HALAHALA NA HABARI YA MJINI

Elie Chansa,
GK Staff Writer
©Terrain Park Safety
Ni imani yangu ya kwamba umeshausikia huu msemo mara kadhaa. Kama bado, basi maana yake huashiria jambo fulani ambalo limeshika kasi mjini na kuwa gumzo kila kona. Inaweza ikawa toleo la simu, mfumo wa uvaaji, aina ya gari, tukio lililojiri, na kadha wa kadha – ili mradi tu ndicho kitu ambacho kina mashiko mjini (sio lazima mjini).


Pamoja nayo, kuna watu wamekuwa wafuasi wa mlipuko wa mambo, mathalani, kama mtu amesikia kwamba simu fulani ndo habari ya mjini, basi naye atafanya juu chini ili aipate hiyo simu, ili mradi tu naye awemo, ‘asipitwe na wakati’. Akisikia kiatu fulani ndio “catalogue”, basi lazima kibubu kivunjwe ili ardhi ipate kukanywagwa na mguu uliofunikwa na “catalogue”. Ili mradi tu nafsi iridhike. Akisikia kwamba kuna sehemu kuna kilabu kizuri cha kukutana na hata kufanya mawindo, moyo unamruka juu na atakazana hadi afike ili naye apate cha kuhadithia - bila kujua kwamba hapo ni yeye ndiye anatokwa na ROHO.


Lakini hapo ndipo nakumbuka habari ya Safina. Wakati Nuhu anajenga Safina, kwa wananchi wengine habari ya mjini ilikuwa dhuluma na machukizo ya kila namna’. Kwa ujanja wao wa kuendelea na habari ya mjini, waliishia kuangamia baada ya gharika kuruhusiwa, na hapo ndipo walikuja kugundua kwamba hatima ya habari ya mjini ilikuwa angamizo. Walikuwa wamechelewa, hakukuwa na namna ya kurudisha wakati nyuma, dakika moja iliyopo muda huu yafaa kutumiwa vema.


Mke wa Lutu, kwa kutamani mali alizokuwa anaziacha nyuma, aligeuka jiwe la chumvi. Hii ni wakati miji ya Sodoma na Gomora inaangamizwa, huku Lutu na familia yake wakielezwa namna ya kujinusuru na “mambo” ya kuchukiza yaliyokuwa yakiendelea mjini hapo. Kwa waliyokuwa wanafanya wakazi wa miji hiyo, ilikuwa ni burudani tosha machoni pao, ndiyo iliyokuwa habari ya mjini - ambayo iligeuka kuwa kiama chao.

Hata sasa, inaonekana habari ya mjini ni kuwa na akaunti nje ya nchi, licha ya kwamba huenda kuna ubadhirifu mwingi hadi kufikia ‘kuhifadhi’ pesa 'Uswisi'. Mkumbo huohuo wa kuwanyonya wasio nacho na kujilimbikizia ndio utaondoa uwepo wa BWANA mahala tunapoishi. "Afadhali mali kidogo pamoja na haki, Kuliko mapato mengi pamoja na udhalimu." Mithali 16:8 imeainisha.

Wacha nimalize kwa kukukumbusha kuwa sio kila jambo unaloliona lafaa kuigwa. Usione mitindo mipya ya nywele ukairukia bila kujua ina maana gani. Usione hao wanaoitwa “vioo vya jamii” wamevaa suruali zilizoachia nafasi utafiriki wanasafirisa taka kama yale 'magari maalum' nawe ukataka kuvaa kama wao. Usione mabinti mtaani kila mmoja ana mtoto asiyemjua baba yake, nawe ukataka hiyo sifa uwe nayo kisa tu wanakusema vibaya kwa kutoendana na fashion ya 'single mothers'

Nukuu mojawapo ambayo hunikumbusha kusimamia kile ninachokiamini kwa mujibu wa muongozo mama (Biblia), inatoka kwa Anatole France, mwandishi wa kale huko Ufaransa. Yeye aliwahi kusema, “If fifty million people say a foolish thing, it is still a foolish thing”. Ukiambiwa sema ndiyo wakati unaona hili jambo ni la kipumbavu, wewe fanya maamuzi yako sahihi.


Habari ya mjini isikuweke kando na Mungu. "Kwanza jijue we ni nani, na unakwenda wapi. Kisha tazama maishani umezungukwa na nani", anasema Angel Benard kwenye wimbo wake wa Linda. Jihadhari na hao wanaoonekana kuwa marafiki zako, tambua ndoto yako ni ipi, isije ikazimwa nao kisa kufuata mkumbo.

BWANA Yesu na atusaidie sote.

elie@inhouse.co.tz
0713554153
Share on Google Plus

About Gospel Kitaa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.