KWA TAARIFA YAKO: HUYU NI MWALIMU ANAYEONGOZA KWA KUFUNDISHA KWAYA NYINGI NDANI NA NJE YA NCHI

Haya msomaji wetu wa Gospel Kitaa karibu katika kipengele chetu maalumu ''KWA TAARIFA YAKO'' ambacho kinakujia kila siku za alhamisi ndani ya GK kikiwa na lengo la kukupatia habari ambayo iliwahi kutukia lakini yawezekana huijui pia yawezekana ilitukia ukawa unaijua lakini GK ikawa imesahau mahali au kuna sehemu haina usahihi utapata fursa ya kusahihisha kwa kuweka comment yako chini kabisa kwenye habari husika. Karibu
KWA TAARIFA YAKO hii leo ni kukutaarifu kuhusu mwalimu mmoja wa kwaya ambaye kwa takwimu za GK ndiye anayeongoza kwa kufundisha kwaya nyingi ndani na nje ya nchi kuliko walimu wote wa kwaya nchini Tanzania. Mwalimu huyu si mbambaishaji linapokuja suala la kunoa watu sauti ushahidi huu unaweza kuonekana katika kwaya mbalimbali alikoitwa ili kuwanoa sauti zao.

KWA TAARIFA YAKO mwalimu anayezungumziwa hapa si mwingine bali ni Samson Kibaso mwalimu kiongozi wa kwaya ya Sabato Kurasini jijini Dar es salaam. Mwalimu huyu anafahamika sana kwa aina yake ya ufundishaji waimbaji na kufuatisha kila anachotaka waimbaji wakifuate. Kati ya kwaya maarufu alizozinoa ni pamoja na Kwaya ya Uinjilisti ya kanisa la Kilutheri Kijitonyama jijini Dar es salaam, na kwaya nyingine nyingi zilizomo jijini humo na mikoani bila kusahau kwaya kutoka Kenya, Uganda, Malawi ambako pia alipata kualikwa kunoa kwaya mbalimbali.

KWA TAARIFA YAKO licha ya kwamba ni mnoaji wa sauti lakini pia hufundisha kwaya hizo nyimbo ambazo hata hivyo muda mwingine huzitoa kwenye kwaya yake ya Kurasini SDA ambao wanakuwa wamesharekodi hivyo kwaya fundishwa nyingi hubakia kuziimba nyimbo hizo katika ibada zao na kushindwa kuzirekodi kwakuwa wenzao walikwisha fanya hivyo. Mwalimu Samson Kibaso amechangia kwa kiasi kikubwa kuinua uimbaji wa kwaya ya uinjilisti Kijitonyama ambako licha ya kuwanoa sauti lakini pia amewafundisha nyimbo mbalimbali ukiwemo wimbo 'Dhambi ni dhambi, Iko wapi Imani ile, Twakaribia Kanani na nyinginezo.


Mwalimu Samson Kibaso akiwa na kwaya ya Uinjilisti Kijitonyama enzi hizo


KWA TAARIFA YAKO kwaya yake anayoifundisha ya Kurasini SDA nadhani ipo kwenye top 3 ya kwaya bora nchini ambazo huimba sauti murua, zenye nguvu na ujazo ukiachia mbali tunzi za nyimbo zake zenye mifano mbalimbali. Mwalimu Kibaso katika tembea tembea yake katika ufundishaji wa kwaya alialikwa kuinoa kwaya kuu ya Kimara Lutherani wanaofahamika kwa wimbo wao 'Katika njia ya injili iendayo kwetu mbinguni' huko alikutana na mwalimu mwingine maarufu katika kanisa la KKKT Dayosisi ya Mashariki na Pwani bwana Amri Hingi ambaye ni mwalimu kiongozi wa kwaya kuu ya Sinza lutheran wanaotamba na kibao cha 'Mimi ni mjanja Ndani ya Yesu'.


Mwalimu Hingi
KWA TAARIFA YAKO mwalimu Hingi aliwafundisha kwaya kuu ya Kimara wimbo mpya uitwao'Nipo katika Safari duniani' wimbo ambao kwa mujibu wa mwalimu Hingi ni remix ya wimbo wa Katika njia ya injili, kutokana na wimbo huo kuwa mzuri kuanzia sauti mpaka maneno ulimfanya mwalimu Kibaso kuuchukua na kuubadilisha baadhi ya maneno na kuifundisha kwaya yake ya Kurasini SDA wimbo ukijulikana kama 'Jerusalem' ambao umetokea kupendwa sana miongoni mwa nyimbo maarufu za kwaya ya Kurasini, kwakuwa Kurasini walikuwa tayari kuingia studio basi waliurekodi na album wakaipa jina la wimbo huo 'Jerusalem' huku pia Kimara bila kujua nao wakarekodi wimbo wao ambao nao ukabeba album 'Nipo katika Safari', kilichotokea baadae nadhani mwalimu Kibaso alijieleza kwa mtunzi halisi wa wimbo mwalimu Hingi kuhusu wimbo huo.

KWA TAARIFA YAKO nyimbo zote mbili Jerusalem pamoja na Nipo katika Safari ambazo sauti na baadhi ya maneno yanafanana ni kati ya nyimbo bora za injili kwa kwaya za noten nchini. Tafuta album hizo utaniambia kwajinsi utakavyobarikiwa. Mwalimu Kibaso ameiwezesha kwaya yake ya Kurasini kurekodi matoleo zaidi ya 37 mpaka sasa na huku Mungu akiwabariki kwa gari ya huduma aina ya Double Coaster. Mungu aendelee kumbariki mtumishi wake huyu ili kwaya nyingi zaidi zikapate kuimba kwa viwango na zaidi watu wakapate kumjua Mungu kupitia uimbaji waoHiyo ni KWA TAARIFA YAKO hii leo vinginevyo tuonane wiki ijayo…….
Share on Google Plus

About Ambwene Mwamwaja

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.