TAARIFA YA IDARA UHAMIAJI KWA UMMA - 18 MACHI 2015


JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI
IDARA YA UHAMIAJI


TAARIFA YA IDARA YA UHAMIAJI KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU HABARI ZILIZOANDIKWA KATIKA GAZETI LA ‘JAMHURI ’ LA TAREHE 10 – 16 MACHI, 2015

TAARIFA KWA UMMA
1.0        UTANGULIZI
Katika gazeti la Jamhuri la tarehe 10-16 Machi 2015, toleo No. 180, iliandikwa makala iliyokuwa na kichwa cha habari katika ukurasa wa kwanza kisemacho “Uhamiaji waamua ‘kuuza’ nchi” na katika ukurasa wa tatu “Uhamiaji wauza nchi”.  Kimsingi kwa mujibu wa yaliyomo katika makala hiyo baadhi ya taarifa zinahitaji ufafanuzi wa Idara ya Uhamiaji.

2.0        UFAFANUZI WA IDARA YA UHAMIAJI
Baada ya kuipitia makala hiyo kwa makini, Idara ya Uhamiaji inapenda kutoa maelezo yafuatayo:
i.               Madai ya kwamba maisha ya watanzania yamo hatarini kutokana na mtandao wa wafanya biashara ya kusafirisha binadamu duniani (Human Traffickers) kutoka nchini Pakistani ni madai ya kushangaza hususan kwa jinsi yalivyohusishwa na habari iliyotolewa katika hiyo makala.  Idara ya Uhamiaji inapenda kuufahamisha umma kuwa hakuna mtandao wa wafanya biashara ya kusafirisha binadamu kutoka Pakistani hapa nchini kama inavyodaiwa katika makala hiyo, na hivyo kauli ya kusema maisha ya watanzania yamo hatarini haina msingi kabisa.
ii.             Madai ya kwamba ‘mtandao huo’ ambao kimsingi haupo kama tulivyokwishaeleza, umeanza kuwateka baadhi ya ‘wakubwa’ katika Idara ya Uhamiaji na kusimika mizizi yake, na hivyo kuwawezesha ‘wanamtandao’ hao kusafirisha Wapakistani na Wasomali bila wasiwasi kupitia hapa nchini kwenda Afrika Kusini ni ya kushangaza sana. Ni vyema ikafahamika kwa umma kama ambavyo mara kwa mara tumekuwa tukieleza, Idara ya Uhamiaji ni Taasisi ya Serikali ambayo watumishi wake wote hutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za nchi. Kwa msingi huo hakuna ‘wakubwa’ wa aina yeyote katika Idara hii waliotekwa, wala hakuna ‘mizizi’ iliyosimikwa ya kuwawezesha wahalifu kusafirisha Wapakistani na Wasomali kupitia hapa nchini kwenda Afrika Kusini kama inavyodaiwa katika makala hiyo.

iii.            Tunapenda kuufahamisha Umma kuwa Idara ya Uhamiaji ipo mstari wa mbele kupambana na wahalifu wa makosa yote ya kiuhamiaji ikiwemo biashara haramu ya usafirishaji binadamu kutoka nchi moja kwenda nyingine inayohusisha watu kutoka mataifa mbalimbali na sio Pakistani na Somalia tu kama ilivyodaiwa katika makala hiyo. Kwa mfano, kwa mwaka 2013, watu 38,776 kutoka mataifa mbalimbali yapatayo 44 walikamatwa kwa makosa ya kiuhamiaji na kwa mwaka 2014 raia wa kigeni wapatao 7568 kutoka mataifa 47 ya kigeni walikamatwa. Pamoja na utendaji wa kila siku, Idara ya Uhamiaji inaendelea kujiimarisha katika utendaji wake ikiwa ni pamoja na kubuni mikakati ya kuimarisha mbinu za utendaji, kuimarisha uwezo wa watumishi kwa kuwapatia mafunzo ya kuongeza weledi na kuongeza vitendea kazi bora zaidi ili kukabiliana na changamoto wanazokabiliana nazo katika kupambana na uhalifu wa makosa ya kiuhamiaji.

iv.           Idara ya Uhamiaji pia, inapenda kuweka bayana kuwa, hakuna mtandao wa Wapakistani wenye mawasiliano na Makamishna katika Idara ya Uhamiaji na wala hakuna viongozi wanaokutana na huo ‘mtandao’ aidha Dar es Salaam au wakati mwingine nje ya nchi kama inavyodaiwa. Idara ya Uhamiaji inasisitiza, taarifa hizo sio za ukweli na zinastahili kupuuzwa.

