WAJIBU WA KANISA KUHUSU UDHIBITI WA VITENDO VYA UKATILI KWA ALBINO

Na Askofu Sylvester Gamanywa.
©Chika Oduah/Huffington Post.
Nchi yetu imegubikwa na janga la kutisha na kusikitisha la imani za ushirikina unaoendesha vitendo vya ukatili na mauaji dhidi ya jamii ya ndugu zetu wenye ulemavu wa ngozi maarufu kwa jina la “Albino”. Tumeshuhudia vitendo hivi vya kinyama vikishamiri mpaka vimeifanya Tanzania kutafsiriwa kuongoza katika bara la Afrika kwa habari za imani za ushirikina. Katika harakati za kupinga vitendo hivi, serikali imekuwa ikitupiwa lawama kwa kushindwa kuwachukulia hatua kali watu wanaosababisha vitendo hivi, na hivi karibuni tumekwisha kutangaziwa kutoka kwenye vyombo vya kisheria adhabu zilizokwisha kutolewa dhidi ya waliopatikana na hatia, ikiwa ni pamoja na hukumu ya kifo. Aidha, hata madhehebu ya dini nayo; kwa nyakati tofauti, yamekwisha kutoa matamko makali ya kupinga vitendo hivi. Ni katika mazingira haya, nimelazimika kuwasilisha mada hii, ambayo naona ni muhimu kulikumbusha kanisa wajibu wake wa kibiblia wa kudhibiti vitendo hivi, badala ya kuishia kwenye kutoa matamko peke yake:

Kanisa la kwanza lilivyo dhibiti
vitendo vya uchawi katika jamii

Msamiati wa kawaida wa neno “Kanisa” kwa mujibu wa dini ya Kikristo, ni makundi ya kiimani yenye madhehebu mbali mbali yenye kuamini Mungu kupitia kitabu cha Biblia takatifu. Sipendi kuingia kwa undani kuchambua ukweli na uhalisia wa makundi yanayojiita kanisa.

Hata hivyo, katika mada hii, ninapenda kurejea kwenye Biblia, katika Agano Jipya, na kulichambua “Kanisa la kwanza” ili kuona lilivyowajibika kushughulikia na kukomesha vitendo vya imani za ushirika katika jamii ya binadamu wa karne ya kwanza.

Kitabu cha Matendo ya Mitume, kimenukuu visa vingi ambavyo Mitume na wahubiri wa Injili wa kanisa la kwanza, walivyokabiliana na wachawi na waganga wa tunguri ambao walikuwa wakiendesha shughuli za uganga na uchawi na kufikia hata kuziharibu kazi zao kwa Injili yenye nguvu za Roho Mtakatifu. Kwa kuanzia leo, hebu tusome sehemu ya maandiko yenye kuonyesha udhibiti wa kishindo dhidi ya vitendo vya ushirikina katika mji wa Efeso:

“Habari hii ikajulikana na Wayahudi wote na Wayunani waliokaa Efeso, hofu ikawaingia wote, na jina la Bwana Yesu likatukuzwa. Na wengi wa wale walioamini wakaja wakaungama, wakidhihirisha matendo yao. Na watu wengi katika wale waliotumia mambo ya uganga wakakusanya vitabu vyao, wakavichoma moto mbele ya watu wote;wakafanya hesabu ya thamani yake, wakaona ya kwamba yapata fedha hamsini elfu. Hivyo ndivyo neno la Bwana lilivyoozidi na kushinda kwa nguvu.” (Mdo.19:17-20)
Kupitia maandiko haya hapa juu, tunasoma habari za mambo muhimu yapatayo kama sita hivi. Tunasoma kwamba, “habari hii ikajulikana na wayahudi na wayunani wa Efeso”, pili tunasoma, “hofu ikawaingia wote”, tatu tunasoma, “Jina la Bwana Yesu likatukuzwa”, nne tunasoma, “walioamini wakaungama”, tano tunasoma, “washirikina wanachoma vitabu vya uganga”, na sita tunasoma, “Neno la Bwana likazidi kushinda kwa nguvu.” 
Maneno haya yanatupa picha kuhusu kishindo cha Injili ya Kanisa la kwanza ilivyoshughulikia vitendo vya imani za ushirikina katika karne ya kwanza, kiasi ambacho, waganga wa tunguri walisalimu amri na tunguri zao kuchomwa moto hadharani.

Maandiko tuliyosoma yanatokana na kisa kimoja ambacho kimesimuliwa kwenye maandiko yaliyotangulia hayo tuliyosoma. Kisa chenyewe kilianza na kikundi cha “waganga wa tunguri” waliojulikana kufanya shughuli za “kupunga pepo”. Kikundi hiki kilivuka mipaka yake na kuingilia huduma za kutaka “kutoa pepo” kwa kutumia mamlaka ya Yesu aliyekuwa akihubiriwa na Mtume  Paulo. 
“Baadhi ya Wayahudi wenye kutanga tanga, nao ni wapunga pepo, wakajaribu kutaja jina la Bwana Yesu juu yao waliopagawa na pepo wachafu, wakisema, Nawaapisha kwa Yesu, Yule anayehubiriwa na Paulo…” (Mdo.19:13)
Kitendo kile kiliwakasirisha wale pepo ambao walianza kukemewa na hawa “wapunga pepo” na kuwahoji kupitia kinywa cha yulle mtu waliyempagaa:
“Yule pepo mchafu akawajibu, akawaambia, Yesu namjua, na Paulo namfahamu, lakini ninyi ni nani? Na Yule mtu aliyeppagawa na pepo mchafu akawarukia wawili, akawaweza, akawashinda, hata wakatoka mbio katika nyumba ile hali wa uchi na kujeruhiwa.” (Mdo.19:15-16)
Baada ya maandiko tuliyosoma hapa, mbeleni ndipo tunakutana na kifungu cha maandiko tulichosoma hapo awali kisemacho “ Habari hii imajulikana na Wayahudi na Wayunani wa Efeso…”! Sasa unaweza kushuhudia kishindo cha Injili ya mitume wa kanisa la kwanza, jinsi kilivyosambaratisha shughuli za uganga na ushirikina uliokuwa ukisimamiwa na “waganga wa tunguri”! 
Kisa hiki kinasisimua sio tu kwamba “wapunga pepo” walioingilia “enzi isiyowahusu” walipata kipigo cha moja kwa moja na pepo ambao walikuwa wakiwakemea; lakini ile habari iliposikika katika jiji la Efeso pia ilisababisha umati mkubwa wa washirikina wengi kujitokeza hadharani na kwenda kanisani ili kujisalimisha kwa kuamua kuvichoma hadharani vitabu na tunguri za uganga. Tunasoma kwamba “hesabu ya thamani ya vitabu vilivyochomwa ilipata fedha hamsini elfu.” Kwa thamani ya fedha ya sasa ya kitanzania maana yake ni shilingi milioni 68!
Katika toleo lijalo, nitaanza kusimulia kwa kina wajibu wa kanisa katika udhibiti wa vitendo vya ushirikina katika jamii kwa mwongozo wa maandiko ya historia ya kanisa la kwanza.

Itaendelea wiki ijayo
Share on Google Plus

About Gospel Kitaa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.