SOMO: KUKATA TAMAA NI KIKWAZO KWA MAFANIKIO YAKO

Na Kelvin Kitaso,
GK Guest Contributor.

“Hata vijana watazimia na kuchoka, na wanaume vijana wataanguka; 31 bali wao wamngojeao BWANA watapata nguvu mpya; watapanda juu kwa mbawa kama tai; watapiga mbio, wala hawatachoka; watakwenda kwa miguu wala hawatazimia” Isaya 40:30,31

Msafiri mmoja alifika kituoni tayari kwa kuabiri gari ili aanze safari ya kuelekea sehemu anayopaswa kuwepo na kwa kawaida gari lilikuwa likipita kila siku mapema sana ila kwa siku hiyo ambayo yeye alikuwa akisafiri gari lilichelewa sana, na katika kusubiri kwingi abiria wengi walimkuta kituoni hapo akiwa na shauku ya kusafiri ila anacheleweshwa na usafiri, alianza kujioji ndani na kusema kuwa mimi nimewahi sana kufika mahali hapa ila naondoka pamoja na hawa ambao wamechelewa kuja na pengine wamechelewa kwa kuwa walilala sana, na katika kujioji kwingi aliazimu moyoni mwake kukata tamaa kusubiri usafiri ambao aliusubiri sana na kuamua kuahirisha safari na kurudi nyumbani na pindi alipoondoka ndipo gari likaingia kituoni pale na kuchukua wale waliokuwepo pale, alipopata taarifa kuwa usafiri ulifika muda ule anaondoka aliumia moyoni mwake sana na kujilaumu sana na maamuzi yake ya kukata tamaa;  akasema ‘ningejua nisingeondoka’, ila alisahau kuwa majuto ni mjukuu. Angeweza kufika ila adui kwake alikuwa ni kukata tamaa kwake.

Mahali popote mtu anapokata tamaa hayakosekani yakukatisha tamaa na yapo mambo mengi sana yawezayo kumkatisha mtu tamaa na mara nyingi watu ukatishwa tamaa kwa yale wayaonayo yakitukia, wayasikiayo kwa wengine au katika maeneo ambayo wamewahi kujaribu kufanya vitu kutokea na wakajikuta wakishindwa. Kukata tamaa ni matokeo ya kushindwa kuvumilia, ukweli ni kwamba kukata tamaa ni kitendo kibaya na cha aibu sana kwa kuwa hakuna aliyewahi kufanikiwa ambaye ni mkata tamaa au wa kurudi nyuma.

Uwepo wa Mungu katika maisha ya mwamini ni sababu kubwa kupita zote za kutokukata tamaa kwa kuwa katika yeye bado lipo tumaini na katika yeye mambo yote yanawezekana wala halipo neno gumu la kumshinda cha msingi ni kwenenda kwa imani na wala si katika kuona.

Wanafunzi wa Yesu walitega samaki usiku kucha pasipo kuwavua na kulipokuwa kunakucha Yesu akawaambia watweke nyavu hata kilindini; ukweli Petro alikuwa amechoka na kukata tamaa ila akasema kuwa “tumejaribu usiku kucha ila kwa neno lako tutafanya” kwa maana nyingine ni kusema kwa kuona haiwezekani ila kwa imani inawezekana. Ikiwa yupo Kristo upande wako ipo sababu kuu ya kutokukata tamaa zaidi ya sababu za kukata tamaa.

Kuna msemo wa kiingereza usemao “winners never give up” kwa kumaanisha “washindi uwa hawakati tamaa”. Hata kama zipo sababu elfu tisa mia tisa na tisini na tisa (9999) za kukufanya kushindwa na kukata tamaa ila washindi huwa hawakati tamaa. Kukata tamaa maana ya wazi ni kukubali kushindwa moja kwa moja. Ukishindwa mara hii inuka tena na uanze kupambana tena hata upate kushinda kwa kuwa ndani yako umepewa kushinda katika mambo yote na zaidi ya kushinda.

