HOJA: YALIYOMO KATIKA MPANGO MKAKATI WA MAADILI KWA KIZAZI

Askofu Sylvester Gamanywa

Tumefikia mwishoni mwa mwaka 2014. Huu ni mwaka wa 4 tangu tulipozindua Mpango Mkakati wa Maadili kwa kizazi kipya mnamo mwaka 2010. Kwa kuwa tunaelekea kwenye mwaka wa 5 ambao tutauingia kwa neema hivi karibu, nimeona niwakumbushe wahusika kuhusu yaliyomo katika Mpango Mkakati huo, na baada ya hapo tuone jinsi ulivyotekelezwa, kisha ndipo tuelimishanne yatakayojiri katika mwaka 2015:

UTANGULIZI

Japokuwa kuna hatua nyingi ambazo zimechukuliwa na Serikali pamoja na vikundi mbalimbali vya kijamii katika kumaliza tatizo la mkengeuko wa maadili, bado tatizo hilo limeendelea kuwa kikwazo kikubwa sana cha ukuaji wa uchumi wa nchi na maendeleo kwa ujumla.
WAPO Mission International (WMI) kwa kulitambua hilo imekuwa ikifanya jitihada kubwa kurejesha maadili kwa njia ya kuhamasisha, kuelimisha na kurejesha maadili ya kibiblia kwa mtu mmoja mmoja na kwa jamii yote kama dira yake.
Taasisi inatambua kuwa ndani ya jamii kuna watu wengi, ili kufikia maono yake ya; “Watanzania asilimia 25 wawe wamezaliwa upya na kubadilika kitabia na kuishi maisha ya maadili ya kiimani ifikapo mwaka 2028”.
Kwa kuzingatia maono haya, WMI imetoa kipaumbele kwa vijana wa kizazi kipya wenye umri 12-35 kama kundi muhimu la walengwa. Hii ni kutokana na kuwa miaka 15 ijayo ndio kizazi, kitakachokuwepo, uongozi utakaokuwa madarakani na wamilikaji wa uchumi wa Taifa hili.
Ili kufikia maono haya, WMI imeandaa mpango mkakati ambao unachangia malengo ya muda mrefu wa WMI, hasa lengo la uendeshaji wa mafunzo na maombezi kwa ajili ya urejesho wa maadili katika jamii. Mpango huu unaongozwa na maandiko yafuatayo:
 • Pasipo Maono watu huacha kujizuia (Mith.29:18)
 • Pasipo utakatifu hakuna atakayemwona Mungu (Ebr.12:14)
 • Pasipo bidii ya masomo/kazi huishia katika umaskini (Mith.10:4)
 • Anasa zisizo za kimaadili huleta umaskini (Mith.23:21; Mith.23:26-27; Mith.23:)
 1. DIRA, DHAMIRA NA MALENGO

Dira ya mpango huu ni kuwa ifikapo mwaka 2028, kizazi kipya kinachoinukia sasa kiwe kimeiva kimaadili, chenye uongozi bora na kinamiliki uchumi endelevu.
Dhamira ya mpango huu ni kuwa kufikia mwaka 2028 asilimia 25 ya vijana wa Tanzania wawe wanaoishi maisha ya maadili ya kibiblia.
Malengo ya muda mrefu ni kuendesha mafunzo ya kurejesha maadili, kuhamasisha na kuinua vipawa vya uongozi na kuhamasisha umilikaji wa uchumi wa vyanzo vikuu vya uzalishaji vya asili.


 1. MIKAKATI YA KUFIKIA MALENGO

  1. Mkakati wa Kurejesha Maadili kwa Kizazi Kipya

Maadili ya sasa yamejengwa na mengine kuboreshwa juu ya yale ya kizazi kilichopita, lakini miaka 15 ijayo kizazi kipya cha sasa kitapitia mabadiliko mengi ya ulimwengu, na mabadiliko hayo yatakuwa katika maeneo mengi na maarifa yataendelea kuongezeka tena kwa kasi, hivyo kizazi kipya kinahitaji kuwekewa msingi imara ya maadili ya kibiblia. WMI katika mkakati huu inalenga kujenga maadili ya kibiblia ambayo yataongoza maadili mengine yote ya kijamii, kitaifa na kitaaluma. Hili litawezekana kwa kushirikisha madhehebu ya dini, familia, wazazi na kuanzisha vituo vya kurekebisha tabia ya vijana mitaani. Mkakati huu umekuwa ukitekelezwa kupitia njia mbalimbali kama ilivyoelezwa hapa chini.
   1. Ushiriki wa vijana
Mkakati wa kuhamasisha maadili unawashirikisha vijana kwa njia kuu tatu:
 • Kuendesha warsha na makongamano kwa ajili ya vijana;
 • Kuunda mitandao na vikundi mbalimbali vya vijana;
 • Kuendesha semina maalumu kwa vijana.
   1. Ushiriki wa Madhehebu ya dini
Kwa kutambua nafasi ya viongozi wa dini katika suala la maadili, mkakati huu unashirikisha viongozi mbalimbali wa dini kwa njia zifuatazo:
 • Kuandaa wawezeshaji wa mafunzo ya maadili kutoka miongoni mwa viongozi wa dini;
 • Kuendesha semina za maadili kwa ajili ya viongozi wa dini wenyewe.

