WAJIBU WA KANISA KUHUSU UDHIBITI WA VITENDO VYA UKATILI KWA WATU WENYE ULEMAVU WA NGOZI (3)

Na Askofu Sylvester Gamanywa.

Peter Ash. ©UTSS
Katika toleo lililopita (soma hapa) tulichambua vipengele vinavyoeleza kwamba; “Mungu amepiga marufuku katika Biblia shughuli za uchawi” pamoja na “Ujio wa Yesu Kristo duniani ulikuwa ni kuzivunja kazi za Ibilisi”. Leo tunapitia vipengele vilivyosalia ambavyo ni: “Jamii ya Wakritso wa kwanza ilijengwa juu ya nguvu za Mungu”; “Jamii ya kizazi chetu inahitaji kuokolewa kiimani kutoka kwenye nguvu za giza; na “Jamii ya kizazi chetu inahitaji kuokolewa kiimani kutoka kwenye nguvu za giza; na kuhitimisha na kipengele kisemacho; “Jamii ya waliookolewa na nguvu za Mungu huendelea kulindwa na nguvu za Mungu:

Utangulizi
Ukristo halisi ambao ulienezwa na mitume na wakristo wa karne ya kwanza, haukuwa ni ukristo wa maneno tu na ibada za kujitungia. Kama ilivyo hivi sasa ambapo, tuna utitiri wa madhehebu mengi ya Kristo, lakini upagani ndio umejaa ndani yake.
Hata ile heshima ya Ukristo ambayo jamii ya watu wa karne ya kwanza waliionyesha kwa kanisa hilo, hivi sasa imekuwa kinyume chake.
Kushamiri kwa vitendo vya uchawi na ushirikina, ni matokeo ya kanisa la leo kupoteza nguvu za Roho Mtakatifu ambaye ndiye aliyetumwa kuliwezesha katika kumwakilisha Yesu na mamlaka yake katika jamii.
Ndio maana ni muhimu sana, kama kanisa la leo linataka kuwa na sauti katika jamii, liache propaganda za maneno ya hekima za kibinadamu, na kurejea kwenye msingi ulioachwa na Kristo mwenyewe kupitia mitume na Wakristo wa kwanza.
Imani ya wakristo wa kwanza
ilijengwa juu ya nguvu za Mungu

Huko nyuma tulikwisha kujifunza kwamba Yesu Kristo alipokuwa akiagana na mitume na wanafunzi wake kabla ya kupaa, aliwaahidi kupokea nguvu za Roho Mtakatifu. Pia tulijifunza huyo Roho Mtakatifu aliwashukia wanafunzi hao siku ile ya Pentekoste, na huo ukawa ndio ndio mwanzo wa moto wa Injili, ulioanzia jijini Yerusalemu, ambapo mamlaka ya Kristo iliendelea kuzivunja kazi za Ibilisi kila siku.
Kwa kadri Injili ilivyokuwa ikienea kwenye mataifa mengine nje ya Israeli ndivyo kanisa lilipokuwa likikabiliana ana kwa ana na utendaji wa nguvu za uchawi na ushirikina kwa sababu huu ulikuwa ni ndio mila na desturi za makabila ndani ya nchi hizo. Mfano halisi ni ziara za kitume za Paulo alipotembelea jiji la Wakorintho ambalo lilikuwa limejaa mahekalu ya ibada za mashetani.
 Kwenye mahekalu hayo, viongozi wake walikuwa na waganga wa tunguri na kazi zao zilikuwa ni kupokea kafara za washirikina waliokuwa wakihudhuria ibada hizo. Paulo alipoingia kwenye jiji hilo, na kushuhudia changamoto ya nguvu za giza zilizokuwa hadharani, naye akaazimu kuhubiri Injili yenye mamlaka ya Kristo ili kupambana ana kwa ana na nguvu za giza katika Korintho:
"Na neno langu na kuhubiri kwangu hakukuwa kwa maneno ya hekima yenye kushawishi akili za watu, bali kwa dalili za Roho na za nguvu, ili imani yenu isiwe katika hekima ya wanadamu, bali katika nguvu za Mungu." (1 KOR. 2:4-5)
Kutokana na maandiko haya, tunamwona Paulo alivyotoa kipaumbele katika kudhihirisha nguvu za Roho Mtakatifu ili kuwafanya washirikina wa jiji la Korintho wazione na kujenga imani zao juu ya nguvu za Mungu. Anajenga hoja yake kwa kusisitiza kwamba “....ili imani yenu isiwe katika hekima ya wanadamu, bali katika nguvu za Mungu..”Jamii ya kizazi chetu inahitaji kuokolewa
Kiimani kutoka kwenye nguvu za giza