Kuna watu ukata tamaa katika mambo machache tu waliyojaribu na kujiona kuwa hawana bahati ila washindi hata wakishindwa mara nyingi bado ugeuka na kurudi tena huku wakiwa na imani kuwa inawezekana

Siku moja nikiwa katika ofisi Fulani nikimsubiri mkurugenzi wa ile kampuni, mara akatokea mfanyakazi wa kawaida tu na kuanza kuzungumza nami katika maneno ambayo alkuwa akisema nami baada ya kusubiri muda mrefu sana ni kuniambia kuwa “kama kuna mtihani mgumu katika ulimwengu huu tunaoishi ni kusubiri, na walioweza kufaulu mtihani huu wamefanikiwa kufika katika mambo makubwa sana,” katika kusubiri kwingi nikakumbuka kuwa niliondoka nyumbani asubuhi pasipo kunywa chai, ndipo nikaamua nikatafute sehemu pale jirani nikanywe chai, na nilipofika na kuagiza chai na kuletewa ndipo nikapigiwa simu na mkurugenzi na akanambia nimefika hapa ofisini na sijakukuta na nilikuja mara moja kuonana na wewe, na kwa kuwa haupo sitoweza kukusubiri kwa kuwa nina majukumu mengine sehemu nyingine, ndipo nikajifunza sana katika kusubiri pasipo kukoma kwa kuwa wakati utakapokoma na kukata tamaa ndipo utimilifu upo karibu kutokea na pengine wakati unapokata tamaa ndipo upo mwishoni kabisa.

Mithali 24:16 “Kwa maana mwenye haki huanguka mara saba akaondoka tena; bali wasio haki hukwazwa na mabaya”

Mwenye haki uweza shindwa na si mara moja ila uondoka akarudi tena/usimama tena na si kwamba ukata tamaa ya kusimama tena.

Kwa mtoto jifunzeni.

Napenda kujifunza kwa mtoto mdogo kwani akiwa mdogo uwaona wakubwa wakitembea naye uingia kwenye shauku ya kutaka kutembea kama walivyo wakubwa kwake na katika kuanza kutamani huko uanza na hatua ya chini kabisa ya kutambaa na anapokuwa katika kutambaa aweza kutana na mambo mengi yawezayo kumuumiza miguu na hata mikono na kumkatisha sana tamaa ila kwa kuwa shauku yake ni kutembea uendelea pasipo kuchoka.

Baada ya hatua hiyo uanza na hatua nyingine ya kusimama na hapo bado uwa ni kazi kidogo kwa kuwa utegemea mtu au vitu ili kumfanya asimame na katika hatua hii ukutana na ugumu mwingi tena na kuumia kwingi ila bado usonga mbele kwa kuamini kuwa siku moja nami nitatembea kama wale wakubwa, akifuzu hatua hii uanza na hatua nyingine ya kutembea taratibu na kuendelea kwa kuongeza mwendo kidogo na hatimaye ukomaa kutembea umbali mrefu sana na zaidi uweza kukimbia kama wawezavyo kufanya wengine.

Kwa mfano huu ndivyo inavyoweza kuwa biashara yako au kitu ukifanyacho kwa maana ya kwamba kabla haujaweza hata kutambaa uliona wengine ukatamani sana na kuanza na hatua ndogo kabisa ya kutambaa (kuanzia chini kabisa) ila taswira yako ni kuja kutembea na ukutanapo na mambo magumu katika hatua hiyo usikate tamaa kwa kuwa “makwazo hayana budi kuja”.

Hatua nyingine ni ya kuanza kusimama baada ya kutambaa kwa kitambo kidogo na kusimama huku bado uanza kwa kutegemea watu na pia bado uwa na vikwazo vingi sana ila kukata tamaa hakutakiwi kwa kuwa safari bado ndefu na uogope sana kuishia njiani kwa kuwa ni bora ukachelewa kufika sehemu upaswayo kwenda kuliko kutokwenda kabisa japo kuchelewa nako ni kubaya sana. Katika hili umalizikia kwa kuweza kutembea kwa kujitegemea pasipo kutegemea wengine na zaidi hata kukimbia.

