SOMO: AGANO LA DAMU (4)

Toleo lililopita tulichambua; Ahadi zilizo bora zaidi za agano lililo bora zaidi; Ahadi za ukombozi na muungano na Kristo. Baadhi ya ahadi tulizozichambua katika toleo lililopita, ni pamoja na: 1.Msamaha wa dhambi na uzima wa milele 2. Mapumziko ya Nafsi, 3.Kiumbe kipya maisha mapya, 4.Uhuru kamili (bofya hapa kusoma). Leo tunaendelea na uchambuzi wa ahadi nyingine muhimu na ambayo ndiyo inayolifanya Agano Jipya liendelee kuwa jipya na kuwa bora zaidi.

Askofu Sylvester Gamanywa

Ahadi ya kumpokea Roho 
Mtakatifu na nguvu zake


Kumpokea Roho Mtakatifu ni ahadi ya Mungu Baba aliyoitangaza kwa manabii wa Agano la Kale akitabiri kuitimiza wakati wa Agano Jipya. Nabii wa mwisho wa Agano la Kale ni Yohana Mbatizaji. Yeye ndiye aliyetabiri sio kutimia kwa ahadi ya ujio na ujazo wa Roho Mtakatifu, bali na Mhusika mkuu ambaye atasimamia utekelezaji wa utimilifu wa ahadi yenyewe.

Mhusika mkuu wa kutimia kwa ahadi hii ni Yesu Kristo mwenyewe. Ndiyo maana Yesu alipofufuka katika wafu na kukutana na wanafunzi wake na mojawapo ya mambo aliyotilia mkazo ni suala la kupokea ahadi ya Roho Mtakatifu kama ambavyo Yohana Mbatizaji alivyokuwa ametangulia kuwatabiria:

"Hata alipokuwa amekutana nao aliwaagiza wasitoke Yerusalemu, bali waingoje ahadi ya Baba, ambayo mlisikia habari zake kwangu;  ya kwamba Yohana alibatiza kwa maji, bali ninyi mtabatizwa katika Roho Mtakatifu baada ya siku hizi chache." (MDO 1:4, 5)

Na maneno ya mwisho ya Yesu kwa wanafunzi wake kabla ya kupaa mbinguni, alirejea tena kutimia kwa ahadi ya ujio wa Roho Mtakatifu ambaye angewashukia na kuwajaza wanafunzi wake:

“Lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi.” (MDO 1:8)

Jinsi ahadi ya kumpokea Roho Mtakatifu
ilivyotimizwa wakati wa Agano Jipya

Baada ya siku kumi tangu Yesu alipopaa, wanafunzi wake walilazimika kubakia Yerusalemu wakisubiri ahadi ya kumpokea Roho Mtakatifu, kama walivyoagizwa na Kristo mwenyewe. Wakati wamejifungia chumba cha juu, huku wakiwa katika hali ya mfungo na sala ndipo ghafla, ikiwa ni sikukuu ya mavuno maarufu kama Pentekoste, wanafunzi wa Kristo walishuhudia utimilifu wa ahadi juu yao kama ilivyoandikwa:

Hata ilipotimia siku ya Pentekoste walikuwako wote mahali pamoja. Kukaja ghafula toka mbinguni uvumi kama uvumi wa upepo wa nguvu ukienda kasi, ukaijaza nyumba yote waliyokuwa wameketi. Kukawatokea ndimi zilizogawanyikana, kama ndimi za moto uliowakalia kila mmoja wao. Wote wakajazwa Roho Mtakatifu, wakaanza kusema kwa lugha nyingine, kama Roho alivyowajalia kutamka. (MDO 2:1-4)

Siku hizi tumezoea kauli za jambo linapotendeka kwa nguvu na kuleta matokeo, au mwitikio mkubwa au mrejesho chana tunasema hicho ni “kishindo”! Hapa tunasoma jinsi Roho Mtakatifu alivyoshuka kwa “kishindo”, na kuwajaza kwa “kishindo” wale wote waliokuwemo; na wote wakaanza kunena kwa “kishindo” lugha nyingine, kama Roho Mtakatifu mwenyewe alivyowakirimia.

