ISHARA NNE ZITAKAZOKUWEZESHA KUTAMBUA UTOFAUTI ULIOPO BAINA YA WATU

Na Faraja Naftal Mndeme,
GK Contributor.
©Mag for Women

1. IMANI
Kila imani unayoijua hapa ulimwenguni ina mfumo wake na uendeshaji wake tofauti na imani nyingine. Mpaka sasa hapa ulimwenguni kuna imani tofauti tofauti zaidi ya 3000 ambazo kila moja ina mfumo wake. Hii ni moja ya kitu ambacho kinaweza kukusaidia kutambua utofauti ulioko kati ya mtu mmoja na mwingine. Imani yoyote huwa na mfumo wa kuishi, na namna ya kuendesha mambo yake. Wanadamu tumejengwa katika misingi ya imani tofauti tofauti na pia imani hututofautisha namna na tunavyofikiria na mambo mengine kadha wa kadha. Mara nyingi unaweza ukakuta mnajaribu kuendana lakini kuna sehemu tu kwa namna moja au nyingine kunakuwa na utofauti mkubwa kwenye namna mnavyoendesha mambo yenu na namna mnavofikiria.

2. AINA YA WATU MNAOWAPENDA/MNAOWAKUBALI
Kuna wakati mimi binafsi niliishi kwenye jamii moja ya watu ambayo ilikuwa inapenda aina fulani ya watu. Kwa maana nyingine walikuwa wanawakubali sana. Haijalishi kama walikuwa wanafanya makosa au la, lakini kwa sababu wao waliwapenda basi kulikuwa hamna jinsi. Tatizo lilikuja pale ambapo nami nilikuwa tayari na watu wangu ambao nilikuwa nawakubali na kuwapenda pia lakini jamii husika ilikuwa haiwapendi na kuwakubali pia. Matokeo yake tukawa tunapishana kwenye mambo mbali mbali na muda mwingine ilinibidi nijifunze kukaa kimya la sivyo kulikuwa hakuna uwezekano wa kuafikiana kwenye maswala mbali mbali. Hii ni ishara nyingine ya utofauti uliopo katika watu.

3. AINA YA WATU MSIOWAPENDA/MSIOWAKUBALI

Kila mtu kuna mtu wake hamkubali kwa namna moja au nyingine. Kutokumkubali mtu haimaanishi kumchukia. Ukifuatilia kwenye maisha yako binafsi kuna mtu unamkubali kwenye kiwango cha juu na mwingine hata afanye nini haumkubali, na ndivyo ilivyo kwa mwingine pia; kuna watu wake anawakubali lakini kuna wengine pia hawakabali. Na watu mnaowakubali na msiowakubali mara nyingi wana ushawishi kwenye maisha yenu kwa sehemu moja au nyingine. Kuna wakati nilikutana na mtu mmoja kwenye maisha yangu siku za kale kidogo, mtu huyu nilikuwa nikimwambia tendwe sehemu fulani alikuwa anatoa visingizio kadha wa kadha au tukienda naye mimi nitafurahi sana uwepo wa lile eneo wakati yeye haoni kama kuna furaha. Baada ya muda kupita niligundua kwamba aina ya watu ambao nilikuwa naenda kuwaona yeye wala, na mara nyingi tuliishia kupishana sana kimtazamo. Unaweza ukawa unapishana sana na mtu bila wewe kugundua haraka. Namna ya kujua hili anagalia watu asio wakubali na wewe unao wakubali ukiona kuna utofauti mkubwa ujue mtapishana kwa sehemu kubwa na msipokuwa makini mnaweza kugombana mara kwa mara.

4. VIPAUMBELE
Je unawezaje kutambua vipaumbele vya mtu? 1. Muhusika anaweza akakuambia 2. Angalia Muda anaoutumia kwenye masuala mbalimbali. Kitu chochote mtu anachokifanya zaidi ya saa moja kwa siku, hicho ni moja ya kipaumbele chake. 3.Matumizi ya fedha zake. Utakuta Mwingine asilimia kubwa ya fedha anatumia kwenye mavazi au simu, vitabu, n.k. Kila mtu kwenye maisha ana vipaumbele mbalimbali, unaweza usigundue moja kwa moja lakini unaweza ukavitazama kwa namna nyingine pia. Hii ni moja ya ishara kubwa sana, na mara nyingi humtofautisha mtu moja na mwingine. Mtu anapokuwa na vipaumbele kwenye maisha yake basi hata mfumo wa maisha yake huyajenga kuendana na vipaumbele vyake. Muda anavyoutumia na rasilimali zake anavyotumia pia. Mtu huyu huwezi kumgeuza mkaendana kwenye jambo lolote kama haukuweza kugeuza vipaumbele vyake kwenye maisha yake. Mnaweza mkawa mnagombana au kuwa na ubishi usikuwa na mwanzo wala kikomo kumbe tatizo ni aina ya vipaumbele mlivyo navyo maishani mwenu.

HITIMISHO.
Kuna aina nyingi ya ishara ambazo unaweza ukawa unazifahamu ambazo zinaweza kukusaidia kutambua utofauti uliopo kati ya mtu moja au mwingine. Lengo la kujua utofauti huo ni kuweza kukusaidia kujenga mahusiano mazuri na ambayo yataweza kukusaidia kufanikiwa maishani kwenye masuala mbalimbali. Kabla haujamkaribisha mtu maishani mwako akawa rafiki au akawa mtu wa namna yeyote ile kwenye masuala mbali mbali, tafuta kujua kwanza utofauti mliyo nayo ili uweza kujua namna ya kuishi naye au kuachana naye. Usiweke mtu kwenye maisha yako ambaye unajua kwa asilimia kubwa mna tofauti ambazo haziwezi kurekebishika, matokeo yake mnaweza mkawa mnapishana kila siku kwenye maswala mbalimbali na mnaweza msiwe na mwisho mzuri.

E-mail:naki1419@gmail.com
+255788454585
God Bless Y’All
Share on Google Plus

About Gospel Kitaa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.