NENO: "UPAKO WA KUFANYA ZAIDI YA WENGINE" (12)

CHAKULA CHA WASHINDI
20, Januari, 2015.

"UPAKO WA KUFANYA ZAIDI YA WENGINE"

Na Mwalimu Dickson Cornel Kabigumila

"Palikuwa na mtu katika nchi ya Usi, jina lake alikuwa akiitwa Ayubu; mtu huyu alikuwa mkamilifu na mwelekevu, ni mmoja aliyemcha Mungu na kuepuka uovu.
Kisha walizaliwa kwake wana saba na mabinti watatu.
Mali yake nayo yalikuwa kondoo elfu saba, na ngamia elfu tatu, na jozi za ng'ombe mia tano, na watu wa nyumbani wengi sana; basi hivi mtu huyo alikuwa mkuu sana kuliko watu wote wa upande wa mashariki.
Nao wanawe huenda na kufanya karamu katika nyumba ya kila mmoja wao kwa siku yake; nao wakatuma na kuwaita maumbu yao watatu ili waje kula na kunywa pamoja nao. Basi ilikuwa, hapo siku za karamu zao zilipokuwa zimetimia, Ayubu hutuma kwao na kuwatakasa, kisha akaamka asubuhi na mapema na kusogeza sadaka ya kuteketezwa kama hesabu yao wote ilivyokuwa; kwani Ayubu alisema, Yuamkini kwamba hawa wanangu wamefanya dhambi, na kumkufuru Mungu mioyoni mwao. Ndivyo alivyofanya Ayubu siku zote.
Ilikuwa siku moja ambayo hao wana wa Mungu walikwenda kujihudhurisha mbele za BWANA, Shetani naye akaenda kati yao. BWANA akamwuliza Shetani, Umetoka wapi wewe? Ndipo Shetani akamjibu BWANA na kusema, Natoka katika kuzunguka-zunguka duniani, na katika kutembea huku na huku humo. Kisha BWANA akamwuliza Shetani, Je! Umemwona mtumishi wangu Ayubu? Kwakuwa hapana mmoja aliye kama yeye duniani, mtu mkamilifu na mwelekevu, mwenye kumcha Mungu na kuepukana na uovu.
Ndipo Shetani akamjibu BWANA, na kusema, Je! Huyo Ayubu yuamcha BWANA bure? Wewe hukumzingira kwa wigo kwa ukigo pande zote, pamoja na nyumba yake, na vitu vyote alivyo navyo? Kazi za mikono yake umezibarikia, nayo mali yake imeongezeka katika nchi. " (Ayubu 1:1-10).

Mambo ya kujifunza:

1. "Siri ya mafanikio, utajiri na ustawi wa Ayubu kuliko watu wote wa Upande wa Mashariki ilikuwa kwenye; Ucha Mungu, Ukamilifu, Uelekevu na Kuepuka uovu"

Hakuna mtu anayeweza kutembea katika mambo yote haya manne na asifanikiwe.
Mtu aliyejaa Ucha Mungu (Hofu ya kweli na ya dhati ya Mungu), Uelekevu (Mtu mwepesi wa kupokea maelekezo na kuyatendea kazi kwa wakati), Mkamilifu (Mtu anayeyapeleleza na kuyatafuta mapungufu yake, kisha kuomba neema na rehema ya Mungu kumsaidia kuyashinda na kuyavuka), mtu anayeepuka uovu (Mtu anayekwepa watu, vitu, kazi, shughuli na mazingira yanayoweza kuharibu uhusiano wake na Mungu), Mtu huyu lazima atafanikiwa na kustawi sana... Kama ukiyajaza mambo haya manne muhimu sana moyoni mwako na kuamua kuyaishi; Hakika maisha yako hayatakuwa ya kawaida.
Kwanini;
Biblia inasema, "Siri ya BWANA iko kwao wamchao.... Naye BWANA atamfundisha katika njia anayoichagua (atampa maarifa na ufahamu wa Kiungu wa namna ya kufanikiwa katika chochote anachofanya); Nafsi yake itakaa hali ya kufanikiwa (atakuwa mtu wa mafanikio), Wazao wake watairithi nchi (kuna uhakika wa future ya watoto wake hata asipokuwepo)" (Zaburi 25:12-14).
Ayubu alimcha BWANA tangu akiwa kijana mdogo, na siri za BWANA zinazomfanya mtu awe mtu wa maajabu na miujiza na mafanikio zilikuwa pamoja naye (Ayubu 29:2-25)!
Unataka kufanikiwa? Msingi wa kwanza kabisa ni mambo manne haya: Ukamilifu, Uelekevu, Kumcha Mungu na kuepuka uovu!
There is always a vast land for God fearing people to possess, will you?

