SOMO: TAFUTA KUJUA NAMNA YA KUSHUGHULIKIA MALANGO YA MJI WAKO (1 & 2)

Mtumishi Gasper Madumla

Bwana Yesu asifiwe…
Mara nyingi tumesikia neno ” malango ” Neno hili ni pana na kubwa sana katika ulimwengu wa roho. Ni bora ukosee kushughulikia vitu vingine kuliko ukosee kushughulikia malango ya mji wako,sababu itakugharimu sana usipo shughurikia malango ya mji wako. Ndio maana mahali hapa siku ya leo tunatafuta kujua namna ya kushughulikia malango ya miji yetu tulikotoka maana kila mmoja wetu ametokea katika mji fulani na yupo katika mji fulani.

Lango ni sehemu ya maingilio na matokeo ya mtu au kitu fulani. Ili uweze kuingia ndani ya jengo basi huna budi kuingia katika lango lake,alikadhalika unapohitaji kutoka katika jengo hilo basi utapitia katika lango hilo hilo.

Kwa lugha nyingine ni kwamba ulipoingilia ndipo utakapotokea kama vile usaa ulipotunga ndipo mwiba ulipochoma,Mfano ikiwa umeingia katika chumba cha mlango mmoja basi ni dhahili utatokea katika mlango huo huo maana huwezi kutokea ukutani.
Hii ni kanuni rasmi ya maingilio na matokeo katika malango,yaani kama ukiwa umeingia katika jengo lenye malango saba,basi hata ukitoka utapitia malango hayo hayo saba,maana huwezi kupaa,ni lazima utatokea kuanzia lango la mwisho la saba kurudi hata lango la kwanza.
Lango la kuingilia halipo tu katika vyumba au nyumba,au jengo fulani hivi,bali sehemu yoyote ile mahali ambapo watu wanaingia na kutoka. Tukiangalia miji yetu,ni ukweli usiopingika kwamba hata katika miji kuna malango,maana watu huingia na kutoka.


Lango lililofungwa sawa sawa.

Kila mji una malango yake kama ilivyo katika jengo.Hata kama mji mdogo vipi lakini lazima uwe na malango yake,tena wala hakuna mji usio na malango yake.
Biblia inatupa picha kamili juu ya hili ikituonesha lango lililopo katika mji wa Sarepta.
Imeandikwa

” Basi, akaondoka, akaenda Sarepta; hata alipofika langoni pa mji, kumbe! Mwanamke mjane alikuwako akiokota kuni; akamwita, akamwambia, Niletee, nakuomba, maji kidogo chomboni nipate kunywa” 1 Wafalme 17:10
Biblia inatuonesha lango lilipo katika mji wa Sarepta,Sarepta ulikuwa na lango la maingilio na matokeo yake. Mwanamke huyu wa Sarepta alikuwa ameketi katika lango la mji,mahali pa maingilio na matokeo yake.
Labda pia tuangalie mji mwingine wenye lango lililotajwa katika biblia,

tunasoma;

” Basi, wale malaika wawili wakaja Sodoma jioni; na Lutu alikuwa amekaa mlangoni pa Sodoma. Lutu akawaona akaondoka akaenda kuwalaki, akainama kifudifudi. ” Mwanzo 19:1
Sodoma nayo ilikuwa ina lako lake,Malaika waliingia Sodoma kupitia katika lango lake la mji. Ikiwa malaika wale waliingia Sodoma kupitia lango la mji,basi hata shetani pia anaweza kuingia kupitia lango la mji huo huo,na ndivyo hali ilivyokuwepo Sodoma.

* Hakuna uasi unaoingia katika mji pasipo kuwa na lango. ili jambo baya au zuri lingie basi linahitaji lango la kupitisha.


Na mtumishi Gasper Madumla.

