WAJIBU WA KANISA KUHUSU UDHIBITI WA VITENDO VYA UKATILI KWA WATU WENYE ULEMAVU WA NGOZI (2)

©Under the Same Sun
Na Askofu Sylvester Gamanywa

Katika toleo lililopita (soma hapa) tulianza mada mpya inayohusu “wajibu wa kanisa kuhusu udhibiti wa vitendo vya ukatili dhidi ya Albino”! Katika utangulizi wake tulichambua kwa kifupi kwa kupitia harakati za kanisa la kwanza jinsi lilivyodhibiti vitendo vya uchawi katika jamii ya wakati huo. Leo hii tunaendelea katika kujifunza kusudi la ujuio wa Kristo duniani na jinsi alivyoutekeleza na kisha ukaendelezwa na mitume wake:
Mungu amepiga marufuku
katika Biblia shughuli za uchawi

Leo napenda tujikumbushe kwamba, Biblia inatambua kuwepo kwa uchawi katika jamii, lakini sio ndani ya jumuiya za wachaji Mungu. Isitoshe, Mungu alipiga marufuku kabisa kwa wamchao kujihusha katika shughuli za uchawi, au kushirikiana na wachawi katika uchawi wao:

“Msiwaendee wenye pepo, wala wachawi; msiwatafute; ili kutiwa unajisi na wao; Mimi ndimi BWANA, Mungu wenu.” (LAW. 19:31)

Hapa tunasoma jinsi ambavyo Mungu alivyopiga marufuku kuwaendea wenye pepo (waganga wa tunguri) pamoja na wachawi. Sababu ya msingi iliyotolewa na Mungu ni kwamba ushirikina unasababisha mtu kunajisika nafsini mwake. Hawa wachawi na waganga wanatumikishwa na jesho la pepo wachafu ambao kwa asili ni waovu na kila anayejihusisha nao naye anaathirika kitabia na kimahusiano na Mungu.

Kana kwamba hii haikutosha, Mungu alitangaza adhabu dhidi ya mtu Yule ambaye angekiuka na kuvunja marufuku ya kushirikiana na wachawi. Adhabu yenyewe ilikuwa ya kutisha ili kuonesha Mungu asivyotaka kabisa mtu anaye mcha Mungu kuingia katika mambo ya ushirikina:

“Na mtu yule atakayewaendea wenye pepo, na wachawi, ili kuzini pamoja nao, nitakaza uso wangu juu ya mtu yule, nitamtenga na watu wake.” (LAW. 20:6)

Bila shaka tumesoma marufuku hizi katika maandiko ya Agano la Kale. Lakini hata Agano Jipya nalo limepigaa marufuku vile vile. Tenaa marufuku za Agano Jipya ni nzito zaidi kwa kuwa ni za rohoni zaidi na zinautafsiri uchawi kama tabia hasi iisiyokubalikwa kwa waliokwisha kumwamini Bwana Yesu:

Basi matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya, uasherati, uchafu, ufisadi,  ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi,  husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo, katika hayo nawaambia mapema, kama nilivyokwisha kuwaambia, ya kwamba watu watendao mambo ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa Mungu. (GAL. 5:19-21)

Katika maandiko tuliyosoma tunaona katika orodha ya matendo mabaya ya mwili na “uchawi” nao umo. Tena imewekwa bayana kwamba, wote wanaojihusika na tabia za uchawi hawataurithi ufalme wa Mungu. Kwa maelezo mengine, waamini waliomo makanisa huku wakijihusisha na uchawi, tayari majina yao hayamo katika kitabu cha uzima, na siku ya unyakuo wa kanisa, wao hawatakuwa miongoni mwa watakaomlaki Bwana Yesu mawinguni wakati wa parapanda ya mwisho!