Japokuwa hivi sasa jamii yetu inaonekana kushangazwa na vitendo vya ushirikina na uchawi; haina maana kwamba, hivi ni vitu vigeni kabisa. Vimekuwepo tangu vizazi vilivyopita, na vimekuwa sehemu ya mila na desturi katika makabila yote.
Hali kadhalika, kama vile ambavyo ushirikina umekuwepo katika kila kizazi, hata Injili yenye nguvu za Mungu ilitakiwa kuhubiriwa kwa kila kizazi ili kuendelea kuzivunja kazi za Ibilisi katika jamii ya kizazi husika.
Ninasema hivi kwa sababu, hakuna raia ambaye hajajenga mahusiano ya kiroho na Mungu, ambaye hayuko chini ya nguvu za giza. Wachilia mbali kila mtu asiyeokolewa bado, bado anaishi katika kongwa la dhambi, hali kadhalika, kila mwmenye mwenye dhambi anaishi chini ya utumwa wa nguvu za giza.
Na ndiyo maana, kazi ya Injili ya wokovu ni kuwaokoa wenye dhambi kutoka kwenye nguvu za giza:"Naye alituokoa katika nguvu za giza, akatuhamisha na kutuingiza katika ufalme wa Mwana wa pendo lake;" (KOL. 1:13)
Wokovu wa Yesu Kristo, sio kusamehewa dhambi tu bali kuvunjwa kwa nguvu ya dhambi ndani ya mwenye dhambi anayetubu na kumjia Mungu. Kuvunjwa kwa nguvu ya dhambi kunakwenda sambamba na kufunguliwa katika vifungo vya nguvu za giza, na kisha kuzipokea nguvu za Mungu.

Jamii ya wanaookolewa na nguvu za Mungu
huendelea kulindwa na nguvu za Mungu

Jambo la muhimu kuzingatia, hususan kwa jamii ya kizazi kipya cha kiroho ambacho kimekwisha kufunguliwa kutoka kwenye nguvu za giza; na kisha kikajazwa nguvu za Mungu; mchakato unaendelea ambao ni kuishi maisha ya kulindwa na nguvu za Mungu kwa njia ya imani katika Kristo mwenyewe: "Nanyi mnalindwa na nguvu za Mungu kwa njia ya imani hata mpate wokovu ulio tayari kufunuliwa wakati wa mwisho." (1 PET. 1:5)
Laiti macho ya mioyo yetu yangefunguliwa tukauona ukweli wa maandiko haya. Jamii ya wale waliokwisha kuokolewa kutoka kwenye nguvu za giza, na kisha kuzipokea nguvu za Mungu katika maisha yao; ushahidi wa nguvu hizo ni pamoja na ulinzi kamili ambao huwawezesha kuendelea kuzishinda na kuzidhibiti kazi za Ibilisi katika jamii.
Kwa kadri idadi ya watu wanaookolewa kutoka kwenye nguvu za giza inavyozidi kuongezeka katika jamii, ndivyo na nguvu za Mungu zinavyozidi kuwa kinga dhidi yao walio nazo. Na sio kuwa nguvu za Mungu ni kinga kwa walio nazo tu, bali hata kazi ya kuendelea kuzivunja kazi za Ibilisi katika jamii inazidi kushika kasi yake. Kushamiri kwa vitendo vya uchawi na ushirikina ni fursa kwa kanisa kudhihirisha kusudi la kuwepo kwake.
Ni wakati wa muafaka sasa kwa kanisa kurejea kwenye misingi ya imani yenye nguvu za Mungu na kuachana na falisafa za kibinadamu; ili kuwasaidia wale wanaoonewa na nguvu za Ibilisi katika jamii. Kwa maana ufalme wa Mungu si katika neno bali katika nguvu. "Maana ufalme wa Mungu hauwi katika neno, bali katika nguvu. (1 KOR. 4:20)

MWISHO


Share on Google Plus

About Gospel Kitaa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.