NENO: "UPAKO WA KUFANYA ZAIDI YA WENGINE" (11)

Na Mwalimu Dickson Cornel Kabigumila.
"BWANA asema hivi, Amelaaniwa mtu yule amtegemeaye mwanadamu, Amfanyaye mwanadamu kuwa kinga yake na moyoni mwake amemwacha BWANA.

Maana atakuwa kama fukara nyikani, Hataona yatakapotokea mema; Bali atakaa jangwani palipo ukame, Katika nchi ya chumvi isiyokaliwa na watu.

Amebarikiwa mtu yule anayemtegemea BWANA, Ambaye BWANA ni tumaini lake.
Maana atakuwa kama mti uliopandwa kando ya maji, Uenezao mizizi yake karibu na mto; Hautaona hofu wakati wa hari ujapo, Bali jani lake litakuwa bichi;

Wala hautahangaika mwaka wa uchache wa mvua, Wala hautaacha kuzaa matunda." (Yeremia 17:5-8).

Mambo ya kujifunza:
1. "Unapompa mtu nafasi ya kwanza moyoni mwako badala ya Mungu... Umejitoa kwenye mfumo wa maisha bora alionao Mungu juu yako"
Kinachoweza kumfanya mtu afanikiwe, aongezeke na kustawi si wingi wa mali aliyonayo, Wala elimu, wala mtandao mkubwa wa watu alionao bali BARAKA YA MUNGU HUTAJIRISHA (Mithali 10:22).
Mtu mwenye baraka ya Mungu kichwani mwake, mikononi mwake na maishani mwake anaweza kufanikiwa bila elimu, bila ujuzi mwingi, akiwa ugenini, katikati ya upinzani nakadhalika!
Yakobo alifanikiwa kwa baraka ya Ibrahimu aliyoipata kwa Isaka baba yake... Aliondoka nyumbani kwa baba yake akiwa mikono mitupu na fimbo tu mkononi lakini BARAKA YA MUNGU ILIMFANYA KUSTAWI KATIKATI YA UPINZANI.
Isaka alikuwa katikati ya nchi ya Wafilisti yenye njaa kali... Lakini kwa baraka iliyokuwa juu yake alipanda mbegu (alilima) na kupata mavuno katikati ya njaa!
Akawa mkuu na kufikia hatua ya kuambiwa na Mfalme wa Wafilisti aondoke nchi ile.
Kilichomfanya Ibrahimu, Isaka na Yakobo wafanikiwe katikati ya magumu, changamoto, upinzani na kila mazito waliyopitia ni BARAKA YA MUNGU ILIYOKUWA NAO.
Siri: Baraka haiji kwa kuombewa, haiji kwa kutoa sadaka, haiji kwa namna yoyote ile BARAKA YA MUNGU INAYOTAJIRISHA, KUSTAWISHA NA KUFANIKISHA inapatikana kwa wale ambao MIOYONI MWAO WANA MUNGU.
Kama Mungu hana nafasi moyoni mwako kila utakachokifanya kiko chini ya laana!
"Baraka kwa maana rahisi ni uwepo wa Mungu unaotoa matokeo ya kupita kawaida maishani mwa mtu... Huwezi kutenganisha baraka na uwepo wa Mungu"
Amelaaniwa amtegemeaye mwanadamu na "moyoni mwake amemwacha Mungu"... Kama hakuna Mungu moyoni mwako, laana (kinyume cha baraka) zitakuwa maishani mwako.
Na ili kuupata uwepo wa Mungu moyoni mwako na maishani mwako lazima uwe na moyo safi; "Heri wenye moyo safi (watakatifu) maana hao watamuona Mungu" (Mathayo 5:6-8).
Huwezi kumtegemea Mungu usiyemjua na kukaa naye... Kila aliyejizoeza kukaa na Mungu (uweponi mwake) atakuwa mtu wa kumtumaini Mungu na mwisho wa siku atabarikiwa na kustawi!
Muhimu: Usiruhusu mtu au kitu chochote kichukue nafasi ya Mungu moyoni mwako; Ukimpoteza Mungu moyoni mwako umejitoa kwenye baraka zake. Na ukitoka kwenye baraka ya Mungu maisha hayatakwenda... Hautaona mema yatakapotokea!
2. "Kuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya UWEZO WA KUONA FURSA na kiwango cha mtu kumtegemea Mungu"
Biblia inasema anayewategemea wanadamu na kupoteza uwepo wa Mungu moyoni mwake, atakuwa kama fukara nyikani..."Hataona mema (fursa) yatakapotokea"
Unajua ni kwanini Wakristo wengi wana hali ngumu za kimaisha na umasikini? Sababu mojawapo kubwa ni "kumwacha Mungu na Neno lake" na kutegemea elimu, kazi, mishahara na ujuzi wa wanadamu.
Biblia inasema, "utegemezi wako kwa Mungu (Neno) ukiondoka, basi hautaona mema yajapo (fursa zikijitokeza)" maana ufahamu wako unakuwa umetiwa giza au kupofushwa na elimu na maarifa yenye kuona vizuizi, yasiyoamini miujiza, ya wanadamu!
