SOMO: NGUVU YA KUGEUKA - MTUMISHI MADUMLA

Mtumishi Gasper Madumla.
Bwana Yesu asifiwe sana…

Kati ya jambo kubwa na la msingi katika maisha yako ni ” kugeuka kutoka katika hali ya uaharibifu kuelekea katika njia ya Bwana ”,Kwa sababu hata maana halisi ya kuokoka ni kugeuka kwa kuacha yote maovu na kumpokea Bwana Yesu awe Bwana na mwokozi wa maisha yako.Hivi unajua hata kumuona Mungu ni kumgeukia Yeye kwa kuacha dhambi,tena kwa kuichukia. Shida ya leo ni kwamba watu wamegeuka nusu nusu yaani katika dhambi kidogo,na kwa Mungu kidogo. Neno ” geuka” ni kubadili/kuacha yaliyokuwepo maovu na kuanza kwa muelekeo mpya katika kuyafanya mapenzi ya Mungu Baba.

Hivyo nisemapo ” nguvu ya kugeuka” ni sawa na kusema-Nguvu ya kuyaelekea mapya ya Bwana. Yaani ni kubadili mfumo mzima wa maisha yako kwa kuacha yote maovu uliyoyazoelea kuyafanya.Katika kuacha yote na kumgeukia Bwana ipasavyo ndipo penye mpenyo wako,na ndipo maisha ya wokovu yanapatikana. Ngoja tuliangalie jambo hili kiblia,tunasoma hapa;

” Musa akasema, Nitageuka sasa, niyaone maono haya makubwa, na sababu kijiti hiki hakiteketei.
Bwana alipoona ya kuwa amegeuka ili atazame, Mungu akamwita kutoka katikati ya kile kijiti, akasema, Musa! Musa! Akasema, Mimi hapa.
Naye akasema, Usikaribie hapa; vua viatu vyako miguuni mwako; maana mahali hapo unaposimama ni nchi takatifu. ” Kutoka 3:3-5

Sikia;

Mara tu baada ya Musa kugeuka,tunaona Mungu akianza kusema naye. Mungu hakusema naye pale Musa alipokuwa akitizama kwengine,lakini alipoamua kugeuka,gafla Mungu anaanza kusema naye na kumpa maagizo makubwa sana. Ndiposa nikajifunza baadhi ya mambo kwa habari ya kumgeukia Bwana;01. Ukigeuka,ni lazima Bwana aseme nawe.

Kwa neno hilo,yamkini Musa asingeligeuka basi maagizo hayo yote asingeyapata.Maelekezo ya Mungu yalihitaji utayari wa Musa katika kugeuka. Na ndivyo jinsi ilivyo hata sasa.Maelekezo ya Mungu kwako yanategemea kugeuka namna ya kugeuka kwako,tena hatma ya maisha yako yanategemea mgeuko wako kwa Bwana.Haijalishi unapitia mazingira gani,lakini ukiamua kugeuka basi tegemea kuisikia sauti ya Bwana Mungu wako.

Kwa lugha nyepesi kabisa ni kwamba hata kama Mungu alimuita Musa,lakini Musa asingeligeuka na kuitika basi maagizo yale asingeyapata. Leo,tazama ni mara ngapi umeisikia sauti ya Bwana ikikuita ili ugeuke kutoka katika huo ubaya, lakini hutaki kugeuka kwa sababu ya kuwa na shingo ngumu hatimaye kukosa maagizo ya Bwana Mungu aliye hai.

Watu wengi tumejizuilia haadi zetu kwa sababu hatujaamua kumgeukia Mungu ipasavyo.Yamkini hata kufanikiwa kwako kungekuwa ni kukubwa kuliko hivyo ulivyofanikiwa sasa, laiti kama ungemgeukia Mungu na kuacha vyote kwa ajili yake.Kuacha yote ni kuacha kila namna ya dhambi na kuyaona mambo hayo kama mavi kwa ajili ya kumpata Kristo ( Wafilipi 3:8)

Maagizo ambayo Bwana atakupa mara tu baada ya kumgeukia,mara nyingi maagizo hayo huwa ni magumu kiasi kwamba huwezi kuyatimiliza wewe kwa akili zako mwenyewe pasipo kuhitaji msaada wa Roho mtakatifu.

Mfano;

Maagizo aliyopewa Musa ni maagizo magumu,kwa maana Mungu anamtuma kwa Farao mahali ambapo Musa alipakimbia,na isitoshe yeye Musa hakuwa msemaji mzuri, hivyo Mungu akaachilia msaidizi kwa Musa ambaye ni ndugu yake Haruni. Kwa lugha nyingine Haruni alikuwa kama Roho mtakatifu kwa Musa na Musa alikuwa kama Mungu kwake,na ndiposa mambo yakaenda ipasavyo.

Hata wewe,ukipewa agizo na Bwana baada ya kumgeukia ujue basi utamuhitaji Haruni wako ambaye kwa sasa Haruni ni Roho mtakatifu.02.Kugeuka ni kutubu kila uovu/Kuvua utu wa kale.