v.            Kuhusu madai ya kwamba yapo ‘maafikiano’ ya mwaka 2014 ‘kuwashughulikia’ wote wanaokwenda kinyume na mtandao uliopo Idara ya Uhamiaji kwa kuwahamisha vituo vya kazi ni taarifa ya kushangaza na yenye kuleta maswali zaidi ya majibu. Kimsingi uhamisho ni jambo la kawaida katika utumishi wa umma ambapo watumishi huweza kuhamishwa kutoka sehemu moja ya kazi kwenda nyingine hususan pale inapotokea haja ya kufanya hivyo kwa kuzingatia mahitaji ya nguvukazi katika kituo husika, uimarishaji wa tija, weledi na ujuzi kwa watumishi, na uwezo wa bajeti n.k. Kwa mantiki hiyo inakuwa vigumu kuelewa mtoa taarifa alikusudia nini alipowasilisha madai ya kwamba uhamisho wa mwaka 2014 umefanywa baada ya ‘maafikiano’ ili kuwashughulikia wote wanaokwenda na kinyume na ‘mtandao’. Idara ya Uhamiaji inapenda kuufahamisha umma kuwa haina maafikiano na mtu yeyote, wala kikundi cha watu yanayohusu uhamisho.

vi.           Kuhusu gharama za uhamisho zinazotajwa kufikia shilingi bilioni 2.6, sijui mtoa taarifa amezikokotoa kutoka chanzo kipi kwani Idara ya Uhamiaji haijawahi kutumia kiasi kama hicho kwa ajili ya gharama za uhamisho tu. Hata hivyo ni vyema ikaeleweka kwamba, malipo ya gharama za uhamisho ni haki ya mtumishi na hivyo ni wajibu wa taasisi husika kumlipa mtumishi anaehama malipo anayostahili. Kwa misingi hiyo Idara ya Uhamiaji, kama ilivyo kwa Taasisi nyingine za Serikali hutenga fedha kwa ajili ya gharama za uhamisho wa watumishi kama ambavyo imefanyika kwa mwaka wa fedha wa 2014/2015.


vii.         Kuhusu madai kwamba kuna mtu anaejulikana kwa jina la Ajaz Ahmed ambaye ni kiongozi wa mtandao wa usafirishaji binadamu hapa nchini na kwamba baada ya kuondoshwa nchini amerejea kupitia kituo cha mpakani cha Namanga, kimsingi jinsi taarifa hii ilivyowasilishwa imepotoshwa kwa kiasi kikubwa. Idara ya Uhamiaji inapenda ieleweke kama ifuatavyo; Mtu anaefahamika kwa jina la Ajaz Ahmed Muhammad raia wa Pakistani alishtakiwa kwa kujihusisha na biashara haramu ya usafirishaji binadamu  (Kesi ya Jinai Na. 176/2014) ambapo tarehe 28 Oktoba 2014 alikubali mashtaka na hivyo kuhukumiwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kifungo cha miaka 10 jela au kulipa faini ya shilingi Milioni Tano na Laki Tano (5,500,000). Tarehe hiyo hiyo alilipa faini na kisha akapewa Taarifa ya kuwa ni Mtu Asiyetakiwa Nchini (Prohibited Immigrant Notice) Na. 0050968, ambayo ilimtaka aondoke nchini ndani ya masaa 24. Ndugu Ajaz aliondoka nchini tarehe 29 Oktoba 2014 kwa ndege ya shirika la ndege Qatar.


viii.        Idara ya Uhamiaji inapenda kuufahamisha umma kuwa ndugu Ajaz Ahmed Muhammad ni mtu asiyetakiwa nchini (Prohibited Immigrant) kwa mujibu wa kifungu cha 10 cha sheria ya Uhamiaji ya mwaka 1995 sura ya 54, na hivyo madai ya kwamba, mtu huyo ana mawasiliano ya karibu na ‘watu wake’ waliopo idarani waliofanikisha yeye kurudi nchini; au utaratibu uliotumika kumuondosha nchini sio ule wa kumpa taarifa ya mtu asietakiwa nchini  (Prohibited Immigrant Notice) na badala yake aliamriwa tu kuondoka nchini  (Order of Departure-OD) ni taarifa zisizo sahihi. Ukweli ni kama ulivyoelezwa hapo juu, ndugu Ajaz Ahmed Muhammad aliamuriwa kuondoka nchini na alikwishaondoka tokea tarehe 29 Oktoba 2014, na hajarudi tena nchini kama inavyodaiwa.