Bwana Yesu Kristo naye alipoingia katika mji wa Naini ilimpasa apitie katika lango lake,

tunasoma;
” Baadaye kidogo alikwenda mpaka mji mmoja uitwao Naini, na wanafunzi wake walifuatana naye pamoja na mkutano mkubwa.
Na alipolikaribia lango la mji, hapo palikuwa na maiti anachukuliwa nje, ni mwana pekee wa mamaye ambaye ni mjane, na watu wa mjini wengi walikuwa pamoja naye.” Luka 7:11-12
Katika lango la mji wa Naini kulikuwa na roho ya mauti,maana maiti ilisimama mlangoni. Kuna jambo zuri au baya linalosimama katika kila lango. Malango mengine katika miji yamejaa roho za magonjwa,malango mengine husimamisha roho za ufukara,na roho za mafarakano. N.K
Mara nyingi malango ya miji hupitisha roho na wala si watu kama watu,tena malango ya miji inawezekana isionekane katika macho ya damu na nyama ila malango haya yanaonekana katika ulimwengu wa roho…

Bwana Yesu asifiwe…

Fundisho hili ni fundisho lenye maana sana kwako wewe mpendwa pamoja na familia yako yote sababu linakuhusu asilimia mia moja,maana wewe pia umetoka katika moja ya mji na pia upo katika mji fulani hivi sasa.Kama nilivyosema katika miji yote ina malango yake hivyo ni lazima utafute kujua namna ya kuishughulikia milango hiyo.

Dhambi inaweza kusimama katika lango la mji wako ikiwa wazee walitenda dhambi pasipo kuitubia. Jambo hili ndilo lilisumbua ukoo,au mji wa Kaini baada ya Kaini kutenda dhambi ya kumuua ndugu yake Abili ,biblia inasema;

“Kama ukitenda vyema, hutapata kibali? Usipotenda vyema dhambi iko, inakuotea mlangoni, nayo inakutamani wewe, walakini yapasa uishinde. ” Mwanzo 4:7

Dhambi ya Kaini ilisimama mlangoni,hata kama Kaini alikufa hapo baadaye, lakini dhambi haikufa. Dhambi kamwe haifi kwa kufa kwa mtu aliyetenda dhambi pasipo kuitubia sababu dhambi ya mtu aliyekufa ni roho kamili. Kwenye toba ndipo mahali ambapo dhambi haiwezi kuendelea kusimama tena.

Katika maisha ya leo,wengi tunaishi pasipo kushughulikia dhambi zilizosimama katika malango ya miji yetu tukidhani kuwa kwa kuhudhulia kanisani kila siku inatosha ! Nakuambia pasipo kuokoka na kukaa ndani ya Yesu Kristo wa Nazareti,dhambi haitafutika,dawa ni kuokoka na kukaa ndani ya Yesu Kristo.


Sehemu ya 2

Tazama hapo,Kaini alipotenda vibaya dhambi ile ile ikasimama mlangoni na kwa kupitia dhambi ile,ikamuotea kwa mji wake sababu malango ya dhambi ile katika mji wake bado yalikuwa wazi. Jambo hili linaonekana wazi pale Lameki ambaye ni kizazi cha tano cha Kaini katika mji wake,naye anamuua mtu kama vile mzee wao Kaini alivyofanya.

” Lameki akawaambia wake zake, Sikieni sauti yangu, Ada na Sila; Enyi wake za Lameki, sikilizeni usemi wangu; Maana nimemwua mtu kwa kunitia jeraha; Kijana kwa kunichubua; Kama Kaini akilipiwa kisasi mara saba, Hakika Lameki atalipiwa mara sabini na saba. ” Mwanzo 4:23-24

( Maana kizazi cha kaini kimeanzia kwa kizazi cha kwanza yaani Henoko,Iradi,Mehuyaeli,Methushaeli, mpaka kizazi cha tano ambaye ni Lameki -Mwanzo 4:17-18)

Shida hii imeendelea kujitokeza kwa sababu dhambi iliyosimama mlangoni haijashughulikiwa. Wewe ni shaidi mkubwa kwa habari ya dhambi iliyosimama kwenye mji wenu,maana yapo mambo mabaya mliorithi ninyi watoto ambayo hata maasi hayo yalipokuwa yakitendeka ninyi hamkuwepo.

