HOTUBA YA RAIS KIKWETE KWENYE UZINDUZI WA SERA YA ELIMU NA MAFUNZO YA MWAKA 2014

Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akizindua Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 katika hafla iliyofanyika katika shule ya sekondari Majani ya Chai, Kipawa jijini Dar es Salaam Februari 13,2015 .Kushoto ni Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Dkt.Shukuru Kawambwa, na kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Bwana Said Meck Sadik ©Ikulu
Makamu wa Rais Mheshimiwa Dkt. Mohamed Ghalib Bilal;
Waziri Mkuu Mheshimiwa Mizengo Kayanza Peter Pinda;
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Mhe. Dkt. Shukuru Kawambwa;
Waziri wa Nchi OWM- TAMISEMI, Mhe.  Hawa A Ghasia;
Naibu Waziri wa Elimu– OWM-TAMISEMI, Mhe. Kasimu Majaliwa;
Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Mhe. Anne Kilango Malecela;
Waheshimiwa Mawaziri wote mlioko hapa,
Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Mheshimiwa Said Meck Sadiki;
Katibu Mkuu Kiongozi , Balozi Ombeni Sefue,
Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi;
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi;
Naibu Katibu Mkuu –OWM-TAMISEMI;
Katibu Mkuu- OWM-TAMISEMI;
Mabalozi
Wahisani wa Maendeleo;
Wakurugenzi wa Wizara na Wakuu wa Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi;
Viongozi mbalimbali wa Chama na Serikali;
Walimu, Wanafunzi, Wanahabari,
Mabibi na Mabwana.

Leo ni siku muhimu katika historia ya maendeleo ya elimu nchini.  Tunakutanishwa kwa ajili ya kufanya jambo kubwa, la kihistoria na la kimaendeleo la uzinduzi wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014.  Uzinduzi wa Sera mpya unaashiria mwanzo wa ngwe mpya katika safari ya kuimarisha, kuendeleza na kuipaisha elimu nchini kufikia viwango vya juu vya kukidhi ubora na mahitaji ya taifa.  Ni kielelezo cha utashi na azma yetu ya kuboresha mfumo wetu wa elimu uende na wakati na kuiwezesha jamii kuzikabili ipasavyo changamoto na maendeleo na maisha yao.  Maisha bora kwa Mtanzania yanaanzia na kutegemea uwezekano wa kila Mtanzania kupata fursa ya kupata elimu iliyo bora, elimu itakayomuwezesha kutawala mazingira yake na kukabili changamoto za maisha.

         Nakupongeza sana Mheshimiwa Waziri, Dkt. Shukuru Kawambwa,  Katibu Mkuu, Prof. Sifuni Mchome pamoja na wataalamu wenu na wadau wengine wa elimu kwa kuongoza na kusimamia mchakato huu ulioanza kwa kupitia Sera mbalimbali zilizokuwapo katika sekta ya Elimu na kuzihuisha kwa kuandaa Sera hii.  Napenda pia kumtambua Naibu Waziri, Mheshimiwa Anne Malechela Kilango pamoja na upya wake katika Wizara.

Mheshimiwa Waziri;
 Nakushukuru pia kwa uamuzi wenu wa kuzindua Sera hii katika eneo la shule.  Tunapata fursa maridhawa ya kuoanisha kile kilichopo na kile tunachoazimia kutekeleza kwenye Sera.  Nimepata fursa ya kutembelea maabara na kuwaona vijana wetu wanavyopata elimu ya sayansi kwa vitendo.  Aidha, mnanipa nafasi ya kusema na walimu na wanafunzi ambao ndiyo wadau wakuu wa Sera hii ya Elimu.  Ni jambo la faraja kwangu kuona tulipofikia na mafanikio tuliyoyapata, kama haya niliyoyaona katika shule hii.  Inatupa kila aina ya sababu kuongeza bidii na kasi zaidi ya kufikia malengo makubwa zaidi.