Jambo la msingi ambalo nataka kulitilia mkazo katika suala ujio na ujazo wa Roho Mtakatifu, ni jinsi tukio lenyewe ambalo halikuwa la faragha, au la siri, japokuwa wahusika wenyewe walikuwa mafichoni. Narejea kusema kwamba, tukio la ujio na ujazo wa Roho Mtakatifu halikuwa tendo la uficho na siri kwa ajili ya wanafunzi wa Yesu peke yao.

Tunafahamu kwamba, wanafunzi walikuwa wamejifungia chumbani, lakini Roho Mtakatifu aliposhuka, na alipokwisha kuwajaza, jamaa hawakuweza kujificha tena, bali walianza kusema kwa lugha ambayo sauti zao ziliweza kusikika nje na kufika mbali mitaani, kiasi kwamba, watu waliokuwa wakipita mtaa ule walilazimika kusimama na kuwachungulia kule juu ghorofani walikokuwa.

Wakati umati mkubwa watu ukijaribu kutafakari kwa mshangao kile kitendo cha wanafunzi kusikika wakisema kwa lugha, ghafla Roho Mtakatifu aliyekuwa tayari ndani ya wanafunzi aliamua kutafsiri maneno ya lugha waliyokuwa wakinena ipate kueleweka kwa kila mtu kwa lugha yake ya asili.

Najua hapa kuna mjadala wa miaka mingi kuhusu aina za lugha ambazo wanafunzi waliziongea kwamba zilieleweka kwa waliozisikia, na wanahoji kuhusu uhalali wa ujazo wa Roho Mtakatifu wa siku za leo ambalo lugha inenwayo haijulikani kwa wanaosikia.

Nitalifafanua hili huko mbele, lakini kwa sasa hoja yangu inalenga kuweka mkazo kwamba, Tukio la kumpokea Roho Mtakatifu, halikuwa tukio la faraghani bali lilitendeka na kudhihirika hadharani kwa watu wote, wenye imani na wasio na imani.

Kumpokea Roho Mtakatifu ni
“ahadi endelevu” ya Agano Jipya

Sababu kubwa ya kuweka mkazo katika “uwazo wa ujazo wa Roho Mtakatifu” ni kurekebisha mtazamo wa kimapokeo unaoendelea kutafsiri kwamba tendo la kumpokea Roho Mtakatifu ni “tendo la faragha na mtu binafsi,” na eti halitakiwi hata kufanyikia kwenye mazingira ya kiibada kwenye mkusanyo wa watu! Mtazamo huu ndio ambao umesababisha kukoma kwa utimilifu wa ahadi iliyotolewa na Mungu Baba kwa ajili ya kipindi cha Agano Jipya.

Aidha nataka kuendelea kuweka hadharani kwamba, kumpokea Roho Mtakatifu ni “ahadi endelevu” katika Agano Jipya kwa kila kizazi na kwa kila kundi la kijamii hapa duniani.

“Petro akawaambia, Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu. Kwa kuwa ahadi hii ni kwa ajili yenu, na kwa watoto wenu, na kwa watu wote walio mbali, na kwa wote watakaoitwa na Bwana Mungu wetu wamjie.” (MDO 2:38-39)

Maandiko haya ni hotuba ya Petro iliyokuwa ikijibu maswali ya watu waliokuwa wamekusanyika kwenye tukio la ujazo wa Roho Mtakatifu na wengine wakaanza kukashfu kwamba hao wanenao kwa lugha wamelewa pombe. Katika kutoa ufafanuzi ndipo tunasoma Petro aliainisha kuhusu “ahadi ya Roho Mtakatifu haikutakiwa kuishia kwa wanafunzi wa Yesu peke yao, bali hata kwa ajili ya wote waliokuwa wakishuhudia tukio hilo kwa siku hiyo, na kwa ajili ya vizazi vitakavyofuata, na kwa ajili ya wote watakakoitwa na Mungu kumjia Kristo.Kimsingi, ahadi ya kumpokea Roho Mtakatifu ni zoezu na tukio lililotarajiwa na kutakiwa kufanyika kwa kila mtu anayetubu, kubatizwa na kumwamini Kristo.

Itaendelea toleo lijalo

Share on Google Plus

About Gospel Kitaa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.