Kama unadhani umechoka sana hata kutojaribu tena jifunze kwa huyu.

Wapo watu waliowahi kuishi duniani na kuweka nia katika mambo wayafanyayo na wakiamini kuwa wanaweza wakafanya mambo makubwa na katika kujaribu kwao wamekutana na kushindwa kwingi, hawa watu wametolewa mfano na watu wengi kwa kuwa historia yao inavutia sana kuwa sababisha wengine kuamasika.

Thomas Edson wakati akiwa mdogo alipelekwa shuleni ila alikuwa mwanafunzi mzito sana katika kujifunza darasani, ilimradhimu mwalimu amchukue mtoto Yule na kumpeleka kwa mama yake na kumwambia kuwa mwanae ni mtoto asiyeelewa lakini mama yake akajibu kwa kukanusha kuwa “mwanangu si mjinga nitamfundisha mwenyewe” na alifanikiwa kwa sababu hakukiri udhaifu juu ya mwanae na hakumkatia tamaa alipokuwa Tommy aliwekeza muda wake kufanya ugunduzi wa bulb ‘taa za umeme’ na katika kufanya hivyo alijaribu majaribio yake mara 9999 na mara ya 10000 (mara elfu kumi) akafanikiwa pasipo kukata tamaa. Ni mfano mzuri kwa mtu mwenye nia ya kufanya mambo.

Pia Abraham Lincoln alishawahi kujaribu kugombea nafasi mbali mbali Marekani na kushindwa zote ila hakukata tamaa kwani alipokuja kugombea uraisi ndipo aliposhinda na kutimiza ndoto zake.

Kukata tamaa ni kuyaua maono uliyonayo, ni vyema ukaendelea mbele kwani utimilifu wa ndoto uliyonayo utawadia.

Kuweza kuendesha baiskeli.

Nikiwa mdogo nilitamani sana kujua kuendesha baiskeli na katika kutamani kwangu walinambia kuwa ukitaka kujua baiskeli ni lazima niumie na kutoka kovu na ndivyo ilivyokuwa na katika wakati ule niliamini kuwa ili kujua baiskeli ni mpaka kuumia na kutoka kovu, kila nilipodondoka na baiskeli na kuumia pamoja na maumivu makali niliingiwa na imani kuwa ni njia kuu ya kunifanya kujua baiskeli na katika kuvumilia kudondoka na kuumia sana baadae nikaweza kuendesha baiskeli. Si kufahamu wakati huo kuwa wapo ambao wanaweza jua kuendesha baiskeli pasipo kuumia na kutoka makovu.

Kauli hii inauhalisia sana katika mchakato wa kuelekea mafanikio yako ni vyema kufahamu kuwa kama shauku yako ni kufanya kitu Fulani hata kama utaumia na kutoka makovu makubwa usikate tamaa inuka jifute na usonge mbele kwani katika kila ugumu kuna mlango wa kutokea. Katika safari ya kuelekea utimilifu wa ndoto zako kupo kushindwa na kushinda kwingi usikate tamaa kwa kuishia njiani wewe songa mbele hata utakapofikia hatima yako.

Ukiweka nia na kumtumaini Mungu mambo yote yanawezekana usije ukakata tamaa kwa ugumu upatao jua kuwa washindi kama wewe upitishwa katika sehemu ngumu.

Shiv Khera anasema “Safari yako ya kuwa mtu mkubwa si nyepesi. Imejaa vikwazo vingi sana. Washindi wanaouwezo wa kushinda…”

Somo hili ni sehemu ya kitabu kiitwacho "Huyu Ndiye Adui wa Mafanikio Yako". Mwandishi anapatikana kupitia 0769190019, 0713804078, kitasokelvin@gmail.com
Share on Google Plus

About Gospel Kitaa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.