         Vilevile, nakushukuru,  Mheshimiwa Waziri, kwa maneno yako ya utangulizi kuhusu Sera hii.  Kama ulivyokwishasema, Sera hii ni matokeo ya mapitio na uhuishaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 1995, Sera ya Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya mwaka 1966 na Sera ya Taifa ya Elimu ya Juu ya mwaka 1999.  Kipindi cha zaidi ya kipindi cha miaka 14 ya utekelezaji wa sera hizo na maamuzi mengine kuhusu elimu kimekuwa cha mabadiliko mengi ya kijamii, kiuchumi na teknolojia ndani na nje ya nchi.  Uchumi wetu umekua na kutanuka na kuzua mahitaji mapya ya rasilimali watu na stadi mbalimbali ambazo hazikuhitajika siku za nyuma.  Aidha, mipango mitatu ya miaka mitano ya maendeleo kuelekea mwaka 2025 nayo imezaa mahitaji mengine.  Yote haya pamoja na maoni ya wadau mbalimbali yamezingatiwa katika Sera hii ya mwaka 2014.

Hali ya Sekta ya Elimu
Mheshimiwa Waziri;
Ndugu Wadau wa Elimu;
         Elimu ni kitu kinachomgusa na kumhusu kila mtu hapa Tanzania.  Sisi katika Serikali, tunatambua wajibu wetu na nafasi yetu maalum kwa upatikanaji wa elimu nchini.  Kwa ajili hiyo, elimu ni jambo la kipaumbele cha juu, ni la kufa na kupona.  Ukweli wa usemi wangu huo unajihidhirisha katika uwekezaji mkubwa tunaoufanya katika kuendeleza elimu.  Bajeti ya Elimu ndiyo iliyo kubwa kuliko zote kwa miaka mingi  na imekuwa ikiongezeka.  Kwa mfano, mwaka 2005/2006 zilitengwa shilingi bilioni 669.5 wakati mwaka 2014/2015 zimetengwa shilingi trilioni 3.1.  Katika kipindi hicho, bajeti ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu imeongezeka kutoka  shilingi bilioni 56.1 hadi shilingi bilioni 345. Kwa sababu hiyo idadi ya wanafunzi wanaofaidika imeongezeka kutoka 16,345 mwaka 2005 hadi 98,000 mwaka 2014.  Shule za msingi zimeongezeka kutoka 14,257 mwaka 2005 hadi 16,343 mwaka 2014 na hivyo kufanya idadi ya wanafunzi nayo kukua kutoka milioni 7.54 hadi milioni 8.23.  Kwa upande wa sekondari shule zimeongezeka 531 mwaka 2005 hadi 4,576  mwaka 2014.  Idadi ya wanafunzi nayo imeongezeka kutoka 524,325 mwaka 2005 hadi 1,804.056 mwaka 2014.

Upanuzi huu mkubwa na wa kihistoria  umetokea pia kwenye vyuo vya elimu ya ufundi stadi ambapo vyuo vimeongezeka kutoka 184  hadi 744 kati ya mwaka 2005 na 2014.  Kwa upande wa elimu ya juu, idadi ya vyuo imeongezeka kutoka 26 hadi 50 kati ya mwaka 2005 na 2014 na kufanya idadi ya wanafunzi wa vyuo vikuu iongezeke kutoka wanafunzi 40,719 mwaka 2005 hadi wanafunzi 200,986 mwaka 2014.  Leo hii tunapokutana hapa, hatuna tena tatizo na fursa ya kupata elimu kwa elimu ya msingi,  sekondari, ufundi na elimu ya juu.

