SABABU YA KUOMBA KWA AJILI YA MCHAKATO WA KATIBA MPYA

KWA NINI MTU WA MUNGU AOMBE KWA AJILI YA MCHAKATO WA UPATIKANAJI WA KATIBA MPYA.

Na Kelvin Kitaso,
GK Guest Writer.
Rais Kikwete akipokea nakala ya Katiba Inayopendekezwa kutoka kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, Mhe. Samuel Sitta
Tanzania ni taifa ambalo limechaguliwa na BWANA kwa ajili ya utukufu wa mwisho kama Mungu alivyokwisha sema na wazee wetu wengi na kuwasisitiza kuhusu jambo hili. 
Na taifa la BWANA linapaswa kwenda kama vile BWANA anavyotaka liwe na lazima tufike mahali na kuogopa sana kama kuona misingi ya taifa letu inabomoka katika kipindi ambacho tupo na tunaishi. Na daima Mungu hutumia watu kubadilisha mahali na ukiona mahali panakaa vibaya tatizo huweza kuwa ni mmiliki wa mahali pale na siyo mtu aliyempa eneo hilo. Lango laweza amua nini kiwe ndani. Na lango likiwa vibaya basi na mambo mabaya huweza ingia ndani yake.

Inasikitisha na kuumiza sana unapoona mtu wa Mungu hajali, bali kuchukulia kawaida sana kwa jinsi mambo yanavyoenda ndani ya nchi. Tupo vitani, ukilemaa adui lazima akupige. Shetani yupo kwenye harakati za kuhakikisha anatumia mawakala wake na amewatuma na hata bungeni ili kuhakikisha mambo yanaharibika.

Tupo kwenye mchakato wa upatikanaji wa katiba lakini wengi wanajua kuwa mchakato huu ni kwa ajili ya watu wa jamii fulani tu. Ila kiukweli mchakato huu wa upatikanaji wa katiba mpya unategemea sana watu wa Mungu kuliko hao wengi wanaowaangaliwa kuwa ni wahusika. Ni lazima watu wa Mungu wawe na kitu cha kufanya ili kufanikisha upatikanaji wa katiba mpya.

Waweza sema kuwa maombi yako hayana nguvu sana kwa kuwa uko nje ya bunge, ila si kweli na unajidanganya sana kwa kuwa Waraka wa Yakobo 5:16 unasema, 16 Ungameni dhambi zenu ninyi kwa ninyi, na kuombeana, mpate kuponywa. Kuomba kwake mwenye haki kwafaa sana, akiomba kwa bidii. Na pia nikukumbushe kuwa Esta na Waisrael walitaka haki yao kwa maombi mbele za Mungu na Mungu akawafanikisha kwa kuwapa kibali kwa kile kitu walichotaka.

Hagai 1:2-5 inasema, “2 Bwana wa majeshi asema hivi, ya kwamba, Watu hawa husema, Huu sio wakati utupasao kuja, huu sio wakati wa kujenga nyumba ya Bwana. 3 Ndipo neno la Bwana lilikuja kwa kinywa cha nabii Hagai, kusema, 4 Je! Huu ndio wakati wa ninyi kukaa katika nyumba zenye mapambo ya mbao, iwapo nyumba hii inakaa hali ya kuharibika? 5 Basi sasa, Bwana wa majeshi asema hivi, Zitafakarini njia zenu”.

Bwana anasema na watu ambao wanaishi katika wakati ulioharibika ila hawaoni kuwa kuna umuhimu wa wao kujenga kwa wakati ule na pengine watu hawa hawakuona kama kazi hii ya ujenzi inawahusu wao, kuna jambo la msingi Bwana anauliza kuwa, je? huu ni wakati wa ninyi kukaa katika nyumba zenu nzuri na kwa kila uzuri wa kustarehe huku mkiacha nyumba (Tanzania) inaharibika? Bwana ananena kuwa twapaswa tafakari vyema njia zetu kama kweli tupo sahihi.