Taarifa zote za wanadamu tofauti na Neno zimejaa hofu, mashaka, habari mbaya na kutokuamini. Ukizipa nafasi kuliko Mungu (Neno) hauwezi kuona fursa (mema) zinapokuja.
Utaishia kuwa mtu wa wastani (average person) kama mwanadamu mwingine asiye na Mungu.
Ukitaka kufanikiwa na kuanza kuona fursa maishani mwako kaa na Neno (Mungu) na uliruhusu na kusimamia hilo bila kusikia kingine chochote.
Tangu nilipojifunza kumtegemea Mungu (kuliamini na kulitenda Neno), nimekuwa mtu wa miujiza. Imeleta watu sahihi maishani mwangu, Imenifungulia ufahamu na maarifa na kiwango changu cha kuwaza, kupanga na kufanya vitu kimeongezeka... Naweza kuyaona mema mahali ambapo wengine wanaona hatari... Kila anayeliamini Neno na kuliishi (kumtegemea Mungu) lazima atakuwa na fursa zisizo na kikomo!
Je, unataka kuyaona mema yatakapokuja? Ni rahisi liamini na kulitenda Neno la Mungu sawa na lilivyosema bila kujali wataalam, wasomi, wajuzi wamesemaje halafu utashangaa fursa zitakazozaliwa maishani mwako!
Watu wa imani katika Neno (alichosema Mungu) ni watu wa fursa;
Ibrahimu aliyemtegemea Mungu na kutii kila Neno lake alikuwa mtu wa kwanza kugundua teknolojia ya kuchimba visima.
Isaka aliyemtegemea Mungu alikuwa mtu wa kwanza kugundua kilimo cha umwagiliaji; Katikati ya njaa na ukame aliweza kupanda mbegu na kuzibua visima vya Ibrahimu babaye na kufanya kilimo cha umwagiliaji; Akili na fursa hii aliipata kwa BWANA.
Yakobo akiwa kwa Labani kama mchunga mifugo wa kawaida, kutokana na kumtegemea Mungu alikuwa mtu wa kwanza kugundua teknolojia ya "uhamilishaji (kuchanganya mbegu na aina za wanyama tofauti ili kupata aina mpya ya wanyama)" na kuwa tajiri kuliko Isaka!
Onyo: Kadri unavyotegemea elimu, ajira, mshahara, hali nzuri ya wazazi, marafiki na kuacha kumtafuta Mungu ili abadilishe maisha yako, unapoteza Fursa nyingi zilizokuzunguka!
3. "Baraka ni urithi wa kila anayetembea na Mungu... Na kila anayemtegemea Mungu anakuwa na maisha ambayo yanajitofautisha na ya wanadamu wa kawaida"
Ebu fikiria wakati wa hari (jua kali), mimea yote hupukutisha majani (hupoteza uwezo wa kuzaa na kupata faida), lakini ni kinyume kwa "mti uliopandwa kando ya mto (aliye karibu na Bwana aliye kisima cha maji yaliyo hai: Yeremia 17:13)"
Kila mwenye uwepo wa Mungu anaweza kuwa na tofauti na wasio na Mungu tena tofauti ya waziwazi.
Uwepo wa Mungu unaweza kupandisha thamani yako na kukufichia aibu.
Mfano binafsi; Mara kadhaa nimepigiwa meseji au kupigiwa simu na watu (marafiki/ ndugu) wakiomba niwasaidie pesa au niwakopeshe kiasi cha pesa ambacho hata mimi sijawahi kukishika mkononi kwa wakati mmoja... Nini kinakuwa kimetokea hapa??
Mungu anakuwa ameipandisha hadhi na thamani yangu kupitia uwepo wake na kunifanya nionekane kama mtu mwenye majibu yao... Japo mfukoni au benki sina hicho wanachokitaka.
Hiki ndicho kilichomtokea Isaka... Uwepo wa Mungu ulimfanya aonekane kuwa ana nguvu kuliko taifa zima la Wafilisti kiasi kwamba mkataba kwamba asije akawapiga... Hii si kawaida, ni uwepo na utukufu wa Mungu!
We are all human beings but the presence of God between one and another makes the difference!
We are all ordinary people but His glory makes someone extraordinary!
Jenga msingi wako kwenye Neno la Mungu, litende bila kujali mazingira, likiri kwa ujasiri, liseme kwenye mazungumzo yako yote na tarajia mabadiliko na miujiza kila sekunde toka kwa BWANA!
Na hiki ndicho chakula cha Washindi leo,
Umebarikiwa,
Mwl D.C.K
www.yesunibwana.org

Share on Google Plus

About Ambwene Mwamwaja

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.