ix.           Kuhusu madai kuwa ndugu Ajaz Ahmed Muhammad anajipanga kuhakikisha kuwa anawashughulikia wote walioshughulikia kuondoka kwake, ni madai yasiyo na msingi na yenye kushangaza. Idara ya Uhamiaji inajiuliza ni kwa jinsi gani mtoa taarifa ameweza kujua kuwa ndugu Ajaz Ahmed Muhammad ana hiyo mipango ya kuwashughulikia waliohusika kumwondosha. Ni vyema ikaeleweka wazi kuwa, watumishi wa Idara ya Uhamiaji hutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria na maelekezo halali ya uongozi wa Idara, na kwamba hakuna mtumishi anaefanya jambo lolote kwa utashi wake mwenyewe au kumfurahisha mtu, vinginevyo atakuwa hajui wajibu wake na bila shaka atakuwa anakwenda kinyume na kanuni za utumishi wa Umma.  Kwa misingi hiyo, ni dhahiri hakuna mtumishi wa Idara ya Uhamiaji anayetekeleza majukumu yake kwa kumwogopa mtu yeyote, au kundi la watu na kwamba mtumishi yeyote anaetekeleza majukumu yake kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za kazi anayo haki ya kulindwa na Sheria zinazompa mamlaka hayo.

x.             Kuhusu madai ya watu ambao wametajwa kuwa raia wa Pakistani walioondoshwa nchini baada ya kubainika kujihusisha na biashara haramu ya kusafirisha binadamu, Idara ya Uhamiaji inajiuliza hivi mtoa taarifa ana lengo gani? Je mtoa taarifa ni mtu ambae alikuwa na fursa ya kupata taarifa hizo na kisha kuamua kuzitoa kwa mwandishi? Kama ndivyo, je kufanya hivyo ni sahihi kiutendaji? Je mbele ya jamii inayomfahamu anaonekana ni mtu wa aina gani? Mtu asie mwaminifu? Mtu asie stahili kukabidhiwa dhamana nyeti au ni mtu asiefahamu hata wajibu wake? Ni maswali mepesi lakini yanayoweza kuwa na majibu mengi. Kimsingi, watu waliotajwa katika makala hiyo ni raia wa Pakistani, na kwamba ni kweli walipewa hati za kuwataarifu kuwa ni raia wa kigeni wasiotakiwa kuwepo nchini  (Prohibited Immigrants Notice) na uamuzi wa kuwaondosha nchini haukubadilika. Vilevile katika makala hiyo mtoa taarifa yaelekea ana ufahamu mzuri wa njia zinazotumiwa na watu wanaofanya biashara haramu ya kusafirisha binadamu kwani amejitahidi kuelezea sehemu wanazopitia na hata usafiri wanaoutumia. Idara ya Uhamiaji imezichukulia taarifa hizo kwa uzito mkubwa na inaendelea kuzifanyia kazi kwani kama anayoyasema ni sahihi haiyumkini anaweza kuwa ana taarifa zaidi za mitandao ya uhalifu wa kiuhamiaji na hata wa makosa mengine ya jinai.


xi.           Kuhusu madai kuwa ‘wanamtandao’ hao wamejizatiti kuboresha mtandao wao kwa kujiweka karibu na vigogo wenye nia ya kuwania ubunge kwa kuwawezesha kifedha na kwamba mmoja wao anadaiwa kuandaliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi ni taarifa za kushangaza na zinazoleta maswali mengi zaidi ya majibu. Idara ya Uhamiaji imeshindwa kuelewa mtoa taarifa amepata wapi taarifa hizo. Ni vyema ikaeleweka wazi kuwa, masuala ya uchaguzi yanaongozwa na Sheria za nchi, na ni jambo la kushangaza pale mtu anapofikiria kuwa ni rahisi kwa mtu mmoja au kundi la watu wenye dhamira ya kutenda uhalifu kumsaidia mtu kufikia malengo yake katika uchaguzi na hata kupata nafasi ya uwaziri. Idara ya Uhamiaji inasisitiza kuwa fikra kama hizi sio tu kwamba ni potofu, bali pia hazina mashiko na zinastahili kupuuzwa.

