KWA TAARIFA YAKO MTUNZI WA WIMBO MAARUFU DUNIANI ALIYEFIKA TANZANIA KIMYA KIMYA

Haya msomaji wetu wa Gospel Kitaa karibu katika kipengele chetu maalumu ''KWA TAARIFA YAKO'' ambacho kinakujia kila siku za alhamisi ndani ya GK kikiwa na lengo la kukupatia habari ambayo iliwahi kutukia lakini yawezekana huijui pia yawezekana ilitukia ukawa unaijua lakini GK ikawa imesahau mahali au kuna sehemu haina usahihi utapata fursa ya kusahihisha kwa kuweka comment yako chini kabisa kwenye habari husika. Karibu
KWA TAARIFA YAKO hii leo ni kumuhusu mtunzi wa wimbo maarufu wa kuabudu ulimwenguni anayetokea jijini London nchini Uingereza, GK inataka kukujulisha kuhusu mtunzi wa wimbo wa 'Here I am to Worship, Happy Day na nyinginezo, huyu si mwingine bali ni mchungaji Tim Hughes kiongozi wa muziki na kuabudu kanisa la Kianglikana Holy Trinity Brompton (HTB) jijini London kanisa ambalo mchungaji wake kiongozi Nicky Gumble ni maarufu kwa kuanzisha huduma ya kujifunza neno iitwayo 'Alpha Course' inayofanywa na takribani makanisa yote ya Kianglikana nchini Uingereza.

KWA TAARIFA YAKO Tim Hughes ambaye licha ya kuwa ni mwimbaji binafsi pia ni kiongozi wa kundi lingine maarufu la muziki wa injili nchini Uingereza la 'Worship Central' ni baba  wa watoto wanne, baba yake mzazi ni mchungaji, ambapo Tim alikulia katika eneo la High Wycombe kisha kuhamia katika jiji la Birmingham alitawazwa kuwa mchungaji mwezi june 2013 katika kanisa kuu maarufu la Anglikana la St Paul Cathedral lililopo mashariki mwa jiji la London. 


Akiimba 'Here I am to Worship'


KWA TAARIFA YAKO mwimbaji huyu alianzia kupata umaarufu alipokuwa akihudumu katika huduma ya Soul Survivor chini ya mchungaji na kiongozi wa huduma hiyo Mike Pilavachi ambako Tim alikuwa akitumika kuongoza band ya huduma hiyo katika makambi maarufu ya vijana ya Soul Survivor yanayofanyika kila mwezi August nchini Uingereza, Tim alichukua nafasi ya mwimbaji mwingine maarufu aitwaye Matt Redman a.k.a Heart of Worship wimbo unaofahamika zaidi Tanzania na wengi waliojitahidi kutoka kwenye ukayumba na kuongeza ufahamu wa lugha.

KWA TAARIFA YAKO hiyo ilikuwa mwaka 1997 ndipo alipoanza na Soul Survivor, lakini kama
ilivyo kawaida ya Waingereza hawawezi kung'ang'ania sehemu moja kwa muda mrefu kabla ya kuhamia sehemu nyingine ili kupata uzoefu mpya ndivyo ilivyokuwa kwa Tim kwani mwaka 2005 aliamua kuhamia kanisa la HTB ambalo ni maarufu pia linapokuja suala la muziki wa injili jijini London, nathubutu kusema ndilo kanisa linaloongoza kwa upande wa makanisa ya Anglikana jijini London kuwa na waumini wengi hususani vijana wanaohudhuria ibada kila jumapili na katikati ya wiki

KWA TAARIFA YAKO Tim Hughes amewahi kuja Tanzania, kama nilivyowahi kugusia katika moja ya taarifa nilizowahi kuandika siku zilizopita, alikwenda mpaka Iringa pamoja na huduma ya kampuni ya Tear Fund ya Uingereza ambayo husaidia watu wenye matatizo mbalimbali na kusaidia huduma, kwa bahati mbaya ujio wake haukutambulishwa kwa watanzania waliowengi hususani wanamuziki ambao wangepata mawili matatu kutoka kwa mwimbaji huyu aliyejawa na tabasamu kila mara azungumzapo na watu. Ni mtunzi mkubwa wa nyimbo za muziki wa injili ambapo licha ya kutunga peke yake lakini pia huwa anashirikishwa na waimbaji wengine katika utunzi wa nyimbo zao, ambapo hivi majuzi alikuwa pamoja na mtunzi mahiri wa Hillsong Ruben Morgan wakishirikiana kutunga wimbo mpya kwaajili ya album mpya ijayo ya Hillsong Worship.


Akiimba 'Be My Everything' wimbo niupendao wakati wote


KWA TAARIFA YAKO kama nilivyosema hapo juu, Waingereza huwa wanapenda kupata ujuzi mpya kila wakati na ndio maana hawakai sehemu moja kwa kipindi kirefu, sasa ni hivi wiki hii imefahamika kwamba mwimbaji huyu ambaye pia ni mchungaji ametangaza kuhama kanisa la HTB na kuhamia jijini Birmingham ambako amepewa usharika wa St Luka uliopo katikati ya jiji hilo la Birmigham ambako ndiko amekulia. Kutokana na hilo Tim anatarajia kuachia uongozi wa kiongozi wa sifa HTB ila ataendelea kuongoza kundi la 'Worship Central'. Ambapo Tim ameonyesha kufurahia sana pamoja na mkewe huduma mpya wanayoiendea kuianza.


Akiimba 'Happy Day' alioshirikiana kuutunga na mwimbaji Ben Cantelon Nikiwa na Tim Hughes Disemba 2011 kanisani HTB, siku ambayo Darlene Zschech alitembelea na kutangaza kuhama Hillsong.Hiyo ni KWA TAARIFA YAKO hii leo, vinginevyo tukutane wiki ijayo…..


Share on Google Plus

About Ambwene Mwamwaja

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.