   1. Miongozo ya maadili ya kifamilia kwa wazazi
Kwa kutambua nafasi ya familia imara katika suala la maadili, mkakati huu unazishirikisha familia na wazazi kwa njia zifuatazo:
 • Kuendesha semina kwa wanandoa juu ya maadili ya kifamilia;
 • Kuendesha semina kwa wazazi juu ya malezi ya vijana;
 • Kuedesha semina kwa vijana juu ya uchumba hadi ndoa.


   1. Vipindi vya Redio na Matangazo
Katika kuhakikisha walengwa wa mkkati wamaadili wanafikiwa kwa urahisi mahali popote walipo, mkakati huu unafanya yafuatayo:
 • Kuandaa na kuendesha vipindi vya redio;
 • Kurusha matangazo redioni kuwaalika vijana katika makongamano, semina na warsha mablimbali.
   1. Uanzishwaji wa vituo vya kurekebisha tabia mitaani (VKTM)
Katika kuhakikisha walengwa wanafikiwa mahali popote walipo, mkakati huu unafanya yafuatayo:
 • Kujenga mawasiliano na taasisi za kimataifa zinazoendesha VKTM;
 • Kuandaa michanganuo ya kuazishwa kwa VKTM.

  1. Mkakati wa Kuandaa Uongozi wa Kizazi Kipya

WMI inatambua kuwa tafsiri ya uongozi ni pana sana lakini uongozi wa kizazi kipya utakuwa ni ule wenye uwezo wa kushawishi, wenye ubunifu, kuangalia mbele, kuonesha njia, ujasiri wa kutenda, kufahamu nia na mwelekeo, wenye kumcha Mungu, upendo na maono. Pamoja na kuwa ziko sifa nyingi za kiongozi lakini kwa ujumla wake sifa za kiongozi wa kizazi kipya atakuwa na sifa za familia, kiroho, binafsi na sifa za kutawala na kiutendaji. Mkakati huu utatilia maanani kuwaanda vijana waweze kuwa na sifa hizo, shuleni, na vyuoni ikiwemo kuwaanda wazazi wao ambao inalazimu wawe mfano kwa vijana.
   1. Uandaaji wa Mitaala mashuleni
Mkakati huu unahusisha suala la mitaala mashuleni kwa njia zifuatazo:
 • Kuandaa mitaala ya maadili kwa kushirikisha jumuia kuu na vituo vya elimu ya medhehebu ya dini
 • Kufundisha maadili mashuleni kwa kushirikisha waalimu
   1. Ujenzi wa Chuo Kikuu cha uongozi wa kimaadili
Ili kupandikiza fikra za maadili kwa kiwango cha juu, mkakati huu unalenga kujenga chuo kikuu ambapo mabo yafuatayo yamekwishafanyika:
 • Kumiliki kisheria maeneo kwa ajili ya ujenzi wa Chuo Kikuu;
 • Kuundwa baraza la MoLUT pamoja na utawala wake;
 • Kuandaa michoro na ujenzi wa Chuo Kikuu.
   1. Uendeshaji wa Shule za Msingi na Sekondari
Kwa kutambua kuwa uhamasishaji endelevu wa maadili ni lazima uanzie kwa watoto na hatimaye vijana, mkakati huu unajihusisha na uendeshaji wa shule za masingi na sekondari, ambapo mambo yafuatayo yanafanyika:
 • Kumiliki ardhi kwa ajili ya ujenzi wa shule;
 • Kuanzisha Shule za Msingi na Sekondari;
 • Kuratibu mitaala yenye maadili ya kibiblia.