2. "Kuwa mcha Mungu, kuepuka uovu, ukamilifu na uelekevu huzalisha NGUVU YA KUPATA UTAJIRI ila havitakufanya tajiri mpaka pale utakapovounganisha na kuwekeza kwenye fursa za uchumi zilizokuzunguka... Unganisha kanuni za kiroho na za mwilini pamoja ili kupata matokeo"

Biblia inasema, "Asiyefanya kazi na asile"
Pia inasema, "Utafuteni Ufalme wa Mungu na mengine yote mtazidishiwa"
Kanuni ya Mungu ya kumfanya Mtu awe na vitu vya kumtosha yeye na mahitaji yake ni kuongeza.... Ila kanuni ya Mungu ya kumtajirisha Mtu mpaka awe mkuu na kugusa maisha ya maelfu ya watu wengine ni kuzidisha!
Aliye nacho ataongezwa... Asiyekuwa nacho hata kile anachodhani anacho atajikuta siku moja hakipo tena!
Kama una sifuri, Mungu akizidisha utakuwa na sifuri tu!
Tengeneza mazingira ya uchaji, ukamilifu, kuepuka uovu na kuelekezeka (hali za kiroho chako) lakini pia Wekeza kwenye fursa za kiuchumi Mungu anazokupa kuziona zilizokuzunguka!
Biblia inasema, "Kila utakachotia mikono kukifanya atakibariki (Atazibariki kazi za mikono yako)"
Ayubu alikuwa Mfugaji, alifuga ng'ombe, punda, ngamia, kondoo... Na pia alikuwa amewekeza kwenye ardhi... Hauwezi kuwa na maelfu ya mifugo bila kuwa na ardhi kubwa na ya kutosha... Na kupitia ufugaji na kilimo Biblia inasema alikuwa na watu wengi sana nyumbani kwake (alikuwa mwajiri)!
Unganisha kanuni hizo nne za kiroho na kanuni za uwekezaji ili kuiruhusu Nguvu ya kiroho ya kupata utajiri (Kumbukumbu 8:18, Mithali 8:18-21, Mithali 10:6,22) ifanye kazi na kukufanya mtu mkuu!

3. "Kama wewe ni mzazi au una mpango wa kuwa mzazi; jizoeze kuwaunganisha wanao na uwepo/ madhabahu ya Mungu kwa maombi yako na sadaka"

Biblia inatuambia Ayubu alikuwa akituma wanae waje kisha "aliwatakasa na kutoa sadaka kwa ajili yao" mbele za BWANA (mstari wa 5).
Na Biblia inasema alifanya hivyo siku zote.
Mimi naamini Wazazi wa kwanza, Adam na mkewe Eva mbali ya kwamba walianguka dhambini, waliwafundisha watoto wao kumtafuta Mungu.
Na ndio maana tunaona walipokua walikuja wenyewe Kaini na Habili kutoa sadaka na kuomba kwa BWANA (Mwanzo 4).
Haikuwa kwa bahati, ulikuwa ni mfumo walioupokea kwa wazazi wao!
Ibrahimu alimuunganisha mwanae Isaka na madhabahu ya Mungu aliye hai tangu akiwa mdogo kupitia sadaka na maombi.... Na alikuwa akienda naye kila alipokuwa akienda kuomba na kumtolea Mungu.
Na ndio maana siku ile alipokwenda "kumtoa Isaka" Isaka huyohuyo alimuuliza baba yake swali, "Kuni tunazo lakini sadaka iko wapi? Mbona hatujabeba sadaka" na Ibrahim akamjibu BWANA atajipatia (Mwanzo 15).
Isaka aliwafundisha na kuwakuza wanae Esau na Yakobo kwenye mfumo huu pia. Na ndio maana hata wakati Yakobo anamkimbia Esau, alipopata maono na kumwona Mungu juu ya ngazi alielewa yule ni Mungu wa baba zake, akamimina mafuta pale na kutoa sadaka akaweka nadhiri kuwa akirudi salama na kufanikiwa atamtolea Mungu "sehemu ya kumi (zaka)" ya atakachopata!
Haya maarifa hayakuja from no where... Ni ujuzi alioupata kwa Ibrahim na Isaka baba zake!
Kama unataka mafanikio ya kweli... Usiwaache nyuma watoto wako linapokuja swala la kumjua Mungu.
Wafundishe kuhusu Mungu wa Biblia, waombee kila siku kwa mzigo, toa sadaka maalum kwa ajili ya masomo yao, future zao, hakikisha unawaunganisha na Mungu wako unayemuabudu katika Kristo Yesu!
Haipendezi wewe kufanikiwa na kustawi na kutembea na Mungu halafu uzao wako ukaishi nje ya kusudi la Mungu na kuupoteza uwepo wa Mungu.
Kama Mungu alikuwa na Ibrahimu, afike na kwa Isaka na Yakobo, na Israeli nzima!
"Mlee mtoto katika njia impasayo, naye hataiacha hata atakapokuwa mzee" (Mithali 22:6).
"Waarifuni watoto wenu habari yake, watoto wenu wakawaambie watoto wao,
Na watoto wao wakakiambie kizazi kingine" (Yoeli 1:4).
" Nawe uwafundishe watoto wako kwa bidii, na kuyanena uketipo katika nyumba yako, na utembeapo njiani, na ulalapo, na uondokapo" (Kumbukumbu 6:7).
Ukishindwa kuwa na uzao bora unaomjua Mungu wa kweli ni kosa lako... Biblia imejaa kanuni za malezi bora... Na mimi nimekupa mtaji wa kuanzia!

