SOMO: AGANO LA DAMU (1)


Askofu Sylvester Gamanywa
Leo nimewajibika kuwasilisha mapema somo jipya la mwaka mpya ambalo kichwa chake ni “Agano la damu”! Naliita somo jipya kwa ajili ya mwaka mpya, lakini somo lenyewe ni kongwe kwa karne nyingi kiasi kwamba, kwa wasomaji wa kizazi hiki kwao ni somo jipya na geni kwao. Madhumuni ya kuliwasilisha somo hili, ni kuweka uzito wa kampeni mpya ya OPERESHENI MAVUNO ambayo tumeiweka wakfu mwanzoni mwa mwezi huu, kwa sababu siri zote za mafanikio yanayokwenda kupatikana na kuonekana mwaka huu asili yake ni Agano la damu: 

Utangulizi
Kuna tofauti kubwa kati ya misamiati ya maneno mawili ambayo wengi hufikiri yana maana moja. Maneno hayo ni “agano” na “mkataba”! Kamusi ya Kiswahili sanifu yenyewe imejaribu kuyatafsiri kwa maelezo ambayo yanaonesha kuwepo kwa tofauti japokuwa tofauti yake ni kidogo na ndiyo maana yanazidi kuwachanganya watu.

Agano ni “tokeo la kukubaliana; ahadi, mapatano.” Na neno “mkataba” maana yake ni “makubaliano yanayofikiwa kwa kuandikiana baina ya watu au vikundi viwili au zaidi ili kufanya jambo au kazi fulani”

Tofauti iliyomo kati ya tafsiri hizi mbili. Ya kwanza ni neno “kuandikiana”! Kwa maana “agano” kwa asili yake halikuwa na haja ya “kuandikiana” lakini lilikuwa na “kiapo cha kuaminiana”. Mkataba ni “makubaliano” yanayofikiwa kwa njia ya kuandikiana ambapo wahusika wanawajibika kutia saini zao na mihuri ya taasisi zao ili kuweka uzito wa makubaliano yao.

Tofauti ya pili iliyopo katika ya “agano” na “mkataba” ni jinsi inavyotekelezwa na masharti yake. Kwenye “agano” wahusika “wanaungana na kuwa kitu kimoja, na mali zilizokuwa za mktu binafsi zinakuwa mali ya kila mmoja” Na ni agano la kudumu na kurithi kutoka wazazi waasisi, na watoto wao, na wajukuu zao.

Wakati “makataba” kinachozingatiwa ni yale yaliyomo ndani ya maandishi peke yake. Wahusika wanafungwa na yale waliyokubaliana kuchangia au kushirikiana, lakini hawaugani na kuwa kitu kimoja na kuunganisha mali zao kama ilivyo upande wa “agano”!

Kutokana na tofauti hizi za kihistoria na uzito wake, neno “Agano” kwa kizazi hiki limekuwa msamiati mgumu kwa sababu hakuna utamaduni huu wa kale wa “kufanya agano” kwa “kiapo cha kuaminiana” na badala yake tumezoea utamaduni wa “mikataba ya kuandikiana” na hivyo hatujui wala kuthamini “Agano la damu ya Yesu” ambalo lilifanyika kwa utamaduni wa kale. 

Katika hoja hii nakusudia kuchambua kwa upya na kina uzito wa “agano la damu” nikianza na historia yake kibiblia, masharti yake, na faida zake, na kisha tujitathmini kama kweli tunaishi ndani ya “Agano la damu ya Yesu” au tuko nje?
Historia fupi ya agano la
damu kwa mujibu wa Biblia

Chimbuko la “agano la damu” katika Biblia tunaweza kuliona kwa hali ya fumbo kuanzia ndani ya bustani ya Edeni! Mara tu baada ya binadamu wa kwanza kuanguka dhambini, Mungu alifanya tendo la kumwaga damu ya kiumbe hai ambapo ngozi yake ilitengeneza mavazi ya kuwafunika uchi akina Adamu na Eva. “BWANA Mungu akawafanyia Adamu na mkewe mavazi ya ngozi akawavika.” (MW.3:21)

Tukio la pili, la agano la damu tunalikuta likijitokeza kwa watoto wa kwanza wa Adamu na Eva, ambao ni Kaini na Habili. Tunasoma habari za utoaji wa sadaka ambao Habili alitoa sadaka ya wanyama walionona. “Habili naye akaleta wazao wa kwanza wa wanyama wake na sehemu zilizonona za wanyama. BWANA akamtakabali Habili na sadaka yake.” (MW.4:4)