Bwana akamwambia Musa avue viatu,akimaanisha ayaache mambo ya kele,auache uovu,aziache dhambi zake,atubie kila uaovu. Tazama neema hii,ni neema ya namna gani,yaani mara tu ya kugeuka Mungu anaachilia fursa ya kuziungama madhambi yako. Wakati utakapoamua kumgeukia Bwana basi ujue Bwana atakuona angali u mbali,tazama jinsi mwana mpotevu alivyogeuka,tunasoma;

” Alipozingatia moyoni mwake, alisema, Ni watumishi wangapi wa baba yangu wanaokula chakula na kusaza, na mimi hapa ninakufa kwa njaa.
Nitaondoka, nitakwenda kwa baba yangu na kumwambia, Baba, nimekosa juu ya mbingu na mbele yako;
sistahili kuitwa mwana wako tena; nifanye kama mmoja wa watumishi wako.
Akaondoka, akaenda kwa babaye. Alipokuwa angali mbali, baba yake alimwona, akamwonea huruma, akaenda mbio akamwangukia shingoni, akambusu sana.” Luka 15:17-20

Biblia inasema huyu kijana ” alipozingatia moyoni mwake” kumbe! Kugeuka ni kuzingatia moyoni kuacha maovu. ” Kuzingatia moyoni ” ni kugeuka kwa moyo kutoka njia moja na kuelekea njia nyingine,au kwa lugha nyepesi ni ile hali ya kugeuza nia yako ya ndani. Biblia imesema pia ” Wala msiifuatishe namna ya dunia hii; bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, …” Warumi 12:2

Kijana alipozingatia moyoni mwake,akageuka akaondoka mpaka kwa babaye,na tazama babaye akamuona angali mbali naye. Na hivi ndivyo inavyokuwa hata sasa,Yeyote aliyegeuza nia yake -Bwana humuona mtu huyo tangia mbali.

Zipo faida nyingi sana kwa kumgeukia Mungu kwa toba halisi.Mfano huo mdogo wa kijana aliyekuwa amepotea mbali na uso wa babaye unatuonesha jinsi gani alivyopewa vitu vya thamani pasipo kuviomba apewe.Na ndivyo hali ilivyo hata sasa,Ukigeuka na kuacha dhambi,basi ujue kwamba utapokea mambo mazuri makubwa hata kama hukuyaomba.Faida ya kwanza kwa yule amgeukiaye Mungu ni kuheshimishwa mno.

Kijana aliyepotea,aliporudi kwa babaye aliheshimishwa mno kiasi kwamba hata yeye mwenyewe alijishangaa jinsi ambavyo baba yake alivyompokea.Hata kwako inawezekana kuheshimishwa mno endapo ukiamua leo kuyaacha ya kale,na kumgeukia Mungu aliye hai.

Nampenda Zakayo jinsi anavyotufundisha kwa habari ya kugeuka.Alipotaraji kumuona Bwana Yesu alibidi apande juu ya mkuyu sababu alikuwa mfupi wa kimo. Biblia inasema;

” Na Yesu, alipofika mahali pale, alitazama juu, akamwambia, Zakayo, shuka upesi, kwa kuwa leo imenipasa kushinda nyumbani mwako. ” Luka 19:5

Bwana Yesu alipomuita Zakayo,Zakayo aligeuka na kumtizama kisha Yesu akamwambia ” shuka upesi kwa kuwa leo imenipasa kushinda nyumbani mwako” Kwa lugha nyingine pata picha kama Yesu alivyomuita Zakayo,kisha Zakayo asingemgeukia Yesu na kuendelea kuungangania mkuyu unafikiri wokovu mkuu ungeliingia nyumbani mwake?

Ukiamua kwa dhati kuachilia mkuyu ulioushikilia,na kumgeukia Bwana basi tegemea wokovu mkuu ndani ya maisha yako.Mkuyu wa leo inawezekana ukawa ni mitazamo yako ya kiimani kwamba umengangania dini yako na wala si wokovu.Au mkuyu wa leo unawezekana ukawa ni kuukataa wokovu ulio mkuu,Lakini leo Bwana akuambia shuka upesi kutoka katika huo mkuyu,kisha ukauone wokovu mkuu ndani ya maisha yako.

Nguvu ya kugeuka inakufanya kushuka zaidi mbele za Bwana,yaani kunyenyekea ili Bwana akupandishe Yeye,na hapo ndipo ukristo halisi hupatikana.

Wapo watu wenye kungangania dhambi kidogo,wokovu kidogo kwamba hawataki kugeuka moja kwa moja mbele za Bwana.Nao hujikuta wakipita katika hali ngumu,sababu wamegeukia mambo mengi ya kidunia na wala sio Mungu aliye hai.Bwana Mungu aliye hai ameweka fursa ya kumrudia Yeye sasa,* Tafadhali nipigie tuombe pamoja,piga kwa namba yangu hii;

0655-11 11 49.

Mch.Gasper Madumla.

Beroya bible fellowship church.

S.L.P 55051,Dar.UBARIKIWE.
Share on Google Plus

About Ambwene Mwamwaja

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.