KUKOSA MAONO NI SABABU YA KUSHINDWA KWAKO (1)

Mwalimu Kelvin Kitaso,
GK Guest Writer.


Maono ni kama kesho ya mtu.
Kesho ni siku ambayo hutarajiwa na haijaonekana bayana bado, na hakuna mwanadamu yeyote chini ya jua aijuaye kesho yake ipoje, isipokuwa amejuzwa na Mungu ajuaye mambo yote kabla hayajatukia. Kesho ni siku ambayo ni matokeo ya kile kitu ambacho kimefanyika leo; kesho huandaliwa ndani ya leo, Mungu ndiye hutoa jawabu kama iwe kama vile ulivyoiandaa.
Kuna msemo wa Kiingereza usemao, “Yesterday has passed, today is here, tomorrow never come” hii inaonyesha kuwa katika maisha yote ya mwanadamu kuna siku tatu tu yaani jana, leo na kesho na mwanadamu anapaswa kuzitumia siku zote hizo kwa faida yake mwenyewe na kunufaisha jamii inayomzunguka pia.
Jana ni siku ambayo imepita na hukutengenezea uzoefu (CV) ambao waweza kuwa mzuri au mbaya na kamwe hautoweza kurudi jana kuibadilisha jana yako ila unaweza kuitumia Leo kuifanya kesho isije kuwa kama jana. Jenga tabia njema ya kutojisifia kwa mazuri uliyofanya jana kwa kuwa kujisifia kutakufanya ujisahau kuwa unapaswa kusababisha mambo makubwa kutokea tena na tena kamwe usijaribu kujilaumu kwa vile ulivyoshindwa jana kwa kuwa itakufanya uwe muoga wa kujaribu kufanya mambo makubwa leo. Lakini mazuri ya jana yanaweza kutumika kama marejeo; kama jana nilishinda basi na leo pia naweza kushinda kama ilivyokuwa kwa Daudi aliporejea kuua simba na dubu alipotaka kupambana na Goliathi.
Kesho ni mimba ambayo imetungwa leo na yapaswa kujifungua. Ni muhimu sana kuzingatia ili kuweza kujifungua mtoto aliye mzuri na hii inatokana na mimba hiyo imetungwaje na katika hali gani. Kujifungua mimba hii kunahitaji nguvu ya mbeba ujauzito na pia Mungu akusaidie kujifungua salama.
Kesho ni ahadi ambayo imetoka kwa Bwana kwa kuwa ahadi ni mambo yatarajiwayo na hayajaonekana bayana bado, hapa ninazungumzia zaidi ndoto au maono ya mtu ambayo ndiyo kesho yenyewe na hutarajiwa kutimia na hayajaonekana bayana bado.
             Kitu chochote unachokifanya leo kinaonyesha kuwa kesho yako itakuwaje.

