KUKOSA MAONO NI SABABU YA KUSHINDWA KWAKO (2)


Mwalimu Kelvin Kitaso,
GK Guest Writer.


Wiki iliyopita tulitazama dhana nzima ya neno Maono, na kisha kuingia ndani zaidi kuona namna ambavyo kadri maono yanavyokuwa makubwa, ndivyo ambavyo taabu huwa kubwa zaidi. bofya hapa kusoma mwanzo wa somo hili. Leo basi na tunaendelea kutokea tulipoishia.
Mfumo wa kuzaa kwa viumbe
Nikiwa na rafiki yangu tunazungumza na kutiana moyo kwa habari ya safari tuliyonayo, akazungumza neno jema sana kuhusu maono kwa kufananisha na wanyama; kwamba wanyama wadogo hubeba mimba na kujifungua kwa muda mfupi; wengine huwa miezi mitatu (3), wengine ni sita (6) na wengine ni tisa (9). Tofauti huwa kwa wanyama wakubwa kama tembo. Wao hubeba mimba kwa muda mrefu sana ukilinganisha na wanyama wengine, hii ni kwa sababu ya ile asili yao ya ukubwa ambayo Mungu amewawekea.
Kwa kuutazama mfano huu ndivyo ilivyo kwa sisi wanadamu ya kuwa maono makubwa huweza chukua muda mrefu sana kabla ya kutoka na mtu mwenye maono makubwa huchukua muda mrefu pia kufikia utimilifu wa maono yale. Usiumie kwa nini wengine wanatoka upesi na wewe unapambana ila bado; fahamu aina ya maono uliyobeba pengine ni mazito kama mimba ya tembo na kama ndivyo yaweza kaa muda mrefu hata utimilifu wake ila yatatokea tu kwa kuwa maono ni kama mimba.
Mbali na wanyama pia kwa mimea kuna neno jema la kujifunza kwa kuwa kuna miti ambayo hupandwa na kukua kwa muda mfupi na huvunwa ndani ya muda mfupi huo ila kuna mimea ambayo hukaa sana na huchukua miaka mingi sana hata kufikia utimilifu wake. Kwa kuchukulia mifano kama mnazi. Hata mbuyu hukaa kwa kitambo kirefu sana hata kuja kutoa matunda yake. 
Hii inaonyesha kuna utofauti mkubwa sana wa utimilifu wa maono ya mtu mmoja mpaka mwingine. Kuna wengine ambao hushuhudia utimilifu wa maono yao kwa haraka sana ukilinganisha na wengine. Muda wa kuchelewa kwa maono ya mtu, Ibilisi huutumia sana kuwa shawishi watu kuona kuwa Mungu hayupo pamoja nao, na uweza sema, mbona hujabarikiwa kama fulani na fulani na wewe unamtumikia Mungu kama wao, au ulimaliza nao chuoni au shuleni au ni marafiki wa karibu ukishiriki nao mengi sana ila wao wamekupita kufanikiwa kwa kuwa Mungu hajali mambo yako na huwapenda wenzako kuliko wewe; wewe usikatishwe tamaa na sauti ya kinyonge namna hiyo songa mbele maana utimilifu wako unakuja na ufanikiwaji wa mtu mmoja na mwingine huwa tofauti na kwa nyakati tofauti tofauti. 
Mtu mwenye maono hawezi kutulia hata atimize maono aliyonayo na hata akishindwa mara moja huinuka na kujitia nguvu na kutokata tamaa na ni maono ambayo humsaidia mtu kuishi kwa kuukomboa wakati, kuweka vipaumbele vya maisha ambavyo vitampelekea kufikia utimilifu wa maono hayo, kuchagua watu sahihi wa kuambatana nao ambao watamsaidia kufikia hatima ya maisha yake.
 
