SOMO: KABLA YA MAMBO YOTE YAKUPASA UFANYE SHUKRANI & MAOMBI


Na Mtumishi Gasper Madumla

Bwana Yesu asifiwe…

Tunasoma;

“ Basi, kabla ya mambo yote, nataka dua, na sala, na maombezi, na shukrani, zifanyike kwa ajili ya watu wote; ” 1 Timotheo 2:1

Paulo anamwagiza mtoto wake wa kiroho Timotheo ya kwamba dua,sala na maombezi na shukrani vifanyike kwanza kabla ya mambo yoyote yale. Maneno haya siku ya leo unaambiwa wewe usomaye ujumbe huu,kwamba kabla ya chochote kile shukrani na maombi yafanyike kwako,maana Timotheo wa leo ni wewe. Maneno haya ni maneno ya kichungaji,kwa sababu;

Ikumbukwe kwamba;

Nyaraka mbili za Paulo kwa Timotheo pamoja na waraka kwa Tito ni nyaraka za kichungaji kwa sababu zinashughulikia maisha ya kanisa.Yaani nyaraka hizi zinashughulikia uhai wa kanisa.
Wakati zilipoandikwa,tayari kanisa lilikuwa hai kwa muda wa miaka thelathini na ndipo baadhi ya mitume walishaanza kufa.

Hivyo nyaraka kwa Timotheo ni nyaraka za kichungaji. Ikumbukwe pia,Timotheo aliachwa kule Efeso kuilea jamii kubwa ya kiKristo ambayo ilikuwa inakuwa kwa kasi zaidi,jamii hii ya Efeso ilikuwa imejaa mafundisho ya uongo mno kwa kuiabudu miungu ya kigeni. Hivyo katika hali kama hiyo,Paulo anamsisitizia aanze na maombezi na shukrani maana anajua katika maombezi na maombi pamoja na shukrani pana nguvu ya ajabu yakuweza kubadili yote maovu.

Paulo angeliweza kumwambia Timotheo aanze na kukusanya sadaka,au labda angeliweza kumuambia kabla ya mambo yote aanzie na matangazo kwa waamini,lakini la! Paulo akatambua thamani ya nguvu iliyopo katika kushukuru na maombi,na ndio maana hakutaka chochote kile kianze isipokuwa maombi, ndivyo ikupasavyo wewe Timotheo wa leo. Paulo analiambia pia kanisa la leo,kwamba kabla ya kuanza kwa ratiba yoyote ile katika kanisa,basi maombi,dua,na shukrani yaanze kwanza.
Mkazo mkubwa katika andiko hilo ni kuyapa kipaumbele maombi,maombezi na shukrani.

Haipendezi hata kidogo kuanza jambo lolote lile pasipo maombi. Sababu wapo watu wenye kufanya mambo mengi pasipo kuomba,kisha wanajikuta mambo yao hayaendi ipasavyo. Lakini leo,neno linakutaka uanze kwanza na ibada ya maombi,haijalishi upo sehemu gani,hajalishi upo na nani mbele yako,wala hajalishi umekaa au umesimama bali anza maombi kwanza kisha uone mambo yatakavyofunguka.

Yaani,sikia;
Mfano hata kama umeingia ofisini kwa mtu,wewe piga maombi hata kama ni maombi ya kimya kimya,au ikiwa umefika nyumbani kwako au kwa jirani dawa ni ile ile ,piga maombi ipasavyo,usikae kimya!. Sababu majibu yako yapo katika maombi,miujiza yako yapo katika maombi na shukrani.

Jamii ya Kikristo ya huko Efeso,ilikuwa ni jamii yenye michanganyo ya mafundisho ya kweli na ya uongo ndani yake. Jamii hiyo ni sawa sawa kabisa na jamii tunayoishi sasa. Hivyo huwezi kujua njia sahihi ni ipi usiposimama imara katika ibada ya maombi. Maombi ni ibada kamili.Maombi ya kina yakikosekana katika ibada yoyote ile,basi ujue ibada hiyo hajakamilika katika ukamilifu wake. Ngoja nikupe mfano mdogo;

Siku moja tulipokuwa kanisani katika ibada,kabla ya maombi kila mtu alikuwa akimsifu Mungu wake.Na kipindi hicho cha sifa hakuna aliyegundua mtu mwenye mapepo ni yupi maana kila mmoja alikuwa akionekana akimsifu Mungu wake. Lakini tulipoaanza maombi tu,gafla tukasikia binti mmoja akipiga kelele ” naungua…naungua..” akadondoka chini na mapepo yakaanza kumgalagaza chini. Kumbe maombi yana moto katika kila aina ya nguvu za giza.Umeonaa!Nguvu za giza,hazifukuzwi kwa kitu kiwayo chochote kile,Bali kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti aliye hai katika maombi,kwa jina hilo hakuna kitakachosalia.Ukitaka kujaribu hili nikuambialo,wewe omba kwa jina hili lenye nguvu,mamlaka,na utiisho wa kipekee.

