UTEKAJI: M/KITI WA WALIOKOSA AJIRA JKT ASIMULIA ALIVYOTEKWA

George Mgoba akiwa hospitalini.
Mwenyekiti wa askari wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) waliokosa ajira baada ya mafunzo, George Mgoba, amedai kutekwa na kuteswa na watu wasiofahamika huku wakimtaka kuwataja wanaowashinikiza kwenda Ikulu.
Akizungumza na NIPASHE Jumamosi katika mahojiano maalumu kwa njia ya simu, mwenyekiti huyo ambaye amelazwa Hospitali ya Amana alisema kuwa, Jumatatu ya wiki hii alipigiwa simu na mtu aliyejitambulisha kuwa ni mmoja wa askari wa JKT ambaye alimtaka wakutane kituo cha mabasi cha Mabibo.
Alisema alipofika kituoni hapo aliwakuta wanaume wawili na mwanamke mmoja ambao baada ya kusalimiana kwa kupeana mikono mmoja wao alimweleza kuwa, atoe mdudu kwenye sikio.
“Mkono ambao nilitoa kusalimiana nao ndiyo niliounyanyua kumtoa mdudu niliyeelezwa cha ajabu ni kwamba baada ya tendo hilo nilipoteza fahamu,” alisema na kuongeza:
“Nilipopata fahamu nilisikia mwangwi na nilipofungua macho niliona nashushwa chini kwenye jengo la ghorofa, wakati tunakaribia kufika chini nilisikia sauti ya redio call inaongea, lakini sikujua kilichokuwa kikizungumzwa  kwa sababu ilikuwa mbali,” alisema.
Mgoba alisema alisikia mmoja wa wale alioenda nao, wakiamuru redio call hiyo izimwe na baada ya kufikishwa chini alifunikwa macho na kitambaa cheusi.
“Waliniamuru nitoe simu na namba ya siri, lakini kwa sababu walikuwa wameniziba macho na namba yangu ya siri ni ya kuchora niliwaomba wanifungue kitambaa, walinitoa upande mmoja wa jicho nikaifungua simu,” alisema.
Alisema alifunguliwa jicho moja na kuona buti la jeshi pamoja na mwanamke mmoja ambaye alikuwa amesimama mbele yake ambaye hamfahamu.
Alisema watu hao walimbana wakimtaka aeleze anayewatuma kama ni Ukawa au Lowassa.
Pia alisema walimuuliza endapo watapata nafasi ya kwenda kwa Rais watamweleza nini.
“Wakati naulizwa maswali hayo walikuwa wananibana sehemu za siri ili niseme ukweli ni Ukawa au Lowassa aliyetutuma kufanya hivyo, niliwaeleza  kuwa, lengo letu la kukutana na Rais ni kutaka kujua hatma ya barua tunazomwandikia Kikwete na si vinginevyo,” alisema.
Mgoba alisema watu hao kwa kuwa walikuwa na lengo la kutana kujua anayewatuma, waliendelea kumtesa kwa kumpiga fimbo mgongoni na kumwingiza kichwa kwenye maji.
Alisema baada ya mateso hayo siku iliyofuata asubuhi, aliletwa mwanamke ambaye alitakiwa afanye nae mapenzi.
“Sikuweza kutekeleza hilo kwa sababu mwili ulikuwa hauna nguvu na sehemu zangu za siri zilikuwa zinauma sana, wakati wakinishinikiza nitekeleze hilo, alifika mtu mwingine ambaye ni kiongozi wao na kutaka kujua walikofikia hivyo alielezwa,” alisema kuongeza:
“Aliwaamuru wanimalizie, nilinyolewa nywele wakataka kunipiga sindano sikujua ilikuwa imewekwa nini  lakini mshipa wa kichwani haukuonekana hivyo wakakubaliana wanichome mkono wa kulia baada ya kutekeleza hilo mwili ukafa ganzi,” alisema.
Mgoba alisema baada ya hapo, aliingizwa kwenye gari na kutelekezwa kwenye moja ya mapori mkoani Pwani majira ya jioni ambapo alisikia mmoja wao akiamuru simu yake ichukuliwe lakini hawakufanya hivyo.
Alisema baada ya kupata nguvu kidogo alijikokota hadi barabarani ambapo huko alipita dereva wa pikipiki ambaye alimsaidia kumpeleka kituo cha polisi cha Mkoa wa Pwani.
