JANA YAKO NI HISTORIA YA LEO, NA LEO NI HISTORIA YA KESHO, NA KESHO YAKO ITAKUWA LEO YAKO

Na Faraja Naftal Mndeme.
GK Contributor.
©ceo methodology.
Maisha yetu ya leo ni maamuzi mengi tuliyoyafanya jana. Maamuzi yetu mengi ya leo ndio yanaweza kuamua kesho yetu itaonekana namna gani. Mara nyingi kwenye maisha yetu ya kila siku tumejikuta tupo pale pale kwa miaka nenda rudi si kwa sababu hatuwezi kusonga mbele bali ni namna tunavyofanya maamuzi yetu kuelekea kesho. Matokeo ya mengi tunayoyafurahia leo au tunayoyajutia leo ni kwa sababu kuna sehemu fulani tulikosa kufanya maamuzi jana.

Maamuzi ya jambo lolote kwenye maisha ni mchakato ambao unahitaji umakini wa hali ya juu ambao unakutaka uwe unajua vitu kadha wa kadha kabla ya kufanya maamuzi. Kila mtu ana falsafa yake ya kufanya maamuzi. Falsafa ni kama kanuni au ni kama alama za vidole ambazo zinaweza kumtofautisha mtu mmoja na mwingine. Matokeo mengi ya maisha yetu ya leo si miujiza ila ni maamuzi yetu ya jana. Iwapo uliamua kudandia treni kwa mbele, huwezi kuamua nini kitakachotokea mbele ya Safari.

1. AINA YA MASWALI UNAYOJIULIZA.

Moja ya hatua muhimu ya kufanya maamuzi kwenye kila jambo unalolifanya linategemea aina ya maswali ambayo unajiuliza. Unapojiuliza maswala ambayo yapo chini ya kiwango basi tambua hata majibu yake yatakuwa chini ya kiwango. Maendeleo yote unayoyaona leo ni mkusanyiko wa maswali mengi ambayo watu walijiuliza na kuamua kuyatafutia majibu yake. Hakuna mtu ambaye anaweza kukusaidia kutafuta majibu kwenye maswali yako. Hakuna mtu ambaye anaweza kukusaidia kuongeza ubora wa kujiuliza maswali bora kama wewe haukuamua kujiuliza binafsi. Mwanzo wa mchakato wa maamuzi mazuri huanza kwenye aina ya maswali ambayo unajiuliza.

2. FALSAFA UNAYOTUMIA KUFANYA MAAMUZI.

Kila mtu ana falsafa yake ya kufanya mamuzi kwenye maisha. Wengine huamua kutumia falsafa za kidini, kijamii, kisiasa na kiuchumi. Kuna aina nyingi ya falsafa unazoweza kuamua kutumia kufanya maamuzi yako. Falsafa unayoamua kuitumia kufanya maamuzi yako inategemea unataka ikupeleke mahali gani. Kila falsafa ina athari zake; nzuri na mbaya. Unapotumia muda mwingi pia kuirekebisha falsafa yako ya maamuzi inakusaidia kuweza kufanya maamuzi bora kila siku kwenye maisha yako.

3. MATOKEO UNAYOYATARAJIA.

Mara nyingi matokeo tunayoyaona leo kwenye maswala mbali mbali ni mkusanyiko wa mambo kadha wa kadha. Mara nyingi tuaposhindwa kwenye jambo fulani huwa mara nyingi tunaangalia matokeo ya lile jambo, lakini hatutumii muda kutafakari na kuweza kufwatalia mchakato mzima wa maamuzi ulikwendaje. Mara nyingi huwa nashauri unapoona unataka na unahitaji kufanya maamuzi muhimu kwenye maisha yako ya kila siku, hakikisha unayaweka kila jambo bayana kupitia maandishi. Hakikisha unakuwa mwandishi mzuri ili pindi unapoona matokeo hayakutokea vile ulivyotarajia ni rahisi kufwatilia mchakato mzima ulikwendaje.

4. JIFUNZE KUWEKA KUMBUKUMBU.

Watanzania wengi tumekuwa wavivu wa kuandika na kutunza kumbukumbu muhimu za maamuzi na michakato muhimu kwenye maisha yetu. Matokeo yake ikifika kesho unapotaka kufanya maamuzi kama ya jana ambayo ulipatia unakuta hauna kumbukumbu zozote muhimu. Matokeo ya kutokuwa na kumbukumbu utahisi kwamba ulibahatisha kwa namna fulani. Na inawezekana kila mara ukawa unarudia kutumia muda mwingi kwenye kufanya maamuzi mbali mbali ya maisha. Unapokuwa na kumbukumbu ni rahisi kwenda kufanya hadidu rejea na iwapo kuna marekebisho basi yatakuwa kwa kiasi fulani tu,itakusaidia kuepuka kuanza moja tena kwenye kutengeneza falsafa na mfumo mzima wa maamuzi. Hakikisha unaandika kila jambo maana inaweza pia ikawa urithi wa kizazi kijacho.

E-mail:naki1419@gmail.com
+255788454585
God Bless Y’All
Share on Google Plus

About Gospel Kitaa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.