ALARM INAYOKUKERA NDIO INAYOKUFAA ZAIDI

Elie J. Chansa,
GK Staff Writer
©Clip Art Panda
Awali ya yote nimshukuru Mungu kwa kunipa fursa ya kuanza kuandika upya kwa mwaka 2015, ni matumani yangu kwamba atasema nawe kwa namna alivyonuia. Amen!

Juzijuzi nikiwa nimelala, nilikerwa mno na alarm ya simu niliyoitegesha mwenyewe. Maana niliiacha simu kwenye chaji, nami nikalala. Muda ulipowadia, ule muda niliopanga kuamka na kuendelea na ratiba - simu ikaanza kunikumbusha kama nilivyoipangia. Kwa kuwa nilikuwa nimechoka, nilitamani niizime simu niendelee kulala, ila nikaona kuliko niifuate kutoka kitandani – ngoja tu itanyamaza yenyewe.

Bahati mbaya sana (nzuri), simu haikukata, ikaendelea kulia kwa takribani dakika kumi bila kukata, hapa nikakereka sana na kuamua kuamka. Nikaizima na usingizi ulishatibuliwa. Lakini nikajifunza jambo hapa, kwamba hii alarm ingeamua kunibembeleza, ingekuwa alarm mbovu kuwahi kutokea, lakini kwa sababu iliendelea kutoa sauti ya juu hadi ipate mtu wa kuizima.

Kuna alarm nyingi umekuwa ukizikia maishani mwako, nawe ukaona ya kwamba ni makelele na yanakusumbua, bila kutambua kwamba hayo unayoyaona kama makelele kwa sasa, ni faida yako baadae, aidha kwa kujua ama bila kujua.

Wengine wakiambiwa jambo na mama ama baba zao, wanaona ya kwamba ni makelele, wanasahau ya kwamba mzazi ndiye aliyetangulia kuzaliwa, ana uzoefu wa kuishi zaidi yako, maana umri wake ni mkubwa, hata kama haishi Australia ama Urusi kama wewe, hata kama hajawahi kupanda ndege kama wewe, hata kama hajui kiingereza na kifaransa kama wewe, hata kama hayuko kwenye mitandao ya kijamii kama wewe, hata kama wewe ndiye uliyemfundisha kutumia 'rimoti' ya Radio, bado ana ujuzi wa maisha zaidi yako. (ili mradi akuambiacho kisikutoe nje ya Ufalme wa Mungu)

Samweli alipokuwa amelala, alisikia sauti akiitwa, naye akaenda kwa Eli, akidhani kwamba ndiye aliyemuita. Eli alimrudisha Samweli, mara ya pili ikatokea hivyo, na mara ya tatu pia ikatokea hivyo, hadi alipoelekezwa namna ya kuitikia atakaposikia sauti kw amara nyingine. Sauti ilipomjia kwa mara ya nne, Samweli aliitika kama alivyoelekezwa na Eli, ndipo hapo BWANA akanena naye. (Samweli 1:3)

Kwa Samweli, kuitikia mara zote hakuona kwamba ni usumbufu, si ajabu kwa mazingira ya sasa ulipo ungeweza kusema, "ah, huyu mzee naye mbona anasumbua hivi, naona anazeeka vibaya" kisha usiitikie tena mara ya tatu. Kumbe wakati inaonekana ni usumbufu, ndio wakati ambao kuna mema mbele yako iwapo utaiitikia sauti.

Huenda 2015 kuna alarm ambayo umekuwa ukibishana nayo, na hata kuizima kwa muda ili ikukumbushe baadae. Alarm inakuambia kwamba 2015 lazima uingie mtaani kuhubiri injili, lakini wewe unaikaidi. Alarm inakuambia kwamba lazima utoke hapo ulipo uanze biashara ndogondogo – wewe unaikatalia. Alarm inakuambia huu ndio muda wa kuwa mwaminifu kwa Mungu na matoleo yake yote, wewe unashupaza shingo. Pamoja na hilo, kuna alarm zingine hazisumbui – zikilia bila kusikika, zitaacha zenyewe. Hapo unakuwa umepitwa na jambo jema. Sauti nyingine huja mara moja tu, na kama ukiiringia basi – fursa haipo mikononi mwako tena.

Ni maombi yangu Mungu akuwezeshe kuitii sauti yake ambayo unaisikia kupitia vyombo vyake lakini unajikausha – na kujifariji kwa kukemea eti kwamba ni ibilisi huyo. 2015 ni tofauti na ulivyokuwa miaka ya nyuma. Hata leo ni tofauti na jana, anza sasa kufanya kilicho ndani ya moyo wako, na Mungu atakuwa nawe njia nzima. Amen!

+255713554153
elie@inhouse.co.tz

Share on Google Plus

About Gospel Kitaa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.