Kana kwamba hii haijatosha, tunamkuta Bwana Yesuatakaporudi duniani, wakati wa hukumu ya mwisho, imetajwa orodha ya watu watakaotupwa katika ziwa la moto. Katika orodha hiyo ya watakaochomwa moto na wachawi nao wametajwa waziwazi:

“Bali waoga, na wasioamini, na wachukizao, na wauaji, na wazinzi, na wachawi, na hao waabuduo sanamu, na waongo wote, sehemu yao ni katika lile ziwa liwakalo moto na kiberiti. Hii ndiyo mauti ya pili.” (UFU. 21:8)

Ujio wa Yesu Kristo duniani
ulikuwa ni kuzivunja kazi za Ibilisi

Mara nyingi tunaposoma habari za ujio wa Yesu Kristo duniani, mkazo mkubwa huwa unalenga ondoleo la dhambi zetu. Na ni kweli kwamba dhambi ndio chanzo cha matatizo yote ya binadamu na Yesu alikuja kushughukia kiini cha matatizo ya binadamu duniani.

Lakini , kabla ya Kristo kukamilisha shughuli hii ya tatizo sugu la dhambi duniani, tunasoma jinsi alivyotumia muda mwingi akitembea huku na huko akihubiri habari za ufalme wa Mungu na wakati huo huo akizivunja kazi za Ibilisi katika maisha ya binadamu.

Mtume Yohana, anapomtaja Yesu anaweka bayana kwamba dhambi yenye ni kazi ya Ibilisi, na kwamba alikuja duniani ili kuzivunja kazi za Ibilisi: “atendaye dhambi ni wa Ibilisi; kwa kuwa Ibilisi hutenda dhambi tangu mwanzo. Kwa kusudi hili Mwana wa Mungu alidhihirishwa, ili azivunje kazi za Ibilisi.” (1 YOH. 3:8)

Kwa maandiko tuliyosoma tunaona waziwazi kwamba, dhambi imehusihwa na Ibilisi moja kwa moja, na kwa njia hii kila mwenye dhambi ametajwa kuwa ni “wa Ibilisi”! Kibinadamu uzoefu unaonesha kwamba mwenyedhambi anakubali kuitwa kwamba ni mwenye dhambi; lakini hakuna mwenye dhambi anayefurahia kuitwa  “yeye ni Ibilisi”!

Kwanini? Kwa sababu kila binadamu kwa asili anamjua Ibilisi kuwa ni kiumbe mwovu na asiyefaa kuitwa kwa jina lake. Ndiyo maana ni vugumu kumkuta mwenye dhambi kamwita mwanawe kwa jina la Ibilisi, au Shetani! Lakini ukweli wa maandiko haubadiliki hata kidogo. Kila mwenye dhambi ni wa Ibilisi.

Sasa kuna kuitwa mwana wa Ibilisi, au mfuasi wa Ibilisi kwa sababu ya dhambi. Lakini kuna jina jingine ambalo ni matokeo ya kuwa “mwana wa Ibilisi” ambalo ni “kuonewa na Ibilisi”.  Wenyedhambi wote ni watumwa wa Ibilisi. Na kwa kuwa Ibilisi ni kiumbe mwovu na katili, kazi zake ni pamoja na kuwatesa na kuwaonea binadamu ambao amewafunga kwa vifungo vyake. `Baadhi ya vifungo hivyo ni pamoja na magonjwa na kila aina za ulemavu. Ndipo tunajifunza jinsi ambavyo Yesu Kristo alikuwa akizivunja kazi za Ibilisi kwa “kuwaponya wote walioonewa na Ibilisi:

habari za Yesu wa Nazareti, jinsi Mungu alivyomtia mafuta kwa Roho Mtakatifu na nguvu naye akazunguka huko na huko, akitenda kazi njema na kuponya wote walioonewa na Ibilisi; kwa maana Mungu alikuwa pamoja naye.” (MDO 10:38)

Ujumbe mkuu katika maandiko haya; tofauti na shughuli za waganga wa tunguri ambazo mikakati yake ni kuwafungia watu kwenye vifungo vya Ibilisi; tunajifunza kwamba ujio wa Yesu Kristo duniani, ulikuwa ni kuzivunja kazi za Ibilisi na mawakala wake duniani.

itaendelea toleo lijalo

Share on Google Plus

About Gospel Kitaa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.