Mwaka 2005, urari wa wanafunzi kati yetu na wenzetu wa Afrika Mashariki ulikuwa wa chini mno kwa upande wetu.  Kenya walikuwa na wanafunzi wa sekondari 925,341 na wa vyuo vikuu 108,407  ikilinganishwa na Tanzania iliyokuwa na wanafunzi 524,325  wa sekondari na 40,719 wa vyuo vikuu.  Uganda ilikuwa na wanafunzi 728,393 wa sekondari na 124,313 wa vyuo vikuu.  Sasa hali ni tofauti.  Kwa mwaka 2013, kwa mfano, Kenya ilikuwa na wanafunzi wa sekondari 2,104,300 na wanafunzi wa vyuo vikuu 324,600.  Katika mwaka huohuo, Uganda walikuwa na wanafunzi wa sekondari 1,362,739 na wa vyuo vikuu 140,403.  Ongezeko hili linatuweka katika hali nzuri ya ushindani tunapoelekea katika ushindani wa soko la pamoja ndani ya Afrika Mashariki ikilinganishwa na hali ilivyokuwa miaka 10 iliyopita.  Jukumu letu ni kuimarisha ubora wa elimu yetu na hasa iwe ni ile inayokidhi mahitaji ya soko la ajira nchini, Afrika Masharini na dunia.
 Juhudi zetu hizi za kuendeleza elimu zimetambulika duniani na kutupatia heshima kubwa zikiwemo tuzo mbalimbali.  Tumekuwa nchi ya kupigiwa mfano katika kutekeleza Malengo ya Milenia (MDGs) yanayohusu fursa ya watoto kupata elimu ya msingi, na usawa wa kijinsi baina ya watoto wa kiume na wa kike kupata elimu ya msingi na sekondari.  Haya na mengine mazuri tuliyofanya ni mambo ya kujivunia.  Ni mafanikio yanayotokana na utekelezaji mzuri wa Sera tatu za elimu ya Msingi, Ufundi na Elimu ya Juu zilizokuwepo.

Ndugu Wadau wa Elimu;
         Mafanikio hayo makubwa nayo yamezua changamoto mpya mbalimbali.  Miongoni mwake ipo ile ya malengo ya Elimu kuwa sawa na goli linalohama kila unapolikaribia.  Hali hii haipo hapa nchini kwetu pekee, bali ipo kote duniani.  Nimebahatika kutembelea nchi nyingi na kuona yanayofanyika. Hali kadhalika nimesoma yanayoendelea kwenye nchi mbalimbali kuhusu elimu.  Ukweli ni kwamba hakuna nchi duniani ambayo imemaliza changamoto zote zihusuzo elimu.  Katika kila nchi kuna mjadala unaoendelea kuhusu ubora wa elimu.  Na, sababu ni moja, uboreshaji wa elimu ni jambo endelevu.  Iko hivyo kwa nchi zinazoendelea kama yetu na hata zile zilizoendelea.  Tofauti yetu ipo kwenye aina ya changamoto zilizopo.  Nchi zilizoendelea hazina matatizo yanayozikabili nchi zinazoendelea.

Ni jambo la kutia moyo kuwa tangu uhuru mpaka sasa matatizo mbalimbali yanayoisibu elimu yametambuliwa na kushughulikiwa.  Katika awamu hii ya uongozi wa nchi yetu tumetoa msukumo maalum tena mkubwa katika kutafuta majawabu ya changamoto zinazokabili sekta ya elimu nchini.  Bahati nzuri tumepata mafanikio kwenye nyanja nyingi.  Nimekwishaelezea jinsi idadi ya shule za msingi na sekondari pamoja na vyuo vya ufundi na vyuo vikuu vilivyoongezeka.  Mambo hayo yameongeza sana fursa za elimu nchini.  Hivi leo watoto wote wenye umri wa kwenda shule wanaweza kuwa shule labda wakatae wenyewe au wakatazwe na wazazi au walezi wasioona mbali.  Watoto wote wanaofaulu darasa la saba wana hakika ya kwenda sekondari na vyuo vikuu vina nafasi wazi zinazosubiri wanafunzi wenye sifa kuzijaza.