Mithali 28:2 inasema, “2 Kwa sababu ya maasi ya nchi wakuu wake huwa wengi; Bali kwa wenye ufahamu na maarifa hali ya nchi hudumishwa” Jinsi hali ya nchi ilivyo sasa inanitaji watu wenye ufahamu na maarifa kama Daniel na Nehemia na watu kama hawa hupatikana kwa Mungu, ila wasipojitambua ni kazi sana wakafanya mabadiliko; na tena BWANA h usema kuwa

watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa” tatizo si kwamba Mungu hana watu wa kusimama nao ila tatizo ni kwamba watu wake waliopo hawajui wala hawafahamu kama inenavyo katika kitabu cha Zaburi ya 82:5, 5 Hawajui wala hawafahamu, hutembea gizani; Misingi yote ya nchi imetikisika.” Tatizo kuu ambalo ni kubwa ni kuwa watu wa Mungu ambao ndio wanakusudiwa wapo ila hawajui tena hawana ufahamu, nao hutembea gizani wote pia gizani ni sehemu ambayo si mpango wa Mungu sisi tuwepo huko ila tunalazimika kuwepo huko kwa sababu ya kukosa maarifa.

KWA NINI WATU WA MUNGU KUOMBA

  1. Katiba ni msingi wa nchi kwa vizazi vingi vijavyo na ukiharibiwa, mwenye haki huondoshwa.
Zaburi 11:2-3, inasemaMaana, tazama, wasio haki wanaupinda uta, Wanaitia mishale yao katika upote, Ili kuwapiga gizani wanyofu wa moyo. 3 Kama misingi ikiharibika, Mwenye haki atafanya nini?”

Katiba ni msingi wa kulijenga taifa, hivyo ikiharibika mwenye haki atakuwa wapi? Msingi mbovu hujenga nyumba mbovu, ni muhimu sana kwa mwamini kuwa makini katika kuujenga msingi huu ambao vizazi vingi vijavyo vitakuja kukaa juu yake.

Sura ya 2 inaelezea kabisa kuwa wapo watu wabaya ambao wanajihusisha na kuwapinga wenye haki na wanataka haki. Na kama watafanikiwa kufanya hivyo basi taifa litakuwa kwenye hali mbaya. Hawa ni watu wanaoangalia misimamo yao na vyama vyao pasipo kuangalia maslahi ya taifa lao na wapo radhi kumpotosha mwenye haki yake ili wapate matakwa yao.

Kama watu wenye kupenda taifa na vizazi vijavyo baada yetu vikae salama katika misingi iliyo bora ni lazima tutie juhudi ya kuombea taifa katika upatikanaji wa katiba hii ili katiba ibebe misingi mizuri.
  1. Kazi hii inamuhusu mwenye haki.
Tunaweza kabisa tukaona kuwa mambo haya ni ya wanasiasa tu ila kazi hii ni lazima uone kuwa inakuhusu wewe na ni lazima uinuke ukaitende kama inenavyo katika kitabu cha Ezra 10: 4 “Inuka; maana shughuli hii yakuhusu wewe; na sisi tu pamoja nawe; uwe na moyo mkuu, ukaitende.

Esta 4:13-16 inasema, “13 Naye Mordekai akawaagiza wampelekee Esta jibu la kusema, Wewe usijidhanie kuwa wewe utaokoka nyumbani mwa mfalme, zaidi ya Wayahudi wote.
14 Kwa maana wewe ukinyamaza kabisa wakati huu, ndipo kutakapowatokea Wayahudi msaada na wokovu kwa njia nyingine; ila wewe utaangamia pamoja na mlango wote wa baba yako; walakini ni nani ajuaye kama wewe hukuujia ufalme kwa ajili ya wakati kama huo? 15 Basi Esta akawatuma ili wamjibu Mordekai, 16 Uende ukawakusanye Wayahudi wote waliopo hapa Shushani, mkafunge kwa ajili yangu; msile wala kunywa muda wa siku tatu, usiku wala mchana, nami na wajakazi wangu”.

Malkia Esta alistarehe na kuusahau wajibu wake kuwa yupo mahali pale kwa wakati ule kwa kusudi, na akawa anayatazama mambo kwa ukawaida tu kwa kuwa aliridhika kuwa malkia tu, na kusahau kuwa kuna watu wapo kwenye dhiki. Ila tu alipopata UFAHAMU maana tatizo lilikuwa ni kukosa ufahamu na maarifa na kwa kupata tu kufahamu ndipo anapoanza kuhimiza watu waanze kuomba ili kufanikisha shauku yao waitakayo.