xii.          Kuhusu madai kuwa Wizara (haikufafanuliwa ni Wizara ipi katika taarifa yake) ilimtaka Kamishna Mkuu wa Uhamiaji Sylvester Ambokile kueleza ni kwa nini Ajaz amerudi nchini, na kwamba hakuwahi kufanya hivyo ni madai yasio na ukweli. Idara ya Uhamiaji imeshindwa kuelewa mtoa taarifa kwenye Gazeti la Jamhuri  ya kwamba Wizara  ilimtaka Kamishna Mkuu kutoa maelezo kuhusu kurejea kwa Ajaz amezipata vipi. Kimsingi mawasiliano ya Serikalini yana taratibu zake ikiwemo kuwasiliana kwa maandishi kutoka ngazi moja ya maamuzi kwenda nyingine. Sasa jambo ambalo Idara ya Uhamiaji inajiuliza huyo mtoa taarifa aliona wapi barua au waraka unaotoa maelekezo kwa Kamishna Mkuu kama anavyodai kama sio kauli ya uzushi au kufikirika? Kama ilivyoelezwa hapo juu Ndugu Ajaz Ahmed Muhammad alikwishaondoshwa nchini tangu tarehe 29 Oktoba 2014 na hajarudi tena nchini kwa kuwa amri ya kumuondosha nchini bado ipo kwa mujibu wa sheria. Hivyo suala la Kamishna Mkuu kutakiwa kutoa maelezo ya kurejea kwake halipo, na taarifa hii dhahiri ina lengo la kupotosha umma na inapaswa kupuuzwa.

xiii.        Kuhusu madai kuwa kumekuwa na makundi ndani ya Idara ya Uhamiaji katika utekelezaji wa majukumu yake kutokana na kuvurugwa na mtandao huo, ni taarifa zisizo na ukweli. Kama tulivyoeleza hapo juu, hakuna mtandao wowote hapa nchini unaojihusisha na biashara haramu ya kusafirisha binadamu na kwamba mtoa taarifa alipokusudia kutoa taarifa hii, huenda alikuwa amesukumwa na nia au lengo la kutaka kuichafua Idara ya Uhamiaji ili aweze kupata alichokikusudia. Kimsingi, Idara ya Uhamiaji inafanya kazi kwa kuzingatia muundo rasmi ulioidhinishwa na Mh. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na hivyo ni vyema ikaeleweka bayana kuwa, hakuna makundi ndani ya Idara ya Uhamiaji kama inavyodaiwa.

3.0        HITIMISHO
Idara ya Uhamiaji inapenda kuhitimisha taarifa hii kwa maelezo yafuatayo:
·               Pamoja na kwamba Kichwa cha habari cha makala tuliyoielezea kinasomeka “Uhamiaji waamua kuuza Nchi”, kama kilivyokusudiwa na mtoa taarifa, hata hivyo maelezo yaliyo katika makala hiyo hayafanani kabisa na kichwa cha habari na hivyo kuleta maswali mengi kuliko majibu.  Idara inajiuliza je, lengo la mtoa taarifa ni kufikisha ujumbe gani?  Kama ana ujumbe alitaka kuufikisha je ni kwa faida yake au ya mtu mwengine? Na kwa nini aamue kutumia njia hiyo wakati anafahamu Idara ya Uhamiaji ipo na angeweza kuzifikisha taarifa zake? Bila shaka kama alikuwa na ujumbe unaomkera yeye binafsi angetumia njia zinazotambulika ili kupata ufumbuzi wa kinachomkwaza na sio utaratibu alioutumia wa kutoa taarifa zisisizo na ukweli kupitia gazeti, njia ambayo tunaiona imelenga kuichafua Idara ya Uhamiaji kwa ujumla wake bila kujua athari zake.  

·               Idara ya Uhamiaji inapenda kuwakumbusha wananchi kuwa inathamini na itaendelea kuthamini mchango wao na jamii kwa ujumla katika mapambano dhidi ya uhalifu wa makosa ya kiuhamiaji na kwamba inatoa rai kwa wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa Idara, kwa kutoa taarifa pale wanapobaini watu wanaotaka kutenda au wanaotenda makosa ya kiuhamiaji na inaahidi kuchukua hatua stahiki na za haraka pindi itakapo pata taarifa.IMETOLEWA NA KITENGO CHA UHUSIANO
IDARA YA UHAMIAJI MAKAO MAKUU
DAR ES SALAAMShare on Google Plus

About Gospel Kitaa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.