Kimsingi tunaweza kusema kuwa suala la watoto  na vijana wetu chini kupata fursa ya kupata elimu inayolingana na umri wao siyo tatizo kubwa tena la kutuumiza vichwa.  Hata hivyo, kazi kubwa inayohitajika kuendelea kufanyika ni kuhakikisha kuwa elimu wanayopata watoto na vijana wetu ni bora.  Kwa ajili hiyo, hatuna budi kuendelea kuboresha mazingira ya kutolea elimu.  Walimu wa kutosha wawepo kwa masomo yote.  Tena wawe ni walimu wanaoyamudu vyema masomo wanayofundisha.  Hali kadhalika, huduma za msingi kwa maisha na utendaji kazi wa walimu ziboreshwe pamoja na maslahi yao.

Vifaa vya kufundishia na vile vya kusomea na kujifunzia vipatikane kwa uhakika.  Majengo ya kufundishia na huduma mbalimbali shuleni na vyuoni yawepo ya kutosha tena yaliyo bora.  Pamoja na hayo, mifumo na miundo ya uendeshaji na usimamizi wa elimu nchini iendelee kuboreshwe zaidi na zaidi.

Sera Mpya na Matumaini Mapya

Ndugu Wadau wa Elimu;
         Sera Mpya ya Elimu inatupa mwanzo mpya na matumaini mapya ya kututoa hapa tulipo sasa na kutupeleka mbele kwenye neema na mafanikio makubwa zaidi.  Mahali ambapo nyingi ya changamoto zinazotukabili sasa zitakuwa hazipo ila zitakuwepo zile za kupeleka elimu yetu mbele zaidi.  Sera mpya inatambua umuhimu na nafasi ya elimu kwa maendeleo ya nchi yetu na watu wake.  Sera inatambua kuwa Elimu ni silaha ya ukombozi kwa Watanzania dhidi ya umaskini na madhila yake.  Ni nyenzo ya uhakika ya kutupeleka kwenye uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.   Kwa sababu hiyo, Sera inasisitiza umuhimu wa kuendelea kupanua fursa kwa kila mtoto mwenye umri wa kwenda shule aende shule.  Sera Mpya inatoa dhima kwa taifa kuanza safari ya kumuwezesha kila mtoto anayeanza darasa la kwanza aweze kupata elimu ya sekondari ya mpaka kidato cha nne.  Hili ni lengo la muda mrefu kwamba elimu ya msingi iwe mpaka kidato cha nne badala ya darasa la saba kama ilivyo sasa.  Hili ni lengo ambalo halitakamilika mara baada ya uzinduzi huu.  Yanahitajika maandalizi makubwa.  Katika kuanza safari ya kuelekea huko, Serikali imeamua kufuta ada ya elimu ya sekondari kuanzia mwaka 2016 ili wale waliofaulu kwenda kidato cha kwanza wasishindwe kusoma.

         Sera Mpya ya elimu imeweka msisitizo wa pekee kwa kila mtoto kupata elimu ya awali kabla ya kupata elimu ya msingi.  Tumedhamiria pia kuwekeza zaidi katika stadi za Kuandika, Kusoma na Kuhesabu (KKK) katika miaka miwili ya elimu ya msingi.  Azma yetu ni kujenga msingi imara wa elimu kwa wanafunzi nchini ambao hutegemea sana upatikanaji wa stadi hizo.  Watoto wanapoimarishwa vya kutosha kwa upande wa kusoma, kuandika na kuhesabu, aghalabu humudu vyema masomo yao shuleni.  Aidha, itasaidia kurekebisha upungufu uliopo sasa.

Ndugu Wadau wa Elimu;    
Ni ukweli ulio dhahiri kwamba ili tuweze kupata maendeleo makubwa ya kiuchumi lazima tuongeze matumizi ya sayansi na teknolojia nchini.  Tunaweza kufanya hivyo tu kwa kuwa na wanasayansi wengi.  Sera hii inasisitiza kuimarishwa kwa muundo na utaratibu wa ufundishaji wa masomo ya Hisabati, Sayansi na Teknolojia katika ngazi zote.  Kazi hii tayari tumekwishaianza na tunaendelea nayo kwa ari na nguvu.  Tumetoa msukumo mkubwa katika ujenzi wa maabara na naamini, Juni, 2015 tutafikia malengo yetu.