“Mmoja wa askari aliwasiliana na mkuu wa kituo hicho akimweleza tukio langu na hali niliyokuwa nayo wakati huo, lakini mkuu huyo alimjibu waniweke mahabusu, yule askari na wenzake nilisikia wakishauriana kuhusu kauli ya mkubwa wao, wakakubaliana wanipeleke Hospitali ya Tumbi kutokana na hali yangu,” alisema.
Alisema ndugu zake walipofika hospitalini aliwaeleza kuhusu sindano aliyochomwa na kumuomba daktari mara baada ya vipimo wamchukue kwenda  Dar es Salaam kwa matibabu zaidi, ombi ambalo lilikubaliwa.
Alisema juzi asubuhi aliruhusiwa lakini katika hali isiyo ya kawaida, polisi walimtaka arudishwe kituoni kwa maelezo zaidi na walipofika walimng’ang’ania kuwa watampeleka hospitali wenyewe.
“Baada ya mvutano baina ya wazazi wangu na polisi, wazazi walikasirika na kuondoka, hivyo polisi walinichukua kuja Dar es Salaam hadi Kituo cha Polisi Kati badala ya hospitali,” alisema na kuongeza:
“Walinitaka niandike maelezo ambayo nilishindwa kutokana na hali yangu kutokuwa nzuri, waliandika wao wanachokijua na kunitaka nisaini nilikataa ndipo wakaniweka mahabusu,” alisema.
Alisema baada ya dakika kadhaa walimtoa na kumpa maelezo waliyoandika ili ayasome ambayo baadhi ya vipengele kama vya kuwekwa mahabusu vilikuwa havijawekwa.
“Niliwaomba waweke na hilo lakini walikataa na kunilazimisha nisaini, nilitekeleza ndipo wakaniambia niandike barua ya kujidhamini na waliniachia saa 3:00 usiku na kunipa Sh. 2,000 baada ya kuwaeleza sina hela,” alisema.
Alisema baada ya kutembea kidogo alidondoka na alipozinduka alijikuta hospitali ya Mnazi Mmoja ambapo baadaye alihamishiwa hospitali ya Amana kwa matibabu zaidi.
Alisema tatizo linalomsumbua hivi sasa ni mwili kupata ganzi mara kwa mara na maumivu makali sehemu za siri na kwenye majeraha ya vipigo.
Alisema kwa sasa daktari wake amempatia dawa ya kuondoa sumu ya sindano aliyochomwa.
Alisema simu yake ya mkononi, leseni ya udereva na kadi mbili za benki zinashikiliwa na jeshi la polisi mkoani Pwani.
Awali, akizungumza na gazeti hili, Parali Kiwango ambaye ni makamu mwenyekiti wa askari hao, alisisitiza kuwa, lengo lao la kwenda Ikulu ni kushinikiza kwa nini barua zao wanazomwandikia Rais hazimfikii na siyo kwenda kudai ajira.
Kiwango na askari wenzake jana walikusanyika eneo la uwanja wa mpira nje ya Shule ya Msingi Msimbazi Mseto na Mivinjeni, wakijadili hatma ya mwenzao.
Katika mkutano huo watumishi kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) walifika kwa ajili ya kupata maelezo kuhusu tukio hilo na baadaye walielekea hospitali ya Amana kwa mahojiano zaidi. 
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Pwani, Ulrich Matei, alipopigiwa simu kuzungumzia tukio hilo alisema anashangaa kusikia cheo cha uwenyekiti kwenye jeshi wakati cheo hicho hakipo.
Alisema mtu huyo aliokotwa barabarani na watu bila kuitaja hospitali aliyopelekwa huku akimtaka mwandishi awasiliane na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Camilius Wambura, kwa maelezo zaidi.
Kamanda Wambura alisema mtu huyo aliokotwa mkoa wa Pwani na kwamba hafahamu chochote kuhusiana na tukio hilo huku akimtaka mwandishi azungumze na kamanda wa mkoa wa Pwani.
Hata hivyo, alipoelezwa majibu ya kamanda wa mkoa wa Pwani, alisisitiza kuwa, tukio hilo lilitokea huko. 
Naye, Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, alisema wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo kwa sababu mhusika alidai kutekwa eneo la Mabibo, utakapokamilika atazungumza na waandishi wa habari.


Share on Google Plus

About Gospel Kitaa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.