  1. Mkakati wa Kumilikisha Uchumi kwa Kizazi Kipya

Kufuatana na maandiko, WAPO Mission International (WMI) inatambua vyanzo vikuu 5 vya uzalishaji mali vya asili navyo ni; ardhi, maji, mimea, mifugo, na madini. WAPO Mission International inahamasisha na kushiriki katika kuwezesha uwekezaji katika vyanzo hivi vya asili. Sababu kuu za kuwekeza katika vyanzo vikuu vya asili ni zifuatazo:
 • Uzalishaji na ukuaji wake unamtegemea Mungu;
 • Vinakidhi mahitaji ya lazima ya binadamu;
 • Vimedumu kutoka vizazi hadi vizazi;
 • Uzalishaji mwingine wote ulimwenguni unavitegemea;
 • Vinaweza kumilikiwa na kila binadamu atakaye;
 • Tanzania inao utajiri mkubwa wa vyanzo vikuu vya uzalishaji vya asili.
Ili kufanikisha adhma hiyo, mkakati huu unafanya yafuatayo:


   1. Uhamasishaji wa maadili yanayohusu uendeshaji wa miradi na huduma
Mkakati huu unahamasisha maadili yanayohusu uendeshaji wa miradi na huduma kama ifuatavyo:
 • Kuendesha semina na kongamano za maadili zinazohusu miradi na huduma;
 • Kuainisha na kutambua miradi na huduma zinazotumia maadili ya kibiblia;
 • Kutengeneza mifano ya maandiko ya miradi na huduma (Business Plans).


   1. Uundwaji wa mitandao ya vikundi maalumu vya uchumi
Mkakati huu unahamasisha na kutekeleza uundwaji wa vikundi maalumu vya uchumi, ambapo mambo yafuatayo yanafanyika:
 • Kuuunda vikundi na kanuni zinazoongoza na taratibu za uendeshaji;
 • Kuendesha mafunzo maalum juu ya tabia za vikundi;
 • Kujenga na kuimarisha mitaji ya vikundi.
   1. Umiliki wa ardhi kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji
Katika kuhakikisha kila kijana aliyeamua kubadilika kimaadili anamiliki sehemu ya ardhi na kufanya uzalishaji juu ya ardhi hiyo, mkakati huu unahusisha yafuatayo:
 • Kufuatilia, kununua na kumiliki ardhi;
 • Kushirikisha na kuingia ubia na wananchi, serikali na mamlaka husika;
 • Kutafuta vyanzo vya mitaji kutoka taasisi za fedha;
 • Kuanzisha viwanda vya kusindika mazao mbalimbali;
 • Kutafuta masoko na kuuza mazao yatokanayo na kilimo.
   1. Uundwaji wa makampuni na umiliki wa hisa katika makampuni ya madini
Ili kuwezesha vijana kushiriki katika uzalishaji na umiliki wa rasilimali madini, mkakati huu unahusisha yafuatayo:
 • Kutambua maeneo ya madini na kuonana na uongozi husika;
 • Kuunda makampuni ya vikundi vya vijana;
 • Kuingia ubia na kumiliki hisa ndani ya makampuni ya madini.


   1. Uboreshaji vipawa vya sanaa na michezo
Ili kuhakikisha kuwa vijana wananufaika na vipaji vyao ambayo ni karama kutoka kwa Mungu, mkakati huu unahusisha:
 • Kutambua vijana wenye vipawa na aina za vipawa;
 • Kuuunda mitandao na vikundi vya sanaa na michezo;
 • Kutoa mafunzo maalumu na kuwawezesha kufikia viwango vya kimataifa.
  1. Walengwa

Ili kuhakikisha kuwa mipango ya utekelezaji mpango huu na mikakati yake kwa kuzingatia mahitaji halisi ya walengwa, walengwa wamebainishwa katika makundi maalumu – kwa kila mkakati, kama ifuatavyo:
   1. Walengwa wa Urejesho wa maadili
Walengwa wahuu atika mkakati huu ni vijana wanataaluma na wafanyakazi, jumuia mbalimbali za vijana, wanafunzi mashuleni, vyuoni na vyuo vikuu, vijana wajasiriamali, vijana waishio vijijini na wasichana wanaofanya biashara ya miili yao.
   1. Walengwa wa elimu na mafunzo
Hawa ni vijana wote wenye wito wa uongozi na wana elimu ya awali.
   1. Walengwa wa kumilikishwa uchumi
Walengwa wa mkakati huu ni kama ifuatavyo:
 • Vijana wanaohitimu katika vyuo vya kati na vyuo vikuu na wanashindwa kupata ajira
 • Vijana waishio mijini kwa kufanya biashara ndogo ndogo zisizoweza kukidhi mahitaji yao Vijana waishio vijijini wenye kutegemea kilimo cha jembe la mkono peke yake
 • Vijana wajasiriamali walioanzisha miradi midogo ya biashara
 • Wanandoa na wazazi/walezi kama wadau muhimu kwa urithishaji uchumi


Itaendelea toleo lijalo


Share on Google Plus

About Gospel Kitaa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.