Tunapanua mafunzo ya walimu wa sayansi.  Tutakapotekeleza mradi wa matumizi ya computer mashuleni tutakuwa tumepiga hatua kubwa muhimu.  Sera hii imetoa mwongozo kwa changamoto nyingine nyingi muhimu ambazo zimetolewa maoni na wadau mbalimbali.  Kwa mfano, Sera inaelekeza sasa kutumika kwa utaratibu wa kila somo kitabu kimoja kwa shule zote badala ya utaratibu wa awali wa kila shule kuwa na kitabu chake.  Sera inatoa msisitizo kuwa elimu ni huduma na inaelekeza kuwekwa kwa utaratibu utakaodhibiti upangaji wa ada katika shule za binafsi kwa utaratibu wa kuweka ada elekezi (indicative fees) kwa msingi wa gharama halisi kwa mwanafunzi (Student Unit Course).  Hii itatoa ahueni kwa wazazi na walezi na kuwawezesha kumudu gharama za kusomesha watoto wao katika shule za binafsi.

         Suala la ubora wa elimu inayotolewa tumeliwekea mkazo wa kipekee katika sera hii mpya.  Tutaimarisha mfumo wetu wa usimamizi na ukaguzi wa shule zetu kwa lengo la kuimarisha ubora wa elimu inayotolewa.  Tutajenga uwezo wa Wizara kwa kutenga fedha za kutosha kwa shughuli za ukaguzi, kuajiri wakaguzi wa kutosha na kuwapatia vitendea kazi vya kuwawezesha wakaguzi kufanya kazi zao kwa ufanisi nchi nzima.  Madhali tumeshapata mafanikio ya kutosha kwenye kupanua fursa ya kupata elimu, sasa tunaelekeza nguvu zetu kwenye kusimamia ubora wa elimu inayotolewa.

Wito kwa Wadau

Mheshimiwa Waziri;
Ndugu Wadau wa Elimu;
         Mafanikio yote tuliyoyapata katika Sekta ya Elimu yamepatikana kutokana na ushirikiano wa wadau wote wakiwemo walimu, wazazi, wananchi wetu wote na wadau wa maendeleo.  Mafanikio haya hayana budi kuenziwa na kuendelezwa.  Tunapoanza utekelezaji wa Sera Mpya ya Elimu, hatuna budi kukumbushana tena wajibu wetu na kushirikiana kufikia malengo yetu haya mapya.
         Mdau mkubwa wa kwanza katika elimu ni mzazi na mlezi ambao ndiyo viongozi wa kaya wanazotoka wanafunzi wetu.  Ninyi mnao wajibu wa kipekee wa kuwahamasisha na kuwahimiza watoto wenu kupenda shule kwa kuwajengea mazingira mazuri ya kuwawezesha kusoma.  Jihusisheni na elimu ya watoto wenu, na jengeni uhusiano na walimu wao katika kufuatilia maendeleo ya watoto wenu.  Wakati mwingine inashangaza sana kuona wazazi na walezi kutojali kujua maendeleo ya watoto wao shuleni.  Hawakagui maendeleo yao, wala hawajihusishi na kamati za elimu za shule za watoto wao na kata wanazoishi.  Njia bora ya kutatua changamoto za elimu za nchi ni kwa kila mmoja wetu kushiriki katika kutatua changamoto zilizoko katika shule iliyoko katika eneo lake analoishi.

