NENO: "UPAKO WA KUFANYA ZAIDI YA WENGINE" (4)
CHAKULA CHA WASHINDI

05, Januari, 2015

"UPAKO WA KUFANYA ZAIDI YA WENGINE"

Na Mwl Dickson Cornel Kabigumila.

"Isaka akapanda mbegu katika nchi ile, akapata mwaka ule vipimo mia kwa kimoja, BWANA akambariki. Na mtu huyo akawa mkuu, akazidi kustawi, hata akawa mkuu sana. Akawa na mali ya kondoo, na ng'ombe, na watumwa wengi. Hao wafilisti wakamhusudu. Na vile visima vyote walivyochimba watumwa wa baba yake, siku za Ibrahim babaye, Wafilisti walikuwa wamevifukia, wakavijaza kifusi. Abimeleki akamwambia Isaka, utoke kwetu, maana wewe una nguvu sana kuliko sisi. Basi isaka akatoka huko akapiga kambi katika bonde la Gerali, akakaa huko.

Isaka akarudi akavichimbua vile visima vya maji walivyovichimba siku za Ibrahimu babaye; Maana wale Wafilisti walikuwa wamevifukia baada ya kufa kwake Ibrahimu; Naye akaviita majina kufuata majina alivyoviita babaye.

Watumwa wa Isaka wakachimba katika lile bonde, wakapata kisima cha maji yanayobubujika. Wachungaji wa Gerari wakagombana na wachungaji wa Isaka wakisema, Maji haya ni yetu. Ndipo akakiita kisima jina lake Eseki, kwa sababu waligombana naye. Wakachimba na kisima kingine, wakagombania na hicho tena. Akakiita jina lake Sitna. Akaondoka huko akachimba kisima kingine, wala hicho hawakukigombania. Akakiita jina lake Rehobothi, akasema, Kwakuwa sasa BWANA ametufanyia nafasi nasi tutazidi katika nchi. " (Mwanzo 26:12-22).

Mambo ya kujifunza:

1. "Mungu hatageuza maisha yako mpaka pale utakapochukua hatua ya kwanza ya kupanda mbegu aliyokupa"

Biblia inasema Mungu ndiye ampaye mbegu "mwenye kupanda" (Isaya 55:10, 2Kor 9:10).
Na hiyo mbegu uliyonayo imebeba ukuu wako.
Biblia inasema Isaka alipopanda mbegu, ndipo Mungu akambariki. Akawa mtu mkuu.
Mungu hatafanya chochote kukupeleka kwenye ukuu mpaka pale wewe utakapochukua hatua ya kwanza kupanda mbegu.
Mawazo (ideas) uliyonayo ni mbegu, Mungu anasubiri uipande ili akubarikie kupitia hiyo. Na akikubarikia, lazima utakuwa mtu mkuu.
Nakusihi leo... Kila anachokupa Mungu kukifikiri na kukiona ndani yako ni mbegu ya ukuu aliokukusudia, ila Mungu hatakuja hata siku moja kukupandia mbegu.
Panda mbegu yako, watumishi wa Mungu tutaimwagilia, na Mungu ataikuza (Atatoa matokeo/ mavuno)!

2. "Kila mafanikio yatakapoanza kuonekana maishani mwako, utaibuka upinzani kutoka kwa uliowakuta"

"Abimeleki akamwambia Isaka, Utoke kwetu, maana wewe una nguvu sana kuliko sisi"
Kama una mpango wa kubarikiwa na kufanikiwa na kuwa mtu mkuu kwenye chochote unachokifanya, Jiandae kukutana na akina Abimeleki watakaokufukuza uwapishe.
Hawa hawaonekani wakati ukiwa na hali ngumu, hawaonekani kabla haujawa mtu mkuu... Wanakupenda na kukumbatia ukiwa chini yao kimaisha kwa vile unaomba kwao... Hawatakuchukia ukipata unafuu wa kimaisha maana bado haujawapita... Ila ukiwapita na kuwa na nguvu kuliko wao... Watafanya chochote kukuondoa!
Kama unataka kuwa mtu mkuu jiandae kukataliwa na kupingwa.
Yesu alipokuwa fundi Seremala, hakuna aliyempinga au kupanga kumuua, lakini alipoanza kutembea katika ukuu, ikaibuka vita.
Upinzani upo na hautakoma, lakini katika mambo yote tunashinda na zaidi ya kushinda kwake Yesu aliyetupenda.
Lazima ujue hili; "Mungu akitaka kukuandalia meza hatawaondoa maadui zako, atakuandalia meza mbele ya macho yao"
Jiandae kustawi katikati ya upinzani.
Upinzani ni chakula cha washindi.

3. "Kama baba yako aliwahi kufanya kitu cha maendeleo na kupata hata matokeo madogo hiyo ni ishara kwamba nawe una nguvu ya kuchomoza"

Biblia inasema Isaka alimwona baba yake akichimba visima.
Hata baba yake alipokufa na yeye alijiingiza kwenye kuchimba visima.
Mungu ameweka aina fulani ya baraka inayokuwa juu ya mzazi ambayo inaweza kuendelea juu ya watoto wake.
Kama baba alifanikiwa kwenye biashara hata kwa kiwango kidogo, ni ishara kwamba iko neema hiyo kwa watoto wake pia.
Ahadi na vipawa vya Mungu hutoka kizazi hata kizazi.
Kachunguze kwenu ni eneo lipi wazazi wako walikuwa bora, linaweza kukutoa kwenye maisha.
Haijalishi adui amevifukia visima vya baba yako, kama utaamua kufufua hicho kipawa na kufukua hivyo visima utapata maji.
Isaka alifukua visima vilivyofukiwa (vipawa, karama, huduma zilizozima/ kufa) vya Ibrahimu baba yake.
Baba yako aliwahi kuwa stadi kwenye kitu gani?
Wazazi wako walikuwa na nyota kwenye jambo gani?
Unaweza kufukua hivyo visima na kupata maji kama Isaka.

Hiki ndicho chakula cha washindi leo,
Umebarikiwa mno,
Mwl D.C.K
www.yesunibwana.org
Share on Google Plus

About Ambwene Mwamwaja

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.