Kutokuwa na vipaumbele katika maisha.
Kukosa maono kunapelekea mtu kushindwa kujizuia na huku kushindwa kujizuia ndiko kutokuwa na vipaumbele. Mtu yeyote mwenye maono ni lazima atakuwa na vipaumbele vya msingi katika maisha yake na vipaumbele hivyo humpelekea kufikia utimilifu wa maono aliyonayo.
Vipaumbele ni vitu ambavyo hupewa umuhimu wa hali ya juu na hupewa umakini mkubwa zaidi ya vitu vingine vyote. Na vitu hivi uweza chukua muda mwingi wa mtu kuliko vitu vingine vyote, na mtu huwa makini sana kutoruhusu vitu vingine ambavyo vitaharibu utaratibu uliopo. Vipaumbele hupelekea utimilifu wa maono aliyonayo mtu na humfanya mtu kuzingatia kuwa sehemu sahihi, wakati sahihi na watu sahihi.
Kwa mfano, mwanafunzi awapo shuleni ni lazima awe na vipaumbele vya msingi kama kumtumikia Mungu kama balozi wa Yesu katika eneo asomalo na kusoma kwa bidii zote kwa kuwa ni jukumu la msingi pia lililompa kuwepo mahali hapo. Na si kwa wanafunzi tu bali hata aliyepo kazini ni lazima awe na vipaumbele vya msingi vitakavyompelekea kufanikiwa katika kufikia hatima yake iliyo njema.
Asiye na vipaumbele hufanya mambo yake pasipo mpangilio na huwa ni mtu asiye na misimamo juu ya yale ayafanyayo na pia hukosa kujitoa kikamilifu katika mambo ayafanyayo.
Katika vipaumbele ni vyema kuzingatia kuwa kila jambo katika ulimwengu huu lina majira yake, na nyakati zake na utambuzi huu utamfanya mtu kufanya kitu sahihi katika wakati sahihi na kuepuka kufanya jambo ambalo lipo nje ya wakati.
MAMBO YA MSINGI KATIKA KUFANIKISHA VIPAUMBELE VYAKO.
·    Chagua marafiki sahihi.
·    Kuwa mahali sahihi, sehemu sahihi na ukifanya jambo sahihi.
· Kila jambo ulifanyalo zingatia wakati kwa kuwa kila jambo lina wakati wake na majira yake/ukomboe wakati.
·    Ishi kwa malengo, timiza malengo yako.
·    Usiishi maisha ya kuigiza, ishi maisha yako.
·    Tumia vyema fedha uzipatazo hata kuweka akiba ya kukusaidia baadae.
·   Kuwa hodari na moyo wa ushujaa/ usiogope kwa kuwa yapo mengi yaogopeshayo ila sababu ya kutoogopa ni kuu zaidi ya hayo yote.
·     Mwamini Mungu.
·     Jiamini wewe mwenyewe kuwa unaweza.

Matumizi mabaya ya muda.

Kukosa maono pia kunamsababisha mtu kutotumia muda wake vizuri. Hii ni kwa sababu hana kitu kinachomchochea kutumia vizuri muda wake kwa kuwa maono ni kama muongozo unaomchochea mtu kufanya kazi. Kuna msemo unasema, ‘Time wasted, life wasted’ kwa kumaanisha kuwa kupoteza muda ni kupoteza maisha. Hii ni kwa sababu muda kamwe hauwezi kujirudia yaani ukienda umeenda. Kila saa tulipatalo hapa chini ya jua twapaswa kulitumia vyema kwa kuwa halitokuja kurudi tena na haliwezi kukusubiri wewe kutokana na uzembe au kutojitambua kwako.

Matumizi mabaya ya muda ni pamoja na kujishughulisha na kufanya mambo ambayo hayatakusaidia kufikia malengo yako, kwa mfano kutumia muda mwingi kuangalia tamthilia, filamu na kufanya michezo mingi isiyo na mchango wowote wa kukufanya ufanikiwe katika maisha yako.

