SOMO: AGANO LA DAMU (3)

Toleo lililopita tulichambua habari za agano la damu jinsi lilivyofananishwa na ndoa ambapo tulijifunza vipengele vya habari za Mwili mmoja katika ndoa; Mwili wa ndoa mfano wa Mwili wa Kristo; Mume ni kichwa cha Mkewe kama ”Kristo Kichwa cha Kanisa”; na Mke mwili wa mume kama ”Kanisa mwili wa Kristo” bofya hapa kusoma. Leo tunaingia sehemu nyingine inayochambua ”ahadi za agano jipya”:

Askofu Sylvester Gamanywa

Ahadi zilizo bora zaidi
za agano lililo bora zaidi

Baada ya kupitia muhtasari kuhusu Agano la damu ya Yesu historia na mifano yake katika Agano Jipya; sasa tunaingia kwenye sehemu nyingine maalum ya agano la damu, ambayo ni uchambuzi wa “ahadi za agano jipya” ambazo zimetajwa kuwa ni bora zaidi kuliko ahadi za agano la kwanza.
Pengine kabla hatuaanza uchambuzi wa ahadi zenyewe, hebu tuanze na tafsiri ya msamiati wenyewe wa neno “ahadi”. Kwa mujibu wa Kamusi ya Kiswahili Sanifu, neno “ahadi” limetafsiriwa kuwa ni: “sharti analojipa mtu kulitimiza;agano; mapatano;kauli”! Nimefurahishwa sana na hii tafsiri ya “agano” kuwa ni “sharti analojipa mtu kulitimiza.” Tukiileta maana hii katika “ahadi za agano jipya” tunaweza kutafsiri nazo ni “masharti aliyojipa Yesu kuyatimiza”!
Nachukua fursa hii kuweka wazi ukweli kwamba, wahubiri na waalimu wengine wa Biblia katika kutoa mafundisho na mahubiri yao, wameegemea na kulalia katika agano la kale, na kunukuu ahadi za agano la kale na kuzileta katika agano jipya. Pamoja na sehemu ya ukweli kwamba, maandiko ya agano la kale bado yanafaa kwa kufundishia, lakini ufunuo wa kutekelewa kama fundisho la imani umo katika agano jipya. Ndiyo maana mwandishi wa kitabu cha Waebrania amenukuu akisema kwamba Yesu Kristo ni “mdhamini wa agano lililo bora zaidi”:
basi kwa kadiri hii Yesu amekuwa mdhamini wa agano lililo bora zaidi. (EBR. 7:22)
Kwa kule kusema ”agano lililo bora zaidi”; pia ametaja waziwazi kuhusu ”ahadi za agano jipya” kuwa nazo ”ni bora zaidi” kuliko zile ahadi za agano la kwanza:
”Lakini sasa amepata huduma iliyo bora zaidi, kwa kadiri alivyo mjumbe wa agano lililo bora, lililoamriwa juu ya ahadi zilizo bora.” (EBR. 8:6)
Msomaji mpendwa, maandiko haya machache ni ushahidi kwamba, kwanza kuna tofauti kati ya ”agano la kale” na ”agano jipya”; pili, kuna tofauti kati ya ”ahadi za agano la kwanza”, na ”ahadi za agano jipya”! Tofauti kubwa kati yake ni ”viwango vya ubora wake”! Agano jipya ni bora zaidi ya agano la kwanza; na ahadi za agano jipya ni bora zaidi kuliko ahadi za agano la kwanza au kale! 
Haya baada ya kupata ufafanuzi wa awali sasa tuendelee kwenye uchambuzi wa tafsiri ya msamiati wa neno ”ahadi” ambao umetafsiriwa kuwa ni ”sharti analojipa mtu kulitimiza”; ambapo kwa mujibu wa agano jipya ahadi zake nazo ni sawa na ”Masharti aliyojipa Yesu kuyatimiza” kwa ajili yetu.

Ahadi za ukombozi na
muungano na Kristo

Kwa mujibu wa nukuu za maandiko zimo ahadi zaidi ya 250 katika agano jipya. Lakini katika mada hii zitanukuliwa baadhi kwa ajili ya kuelimisha maeneo ambayo yanagusa maisha ya imani ya washiriki wa agano jipya. Ni naona nianze na ahadi zile zinazohusu eneo la ukombozi wa Yesu Kristo na muungano na Kristo:


1.         Msamaha wa dhambi na uzima wa milele
Mfano wa ahadi za ukombozi ni maandiko maarufu sana katika agano jipya kuhusu upendo wa Mungu kwa ulimwengu, ambao umedhihirishwa kwa yeye kumtoa Mwanawe pekee, ili kuukomboa ulimwengu kutoka kwenye laana dhambi na hukumu ya jehanamu.
Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. Maana Mungu hakumtuma Mwana ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye.” (Yh.3:16-17)