Kumbuka jambo moja kwamba,Lango la mji wako linaweza kupitisha jambo zuri au baya ikiwa malango hayo yapo wazi.

Na malango mengi ya miji yetu ya kiafrika hupitisha maroho machafu,maroho ya kichawi,maroho ya chuki,maroho ya mauti,maroho ya uzinzi na uesharati,kila aina ya maroho machafu yaliyokuwa yakitenda kazi kwa mababu na mabibi zetu ndio hayo tunayotembea nayo sasa.

Ngoja nikupe mfano mmoja ulio hai halisi kabisa;

Ipo familia moja ambayo kila mwaka ni lazima wazike mtu mmoja katika ukoo wao. Kinachofanya watu wafe kila mwaka ni magonjwa,hivyo utaona kwamba familia hii ni jinsi gani inavyopitia katika roho ya mauti iliyosimama katika lango la ukoo wao. Sasa huu ni mfano mdogo sana,maana ipo mifano mingi iliyo hai leo hii.

● Mtu mjanja mwenye kuchoshwa na hii hali ni lazima atafute kujua ufumbuzi wa tatizo hili.

~ Hivi,unajua hata mapepo yanapomwingia mtu hupitia katika moja wapo ya mlango ulio wazi,la sivyo hawana uwezo wowote ule kumwingia mtu aliye safi katika jina la Yesu Kristo wa Nazareti.

Siri hii kubwa ya kushughulikia malango yalio wazi katika mji wako hutambulikana na watu walio rohoni wenye kuumanisha,sababu mambo ya rohoni hutambulikana na watu wa rohoni, la sivyo waweza kufikiri kwamba majanga yote unayoyapata katika familia yako yametokana na Mungu mwenyewe.

Bwana Mungu anamakusudi na wewe siku ya leo. Anataka akufungue katika kila aina ya kamba za laana za ukoo wa mababu zako.

● Mara baada tu ya kuokoka yakupasa kushughulikia malango yote ya mji wenu kwamba wewe umepewa neema ya wokovu katika familia yenu ukayafunge malango yote ya laana,malango yote ya mgonjwa,ukayafunge na kuvunja kila aina ya malango ya madhabahu za kipepo.

Labda niseme hivi kwa lugha nyepesi kwamba pindi mtu anafokufa,hafi na malango yake,malango yake huendelea kubakia. Na ndio maana tunaomba sana pindi mtu akufapo,hatuombei yeye marehemu aliyekufa bali tunaombea milango iliyoachwa wazi.Mungu akusaidie katika kunielewa na kuelewa jambo hili la leo. Ipo gharama katika kushughulikia malango yalio wazi katika mji wako. Kuhudhulia ibada za jumpili kila siku sio solution wala sio dawa ya kushughulikia juu ya malango ya mji wako. Wala kuokoka kwa kuongozwa sala ya toba pekee haifui dafu,yaani bado haitoshi.

Kumbuka milango iliyo wazi kwenye mji wenu ni madabahu tosha za nguvu ya giza yenye kubeba laana. Madhabahu za shetani kamwe hazivunjwi kwa kuhudhulia ibada za kila jumapili,bali zinafunjwa na ibada maalumu yenye kulenga jambo hilo tu.

Ipo njia ya kipekee ya kushughulikia milango ya mji wako,

Katika muendelezo wa fundisho la tatu tutazungumzia njia hiyo ya umuhimu sana,maana ukweli ni kwamba familia nyingi kama si zote zimekamatwa na mateso yaliyosimama katika malango ya miji yetu.

ITAENDELEA…

Usije kukosa muendelezo huu kabisa,maana lipo jambo kubwa mahali hapa litakalokusaidia kushughulikia kila aina ya lango katika mji wako.Kwa huduma ya maombi na maombezi,nipigie kwa namba yangu hii;

0655-11 11 49

Njia kweli na uzima blog 

UBARIKIWE

Share on Google Plus

About Ambwene Mwamwaja

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.