Paulo alijua thamani ya maombi na maombezi katika kanisa,thus anamkumbusha mtoto wake wa kiroho aanze na maombi kabla ya chochote kile.

Mimi huwa ninashangaa sana kanisa linalolanza na ratiba nyingine mbali na ratiba ya maombi kabla ya chochote kile. Mafunuo haya nikuelezayo leo,ni mafunuo yake Mungu,wala si yangu mimi.Maana nami nafuata maelekezo yake Baba wa mbinguni.Ukitembea popote iwe barabarani,anza na maombi na shukrani,

Ikiwa katika daladala,fanya maombi na shukrani hata kwa kimya kimya ndugu

Ukiwa popote ngangana kumshukuru Mungu kisha tia na maombi hapo mpaka kieleweke kisha uone mambo atakavyokunyookea wala husiogope kwa sababu Bwana yupo upande wako,mwanadamu atakufanya nini? (Zaburi 118:6)Jambo lolote lile lisifanyike pasipo maombi na Shukrani. Paulo anazidi kusisitiza juu ya MAOMBEZI.

Wapo watu leo,hawataki kuombewa kabisaa! wakijidanganya kuwa mizigo waliyokuwa nayo itaondoka yenyewe. Ndugu,sikia;

Hakuna mzigo wowote ule,iwe ni magonjwa au mateso yatakayo kuonea huruma pasipo jina lake Yesu tu. Mateso hayana huruma,wala magonjwa hayana huruma yaondoke yenyewe pasipo nguvu za Mungu ndani ya jina lake Yesu Kristo. Jamani niseme nini tena! Kweli Mungu anakuona katika shida zako,lakini amekupa fursa ya kuliitia jina lake Yesu Kristo aliye hai ili kwa jina hilo ufunguliwe uwe huru,huru kweli kweli.Haleluya…

Katika andiko letu la siku ya leo ( 1 Timotheo 2:1) mkazo wake ni kuanza na Bwana kabla ya chochote kile. Lakini ikumbukwe kuwa mfalme aliyekuwa akitawala katika kipindi cha kina Timotheo alikuwa ni mfalme dikiteta,mtu asiyetaka hata kushauliwa. Paulo akilijua hilo lakini bado anamwambia kiongozi wa kanisa Timotheo akaze kuomba,kushukuru,maombezi kabla ya chochote kile. Maombi hayo ni kwa ajili ya wafalme na wote wenye mamlaka,anasema

“ Basi, kabla ya mambo yote, nataka dua, na sala, na maombezi, na shukrani, zifanyike kwa ajili ya watu wote; kwa ajili ya wafalme na wote wenye mamlaka, tuishi maisha ya utulivu na amani, katika utauwa wote na ustahivu.” 1 Timotheo 2:1-2

Paulo anatufundisha pia na sisi watu wa imani moja naye,kwamba yatupasa kuwaombea viongozi wote na watawala wote hata kama ni madikteta katika nyadhifa zao. Maana kama usipowaombea wewe,atawaombea nani? Kuna watu wasioombea kabisa watawala wa serikali yetu eti kwa sababu ni mafisadi,au kwa sababu hawatekelezi majukumu yao. Huu ni ujinga wa kawaida kabisa,kwamba usiwaombee viongozi! Sasa awaombee nani?

Acha hao wasiombe,bali wewe muombee raisi wako,waombee viongozi wake wote kisha Mungu mwenyewe aingilie kati. Jukumu la kuwaombea na kuwasimamisha viongozi wetu ni la kwetu sisi tulio ndani ya Yesu pasipo kuangalia madudu yao wayafanyayo huko serikalini.

Sasa';

Ukipenda nipigie ili tuanze maombi,maombezi pamoja na shukrani siku ya leo;

Mtumishi Gasper Madumla

Piga; 0655-11 11 49.

UBARIKIWE.

Share on Google Plus

About Ambwene Mwamwaja

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.