Tukio la tatu la agano la damu tunalipata baada ya gharika ya Nuhu pale ambapo alichinja wanyama na kutoa dhabihu ya kuteketezwa. Ni ni wakati wa Nuhu ambapo tunasoma waziwazi Mungu akiitaja damu kama kitu kitakatifu na kilichotengwa  kwa matumizi maalum. “Bali nyama pamoja na uhai, yaani damu yake, msile.” (MW.9:4)

Tukio la nne tunakuja kukutana nalo kwa Abramu. Na hapa ndipo naweza kusema, uwazi wa chimbuko la agano la damu unapoanzia. Hapa ndipo tunasoma waziwazi kwamba Mungu alifanya “agano la damu” na Ibrahimu na mfano hai tunausoma katika maandiko yafuatayo:

“Akamwambia, Unipatie ndama wa miaka mitatu, na mbuzi mke wa miaka mitatu, na kondoo mume wa miaka mitatu, na hua, na mwana njiwa.  Akampatia hao wote, akawapasua vipande viwili, akaweka kila kipande kuelekea mwenzake, ila ndege hakuwapasua.  Ikawa, jua lilipokuchwa likawa giza, tazama, tanuru ya moshi na mwenge unaowaka ulipita kati ya vile vipande vya nyama.(Mw 15:9-10)

Siku ile BWANA akafanya agano na Abramu, akasema, Uzao wako nimewapa nchi hii, kutoka mto wa Misri mpaka huo mto mkubwa, mto Frati, (MWA. 15:17-18)
Katika maandiko tuliyosoma hapa juu, tumebaini ”agano la damu” jinsi lilivyokuwa likifanyika enzi hizo. Utaratibu wenyewe ulikuwa ni wa kupasua mnyama vipande viwili na kuvilaza chini vikiwa vinaelekeana, na katikati kuwepo nafasi kati yake. 

Kisha watu wanaofanya agano la damu kupita katikati ya vile vipande viwili vya mnyama aliyepasulikiwa. Na walipokuwa wakipita katikati walitakiwa kuapa wakisema: "na iwe hivi kwangu kama nisiposhika agano hili" Hapa kiapo hiki kilimaanisha kwamba, “Ikiwa aliyefanya agano la damu atakiuka na kulivunja, adhabu yake ni kupasuliwa vipande viwili kama alivyofanyiwa mnyama ambaye wanapita katikati ya vipande vyake!

Lakini kwa kisa hiki kati ya Mungu na Abramu, tunasoma kwamba, tanuru ya moshi na mwenge unaowaka ulipita kati ya vile vipande vya nyama. Hatusomi kwamba Abramu alipita kati ya vile vipande vya nyama! Hii ina maana kwamba, Mungu ndiye aliyepita peke yake na akaapa peke yake. Hapa ndipo penye siri kubwa ya agano la damu kati ya Mungu na binadamu.

Inaonesha Mungu ndiye anayeahidi, na kuapa kutimiza ahadi zake kwa binadamu, pasipo kutegemea mchango wa binadamu katika utekelezaji wa ahadi za Mungu. Mungu amejiweka katika nafasi ya kuwa mwaminifu wa kutimiza ahadi kwa binadamu pasipo binadamu kuchagia kitu chochote kwenye agano la damu.

Tangu hapo hsitoria ya agano la damu inaendelea kwa vizazi vilivyofuatia mpaka wakati wa ujio wa Yesu Kristo mwenyewe. Tusisahau kwamba ujio wa Yesu ilikuwa ni Ahadi ya Mungu kwa Ibrahimu. (Mw.12:3) Na Yesu mwenyewe alipokaribia kwenda kusulubishwa msalabani, alifanya agano la damu yake mwenyewe kwa kutamka kwamba anafanya nasi agano kwa damu yake mwenyewe (MT.26:27-28)

Katika agano la damu ya Yesu, hapakuwepo na makubaliano ya kuandikiana mkataba ambao Yesu alisaini na wanafunzi wake. Yesu atoa tamko na kutoa agizo la kushiriki kikombe cha uzao wa mzabibu kama ishara ya damu yake inayomwagika kwa ajili yetu, lakini sisi hatukuchangia damu yetu kwenye agano hilo.
Itaendelea toleo lijalo

Share on Google Plus

About Gospel Kitaa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.