na hayo, kuna suala la wino na idadi ya makaratasi. Kuna maeneo ilibidi uchaguzi uahirishwe kwasababu tu makaratasi yalikuwa machache kuliko idadi ya walijiandikisha. Muda mwingine haivumiliki.


Haya na mengineyo mengi yanaweza kuepusha vurugu zisizo la lazima, ni tumaini letu kwamba yatazingatiwa kwenye chaguzi nyingine zote zinazokuja. Lakini pamoja na hayo, haina budi kutoa pongezi kwa jeshi la Polisi. Kwa awamu hii wananchi wameona kwamba kumbe jeshi liko imara. Namna walivyojitahidi kudhibiti fujo za aina mbalimbali ambazo ilikuwa zitokee. Ikiwemo ya watu ambao hawajaandikishwa kwenye kituo husika kutaka kupiga kura kwa lazima. GK ilishuhudia kwa nyakati tofauti polisi wakidhibiti hilo kwa lugha isiyokera wala isiyo na mabavu.


Kituo chako cha upigaji kura hali ilikuwaje kiujumla? Tuandikie maoni yako hapo chini... GK itakuletea picha kamili za vituo ambavyo ilizungukia. Kaa nasi.

Share on Google Plus

About Gospel Kitaa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.