SOMO: AGANO LA DAMU (5)

Toleo lililopita (soma hapa) tulichambua vipengele muhimu vya; i) Ahadi ya kumpokea Roho Mtakatifu na nguvu zake; ii) Jinsi ahadi ya kumpokea Roho Mtakatifu ilivyotimizwa wakati wa Agano Jipya; na iii) Kumpokea Roho Mtakatifu ni “ahadi endelevu” ya Agano Jipya. Leo tunaendele kuchambua jinsi Roho Mtakatifu alivyo muhimu kwa ajili ya kuzifanya ahadi nyingine za Agano jipya zitimie katika maisha yetu ya imani kwa Mungu:

Askofu Sylvester Gamanywa
Kumsikiliza Yesu Kristo peke yake

Naomba kabla ya kuendelea na jinsi Roho Mtakatifu alivyo wa muhimu kwetu katika kutusaidia kutimia kwa ahadi nyingine za agano jipya katika maisha yetu, nielezee kidogo kuhusu hatari ambayo nimeiona katika jamii yetu ya “kuthamini zaidi” ahadi za agano la kale badala ya zile za agano jipya ambazo ni bora zaidi.

Kila ninaposikiliza mahubiri, au mafundisho, au maelekezo, au mkazo wa maelezo ya mambo yanayoagizwa na na baadhi ya watumishi wa Mungu wa kizazi hiki, nakutana na mtazamo huu kunukuu na kutafsiri ahadi za agano la kale na kuzijengea moja wa moja “fundisho la imani” kana kwamba bado tunaishi katika enzi za agano la kale! Hapa nina maana ya kuchukua mifano ya manabii maarufu wa agano la kale na maisha yao ya kihuduma, (na pasipo marejeo yake katika agano jipya) wanayatolea mafunuo ya kiroho kwa ajili ya utekelezaji wa maisha yetu sisi wa agano jipya.

Tafadhali nisikilize kwa makini. Hapa nisieleweke kwamba, siamini kujifunza kutoka maandiko ya agano la kale. Najua kila andiko lenye pumzi ya Mungu lafaa kwa mafundisho. Ninachotaka kusisitiza hapa, ni tabia na mtindo wa kuyatafsiri maandiko ya agano la kale na kuyafanya “mafunuo ya agano jipya” wakati ambapo “maandiko ya agano jipya yenyewe ndio tafsiri kamili”!

Nahisi bado hatujaelewana bado hapa. Ni nini maana ya “kulifanya agano la kale” kuwa ni “ufunuo wa agano jipya”? Niseme kwa kifupi kwamba, maandiko ya agano la kale kwetu ni “taarifa za kihistoria” na maandiko ya agano jipya ni “maagizo ya kufanyiwa kazi” kwa kizazi chetu cha leo. Ngoja nikupe mifano ya maandiko:

“Alipokuwa katika kusema, tazama, wingu jeupe likawatia uvuli; na tazama, sauti ikatoka katika lile wingu, ikasema, Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye; msikieni yeye.” (Matt.17:5)

Maandiko haya yanashuhudia kwamba, wayahudi waliheshimu na kuzingatia maneno ya kinabii yaliyosemwa na Musa na Eliya. Na ndiyo maana Petro alipowaona Musa na Eliya wakiwa na Yesu akapendekeza vijengwe vibanda vitatu, kimoja cha Musa, pili cha Eliya na tatu cha Yesu. Mungu mwenyewe ambaye ndiye aliyewatuma Musa na Eliya akalazimika kusema nao kwa kumtambulisha Yesu kuwa yeye ndiye “anapaswa kusikilizwa” badala ya Musa na Eliya.

Kwa kusema “Msikieni yeye” maana yake “mamlaka ya kutoa maagizo ya kiimani” imehama toka kwa manabii ya waliotangulia na kuja kwa Yesu Kristo. Hata mwandishi wa kitabu cha Waebrania naye anaanza kwa kurejea ni nani ambaye kizazi cha agano jipya kinatakiwa kumsikiliza:

“Mungu, ambaye alisema zamani na baba zetu katika manabii kwa sehemu nyingi na kwa njia nyingi, mwisho wa siku hizi amesema na sisi katika Mwana, aliyemweka kuwa mrithi wa yote, tena kwa yeye aliufanya ulimwengu…” (Ebr.1:1-2)

Bila sha umepata picha kamili kwa maandiko haya. Hapo zamani, yaani enzi za agano la kale, Mungu alisema kupitia manabii; lakini “siku hizi” yaani enzi za agano jipya, Mungu anasema na sisi kupitia Mwana. Katika majumuisho yangu kuhusu kipengele hiki, napenda kuhitimisha kwamba, tuanze kujifunza kufuatilia kila neno lililonukuliwa kutoka kinywani mwa Yesu, kwa sababu hilo ndilo neno la agano jipya kwetu ni “agizo” ni “amri” kwa ajili ya utekelezaji.
  
Kazi ya Roho Mtakatifu ni kuwasilisha
kwetu anayosikia kutoa kwa Yesu Kristo

Baada ya kupata ushahidi kwamba ili kuweza kunufaika na ahadi za agano jipya; tunashauriwa kuacha kuweka mkazo kwenye ahadi za agano la kale! Tuache kuwaenzi manabii wa agano la kale. Tuanze kumpa Yesu Kristo, mjumbe wa agano jipya, heshima ya kusikilizwa.

Ndiyo maana, hata Yesu Kristo mwenyewe alipokuwa akiwasimulia wanafunzi wake baadhi ya kazi za Roho Mtakatifu atakapokuja duniani, aliweka bayana kwamba, hataongoza kwa mawazo yake binafsi, bali ataendeleza mchakato wa kuwasilisha ujumbe wa maneno ya Kristo na sio manabii wa agano la kale.

“Lakini yeye atakapokuja, huyo Roho wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote; kwa maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena, na mambo yajayo atawapasha habari zake.” (Yh.16:13)

Kumbuka wakati Yesu anasema maneno haya, alikuwa bado hajasulubiwa msalabani, kufa na kufufuka kutoka kwa wafu. Alikuwa bado hajapaa na wala hajarudi kwa Yohana alipokuwa kisiwa cha Patmo alipompa kitabu cha Ufunuo. Ndani ya maandiko haya tunapata picha kamili kuhusu wajibu wa Roho Mtakatifu anapokuja kufanya makao ndani ya waaminio; “kumsikiliza Yesu na kuwasilisha kwetu yote aliyoyasikia kutoka kwa Yesu”. Na ndivyo Roho alivyofanya tangu siku ile aliposhuka hapa duniani.

Ni Roho Mtakatifu aliyeongoza mchakato wa kuandika maandiko ya agano jipya, kuanzia Injili, kitabu cha Matendo ya Mitume na nyaraka zote za agano jipya! Na mpaka hivi sasa, bado Roho Mtakatifu bado anaendelea na mchakato huu, wa kuwasiliana nasi kwanza kutufunulia yale aliyokwisha kuandikwa katika agano jipya, pili, kuwasiliana na Yesu ili aseme na sisi kuhusu yatupasayo kutenda katika kizazi chetu.

Itaendelea toleo lijalo

Share on Google Plus

About Gospel Kitaa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.