Ni lazima uione kesho yako ukiwa leo kwa kuwa kesho yako inategemea sana na wewe unaona nini ndani yako mwenyewe ukiwa leo, na si kuona tu. Pia unakiri nini kwa kuwa kuna nguvu katika ukiri wa maneno. Na si ukiri tu, bali ni nini ukifanyacho leo kinaweza kuitimiza kesho yako. Kitu ukionacho ndani yako, ukikiricho na hata kukifanya hugeuka kuwa tabia. Na kikiwa tabia mwishoni uja katika uhalisia wa utimilifu wake.
Kesho yako haitakuja kama muujiza, yaani umeamka na kuiona tu inatimia, hapana. Ni mchakato mrefu ambao unakuhitaji mwamini kutia juhudi za kutosha ili iingie kwenye utimilifu wake. Kama haujaanza kuwaza kuwa kesho yako itakuja kuweje kamwe usijedhania kama kitakuja kutimia kwako kitu ambacho hujawahi kukiwaza hata siku moja, mtu anaweza kuhangaika na kitu ambacho amewahi kukiwaza hapo awali kuliko kile kitu ambacho hajawahi kuwaza kabisa. 
Lazima uione ndani yako kwanza. Mwanadamu huwa vile anawaza ndani yake kwa kuwa lile wazo humpa  hamasa ya kufanya kazi ili litokee, na wazo pia la ndani yake huweza mfanya kukata tamaa ya kufika mbali. Mtu mmoja akasema, kuwaza ni kuwaza tu kama umewaza mambo makubwa au madogo ni bora ukawaza vitu vikubwa labda waweza kuwa mtu mkubwa. Lakini kuwaza tu pasipo kuchukua hatua hakufai.  
Mithali 23:7 “7 Maana aonavyo nafsini mwake, ndivyo alivyo.” Yaani ukitangulia tu kuona kuwa wewe ni maskini mkubwa ni lazima uwe, ni lazima ujifunze kuona vyema. Watu wakubwa duniani kabla ya kuwa vile walivyo, walitangulia kuona ukubwa ndani yao kwanza na kisha wakaanza kufanya kazi kwa kuwa ile picha waliyoiona ndani yao huwatesa kuifikia. 
Katika Biblia, neno ‘unaona nini?’ limeonekana mara saba na siku za wiki zipo saba, ina maana ya kusema kila asubuhi BWANA uweza kukuuliza ‘unaona nini?’ mpaka zikaisha siku saba za wiki na itakapoanza Jumatatu ataanza na unona nini? tena mpaka Ijumaa huku akiunganisha na neno usiogope kwa kila siku uionayo katika uwepo wako duniani.
Kofi Annan ambaye ni katibu mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa baada ya kuingia UN katika nafasi ya kawaida tu akamwandikia mama yake ujumbe na kumtaarifu kuwa siku moja ni lazima aje kuwa katibu wa Umoja wa Mataifa. Alivyoona ndivyo ilikuja kutokea na kule kuona kwake kulimlazimu kutotulia na kuwa na juhudi kubwa sana ili baadae aje kuwa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa.
Kama kuna picha tayari unaiona ndani yako ya jinsi vile unavyopaswa kuwa ni muhimu sana kuzingatia kuwa picha ile ni nguvu ya kukufanya upigane hata kuitimiza; ila mbaya zaidi ni kwa mtu asiye na maono kwa kuwa hana picha ndani yake. Ni vigumu kwa yeye kufanya kitu cha msingi.
Maandiko yanasema katika Mithali 28:19 kuwa “18 Pasipo maono, watu huacha kujizuia”,  tafsiri ya asili ya Kiebrania kutoka katika neno ‘hazon’ hutafsiri maandiko haya kwa kumaanisha mafunuo ya neno la Mungu, na huendelea kwa kumaanisha kuwa pasipo neno la Mungu kufunuliwa kwa watu ni lazima watu waende katika njia ya upotevuni. Mahali popote ambapo neno la Mungu halijafunuliwa ni lazima watu waangamie na kuendelea katika njia zao wenyewe kwa kuwa bado huwa kwenye mabano ya wafanye kipi na kuacha kipi. 
Kwa kuangalia maono pia mtu yeyote ambaye hajafunuliwa ni maono gani alionayo ni kazi sana kuwa katika njia sahihi. Jamii inayotuzunguka watu wengi hukosa maono na ndiyo maana huishia kufanya vitu vya ajabu sana. Maono ni ile picha ya ndani aionayo mtu kwa habari ya kesho yake na kama mtu haoni picha yoyote ndani yake ni vigumu kufanya vitu vya msingi vya kimaendeleo.
Mtu mwenye maono hata kama anaonekana maskini kwa wakati huo ni mtu wa tofauti kwa kuwa maono ni muongozo wa utendaji kazi wa mtu huyo na ni lazima afanye mambo ambayo yanapelekea utimilifu wa maono hayo na huishi maisha ya kujizuia katika mambo yoyote ambayo hayamsaidii kufikia mwisho wake. Mtu mwenye maono hawezi kutulia hadi maono yake yawe yametimia.
Maono hutoa muongozo wa jinsi mtu apasavyo kuwa na hata jamii ya kushirikiana nayo.