Kutokana na maandiko haya, tunaisoma ahadi maalum ya ukombozi ambayo ni: “kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele”! maneno haya yamebeba sifa ya ahadi kwa sababu mwenye kunufaika ni binadamu, na aliyewa sharti la kuitimiza hadi yenyewe ni Mungu. Ahadi ya pili kwenye maandiko haya ni maneno yasemayo: “Mungu hakumtuma Mwana ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye.”
Kifungu hiki kinatoa mwelekeo ulio wazi kwamba, ujio wa Yesu Kristo duniani kwa awamu ya kwanza ulikuwa ni “kuokoa” na sio “kuhukumu”! Ndiyo maana matendo mengi aliyofanya Yesu yote yalilenga “kusamehe bure bi masharti” kufuta adhabu ya dhambi iliyoambatana na magonjwa na matatizo ya kijamii kwa wote waliomjia Kristo. Hii yote ni kutokana na ahadi ya ukombozi na utekelezaji wake.
Mpaka hivi sasa, jukumu linaloendelea hapa ulimwenguni, bado ni awamu ya ujio wa kwanza wa Yesu, ya kuokoa na sio kuhukumu. Ipo ahadi ya Yesu kurudi mara ya pili ulimwenguni. Hiyo itakuwa ni awamu ya pili ambayo jukumu lake ni tofauti la hili lililopo hivi sasa.

2.         Mapumziko ya Nafsi
Ahadi nyingine inayoendana na ahadi za ukombozi katika agano jipya imo kwenye tamko la Yesu Kristo mwenyewe kama alivyonukuliwa na Mathayo:
”Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu; (MT. 11:28, 29)

Ukisoma maandiko haya unasoma maneno yasemayo: ”...nami nitawapumzisha” na mengine ni...”nanyi mtapata raha nafsi mwenu.”! Hapa ”kupumzishwa na kupata raha nafsini” ni ahadi ya ukombozi inayomhakikishia kila atayemjia Yesu Kristo akiwa na mizigo yake. Ahadi ni kutuliwa mizigo na kupumzishwa. Hii kweli ni ahadi iliyo bora zaidi; tofauti ya agano la kwanza ambalo halikuwa na mapumziko ya kweli.

3.         Kiumbe kipya maisha mapya
Ahadi nyingine inayoendana na ukombozi wa binadamu, ni pale ambapo unawekwa waziwazi muungano kati ya mwamini na Mwokozi wake. Muungano huu unaonesha kwamba, baada ya kumjia Yesu na kupumzishwa, mambo haishii hapo bali kuna kuunganika na Kristo ili kuanza mfumo mpya wa maisha ambayo yametajwa kwenye maandiko yafuatayo :

Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita tazama! Yamekuwa mapya. (2 KOR. 5:17)

Hapa ahadi imo katika maneno yasemayo: “amekuwa kiumbe kipya” “...ya kale yamepita, tazama yamekuwa mapya”! Mtu anakuwa kiumbe kipya rohoni baada ya kufanyika matengenezo na urejesho wa mahusiano kati ya mtu na Kristo. 
Hii ni ahadi ya ulinzi yenye kinga dhidi ya masambulizi ya utu wa kale, na athari za maisha ya kale. Mtu anaahidiwa kwamba akiisha kumwamini Yesu, kinachofuatia ni “kuwa kiumbe kipya na kupokea maisha mapya ndani ya Kristo.

4.         Uhuru kamili
Haya, tumeaona ahadi ya kwanza ya ukombozi, ikaja ya mapumziko na raha nafsini, na sasa tumekutana na ya tatu ambayo inamhakikishia mtu kufanyika kiumbe kipya na kuanza maisha mapya. Sasa tunakutana na ahadi ya nne ambayo inamtangazia muhusika “uhuru kamili” katika maisha mapya aliyoyaanza hapa ulimwenguni:
Sasa, basi, hakuna hukumu ya adhabu juu yao walio katika Kristo Yesu.  Kwa sababu sheria ya Roho wa uzima ule ulio katika Kristo Yesu imeniacha huru, mbali na sheria ya dhambi na mauti. (RUM. 8:1, 2)
Ahadi ya uhuru kamili imo katika maneno yafuatayo: ”hakuna hukumu ya adhabu juu ya walio katika Kristo Yesu.” Kinacholengwa hapa ni hali ya kuhakikishwa kwamba, neema ya wokovu wa Kristo, inamwondolea mashtaki na hukumu ya adhabu kwa ajili ya dhambi zilizokwisha kutendwa kabla. Lakini pia hata kama akikosea pasipo kukusidia, bado ana fursa ya kutubu na kusamehewa bure na asiwepo yeyote wa kumhumia adhabu kwa sababu ana ahadi ya kuwa salama na kutokuadhibiwa kwa sababu sheria ya uzima imemweka huru mbali na sheria ya dhambi na mauti.
Itaendelea toleo lijalo
Share on Google Plus

About Gospel Kitaa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.