Hii hutokea kwa vijana wengi sana kuwa na matumizi mabaya ya muda kwa kutazama mifululizo ya matamthilia kwa muda mwingi na wengine hutumia hata muda wa kusoma au kazi na muda wa kumfanyia Mungu ibada, wengine pia humaliza muda wao mwingi kucheza magemu ambayo huchukua muda mwingi pia sana, na wengine hutumia muda mwingi katika mitandao ya kijamii. Vitu vyote hivi huwa na uzuri wake na ubaya wake na huweza msaidia mtu au kumuharibu kabisa; ila ni vyema kuzingatia sana muda kwa kufanya mambo ya msingi zaidi ambayo husaidia katika kufikia mambo ya msingi na hata kugundua mambo makubwa. Wengine wamekuwa wakiamini kuwa hawawezi kugundua mambo makubwa ila tatizo moja wapo ni matumizi mabaya ya muda.

“ukitaka kufanya mambo makubwa na yakatokea na kuushangaza ulimwengu, hata kuweka historia ya kuishi kwako kwa kugundua na kufanya mambo makubwa ambayo wengine hawayafanyi ni lazima uwe makini katika matumizi ya muda wako kwa faida na kwa busara kwa kukwepa kila kitu kisicho na faida”

Kwa Waafrika suala la matumizi mabaya ya muda kwao limekuwa ni kawaida sana na watu wengi wamekuwa na tatizo la kutoheshimu muda. Kuna msemo ambao umekuwa ni kichocheo kikubwa cha watu kushindwa kutumia muda wao vizuri, na kichocheo hiko ni neno ambalo hupendwa sana kutumiwa haswa nchini Tanzania lisemalo, “muda wa kizungu, na muda wa Kiswahili/Kiafrika.” Maneno haya yamesababisha watu wengi kuendelea na tabia ya matumizi mabaya ya muda katika miadi/mapatano yao na mambo mengine mengi tu. Katika matumizi ya muda waswahili wakitaka kuanza shughuli saa 3:00 hutoa taarifa kuwa tukio litaanza saa 3:00 ya kizungu na huamini kuwa saa 3:00 ya Kiswahili katika miadi ni sawa na saa 4:00 ya Kiswahili au hutoa taarifa kuwa tukio linaanza saa 2:00 wakijua kuwa watu watachelewa mpaka saa 3:00 ndo waanze. Tiba ya tabia hii ni kuanza katika muda wa mapatano hata kama watu wamechelewa kwa kufanya hivyo siku nyingine itafanya wawahi zaidi. Matumizi mabaya ya muda umfanya mtu kutofikia mambo mengi na kuyafanya kwa usahihi. Si kweli kuwa kuna muda wa kizungu na muda wa Kiswahili, ni vyema kwa kila mmoja kuzingatia matumizi ya muda na kuheshimu matumizi hayo.

Mungu Anaona Ambayo Wengine hawaoni juu yako.

Ikiwa Mungu aliona taifa kubwa ndani ya Yakobo mchunga mifugo wa Labani, akaona Waziri Mkuu ndani ya Yusufu mfanya kazi wa ndani na mfungwa kule Misri, akaona mkombozi wa Israeli kwa Musa mchunga mifugo kule Midihani kwa Kuhani Yethro, Akamwona Mwamuzi wa Israeli Gideoni yeye ambaye alikuwa dhaifu na kutoka katika familia ya hali ya chini sana, Akamwona Yefta aliyekataliwa na ndugu zake na kumfanya kuwa mwamuzi wa wana wa Israeli, Akaona Mfalme wa Israeli ndani ya Daudi Mchunga mifugo na hakutazamiwa hata na baba yake, Akaona Mwokozi wa ulimwengu na Mfalme wa mataifa katika Zizi la Ng’ombe (Yesu), Leo hazuiwi na hali uliyonayo wewe kukufanya mtu mkubwa, usiache kumtumaini ni lazima atafanya alichokusudia kwako.

Somo hili ni sehemu ya kitabu kiitwacho "Huyu Ndiye Adui wa Mafanikio Yako". Mwandishi anapatikana kupitia  0769190019/0713804078, kitasokelvin@gmail.com

Share on Google Plus

About Gospel Kitaa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.