         Walimu ni wadau wenye wajibu wa kipekee sana.  Jukumu lao la kuwafumbua macho na kuwaongezea upeo wa ufahamu wa vijana wetu pamoja na kuwandaa kuwa raia wema halina mfano wake.  Halina badala yake.  Mnafanya kazi nzuri lakini mnatakiwa kufanya vizuri zaidi leo na siku za usoni.  Elimu ni kitu chenye unyumbufu mkubwa na mabadiliko mengi na hasa siku hizi.   Lazima muende na wakati.  Ni ninyi waalimu, pengine kuliko watu wengi wengine  mtakaoumba Tanzania ya kesho iliyo bora kupitia elimu mnayowapa wanafunzi.  Ninyi walimu ndiyo wa kutusaidia kuleta mabadiliko chanya katika jamii na nchi yetu.  Nawaomba sana muendelee kujizatiti katika kutambua uzito wa majukumu yenu na kuyatekeleza.  Sisi Serikalini tutaendelea kufanya kila lililo katika uwezo wetu kuboresha maslahi yenu na mazingira yenu ya kazi.

         Nawaomba pia wamiliki wa shule, hususan shule zinazomilikiwa na mashirika ya dini na watu na makampuni binafsi nanyi mtimize ipasavyo wajibu wenu.  Tunatambua na kuthamini mchango wenu mkubwa katika utoaji wa elimu.  Nawaomba mkumbuke kuwa Elimu ni haki ya mtoto hivyo mjiepushe na upendeleo na ubaguzi. Elimu ni huduma, hivyo mtoze ada zinazohimilika.  Aidha, hamna budi kuzingatia mitaala na miongozo inayotolewa na Wizara ya Elimu na Taasisi zake kuhusu elimu.  Serikali inawahakikishia kuwa tutaendelea kuweka mazingira rafiki ya kuwawezesha kutimiza wajibu wenu huo wa kutoa huduma ya elimu.  Ni kwa sababu hiyo tumewatambua katika Sera hii na mmeshirikishwa kwa ukamilifu katika mchakato wote wa kuitunga.  Naomba tuendeleze ushirikiano wetu katika utekelezaji wa Sera hii.

         Sina budi kuwashukuru pia wadau wetu wa maendeleo kwa michango yao muhimu iliyotuwezesha kufikia mafanikio makubwa katika Sekta ya Elimu. Tunapowashukuru, tunawaomba waendelee kushirikiana nasi tunapoianza safari yetu hii ya kutekeleza Sera Mpya ya Elimu.  Utekelezaji wa Sera hii utahitaji rasilimali nyingi na hivyo tutashukuru kupata mchango wao katika kuongezea nguvu jitihada zetu.  Mchango wao utatuwezesha kupata matokeo makubwa kwa haraka.

Hitimisho

Mheshimiwa Waziri;
Ndugu Wadau wa Elimu;
         Ni jambo la faraja kubwa kwangu kwamba, katika kipindi changu cha uongozi kwa ushirikiano wetu tumeweza kupata mafanikio makubwa na ya kujivunia katika kuendeleza Elimu nchini.  Sera hii tunayoizindua leo ni mojawapo ya mafanikio hayo.

         Naamini kuwa tuliyoyafanya yamechangia kwa kiasi kikubwa kuzikomboa kaya nyingi kutokana na kutoa fursa kwa watoto wengi zaidi wa Watanzania kupata elimu ikiwa ni pamoja na watoto wa kike.  Bado tunayo kazi kubwa ya kufanya mbele yetu. Bahati nzuri, tunayatambua na tunaendelea kuyafanya.  Sera ya Elimu tunayoizindua leo inatoa mwongozo na kutupa mwelekeo mzuri wa namna ya kufanya yanayotakiwa kufanyika sasa na miaka 10 ijayo.    Uzinduzi wa Sera hii mpya ya elimu, na yale yaliyomo katika sera hii ni ushahidi tosha wa dhamira yangu na ya wenzetu wote tulioshirikiana kutayarisha sera hii kuona elimu nchini ianzidi kuimarika na kuwa bora zaidi.

         Napenda sasa, kwa heshima na taadhima kubwa kutamka kuwa Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 imezinduliwa rasmi.
         Asanteni sana.

Chanzo: Ikulu
Share on Google Plus

About Gospel Kitaa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.