Nikiwa sehemu Fulani nahudumu baada ya huduma nikamuuliza kijana mmoja unataka kuja kuwa nani? yule kijana akanambia nataka kuja kuwa dereva na alikuwa anasoma na nilipomuuliza kwa nini anataka kuja kuwa dereva akanambia ni kwa sababu wazazi wake hawana uwezo wa kumuendeleza kimasomo, nilitafakari kuwa mtu huyu anataka kuja kuwa dereva kwa ajili ya hali ngumu ya kiuchumi, ni vizuri, ila katika mazungumzo nikagundua kuwa amekata tamaa ya kufanikiwa zaidi kwa sababu ya hali yake ila mwenye maono hata kama ana hali ngumu kamwe hatoacha kuukiri ushindi wake kuwa pamoja na ugumu uliopo ninaweza nikafika pale napokusudia na hata kama nitachelewa kulingana na vikwazo vya hali niliyonayo sasa ila nitahakikisha nimefika.
Pamoja na kuwa mfanya kazi wa ndani kwa Potifa na kisha kupelekwa gerezani na kuwa mfungwa, bado Yusufu aliendelea kuitazama na kuikiri ndoto yake ya kuja kuwa mtu mkubwa. Mazingira mabaya na ya kukatisha tamaa hayakumfanya Yusufu akate tamaa na kubadilisha aina ya ndoto. Ni ukweli sana kuwa ugumu wa maisha ni sababu kuu sana ya kusababisha watu kuyaacha maono yao ya uhalisia na kuingia katika mengine ambayo si maono yao.
Mtu asiye na maono ni lazima mambo yake yawe hovyo hovyo kwa kuwa hakuna mwongozo sahihi unaoweza kumzuia asifanye yale ambayo anataka kufanya. Maono ni muongozo kwa mtu mwenye nayo katika mambo yote na humuongoza kuwa sehemu sahihi kwa wakati sahihi na kuwa na watu sahihi. Na ni nadra sana kumkuta mtu mwenye maono anafanya mambo ambayo hayawezi kumsaidia kufikia utimilifu wa maono yake.
Ni muhimu sana kwa mtu kuiona kesho yake ndani yake na aione katika uzuri ndipo anaweza tumia muda wake vizuri kutimiza yale ayaonayo. Kuona ni jambo jema sana ila mtu aweza ogopa kuwaza mambo makubwa na hii utokana na mtu kujidharau na kuona kuwa ana uwezo mdogo sana ndani yake, hili ni tatizo la kiimani, kutojitambua na kujidharau; ni lazima utoke kwenye eneo hili la kukosa kutokujiamini na uanze kuona kuwa unaweza.
Maono makubwa, huleta taabu kubwa, (The greater the revelation, the greater tribulation)

Wakati Fulani nikiwa na rafiki yangu akanena na kunambia “the greater revelation, the greater tribulation,” akimaanisha kuwa ‘maono makubwa huambatana na taabu kubwa). Ukifuatilia kwenye Biblia utaona kuwa watu wote waliobeba maono makubwa ndio watu waliopata taabu kubwa hata utimilifu wa maono yao. Usikate tamaa unapoona majaribu yamekuwa ni makubwa sana kwa upande wako, kaa utulie huku ukitafakari kuwa ni uzito wa maono uliyonayo ndiyo sababu kuu ya kuteseka kwako.
Mfano ni Mtume Yohana aliyepata maono ya kitabu cha Ufunuo akiwa katikati ya mateso makubwa na kuwekwa katika kisiwa cha Patmo na Mtume Paulo ambaye alipata mateso makubwa kulingana na ukubwa wa maono aliyokuwa amebeba.
Kwani wao waweze wana nini na sisi tushindwe tuna nini?
Katika jamii ya waswahili huu ni msemo ambao umekuwa ukitumika sana na ni miongoni mwa misemo ambayo imejipatia umaarufu mkubwa sana. Ni kweli kuwa wapo watu wafanyao mambo makubwa na yakatokea lakini wengine ushindwa kufanya mambo hayo. Wafanikiwao nao ni watu kama walivyo watu wengine ila utofauti mkubwa hujengwa katika namna ya kufikiria na pia katika namna ya kufanya mambo. Watu wote walio juu ukifuatilia historia zao utakuta walikuwa ni watu wa kawaida sana, ila ndani yao waliweka nia na kuamua kupambana kufikia hatua kubwa na za juu, na watu wa namna hii hata walipopata mafanikio madogo hawakubweteka na kujisahau bali huzidi kusonga mbele kupata mafanikio makubwa zaidi. Kama wao wamejaribu wakaweza kwa kutia nia na wewe ukitia nia kwa lolote ufanyalo ni lazima utaweza tu.

Itaendelea;

Somo hili ni sehemu ya kitabu "Huyu Ndiye Adui wa Mafanikio Yako". Mwandishi anapatikana kupitia 0769190019/0713804078, kitasokelvin@gmail.com

Share on Google Plus

About Gospel Kitaa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.