Ukiona mambo yamebadilika na wewe badilika na ubadilishe hata namna ya kufanya mambo, hata kama ulikuwa unachukulia kawaida na kuomba kawaida ni lazima ubadilike na kuanza kuongeza mwendo zaidi wa vile ulivyokuwa unafanya hapo kwanza.
  1. Katiba ni mwongozo wa nchi kama ilivyo biblia kwa kanisa.
Kitabu cha Zaburi 119:105, inasema Neno lako ni taa ya miguu yangu, Na mwanga wa njia yangu.”

Katiba ni taa ya miguu ya waTanzania na ni mwangaza wa njia yao kwa vile waendavyo uwamulikia wapate kujua ipi ni mielekeo yao. Ni muhimu sana kwa watu wa Mungu kuiombea sana kwa kuwa ndiyo itakuwa inatoa maelezo watu wanapaswa waweje na waishije. Na kama itaharibika swali ni je? Mwenye haki atakuwa wapi na uzao baada yake.

  1. Nchi sasa ni mahali palipobomoka na anatafutwa mtu wa kusimama na kupajenga.

Mtu anayetafutwa hapa licha ya kuwa mwenye haki anapaswa kuwa na uahamu na maarifa ili aweze kujenga mahali hapa palipobomoka.

Kitabu cha Ezekiel 22:29,30 kinasema kuwa “29 Watu wa nchi wametumia udhalimu, wamenyang'anya kwa nguvu; naam, wamewatenda jeuri maskini na wahitaji, nao wamewaonea wageni bila haki. 30 Nami nikatafuta mtu miongoni mwao, atakayelitengeneza boma, na kusimama mbele zangu mahali palipobomoka, kwa ajili ya nchi, nisije nikaiharibu, lakini sikuona mtu.”

Ndugu yangu mpendwa, BWANA wetu anataka kulijenga taifa letu ila imetupasa sana kusimama naye ili tuweze kujenga mahali palipobomoka, kwa kuwa yeye anatafuta mtu tu wakusimama naye.

  1. Mungu anataka kuiponya nchi yetu.

Tulipokuwa kwenye jubilee ya miaka hamsini ya uhuru tulielekeza sana maombi yetu tukitaka ustawi wa taifa letu na yeye asiye kiziwi bali husikia haja zetu na akaona vyema afanye kila kitu upya na hata kupitia viongozi walio madarakani akaweka mzigo ndani yao ili tupate katiba mpya itakayo tufanya tutembee kwa miaka mingine hamsini ya ushindi iliyokabidhiwa kwa Bwana. 

Kuna umuhimu mkubwa sana wa kuiombea katiba ya taifa kubwa sana duniani lililotengwa na Mungu kwa ajili ya utukufu na uamsho wa mwisho duniani.

Pamoja na mambo yote hayo, 2 Nyakati 7:14 inasema “14 ikiwa watu wangu, walioitwa kwa jina langu, watajinyenyekesha, na kuomba, na kunitafuta uso, na kuziacha njia zao mbaya; basi, nitasikia toka mbinguni, na kuwasamehe dhambi yao, na kuiponya nchi yao.” Ni muhimu sana kwa watu wa Mungu kurudi mbele za BWANA kwa kunyenyekea na kumwomba.

Usije dharau jambo hili ni kubwa sana katika ulimwengu wa roho. Ukilemaa usidhanie kamwe kama utakuwa salama.

Ni vyema sana kwa kanisa, fellowships na hata huduma mbalimbali kuweka mkakati wa kuliombea jambo hili si kwa kawaida bali kwa mzigo sana.

Katika familia wanafamilia waweke mkakati mzuri wa kuombea katiba mpya.

Kama una marafiki, shirikiana nao vyema kuombea katiba hii.

Ewe mjenzi kamwe usiogope kutekeleza majukumu yako ya kuliombea na kulijenga taifa letu. Hakika kazi yako itakumbukwa na kupewa ijara njema.

NB: “20 Ndipo nikawajibu, nikawaambia, Mungu wa Mbinguni, yeye atatufanikisha; kwa hiyo sisi, watumishi wake, tutaondoka na kujenga; lakini ninyi hamna sehemu, wala haki, wala kumbukumbu, katika Yerusalemu,” Nehemia 2:20


MUNGU IBARIKI TANZANIA, MUNGU IBARIKI AFRIKA

0769190019/0713804078,
kitasokelvin@gmail.com

Share on Google Plus

About Gospel Kitaa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.