SOMO: AGANO LA DAMU (2)


Askofu Sylvester Gamanywa
Leo tunaingia sehemu ya pili ya uchambuzi wa hoja ya agano la damu. Tulianza na utangulizi na tukapitia Historia fupi ya agano la damu kwa mujibu wa Biblia. Leo tunaingia katika uchambuzi wa mfano ya agano la damu jinsi ulivyofananishwa na ndoa pamoja na nafasi na majukumu ya wanandoa kwa kufananishwa na uhusiano wa Kristo na Kanisa:
Ndoa kama mfano wa hai
kuhusu agano la damu

Kihistoria, agano la damu lina mifano mbali mbali; lakini mfano ambao umeshabihiana na agano la damu ni agano la ndoa. Tukumbuke kwamba taasisi ya ndoa ni ya kale tangu enzi za binadamu wa kwanza katika Bustani ya Edeni  kabla ya kuanguka dhambini.
Ndoa kielelezo kamili cha agano la damu kulingana na jinsi ilivyofananishwa na muungano wa wanandoa wawili kuwa mwili mmoja; na mwili mmoja wa ndoa kufananishwa na mwili wa Kristo ambao ni kanisa. Hebu tupitie baadhi ya ushahidi wa maandiko kama ifuatavyo:
1.    Mwili mmoja katika ndoa
Tukumbuke kwamba, agano ni muungano wa wahusika ambao unawafanya wenye kuungana kuwa kitu kimoja. Tafsiri hii imewekwa bayana kwenye baadhi ya maandiko kuhusu ndoa:
”akasema, Kwa sababu hiyo, mtu atamwacha babaye na mamaye, ataambatana na mkewe; na hao wawili watakuwa mwili mmoja?  Hata wamekuwa si wawili tena, bali mwili mmoja. Basi aliowaunganisha Mungu, mwanadamu asiwatenganishe.” (MT. 19:5, 6)
Tunaposoma kwamba, walioamua kuoana wamekuwa mwili mmoja na si wawili tena; haina maana wahusika wanabadilka na kuwa mtu mmoja kwa sura; la hasha! Kinacholengwa hapa ni kwamba wahusika wamefanya agano la damu na limewafanya kuwa kitu kimoja kimahusiano na mali za wahusika zimekuwa ni mali ya kila mmoja kwa mujibu wa tafsiri ya agano.
Maana yake, wahusika sasa, hawana tena ubinafsi ambapo kila mtu anajifanyia maamuzi yake na kufanya mambo yake kipeke yake; badala yake wanaishi kwa maamuzi ya pamoja na haki ya umiliki wa pamoja wa mali.
2.   Mwili wa ndoa mfano wa Mwili wa Kristo
Baada ya kushuhudia jinsi ambavyo ndoa imejengwa juu ya msingi wa agano la damu kwa mfano wa mwili mmoja; sasa hebu tushuhudie jinsi ndoa imefananishwa na mwili wa Kristo ambao ni kanisa:
“Kwa sababu hiyo mtu atamwacha baba yake na mama yake, ataambatana na mkewe na hao wawili watakuwa mwili mmoja.  Siri hiyo ni kubwa; ila mimi nanena habari ya Kristo na Kanisa.” (EFE. 5:31, 32)
Maandiko hapa yanasema kwamba “mume na mkewe watakuwa mwili mmoja” na mwisho Paulo anasema “Siri hiyo ni kubwa; ila mimi nanena habari ya Kristo na Kanisa.”! Kwa maelezo mengine analinganisha muungano wa ndoa na muungano wa Kristo na Kanisa.
Mume na mke kupitia agano la damu wameungana na kuwa mwili mmoja huku kichwa kikiongoza mwili na mwili nao ukibeba kichwa. Kanisa la Kristo lenye viungo vingi, kupitia agano la damu ni “Mwili mmoja wa Kristo”. Mwili wa Kristo kupitia agano la damu umeungana na Kichwa ambaye ni Kristo
3.   Mume ni kichwa cha Mkewe kaa”
Katika maandiko mengine, Paulo anaendelela kuchambua nafasi na wajibu wa wana ndoa akianza na Mume kuwa ni kichwa cha mkewe; na kuhusisha mfano huo na Kristo naye alivyo Kichwa cha Kanisa:”Kwa maana mume ni kichwa cha mkewe, kama Kristo naye ni kichwa cha Kanisa; naye ni mwokozi wa mwili.” (Efe5:23)
4.      Mke mwili wa mume kama ”Kanisa mwili wa Kristo”
Kwa maandiko hayo hayo tunasoma habari za nafasi na wajibu wa mke katika ndoa kuwa ni ”mwili” wa mume; na maandiko hayo hayo yakalinganisha na mfano wa Kanisa kuwa ni ”Mwili wa Kristo:”Vivyo hivyo imewapasa waume nao kuwapenda wake zao kama miili yao wenyewe. Ampendaye mkewe hujipenda mwenyewe. Maana hakuna mtu anayeuchukia mwili wake po pote; bali huulisha na kuutunza, kama Kristo naye anavyolitendea Kanisa.  Kwa kuwa tu viungo vya mwili wake.” (EFE. 5:28-30)
Majumuisho ya agano la ndoa
Kwa mapitio ya maandiko tumebaini waziwazi jinsi mfano wa ndoa ulivyofananishwa na Kristo na Kanisa. Tumebaini pia muungano wa ndoa unavyofafanua nafasi na wajibu wa kila upande na jinsi unavyoshabihiana na muungano wa Kristo na kanisa ambalo ni mwili wake
Mwisho tunaliona agano la damu jinsi lilivyo na nguvu ya kuunganisha na kufanya viwili kuwa kimoja kwa kupitia kiapo cha agano. Ukitazama mifano yote miwili inalidhihirisha agano la damu kuwa la kudumu kwa wahusika, na linafuta ubinafsi na kuhamasisha umoja wa kimahusiano kiimani na kiroho na ushirikiano wa kiuchumi na kijamii.
Itaendelea toleo lijalo
Share on Google Plus

About Gospel Kitaa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.