4. "Shetani anamjua mtu mwenye uhusiano mzuri na Mungu na anayelindwa na uwepo wa Mungu"

Ukisoma kisa hiki cha Ayubu utagundua kwamba Shetani alijua na kuelewa kwamba Ayubu analindwa, anafanikishwa na kubarikiwa na Mungu.
Alijuaje?
Kila alipokuwa akija kufanya kazi zake kuu tatu; kuiba, kuchinja na kuharibu (Yohana 10:10), alikuwa anakuta wigo wa nguvu na uwepo wa Mungu umewafunika!
Alipotaka kugusa watoto aliukuta uwepo wa Mungu... Alipotaka kugusa mali zake aliukuata wigo... Alipotaka kugusa watu wa nyumbani mwake ili amfirisi kwa magonjwa na mikasa isiyo na kichwa wala miguu, aliukuta moto ukiwaka!
Inawezekana Ayubu hakujua lakini Shetani alijua... Mungu alijua... Na mimi na wewe tunajua!
Watu ambao Mungu anawalinda, wao, watoto wao, mali zao na watu wao, ni wale ambao wamejiungamanisha na Mungu kwenye kila eneo; ni wacha Mungu, wakamilifu, waelekevu, wanaoepuka uovu, wanaounganisha kila walichonacho na uwepo wa Mungu (madhabahu) kupitia maombi na sadaka kila siku kama Ayubu!
Wale wanaotembea katika utakatifu, kudumu katika kuomba daima (na hasa kufunga mara kwa mara ili kukaa na BWANA) pamoja na kumtolea sadaka Mungu kwa uaminifu na kwa kila kinachowahusu... Hawa Shetani anaishia kuwatazama akitamani kuwameza lakini anakutana na moto na wigo wa nguvu za Mungu!
Fanya mambo hayo na Ibilisi atafyata mkia maishani mwako.
"Kwa maana tunalindwa na nguvu za Mungu kwa njia ya imani..." (1Petro 1:5).
"Tazama, nami namtuma malaika aende mbele yako, ili akulinde njiani na kukupeleka mpaka mahali pale nilipokutengenezea" (Kutoka 23:20).

5. "Tabia ya uzururaji na kuzungukazunguka bila mipango na malengo maalum ni ya Ibilisi... Usitoke nyumbani kwako kwenda kokote ambako hauna kitu cha maana na cha faida unakwenda kufanya... Thamini uhai wako, maisha uliyonayo na muda wako"

Biblia inasema alipoulizwa Shetani na Mungu yakuwa anatoka wapi? Alijibu akasema, "Natoka katika kuzunguka-zunguka duniani, na katika kutembea huku na huku na humo" (mstari wa 7)!
Shetani anazurura hovyo... Anatoka na kwenda kufanya chochote kinachojitokeza.
Watu wa Mungu ni watu wa maono. Hawafanyi vitu kwa kushtukiza wala kwa mkumbo. Ni watu wa mipango. Ni watu wa ratiba. Hawaendi kutembelea watu ovyo. Hawaendi mahali ili kupoteza muda au kusogeza siku. Ni watu wanaoukomboa wakati. Ni watu wa kutumia muda kujisomea na kutafuta siri za Mungu na kanuni za maisha ya ushindi.
Wakitoka kwenda mahali wanapeleka habari njema. Wanaupeleka uwepo wa Mungu wenye majibu kwa watu.
Kuliko kupoteza muda kwa kuzunguka-zunguka kama Ibilisi, wanakaa kwenye miguu ya Mungu kupitia maombi na Neno na kufunga!
Usitoke kwenda mahali bila mambo ya msingi na ya baraka ya kufanya huko.
Sisi ni barua za Kristo zilizoandikwa kwa mikono mizuri ya Roho mtakatifu (2 Wakorintho 3:1-3).
Ni mawakili wa siri za Mungu na watumishi wa Kristo (1Wakorintho 4:1).
Chunga miguu yako... Usizunguke ovyo kama Ibilisi... Izuie miguu yako... Siku ukitoka kwenda mahali peleka habari njema (Warumi 10:15).
Naiamuru Roho ya kuzunguka-zunguka ovyo bila makudi na mipango ya faida ikutoke katika jina kuu la Yesu!

Na hiki ndicho chakula cha washindi leo,
Umebarikiwa,
Mwl D.C.K
www.yesunibwana.org
Share on Google Plus

About Ambwene Mwamwaja

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.